Majumba Yenye Kumetameta ya Baharini
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA
“KUNA kilima-barafu mbele tu!” apaaza sauti mlinzi mwenye wasiwasi. Mabaharia walioko kwenye jukwaa la kuongozea meli wanaitikia mara moja. Injini zafanywa ziende kinyume-nyume ili kuepuka mgongano. Lakini ni kuchelewa mno. Upande wa kulia wa meli wakatwa vibaya mno.
Kwa muda usiopita saa tatu, Atlantiki ya Kaskazini yafunika meli ya kistarehe iliyo kubwa zaidi ulimwenguni isafiriyo kwa ukawaida. Mnamo Aprili 15, 1912, siku tano tu katika safari yayo ya kwanza kutoka Ulaya hadi Amerika ya Kaskazini, Titanic yatua kwenye sakafu ya bahari, kilometa nne chini ya uso wa bahari. Abiria wapatao 1,500 na mabaharia wafa baharini.
Na ni nini kilichobakia cha hicho kilima-barafu kikubwa? Kilibaki kikiwa kimeshikana. Ni ncha yacho tu iliyogongana na Titanic. Siku iliyofuata, waokoaji walikiona kikielea kuelekea upande wa kusini kuingia katika maji yenye ujoto zaidi, kana kwamba hakuna kitu kilikuwa kimetendeka. Mwisho wa hicho kilima-barafu, kuyeyuka hatua kwa hatua katika bahari kuu iliyoenea sana, utasahauliwa mara. Ingawa hivyo, kuzama kwa Titanic, bado kunakumbukwa kuwa msiba wa baharini wenye kuogofya.
Vilima-barafu! Ni vyenye kuvutia sana na vyenye fahari, lakini ni imara sana. Je, umepata kuviona kwa ukaribu na kuhisi athari vinavyokuwa nayo kwa mwanadamu na asili? Je, ungependa kujua jinsi vilivyokuja kuwapo na kwa nini? Na nini kinafanywa ili kulinda watu walio baharini kutokana na hatari ziwezazo kutokea za vilima-barafu? (Ona sanduku “Ushikaji Doria wa Kimataifa wa Maeneo Yenye Vilima-Barafu.”)
Mwanzo na Kawaida ya Vilima-Barafu
Vilima-barafu ni kama vijiwe vya barafu vikubwa mno vya maji matamu. Hutoka katika barafuto na barafu tandavu Kaskazini na katika Antaktika. Je, ulijua kwamba utando wa barafu wa Antaktika hutokeza asilimia 90 ya vilima-barafu vya duniani pote? Huo pia hutokeza vilima-barafu vikubwa kuliko vyote. Hivi vina kimo cha meta 100 juu ya uso wa maji na vyaweza kuwa na urefu wa kilometa 300 na upana wa kilometa 90. Vilima-barafu vikubwa sana vyaweza kuwa na uzani wa kuanzia tani milioni 2 hadi milioni 40. Na sawa na fuwele za theluji, hakuna vilima-barafu viwili vinavyofanana. Vingine viko kama meza, au vyenye sehemu ya juu iliyo bapa. Vingine vina ncha iliyochongoka, viko kama mnara, au vina umbo la kuba.
Kwa kawaida ni sehemu moja kwa saba au moja kwa kumi tu ya kilima-barafu ionekanayo juu ya maji. Hili ni kweli kuhusiana na vilima-barafu vilivyo bapa juu. Ni kama vile unavyoona kijiwe cha barafu kikielea juu ya gilasi ya maji. Hata hivyo, uwiano huu wa barafu iliyo nje ya maji kwa barafu iliyo ndani ya maji hutofautiana, ikitegemea umbo la kilima-barafu.
Vilima-barafu vya Antaktika huelekea kuwa na sehemu ya juu iliyo bapa na mbavu bapa, huku vilima-barafu vya Aktiki mara nyingi vikiwa bila umbo hususa au vya kimnara. Hivi vya pili, ambavyo mara nyingi hutoka katika utando mkubwa wa barafu inayofunika Greenland, hutokeza tisho kubwa mno kwa mwanadamu, kwa kuwa vyaweza kuchukuliwa na mkondo wa maji na kuingia katika njia za meli zinazovuka Atlantiki.
Vilima-barafu hutokezwaje? Katika maeneo ya dunia ya kaskazini na kusini, mkusanyo wa theluji na mvua inayoganda mara nyingi hupita kuyeyuka na uvukizo. Hili husababisha hizo tabaka za theluji ambazo huongezeka kwenye uso wa bara, zije kuwa barafuto. Mwaka baada ya mwaka, kadiri theluji na mvua zaidi inavyomwagika, mrundikano wenye kuendelea hutokea. Hili hufanyiza utando wa barafu kufunika maeneo makubwa ya bara kama ule wa Greenland. Hatimaye, barafu hiyo hufikia unene na ugumu ambao husababisha barafuto nzito iteleze polepole mno kutoka miinamo ya milima iliyoinuka hadi kwenye mabonde na kisha baharini. Katika kufafanua uhamaji huu, Benard Stonehouse alitaarifu hivi katika kitabu chake North Pole, South Pole: “Barafu ngumu ni yenye kunyumbuka lakini hupoteza umbo haraka; chini ya msongo mafuwele yayo ya kipembesita hujipanga, kisha huteleza juu ya moja na nyingine ili kufanyiza mtiririko na mwanguko tunaohusianisha na barafuto.”
Ebu wazia mto wa barafu ukisonga kuvuka bara lisilo laini polepole mno, kama machujo ya asali ya miwa yaliyo baridi. Ikiwa tayari na mipasuko ya kina iliyo wima, barafu tandavu hii itaathiriwa zaidi ili kufanyiza hali yenye kutazamisha mara ifikapo mwambao. Kwa sababu ya athari zilizounganishwa za kujaa na kupwa kwa maji, mawimbi yenye kubadilika, na mmomonyoko wa chini ya maji, kipande kikubwa cha barafu ya maji matamu ambacho chaweza kuenea kilometa zipatazo 40 kuingia baharini kitavunjika kwa kishindo kutoka kwenye barafuto. Kilima-barafu kinafanyizwa! Mtazamaji mmoja alikifafanua hiki kuwa “kasri yenye kumetameta inayoelea.”
Katika Aktiki, kati ya vilima-barafu 10,000 na 15,000 hufanyizwa kila mwaka. Hata hivyo, ni vichache sana, kwa kulinganisha, hufikia maji ya sehemu za kusini kwenye pwani ya Newfoundland. Ni nini hupata vile ambavyo hufika?
Uhamaji wa Vilima-Barafu
Baada ya vilima-barafu kuachanishwa, mikondo ya bahari kuu huchukua vingi vyavyo kwa safari ndefu kabla ya kuvigeuza vingine vyavyo kuelekea magharibi na kusini na hatimaye kuingia Bahari Labrador, iliyopewa lakabu Kichochoro cha Kilima-Barafu. Vilima-barafu ambavyo huokoka kuchukuliwa kwavyo na mkondo wa maji kunakochukua miaka miwili hivi kutoka mahali vilipofanyizwa na kuingia katika Atlantiki iliyo wazi kuelekea baharini Labrador na Newfoundland huwa na muda wa kudumu mfupi. Kwa kuelekea kwenye maji yenye ujoto, hivyo hupatwa na mzoroto mkubwa kwa sababu ya kuyeyuka, mmomonyoko, na kuachanishwa zaidi.
Kwa kawaida, wakati wa mchana barafu huyeyuka na maji hujikusanya katika nyufa. Wakati wa usiku maji huganda na kutanuka katika mipasuko hiyo na kusababisha vipande vipasuke. Hili hufanyiza badiliko la ghafula katika umbo la kilima-barafu, likibadilisha kitovu chacho cha uzito. Barafu hiyo kubwa hubingirika majini, ikifunua umbo jipya kabisa la barafu.
Kadiri kawaida hii iendeleavyo na kasri za barafu kupungua zaidi katika ukubwa kwa mpasuko, hizo hutokeza vilima-barafu vyazo vyenyewe viitwavyo “vijilima-barafu,” vilivyo na ukubwa wa nyumba ya wastani, na “growlers,” vilivyo na ukubwa wa chumba kidogo—hivyo vya mwisho vikiitwa hivyo kwa sababu ya sauti vinavyotokeza vinapoelea katika mawimbi. Growlers vidogo zaidi vyaweza hata kugaagaa kuingia katika maji yasiyo na kina ya ufukoni na mahali ambapo maji huingilia baharini.
Haidhuru hali ziwe zipi, mazingira katika maji yaliyo sehemu ya kusini zaidi yatasababisha kuvunjika-vunjika kwa kilima-barafu kuwa vipande vidogo vya barafu ya maji matamu kisha kuwa sehemu ya bahari kuu. Hata hivyo, hadi hilo litukie, lazima watu watende kwa tahadhari kuelekea vilima-barafu.
Jinsi Vilima-Barafu Huathiri Maisha Zetu
Wavuvi wanaotegemea bahari kuu kwa ajili ya kujiruzuku huelekea kuona vilima-barafu kuwa udhia na hatari. Mvuvi mmoja alisema hivi: “Huenda kilima-barafu kikatamaniwa na watalii, lakini kwa mvuvi ni hatari iwezayo kutokea.” Wavuvi wamepata kurudi kuangalia walichoshika, na kupata tu kwamba kilima-barafu, kilichosukumwa na maji yenye kupwa na mkondo, kimeharibu majarife yao yenye thamani pamoja na walichoshika.
Vilima-barafu vyastahili staha. “Ni jambo zuri kukaa mbali,” asema nahodha fulani wa merikebu. “Vilima-barafu havitabiriki! Vipande vikubwa mno vyaweza kuvunjika kutoka vilivyo juu sana, au wakati vinapogonga chini, vipande vikubwa vyaweza kuvunjika na kuwarukia. Pia, kilima-barafu kinaweza kuvurura na kubingirika, yote hayo yakiweza kuwa yenye msiba kwa yeyote anayethubutu kwenda karibu sana!”
Kuparuzwa kwa sakafu ya bahari kuu na vilima-barafu ni sehemu nyingine inayotia wasiwasi. “Ikiwa kina cha maji ambacho kilima-barafu chakokota ni sawa na kina cha maji, inajulikana kwamba sehemu yacho ya chini huchimba mitaro mirefu na yenye kina. Utendaji huo katika maeneo ya uvumbuzi wa mafuta ungekuwa na matokeo yenye uharibifu kwenye viweko vilivyo sakafuni mwa bahari kama vile majengo yaliyo juu ya visima vya mafuta,” kulingana na mchunguzi mmoja.
Kufikia sasa huenda ikawa unafikiria kwamba tungekuwa afadhali bila vilima-barafu. Hata hivyo, si simulizi lote la kilima-barafu lililo hasi. Mtu mmoja kutoka Newfoundland alitoa maelezo hivi: “Miaka mingi iliyopita, kabla ya friji kujulikana, watu katika vijiji fulani vidogo vya pwani wangetoa vipande vidogo vya kilima-barafu na kuvitumbukiza katika visima vyao ili kuyaweka maji yakiwa baridi kama barafu. Zoea jingine lilikuwa kuhifadhi vipande vya barafu ya kilima-barafu katika mapipa ya vumbi ya mbao ili kusaidia katika kutokeza aisikrimu ya kutengenezwa nyumbani.”
Watalii huvutiwa hasa na milima hii mikubwa ya kibarafu yenye kuelea. Wao hutafuta mahali wawezapo kuona vyema kwenye mwambao wenye mawe-mawe wa Newfoundland ili kupata mwono wa eneo lote la Atlantiki na kuburudisha macho yao kwa majitu haya ya baharini. Picha nyingi hupigwa ili kuhifadhi pindi hii pichani.
Vilima-barafu pia vina uwezo wa kutoa ugavi usioelekea kwisha wa maji safi ya kunywa. Ukenekaji na uwekaji maji ya kilima-barafu katika chupa waweza hatimaye kuwa jambo lenye mafanikio katika siku hizi ambapo kuna uchafuzi wa maji usio na kifani. Kuhusiana na kupata maji ya kunywa kwa wingi, huenda likaonekana kuwa jambo rahisi kutafuta kilima-barafu na kukikokota hadi kwenye bandari kwa ajili ya utayarishaji. Kwa uhalisi, ni tatizo kubwa mno ambalo limethibitika kuwa lenye kuogofya.
Ajabu ya Uumbaji wa Yehova
Muumba wa mbingu na dunia auliza hivi: “Barafu ilitoka katika tumbo la nani?” (Ayubu 38:29) Elihu alijua, kwani alikuwa ametangulia kusema hivi: “Barafu huletwa kwa pumzi za Mungu.”—Ayubu 37:10.
Kwa hiyo, tunapoona maajabu haya ya baharini yenye kupanda juu kama minara na yenye kung’aa, mawazo yetu yanamgeukia Muumba wetu, aliyeyaweka hapo. Kama mtunga-zaburi, tunasema: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.” Yeye aongeza hivi: “Matendo yako ni ya ajabu.”—Zaburi 104:24; 139:14.
Kwa kweli, Yehova ni Muumba mtenda-maajabu. Jinsi tunavyotamani kumjua vyema zaidi! Twaweza kufanya hivyo kwa kutoa uangalifu kwa Neno lake.—Warumi 11:33.
[Sanduku katika ukurasa wa 18]
Ushikaji Doria wa Kimataifa wa Maeneo Yenye Vilima-Barafu
Baada ya msiba wa meli ya abiria ya Titanic, shirika la Ushikaji Doria wa Kimataifa wa Maeneo Yenye Vilima-Barafu (IIP) lilianzishwa katika 1914 ili kupambanua mahali palipo na vilima-barafu, kutabiri vinakoelekea kutokana na mikondo ya bahari kuu na ya upepo, na kisha kuandaa maonyo ya maeneo yenye vilima-barafu kwa umma. Kwa kusudi la kuandaa ulinzi kutokana na majitu haya yenye kumetameta ya baharini, kila jitihada imefanywa ili kupata ujuzi wa namna na tabia za barafu. Tekinolojia inayotumiwa hutia ndani uchunguzaji wa kuona na wa kirada unaofanywa na ndege, ripoti za meli utazamaji-barafu, upigaji picha wa satelaiti, na uchanganuzi na matabiri ya bahari kuu.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Chenye umbo la mnara
Chenye umbo la kuba
Chenye sehemu ya juu iliyo bapa