Historia ya Aisikrimu
AISIKRIMU (mtindi-barafu) imetoka mbali tangu ilipoanza. Waroma wa kale walivumbua barafu ya sorbeti. Kitindamlo hicho kilichogandishwa nusu, kilichotengenezwa kwa theluji, matunda, na asali, kingeweza kuliwa na matajiri nyakati fulani. Ustadi kamili wa kutengeneza sorbeti uliboreshwa kwa muda mrefu, na ni wazi ulifikia upeo wakati wa wapishi hodari Waarabu katika Enzi za Katikati. Maneno “soberti” na “sherbeti” labda ni ya Kiarabu kwa asili.[3]
Ingeweza kusemwa kwamba ile sorbeti murua, itengenezwayo hasa kutokana na maji, ndiyo iliyotangulia aisikrimu ya ki-siku-hizi. [4] Hatua ya badiliko kuu ilifikiwa kwa kuanza kutumia maziwa, mayai, sukari, na vikoleza-ladha, kukatokea mchanganyo wenye ladha tamu ulio na krimu (mtindi).[5] Kama wewe ungaliishi katika miaka ya 1600 kwenye baraza la mfalme Mfaransa Louis 14, ungalishuhudia aisikrimu ikitumiwa kwa mara ya kwanza na jamii ya wenye vyeo vya juu.[6] Wakati huo kulikuwa na ubishi miongoni mwa madaktari na wanachuo wengine juu ya kama aisikrimu ingeweza au haingeweza kuyeyushwa na mwili tumboni.[7]
Iliwezekanaje kutengeneza aisikrimu na hali hakukuwa na mashine za barafu za kuhifadhia aisikrimu? Kwanza, viwekeo viwili vya mbao au mabati vilitumiwa, kimoja kikiwa ndani ya kingine. Ule mchanganyo wa aisikrimu ulitayarishwa katika kile kiwekeo kidogo, na nafasi iliyokuwa kati ya viwekeo hivyo viwili ikajazwa barafu na chumvi. Baada ya vichanganyo kuunganishwa, mchanganyo uliachwa ndani ya kiwekeo, na hapo aisikrimu ikawa tayari.[8] Ile barafu ilitoka wapi? Karne kadhaa zilizopita watu waligundua kwamba barafu ingeweza kutengenezwa na kuwekwa akibani kwa kukusanya theluji katika majira ya baridi kali na kupakiwa katika mashimo yaliyofunikwa kwa nyasi kavu na kwa matawi ya mti oki. Katika karne ya 19, mashine za kutengenezea barafu zilibuniwa na kutumiwa kwa utengenezaji wa barafu nyingi. Kule nyumbani hiyo barafu ilihifadhiwa katika masanduku ya barafu yaliyotengenezwa kwa mbao na magome ya miti.[9]
Karne hii imeona marekebisho mengi mazuri zaidi katika mbinu za kutengeneza aisikrimu. Friji, mashine za aisikrimu, na vifaa vingine sasa vyafanya iwe rahisi kufanyiza aisikrimu ya viwandani na nyumbani, kwa kufuata viwango bora vya kanuni za afya.[10]
Ustadi wa Kutengeneza Aisikrimu
Mtengenezaji aisikrimu aliye na ujuzi ni lazima aijue kazi yake, kumaanisha ni lazima awe mchanganyi na mpishi mzuri, nyakati nyingine mstadi, na kwa kiasi fulani awe mwanakemia na mjuzi wa viini. Ni nini hufanya aisikrimu iwe ya kushikana sana, ya mtindi-mtindi, na tamu? Haya basi, kwa kielelezo fikiria aisikrimu iliyofanyizwa viwandani. Wakati wa kuifanyiza, mafuta ya mgando na vitu vilivyofanyizwa kutokana na mboga huongezwa ili kufanya mchanganyo ushikane. Pia kiasi kifaacho cha mayai, sukari, na, ikiwa lazima, rangi ya kiasili na kiongezea-ladha, kama koko, kahawa, na matunda huongezwa. Pia kuna aisikrimu ya siagi ya njugu.
Baada ya vitu hivyo kuchanganywa vizuri kwenye joto la digrii 70 Sentigredi, huletwa kwenye joto la digrii 90 Sentigredi kwa jitihada ya kuua viini vibaya vyovyote ambavyo huenda ikawa vimekuwapo. Baada ya kupozwa ifikie digrii 4 Sentigredi kwa muda wa saa chache, hugandamana. Hatua ya pili ni ya kuigandisha kuwa barafu. Joto hupunguzwa haraka-haraka kufikia digrii ya alama 6 hadi 10 chini ya sifuri Sentigredi, huku ule mchanganyo ukikorogwa polepole. Hiyo huruhusu hewa iingie, na hilo ni mojawapo mambo yachangiayo kuipa aisikrimu kawaida yayo ya kuwa na mtindi ulioshikamana.[11]
Karne nyingi zimepita tangu Waroma walipofurahia sorbeti zao na tangu aisikrimu ilipoanzishwa kwenye baraza la Louis 14. Lakini safari ile nyingine ufurahiapo kitindamlo chako cha kugandishwa ukipendacho sana, kiwe ni sorbeti au aisikrimu, shukuru wale Waroma wa kale kwa kutokeza kitu chenye kuburudisha jinsi hiyo!