Kutoka Kuwa Chupa Hadi Kuwa Shanga Zenye Kuvutia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA
UNA haraka. Unachukua chupa iliyo mezani, lakini yateleza kutoka mkononi mwako, yaanguka sakafuni, na kuvunjika. Unatweta, wafagia vipande vilivyopasuka, na kuvitupa katika kikapu cha kuwekea takataka. Kwa upande wako, huo ndio mwisho wa mambo.
Ikiwa ulikuwa unaishi katika Bida, Nigeria, chupa hiyo iliyovunjika huenda ikawa ndio mwanzo tu. Kwa nini? Kwa sababu miongoni mwa Wanupe ambao huishi huko, wahunzi wanaweza kuchukua chupa iliyovunjika na kutokeza shada la ushanga lenye kuvutia. Ni usanii ambao umepitishwa kutoka kizazi hadi kizazi—usanii ambao umebadilika kidogo baada ya karne nyingi.
Utengenezaji Shanga Katika Bida
Karakana ni ndogo, nyumba ya msonge iliyotengenezwa kwa udongo uliokaushwa. Katikati mwa sakafu kuna tanuri ya udongo. Wahunzi hutupa vipande vya mbao katika tanuri, na kuviwasha moto. Moto unachochewa kuwa mkubwa kwa mivukuto inayoendeshwa kwa mikono. Kadiri kuni zaidi ziongezwavyo, cheche nyekundu inazuka juu ya tanuri. Chupa yaning’inizwa kwenye ufito juu ya tanuri, mara gilasi hiyo yawa laini na kuning’inia ikiwa imeyeyuka.
Mtengeneza-shanga atengeneza ushanga mmoja-mmoja. Anawekelea ufito uliochongoka juu ya moto karibu na ufito unaoning’iniza gilasi. Wakati ncha iliyochongoka inapokuwa nyekundu mno, anaisogeza kwenye kidonge kinachoning’inia cha gilasi iliyoyeyuka. Kisha, kwa kugeuza ufito kwa vidole vyake, yeye auvingirishia sehemu ya gilasi inayotoshana na ushanga.
Kisha, akitumia upanga, yeye alainisha na kufinyanga hiyo gilasi kuwa ushanga. Ikiwa ana ustadi hasa, huenda akafanya kazi kwa kutumia rangi kadhaa za gilasi, akitia umaridadi kwenye kila ushanga anaoufanyiza. Mwishowe, anatumia upanga huo ili kusogeza ushanga polepole na kuuondoa kwenye ufito hadi kwenye sufuria yenye jivu ambapo ushanga huo utapoa. Ushanga umekamilika sasa. Kitundu kilichofanyizwa na ufito chawa kitundu kitakachotumiwa kutia ushanga huo uzi. Kinachobaki tu ni kuosha huo ushanga na kuuunganisha na shanga zingine kwa uzi ili kufanyiza mkufu.
Kujifunza Huo Ufundi
Mtu hujifunzaje ufundi wa kutengeneza shanga? Watoto Wanupe huanza kwa kutazama. Kufikia wakati wanapokuwa na umri wa miaka kumi, wao husaidia kukusanya na kukata kuni.
Hatua ifuatayo ni kujua kutumia vizuri mivukuto. Mivukuto ni vifuko viwili vilivyotengenezwa kwa kitambaa, kila kimoja chavyo kikiwa kimeunganishwa kwenye kijiti. Ili kuendesha mivukuto, ni lazima “mpulizaji” ashike kijiti katika kila mkono na kuvisogeza kwa haraka juu na chini. Yeye anahitaji nguvu na vilevile upatanifu. Ni lazima awe mwenye nguvu vya kutosha kupiga mivukuto kwa kuendelea hadi kipindi cha kutengeneza shanga kiishe, na kipindi kimoja chaweza kudumu kwa saa nyingi!
Anapaswa pia kuwa na upatanifu wa kutosha kudumisha mwendo wa haraka usiobadilika, akipiga mivukuto kwa mwendo wa kasi ulio sahihi. Akipiga polepole sana, joto la moto halitafanya gilasi iwe laini vya kutosha kuweza kufanyiwa kazi. Akipiga haraka sana, joto litakalotokezwa huenda likafanya gilasi ianguke kutoka kwenye ufito na kuingia motoni.
Kwa kawaida, mtengeneza-shanga anayejifunza atafanya kazi ya mivukuto kwa miaka mitano. Mwishowe, ajifunza jinsi ya kurembesha shanga. Sehemu ngumu ya kazi hii ni kujifunza kustahimili joto litokalo motoni, ambalo, likiongezewa joto la jua la kitropiki, laweza kuwa jaribio gumu sana.
Yeye hujifunza hatua kwa hatua. Baada ya kumsaidia mtengeneza-shanga mwenye uzoefu katika kushughulika na fito, mwanafunzi hujifunza kufanyiza shanga ndogo zilizo na rangi moja tu. Baada ya muda, afanya maendeleo na kufanyiza shanga kubwa zaidi na shanga zilizopambwa kwa kigezo kilichowekelewa juu ya gilasi ya rangi nyingine. Watengeneza-shanga wazoefu hufanya hiyo kazi ionekane kuwa rahisi, lakini huchukua wakati ili kujua vyema ustadi unaohitajiwa ili kutokeza mfuatano wa shanga, ushanga mmoja baada ya mwingine, zote zikiwa na ukubwa, umbo, na kigezo sawa.
Utengenezaji shanga ni ufundi wenye kufurahisha. Watengeneza-shanga hufurahi wanapoona watu kotekote nchini wakiwa wamejipamba kwa shanga zao zenye rangi tofauti-tofauti—shanga ndogo mno zinazovaliwa na watoto, shanga zilizoundwa kwa njia nzuri sana zinazovaliwa na wanawake, na shanga nzito za wakati wa sherehe zinazovaliwa na wanaume. Kuna furaha pia wakati wa sherehe wakati ambapo watu hujikusanya kuzunguka karakana ili kuimba na kucheza kufuatana na mwendo wa mivukuto.
Chasema kitabu History of West Africa: “Utokezaji wa kiufundi wa Wanupe kwa kutumia . . . gilasi . . . bado ni moja ya zilizo bora kabisa barani.” Wengine wanakubali. Mishonari mmoja Mkristo alisema hivi: “Tulinunua shanga kutoka Bida na vilevile sehemu nyinginezo ili kuwapa rafiki zetu tulipokuwa tukienda likizo. Tulipofika Marekani rafiki zetu walipendelea shanga za kutoka Bida kila wakati!”
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kutia moto gilasi katika tanuri