Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 1/8 kur. 19-23
  • Sikuwa na Lengo Lakini Nikapata Kusudi Maishani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sikuwa na Lengo Lakini Nikapata Kusudi Maishani
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo Yenye Kuhuzunisha ya Kufanya Makosa
  • Jitihada za Kurekebika
  • Kukosa Kwangu Lengo Kwaendelea
  • Maisha Baharini Nikiwa Mfanyakazi wa Kujifaidi
  • Mwangaza Mdogo wa Maana ya Maisha
  • Kurudi Nyumbani Kulikotamausha
  • Uingereza na Shule ya Drama
  • Kukosa Lengo Kwaanza Kwisha Hatimaye
  • Kurudi Nyumbani Kukiwa na Tofauti
  • “Umekosea Nambari ya Simu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Nilipata Uradhi Katika Kumtumikia Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Nimepata Shangwe Maishani kwa Kufanya Mapenzi ya Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Nilipata Utajiri wa Kweli Katika Australia
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 1/8 kur. 19-23

Sikuwa na Lengo Lakini Nikapata Kusudi Maishani

WAZIA ogofyo langu na hali ya kutostarehe mapema sana asubuhi moja nilipoamshwa bila ya kutazamia na wanaume wawili wenye miili mikubwa waliokuwa wakipekua-pekua chumba cha kulala. Mama yangu alitazama, akiwa amegeuka rangi kuwa mweupe na hoi, bila shaka akiwa ameshtuka. Wanaume hao walikuwa wapelelezi wa polisi.

Mara moja nilijua walichokuwa wakitafuta. Ingawa nilijifanya kuwa sina hofu na mwenye ujasiri, ndani kabisa niliogopa. Nilitambua kwamba juya la polisi lilikuwa likikaribia kunasa genge letu la wevi vijana katika New Jersey, Marekani. Hao wapelelezi wa polisi waliniambia kwa ukali nivae kisha wakanipeleka mbio-mbio hadi kwenye makao makuu ya polisi ili kuhojiwa.

Niliingiaje katika hali hii yenye kuhuzunisha? Mambo yalianza nilipokuwa mchanga. Nilipokuwa katikati ya utineja wangu bado, tayari nilijiona kuwa mwasi mchanga aliye sugu. Wakati wa miaka ya 1960, vijana wengi walilifikiria kuwa jambo la kisasa na la kukubalika na marika kuwa mwasi bila sababu yoyote, na nilikubali kwa moyo wote. Hivyo, nilipokuwa na umri wa miaka 16, nilijipata nikizurura sehemu za kucheza biliadi za ujirani, nikiwa nimefukuzwa shule ya sekondari. Hapo nilijihusisha na genge la vijana ambao walikuwa wakivunja nyumba na kuiba. Baada ya kujiunga nao katika kuiba vitu vidogo-vidogo, nilianza kufurahia ule msisimko na hali ya kutojua litakalotukia nikapata hasa kwamba kila ono la kuiba lilikuwa lenye kusisimua sana.

Basi kikaanza kipindi cha miezi tisa ya kuvunja nyumba bila kukoma. Tukiwa genge, tulikazia fikira zetu hasa kwenye ofisi kubwa-kubwa ambapo viasi vikubwa vya pesa vilikuwa vikiwekwa mara nyingi. Kadiri tulivyozidi kuvunja bila kushikwa, ndivyo tulivyozidi kuwa wajasiri. Hatimaye, tuliamua kufanya unyang’anyi katika tawi la benki ya wilaya.

Kwa mara ya kwanza, mambo yalianza kwenda vibaya. Ingawa tuliweza kuingia katika benki bila magumu yoyote, tulikaa ndani usiku wote wenye kufadhaisha kwa sababu tuliweza kuvunja tu vikabati vya pesa vya keshia. Tatizo zito zaidi lilikuwa kwamba kuvunja kwetu benki kulileta Shirika la Upelelezi la Serikali (FBI) katika hiyo kesi. Huku FBI ikichunguza kesi yetu, haukupita muda mrefu kabla ya sote kushikwa.

Matokeo Yenye Kuhuzunisha ya Kufanya Makosa

Mimi binafsi nilishtakiwa kwa kuvunja nyumba mara 78 na kupata aibu ya kusomwa kwa habari za ndani za kila uvunjaji nyumba kwa sauti kubwa mahakamani. Hili, likiongezwa kwa utangazaji wa uhalifu wetu katika gazeti la habari la kwetu, lilisononesha sana wazazi wangu. Lakini fedheha na aibu niliyokuwa nikiwasababishia haikunihangaisha sana wakati huo. Nilihukumiwa kifungo kirefu katika makao ya serikali ya kurekebishia tabia, jambo ambalo lingemaanisha kubaki kwangu kizuizini hadi nifikishe umri wa miaka 21. Hata hivyo, kwa sehemu kubwa kama tokeo la jitihada za wakili mwenye ustadi, nilihamishwa hadi kwenye shule ya kipekee ya kurekebishia tabia.

Ingawa nilikuwa nimeepuka kufungwa jela, amri ilikuwa kwamba ilikuwa lazima niondolewe kutoka hiyo jumuiya na kutoka kwa washiriki wangu wote wa zamani. Kwa kusudi hili, niliingizwa katika shule ya kibinafsi katika Newark, iliyokuwa ikishughulikia watoto waasi kama mimi. Kwa kuongezea, nilihitajika kuwa na vipindi vya kila juma pamoja na mwanasaikolojia ili kupata msaada wa kiakili. Hali hizi zote zilishughulikiwa na wazazi wangu—kwa gharama kubwa kwao wenyewe.

Jitihada za Kurekebika

Hakuna shaka kwamba kama tokeo la hukumu yetu iliyotangazwa sana, uhariri ulitokea katika gazeti la habari la mji wa kwetu uliokuwa na kichwa, “Kwa Kutotumia Fimbo.” Makala hii ilichambua jinsi genge hilo lilivyopata adhabu isiyo kali. Maelezo ya uhariri huu, kwa mara ya kwanza, yalifikia dhamiri yangu. Kwa hiyo nilikata sehemu hiyo kutoka gazeti hilo la habari nikajiapia kwamba siku moja, kwa njia fulani, nitalipia ule mteseko wote, aibu, na gharama nilizokuwa nimesababishia wazazi wangu.

Niliwaza kwamba njia moja ya kuthibitisha kwa wazazi wangu kwamba ningeweza kubadilika ingekuwa kuhitimu katika shule ya sekondari katika kidato nilichokuwa mwanzoni. Nilianza kujifunza kuliko nilivyopata kujifunza wakati wowote katika maisha yangu. Matokeo yalikuwa kwamba mwishoni mwa mwaka wa shule, wakati, ofisa wangu wa probesheni alipokuwapo, nilienda tena mbele ya hakimu ambaye alinihukumu, uso wake mkali ulibadilika kuwa tabasamu alipoona kwamba nilikuwa nimepata wastani wa B ya daraja la juu kila muhula. Kwa hiyo sasa njia ilikuwa wazi kwangu kurudia shule yangu ya sekondari ya awali, nikahitimu mwaka uliofuata.

Kukosa Kwangu Lengo Kwaendelea

Kufikia sasa ulikuwa mwaka 1966, na ingawa wengi wa wanadarasa wenzangu walienda vitani katika Vietnam, mimi nilienda hadi Chuo cha Concord, West Virginia. Nilipokuwa chuoni nilianza kutumia dawa za kulevya, nikajiingiza katika mikutano ya amani, na mambo mapya kabisa ambayo yalinifanya nitilie shaka maadili ya kidesturi. Nilikuwa nikitafuta kitu fulani, lakini sikujua ni nini. Wakati wa sikukuu za Utoaji-Shukrani ulipofika, badala ya kwenda nyumbani, nilisafiri kusini kwa kuomba lifti kuvuka Blue Ridge Mountains hadi Florida.

Sikuwa nimepata kamwe kusafiri sana hivyo, na nilikuwa na wakati mzuri ajabu kuona mahali pengi papya na tofauti—yaani, hadi Siku ya Utoaji-Shukrani, wakati ambapo niliishia katika gereza la Daytona Beach kwa shtaka la kuzurura. Nilikuwa na aibu sana kuwasiliana na wazazi wangu, lakini wenye mamlaka wa gereza walifanya hivyo. Kwa mara nyingine tena, baba yangu alifanya mipango ya kulipa faini kali sana badala ya kuniacha nitumikie kifungo cha jela.

Sikubaki chuoni baada ya hilo. Badala ya hivyo, nikiwa na mkoba mmoja tu wa nguo na hamu iliyoamshwa upya ya kusafiri, nilianza kusafiri tena, nikiomba lifti bila lengo huku na huko mwambao wa mashariki wa Marekani na kufanya kazi zisizo za kawaida ili kujitegemeza. Mara nyingi wazazi wangu hawakujua nilikokuwa, ingawa mara kwa mara nilikuwa nikiwatembelea. Kwa mshangao wangu sikuzote walionekana kufurahi kuniona, lakini singeweza kutulia.

Sasa kwa kuwa sikuwa chuoni tena, nilipoteza utambulisho wangu wa mwanafunzi, ambao uliniruhusu kutoshiriki katika utumishi wa kijeshi. Daraja langu la kuandikwa jeshini likawa 1-A, na lilikuwa jambo la muda mfupi tu kabla ya kuandikishwa jeshini. Sikupenda wazo la kuwa mwanajeshi na kupoteza uhuru wangu mpya. Kwa hiyo nikaamua kuondoka nchini kwa meli. Wakati huo fursa mpya ya kazi-maisha ilifunguka. Je, hatimaye hili lingeweza kuwa ndilo kusudi kwelikweli la maisha yangu?

Maisha Baharini Nikiwa Mfanyakazi wa Kujifaidi

Rafiki wa zamani wa familia yetu alikuwa nahodha katika meli ya kibiashara ya kitaifa ya Marekani. Aliniambia kuhusu programu iliyoanzishwa hivi majuzi ya mazoezi kwa wahandisi wa baharini. Nilikubaliwa kwa utayari katika programu iliyojaa utendaji ya miaka miwili, ambayo ilikuwa na manufaa mara mbili ya kutoandikwa kazi ya jeshi na mataraja ya digrii ya uhandisi wa baharini. Nilihitimu nikiwa na diploma katika 1969 kisha nikafanya mkataba nikiwa ofisa wa uhandisi wa daraja la tatu kwenye meli yangu ya kwanza katika San Fransisco. Mara moja tulisafiri kuelekea Vietnam tukiwa na mzigo wa silaha. Safari hiyo haikuwa na matukio mengi, kisha nikajiuzulu kutoka meli hiyo tulipofika Singapore.

Katika Singapore nilifanya mkataba na meli ya kamanda iliyokuwa ikiondoka ili kujifaidi. Meli hii ilitumiwa kusafiria pwani ya Vietnam, kutoka Ghuba ya Cam Ranh iliyo kusini hadi Da Nang iliyo kaskazini, karibu na eneo lisilo na majeshi. Hapa milipuko yenye kuvuma ya mabomu yenye kuendelea haikuisha kamwe. Hata hivyo, kifedha njia hii ilikuwa na faida, na kwa hatari ya vita na bahashishi ya hatari ya kushambuliwa wakati wowote tulipokuwa chini ya milipuo ya moja kwa moja, nilijipata nikichuma zaidi ya dola 35,000 kwa mwaka nikiwa mfanyakazi wa kujifaidi wa vita. Licha ya utajiri huu mpya, bado nilihisi nikiwa bila lengo nikijiuliza maana ya maisha ilikuwa nini—nilikuwa nikielekea wapi?

Mwangaza Mdogo wa Maana ya Maisha

Baada ya shambulio moja lenye kuogofya hasa, kutoka kwa adui, Albert, mfanyakazi wangu wa chombo cha kuchemshia maji ya kuendesha mashine, alianza kunieleza jinsi Mungu ataleta amani duniani siku moja karibuni. Nilisikiliza kwa makini habari hii isiyo ya kawaida. Tuliposafiri wakati uliofuata kurudi Singapore, Albert aliniarifu kwamba alikuwa amekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova lakini hakuwa mtendaji tena. Kwa hiyo tukiwa pamoja tulijaribu kutafuta Mashahidi wenyeji katika Singapore. Hakuna mtu aliyeonekana kuweza kutusaidia, lakini usiku tu wa kabla ya sisi kusafiri, Albert alipata gazeti la Mnara wa Mlinzi katika sebule ya hoteli moja. Lilikuwa na anwani iliyopigwa muhuri juu yalo. Hata hivyo hatukuwa na wakati wa kuhakikisha anwani hiyo, kwa kuwa asubuhi iliyofuata tulisafiri kuelekea Sasebo, Japani, ambapo meli ilipangiwa kutiwa gudini kurekebishwa kwa majuma mawili.

Huko wafanyakazi wa meli walipata mishahara yao, na Albert akajiuzulu. Lakini juma moja tu baadaye, nilishangaa kupata telegramu kutoka kwake akiniambia kwamba mkusanyiko wa Mashahidi wa Yehova ulikuwa ufanywe katika Sasebo mwisho-juma uliokuja. Niliamua kwenda nikajionee mkusanyiko huu ulihusu nini.

Siku hiyo—Agosti 8, 1970—itabaki sikuzote akilini mwangu. Nilifika mahali pa mkusanyiko kwa teksi, nikitoka na kuingia miongoni mwa mamia ya Wajapani, wote wakiwa wamevalia kinadhifu mno. Ingawa wengi wao hawangeweza kuongea Kiingereza hata kidogo, ilionekana wote walitaka kunisalimia kwa mkono. Sikuwa nimepata kujionea jambo lolote kama hilo mbeleni, na ingawa sikuelewa neno lolote la programu iliyokuwa kwa lugha ya Kijapani, niliamua kwamba nitakwenda tena siku iliyofuata—ili nione tu ikiwa nitakaribishwa vilevile tena. Ndivyo ilivyokuwa!

Tuliajiri wafanyakazi wapya na juma moja baadaye tulikuwa tumerudi baharini tena, tukisafiri kuelekea Singapore. Jambo la kwanza nililofanya nilipofika lilikuwa kuchukua teksi hadi mahali pa anwani iliyopigwa muhuri kwenye lile gazeti la Mnara wa Mlinzi. Mwanamke mwenye urafiki alitoka nyumbani na kuniuliza ikiwa angeweza kunisaidia. Nilimwonyesha anwani iliyokuwa juu ya Mnara wa Mlinzi, halafu akanialika ndani mara moja. Kisha nikakutana na mume wake nikapata kujua kwamba walikuwa wamishonari kutoka Australia, Norman na Gladys Bellotti. Nilieleza jinsi nilivyopata anwani yao. Walinikaribisha mno na kujibu maswali yangu mengi, kisha nikaondoka nikiwa na mfuko uliojaa fasihi za Biblia. Kwa miezi michache iliyofuata, tukisafiri kuelekea pwani katika Vietnam, nilisoma vingi vya vitabu hivyo, kutia ndani Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele.

Sasa, kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nilipata maana ya kusudi na mwelekezo wa kweli. Katika safari iliyofuata kurudi Singapore, nilijiuzulu kutoka melini.

Kurudi Nyumbani Kulikotamausha

Kwa mara ya kwanza pia, nilitamani kwelikweli kwenda nyumbani. Kwa hiyo majuma machache baadaye, nilifika nyumbani nikiwa na furaha mno, nikitaka kuwaeleza wazazi wangu mambo yote kuhusu Mashahidi wa Yehova. Wao hawakusisimka kama mimi. Hili lilieleweka, kwa kuwa mwenendo wangu haukusaidia. Nilikuwa nimekaa nyumbani kwa majuma machache tu wakati ambapo, kwa mfoko wa hasira, nilizusha vita katika kilabu cha usiku cha mahali hapo. Nilirudia fahamu katika jela.

Kufikia wakati huu nilianza kuamini kwamba hakukuwa na tumaini hakika la kurekebika na kudhibiti hasira yangu yenye jeuri. Labda sikuzote nilikuwa niwe mwasi bila sababu. Sikuhisi kwamba ningeweza kuendelea kukaa nyumbani. Ilikuwa lazima niende. Kwa hiyo baada ya siku chache, nilipanda meli ya mizigo ya Norway iliyokuwa ikielekea Uingereza.

Uingereza na Shule ya Drama

Nilifurahia kuwa Uingereza, lakini ilikuwa vigumu kupata kazi. Kwa hiyo nikaamua kufanya majaribio katika shule kadhaa za drama, na kwa mshangao wangu nilikubaliwa kwenye Shule ya London ya Sanaa ya Drama. Nilitumia miaka miwili katika jiji la London kunywa kupindukia, kufanya marafiki, na bila shaka, kutumia dawa za kulevya za kila aina.

Niliamua ghafula kwamba nilitaka kutembelea tena familia yangu huko Marekani. Waweza kuwazia jinsi sura yangu yenye kutazamisha ilivyowashangaza wakati huu? Nilivalia joho jeusi lenye vichwa viwili vya kidhahabu vya simba vilivyounganishwa na nyororo kwenye shingo, kisibau chekundu cha mahameli, na suruali ndefu nyeusi ya mahameli iliyotariziwa kwa ngozi na kuingizwa ndani ya viatu vifikavyo magotini. Halikuwa jambo la kushangaza kwamba wazazi wangu kwa wazi hawakufurahishwa na kwamba nilihisi nisiyefaa mazingira hayo ya kidesturi kabisa! Kwa hiyo nilirudi Uingereza, ambapo katika mwaka 1972 nilipata diploma katika sanaa ya drama. Sasa nilikuwa nimetimiza lengo jingine. Lakini bado swali lile lenye kusumbua, na kurudi-rudi lilikuwako, Niende wapi kutoka hapa? Bado nilihisi uhitaji wa kusudi la kweli katika maisha.

Kukosa Lengo Kwaanza Kwisha Hatimaye

Si muda mrefu baada ya hili, hatimaye nilianza kuhisi uthabiti fulani ukija maishani mwangu. Ulianza na urafiki na jirani yangu Caroline. Yeye alikuwa mwalimu kutoka Australia na alikuwa mtu wa kidesturi, mwenye uthabiti—kinyume tu cha utu wangu. Tulikuwa tumekuwa marafiki kwa miaka miwili bila ya uhusiano wowote wa kimahaba. Kisha Caroline akaondoka akielekea Marekani kwa miezi mitatu, na kwa sababu ya urafiki wetu mzuri, nilipanga akae na wazazi wangu kwa majuma kadhaa. Yaelekea walishangaa angekuwa na nini la kufanya na mtu kama mimi.

Mara tu baada ya Caroline kuondoka, niliwaambia rafiki zangu kwamba mimi pia nilikuwa naenda nyumbani, nao wakaniaga kwa karamu kubwa sana. Lakini badala ya kurudi Marekani, nilienda hadi South Kensington, London, ambapo nilikodi chumba na kupiga simu kwa ofisi ya Mashahidi wa Yehova katika London. Nilikuja kutambua ni mwendo upi maisha yangu yalipasa kuchukua. Kabla ya juma moja kupita mume na mke wenye furaha walinitembelea na mara moja wakapanga funzo la kawaida la Biblia pamoja nami. Kwa sababu ya vichapo vya Mashahidi ambavyo nilikuwa nimesoma tayari, sasa nilikuwa na hamu kujifunza nikaomba kujifunza mara mbili kwa juma. Akiona idili yangu, baada ya muda mfupi Bob alinialika kwenye Jumba la Ufalme, na muda si muda nilikuwa nikihudhuria mikutano yote ya juma.

Nilipopata kujua kwamba Mashahidi wa Yehova hawavuti sigareti, niliamua kuacha zoea hilo mara moja. Lakini namna gani sura yangu? Sikutaka kuwa mwenye kuvuta uangalifu wa watu tena, kwa hiyo nikanunua shati, tai, na suti. Baada ya muda mfupi nikastahili kushiriki katika utendaji wa kuhubiri nyumba kwa nyumba—na ingawa kwa mara ya kwanza nilikuwa mwenye woga sana, nilikuja kuufurahia.

Jambo la kushangaza lilimngojea Caroline aliporudi, nikawazia. Mambo yalikuwa zaidi ya hilo! Yeye hakuweza kuamini jinsi nilivyokuwa nimebadilika kwa kipindi kifupi sana hivyo—katika kujipamba kwangu na sura na katika njia nyinginezo nyingi sana. Nilieleza jinsi kujifunza kwangu Biblia kulikuwa kumenisaidia kisha nikamwalika yeye pia ajifunze Biblia. Akiwa mwenye shaka mwanzoni, yeye alikubali hatimaye, akiweka masharti kwamba angejifunza nami tu. Nilifurahi kuona jinsi alivyoitikia kwa upesi, na baada ya muda mfupi akaanza kung’amua umaana wa kweli ya Biblia.

Baada ya miezi michache, Caroline aliamua kurudi Australia, halafu akaendelea na funzo lake la Biblia katika Sydney. Nilibaki London hadi nilipoweza kubatizwa, jambo ambalo lilifanyika miezi saba baadaye. Sasa nilitaka kurudi nyumbani Marekani tena ili kuona familia yangu yote. Lakini wakati huu niliazimia kufikia mradi wangu!

Kurudi Nyumbani Kukiwa na Tofauti

Wazazi wangu waliopatwa na mshangao mkubwa walitaka kujua nini kilikuwa kikinipata—nilionekana mwenye heshima zaidi! Lakini nilifurahi sasa kuhisi nikiwa nyumbani kikweli. Ingawa wazazi wangu kwa kawaida walishangaa kuhusu badiliko langu lenye kutazamisha, walikuwa wenye busara na waliitikia kwa fadhili na uvumilivu wao wa kawaida. Kwa miezi iliyofuata, nilikuwa na pendeleo la kushiriki funzo la Biblia pamoja nao. Nilianza funzo la Biblia pamoja na dada zangu wawili wakubwa, ambao bila shaka walikuwa wamevutiwa na badiliko la mtindo-maisha wangu. Kwa kweli, huku kulikuwa kurudi nyumbani kikweli!

Katika Agosti 1973, nilimfuata Caroline Australia, ambapo nilifurahi kumwona akibatizwa kwenye mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova wa mwaka huo pamoja na wengine 1,200. Tulioana mwisho-juma uliofuata katika Canberra, jiji kuu la kitaifa la Australia. Hapa nimetumika katika kazi ya wakati wote ya kuhubiri kwa miaka 20 ambayo imepita na nikiwa mzee katika kutaniko la huko kwa miaka 14.

Kwa sababu ya ushirikiano wa mke wangu, tumelea watoto watatu—Toby, Amber, na Jonathan. Ingawa sisi hukabili matatizo ya kawaida ya familia, bado naweza kushiriki katika utendaji wa kuhubiri wakati wote nikiwa painia na kwa wakati huohuo nikitunza mahitaji ya kimwili ya familia yetu.

Leo, huko Marekani, wazazi wangu ni watumishi waliojiweka wakfu kwa Yehova, na ingawa wote wako katika miaka yao ya 80 bado wanashiriki katika kuhubiri Ufalme hadharani. Baba yangu anatumikia akiwa mtumishi wa huduma katika kutaniko la kwao. Dada zangu wawili wakubwa pia wana bidii kwa utumishi wa Yehova.

Jinsi ninavyomshukuru Yehova Mungu kwa kina kwamba miaka yangu mingi ya kuzunguka-zunguka bila lengo sasa imepita kabisa! Amenisaidia si kujifunza njia bora zaidi ya kutumia maisha yangu tu bali amenibariki pia kuwa na familia iliyounganika na yenye kujali.—Kama ilivyosimuliwa na David Zug Partrick.

[Picha katika ukurasa wa 23]

David na mke wake, Caroline

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki