Sayari Yetu Dhaifu—Vipi Kuhusu Wakati Ujao?
MIAKA 200 iliyopita, mtawala Mmarekani Patrick Henry alisema: “Sijui njia nyingineyo ya kuamua kuhusu wakati ujao ila kupitia wakati uliopita.” Wakati uliopita, mwanadamu amekanyanga-kanyanga mazingira. Je, ataanza kutenda kwa njia afadhali zaidi katika wakati ujao? Kufikia sasa, dalili ni zenye kutamausha.
Ingawa maendeleo yenye kustahili sifa yamefikiwa, hasa yamekuwa ya kinje-nje, yakishughulikia dalili za hali hiyo badala ya visababishi. Ikiwa nyumba imeliwa na mchwa, kupaka mbao rangi hakutazuia kuanguka kwa nyumba hiyo. Ni kwa kuifanyia marekebisho makubwa tu kwamba unaweza kuiokoa. Vivyo hivyo, ni lazima wanadamu warekebishe namna wanavyotumia sayari hii. Kudhibiti tu uharibifu kwaambulia patupu.
Akichanganua matokeo ya miaka 20 ya kusimamia mazingira katika Marekani, mtaalamu mmoja afikia mkataa kwamba “mashambulizi ya mazingira hayawezi kudhibitiwa kwa njia yenye matokeo, bali lazima yazuiwe.” Kwa wazi, kuzuia uchafuzi ni afadhali kuliko kutibu madhara yao mabaya. Lakini kufikia lengo hilo hasa kungehitaji badiliko kuu katika jamii ya kibinadamu na katika mwelekeo wa biashara kubwa. Kitabu Caring for the Earth chakubali kwamba kutunza dunia kwahitaji “kanuni, uchumi na jamii zilizo tofauti na nyingi zilizoenea leo.” Ni zipi baadhi ya kanuni hizi ambazo zahitaji kubadilishwa ili kuiokoa sayari?
Visababishi Vilivyokwisha Kuthibitika vya Hayo Matatizo
Ubinafsi. Kuweka masilahi ya sayari mbele ya yale ya kutumia wanadamu vibaya ni hatua ya kwanza iliyo ya lazima kuelekea kulinda mazingira. Hata hivyo, ni wachache ambao wako tayari kuachilia mtindo-maisha wa kutaka vingi, hata ingawa huenda wachangia kuharibia vizazi vya wakati ujao sayari. Wakati serikali ya Uholanzi—mojapo nchi zilizochafuliwa zaidi za Ulaya Magharibi—ilipojaribu kuwekea mipaka kusafiri kwa magari ikiwa sehemu ya kampeni ya kupinga uchafuzi, upinzani wenye kuenea uligomea huo mpango. Ingawa barabara za Uholanzi ni zenye kusongamana zaidi ulimwenguni, waendesha-magari hawakuwa na nia hata kidogo ya kuachilia uhuru wao.
Masilahi ya kibinafsi huathiri wafanya-maamuzi sawasawa na umma kwa ujumla. Wanasiasa wanakawia kufikiliza sera za kimazingira ambazo huenda zikawakosesha kura, na wanaviwanda hukalia madokezo yoyote ambayo huenda yakahatarisha faida na ukuzi wa kiuchumi.
Pupa. Inapohusu uchaguzi baina ya faida na kuhifadhi, mara nyingi fedha huvunja milima. Viwanda vyenye nguvu hujaribu kuwa na uvutano juu ya maofisa wa serikali ili kupunguza udhibiti wa uchafuzi au kuepuka maelekezo ya serikali kabisa. Uharibifu wa tabaka la ozoni hudhihirisha tatizo hilo. Kuchelewa mno kufikia Machi 1988 mwenyekiti wa kampuni fulani kuu ya kemikali ya Marekani alitaarifu: “Kwa sasa, uthibitisho wa kisayansi hauonyeshi uhitaji wa haraka ya kupunguza mitoko ya CFC.”
Hata hivyo, kampuni hiyohiyo ilipendekeza kuondosha kabisa klorofluorokaboni (CFC). Je, lilikuwa badiliko la maoni? “Haikuhusu kwa vyovyote kama mazingira yalikuwa yakiharibiwa au la,” akaeleza Mostafa Tolba, mkurugenzi-mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). “Hiyo [ilihusu] ni nani atapata marupurupu [ya kiuchumi].” Sasa wanasayansi wengi wanafahamu kwamba kuharibiwa kwa tabaka la ozoni ni mojapo misiba mibaya zaidi iliyofanyizwa na mwanadamu katika historia.
Kutojua. Mambo yale tunayojua ni machache mno yakilinganishwa na yale tusiyojua. “Bado twajua machache kwa kulinganishwa kuhusu wingi wa uhai katika misitu ya mvua ya kitropiki,” aeleza Peter H. Raven, mkurugenzi wa Missouri Botanical Garden. “Kwa kushangaza, twajua mengi—mengi zaidi—kuhusu umbo la mwezi.” Hilo ni kweli pia kuhusu angahewa. Ni kaboni dioksidi nyingi kiasi gani tuwezayo kuendelea kufukiza angani bila kuathiri tabia ya nchi tufeni? Hakuna ajuaye. Lakini kama vile gazeti Time lilivyosema, “ni kukosa akili kushurutisha asili kwa majaribio makubwa mno kama hayo wakati ambapo matokeo hayajulikani na madhara yaelekeayo kutokea ni yenye kutisha sana kuweza kuwaziwa.”
Kulingana na makadirio ya UNEP, yawezekana kwamba upotezo wa ozoni kufikia mwisho wa karne hii hatimaye utasababisha mamia ya maelfu ya visa vipya vya kansa ya ngozi kila mwaka. Tokeo kwa mimea na uvuvi bado halijulikani, lakini latazamiwa kuwa kubwa mno.
Maoni yasiyo na busara. Kinyume na misiba mingineyo, matatizo ya kimazingira hutunyemelea kwa ghafula sana. Hili hukinza majaribio ya kutokeza hatua ya pamoja kabla ya uharibifu wenye kudumu kufanyika. Kitabu Saving the Planet hulinganisha hali yetu ya sasa na ile ya abiria waliohatarishwa kwenye Titanic iliyodunguliwa mnamo 1912: “Ni wachache wanaotambua viwango vya msiba unaoelekea.” Watungaji waamini kwamba sayari yaweza kuokolewa ikiwa wanasiasa na wafanya biashara watauona uhalisi wa mambo na kufikiria masuluhisho ya muda mrefu badala ya faida za muda mfupi.
Mitazamo ya kujifikiria. Kwenye mkutano wa Earth Summit katika 1992, waziri mkuu wa Hispania Felipe González alionyesha kwamba “hilo tatizo ni la kitufe, na suluhisho haliwezi kuwa penginepo isipokuwa tufeni.” Hilo ni kweli kabisa, lakini kupata masuluhisho ambayo yakubalika tufeni pote ni kibarua kigumu. Mjumbe wa Marekani kwenye mkutano wa Earth Summit alisema hivi waziwazi: “Wamarekani hawataachilia mtindo-maisha wao.” Mwanamazingira wa India Maneka Gandhi, kwa upande ule mwingine, alilalamika kwamba “mtoto mmoja katika Magharibi hula chakula kingi kufikia mara 125 kuliko katika Mashariki.” Yeye alidai kwamba “karibu kudhoofika kwote kwa kimazingira katika Mashariki ni kwa sababu ya ulaji katika Magharibi.” Tena na tena, majaribio ya kimataifa ya kuboresha hali yamegonga mwamba kwenye masilahi ya kitaifa ya kujifikiria.
Licha ya matatizo haya yote ya msingi, kuna sababu za kutazamia wakati ujao tukiwa na uhakika. Moja ya hizo ni uwezo wa kujirekebisha wa mfumo wa kinga wa sayari yetu.
Uponyaji wa Dunia
Kama mwili wa binadamu, dunia ina uwezo wa kushangaza wa kujiponya. Kielelezo chenye kutokeza zaidi cha jambo hili kilitukia karne iliyopita. Katika 1883 kisiwa cha kivolkeno cha Krakatau (Krakatoa) cha Indonesia kililipuka kwa mlipuko mkubwa ambao ulisikika umbali wa yapata kilometa 5,000 mbali. Kilometa zipatazo 21 za mraba za udongo zilitupwa angani, na thuluthi mbili za kisiwa zilizikwa baharini. Miezi minane baadaye ishara pekee ya uhai ilikuwa buibui mwenye kuonwa kwa hadubini. Leo kisiwa chote kimefunikwa kwa vuvumko la mimea ya kitropiki, ambalo ni makao ya maelfu ya spishi za ndege, mamalia, nyoka, na wadudu. Kwa wazi kupona huku kumewezeshwa na ulinzi ambao kisiwa hicho kimekuwa nao kikiwa sehemu ya Mbuga ya Kitaifa ya Ujung Kulon.
Uharibifu wa kibinadamu waweza pia kuondolewa. Dunia ikipewa wakati wa kutosha, inaweza kujiponya. Swali ni, Je, wanadamu wataipatia dunia pumziko inalohitaji? Yaelekea sivyo. Lakini kuna Mtu Fulani ambaye ameazimia kuiacha sayari yetu ijiponye—Mmoja aliyeiumba.
“Acheni Dunia Itereme”
Mungu hakukusudia mwanadamu aiharibu dunia. Yeye alimwambia Adamu “ailime na kuitunza” bustani ya Edeni. (Mwanzo 2:15) Hangaiko la Yehova la kulinda mazingira pia lilidhihirishwa katika nyingi za sheria ambazo aliwapatia Waisraeli. Kwa kielelezo, waliambiwa waiache ardhi bila kulimwa mara moja kila miaka saba—mwaka wa Sabato. (Kutoka 23:10, 11) Waisraeli walipopuuza mara kwa mara jambo hili na amri nyinginezo za kimungu, mwishowe Yehova aliruhusu Wababiloni kuwaondosha katika bara lao, ambalo lilikaa ukiwa kwa miaka 70 ‘hata nchi ilipofurahia sabato zake.’ (2 Mambo ya Nyakati 36:21) Kwa sababu ya kitangulio hiki cha kihistoria, si ajabu kwamba Biblia husema kwamba Mungu ‘atawaharibu hao wanaoharibu dunia’ ili kwamba dunia iweze kupona kutokana na mashambulio ya kimazingira ya binadamu.—Ufunuo 11:18.
Hata hivyo, tendo hilo litakuwa tu hatua ya kwanza. Uokokaji wa sayari, kama mwanabiolojia Barry Commoner aonyeshavyo kwa kufaa, “wategemea wakati uleule kukomesha vita na vitu vya asili na miongoni mwetu.” Ili kufikia mradi huo, lazima watu wa dunia ‘wafunzwe na Yehova’ kutunzana na kutunza maskani yao ya kidunia. Kama tokeo, amani yao itakuwa “nyingi.”—Isaya 54:13.
Mungu atuhakikishia kwamba kutakuwa na ukarabatishaji wa mfumo wa mazingira wa dunia. Badala ya kunyemelea kwa kasi, majangwa ‘yatachanua maua kama waridi.’ (Isaya 35:1) Badala ya upungufu wa chakula, kutakuwa na “wingi wa nafaka katika ardhi.” (Zaburi 72:16) Badala ya kuangamizwa kutokana na uchafuzi, mito ya dunia ‘itapiga makofi.’—Zaburi 98:8.
Ni wakati gani badiliko kama hilo litawezekana? Wakati “Yehova mwenyewe atakuwa mfalme.” (Zaburi 96:10, New World Translation) Utawala wa Mungu utahakikisha baraka kwa kila kiumbe kinachoishi duniani. “Acheni dunia itereme,” asema mtunga-zaburi. “Acheni bahari zivume kwa mshindo, na vyote vilivyomo; acheni mashamba yachachawe, na vyote vilivyomo. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa shangwe.”—Zaburi 96:11, 12, New International Version.
Dunia iliyobarikiwa na Muumba wayo na kutawaliwa kwa uadilifu ina wakati ujao mtukufu. Biblia hufafanua matokeo hivi: “Fadhili na kweli zimekutana, haki na amani zimehusiana. Kweli imechipuka katika nchi, haki imechungulia kutoka mbinguni. Naam, BWANA atatoa kilicho chema, na nchi yetu itatoa mazao yake.” (Zaburi 85:10-12) Siku hiyo itakapopambazuka, sayari yetu haitakuwa hatarini milele.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Kama mwili wa binadamu, dunia ina uwezo wenye kushangaza wa kujiponya