Nilipata Utajiri wa Kweli Katika Australia
ILIKUWA Aprili 1971. Baada ya kukaa miaka saba katika Australia, nilikuwa hivi majuzi nimerudi Ugiriki kuzuru familia yangu. Ilikuwa jioni, nami nilikuwa nimeketi kwa utulivu kwenye meza ya mkahawa katika uwanja wa kijiji cha Karies wakati ambapo padri na meya wa hapo walikuja na kuketi wakinikabili. Ni wazi kwamba walikuwa wakitaka sana kuanza kugombana nami.
Bila hata kunisalimu vizuri, yule padri akadai kwamba mimi nilikuwa nimehamia Australia kwa kusudi la kuchuma fedha tu. Nilishangaa sana. Nikajibu kwa utulivu kadiri ilivyowezekana kwamba kwa muda ambao nilikuwa nikiishi katika Australia, niliweza kujipatia utajiri wenye thamani kubwa kuliko fedha.
Jibu langu lilimshangaza, lakini ndipo yeye akataka kujua nilimaanisha nini hasa. Nikajibu kwamba kati ya mambo mengine, nilikuwa nimejifunza kwamba Mungu ana jina. “Na hili ni jambo ambalo wewe hukujali kunifundisha,” nikasema, nikimtazama macho kwa macho. Kabla hajaweza kujibu, nikauliza, “Je! waweza kuniambia tafadhali jina la Mungu ambalo Yesu alirejezea alipotufundisha kusali hivi katika ile sala ya kiolezo: ‘Jina lako litukuzwe’?”—Mathayo 6:9.
Habari kuhusu bishano hilo ilienea upesi katika uwanja wa kijiji, na katika muda wa dakika kumi watu wapatao 200 wakawa wamekusanyika. Yule padri alianza kuhisi akikosa starehe. Hakutaka kujibu swali langu juu ya jina la Mungu, na alitoa majibu manyonge kwa maswali zaidi ya Biblia. Aibu yake ilionekana kwa kuitaita mtumishi wa mkahawa amwongezee ouzo, kileo cha Kigiriki.
Saa mbili za kupendeza zikapita. Baba yangu alikuja akinitafuta, lakini alipoona lililokuwa likiendelea akaketi kwa utulivu katika kona moja na kutazama ile tamasha. Yale mazungumzo machangamfu yaliendelea mpaka saa 5:30 ya usiku, wakati ambapo mwanamume aliyelewa alianza kupiga kelele kwa hasira. Hapo mimi nikadokezea ule umati kwamba kwa sababu saa zilikuwa zimesonga sana, twapaswa sote kwenda nyumbani.
Ni nini kilichokuwa kimesababisha kabiliano hili? Kwa nini yule padri na yule meya walijaribu kutafuta ugomvi nami? Maelezo machache juu ya malezi yangu katika sehemu hii ya Ugiriki yatakusaidia kuelewa.
Magumu ya Mapema
Nilizaliwa katika kijiji cha Karies katika Peloponnisos, katika Desemba 1940. Sisi tulikuwa maskini wa kupindukia, na nilipokuwa sihudhurii shule, nilikuwa nikifanya kazi pamoja na mama kuanzia macheo hadi machweo katika mashamba ya mpunga, tukisimama katika maji yenye kutufika magotini. Nilipomaliza shule ya msingi nikiwa na umri wa miaka 13, wazazi wangu walinipangia nifanye kazi nikiwa mwanagenzi (mfunzwa-kazi). Ili nipokee mazoezi nikiwa fundi wa mabomba na mweka-madirisha, wazazi wangu walimpa mwajiri wangu kilo 500 za ngano na kilo 20 za mafuta ya mboga, zilizokuwa ni kama mapato yao yote kwa mwaka.
Maisha nikiwa mwanagenzi—mwenye kuishi kilometa nyingi kutoka nyumbani na mara nyingi nikifanya kazi kutoka mapambazuko hadi usiku-kati—hayakuwa rahisi hata kidogo. Nyakati fulani nilifikiria kurudi nyumbani, lakini singeweza kuwatenda hivyo wazazi wangu. Wao walikuwa wamejidhabihu sana bila ubinafsi kwa ajili yangu. Kwa hiyo sikuwajulisha kamwe matatizo yangu. Nilijiambia hivi: ‘Ni lazima uvumilie, hata mambo yakiwa magumu kadiri gani.’
Muda wa miaka hiyo, niliweza kuwazuru wazazi wangu mara kwa mara, na hatimaye nikamaliza uanagenzi wangu nilipokuwa na miaka 18. Halafu nikaamua kwenda Athens, jiji kuu, ambako matazamio ya kazi yalikuwa makubwa zaidi. Huko nikapata kazi ya kuajiriwa na kukodi chumba. Kila siku baada ya kazi, nilirudi nyumbani, nikajipikia, nikasafisha chumba, halafu ule wakati mchache sana ambao sikuwa na shughuli nikautumia kujifunza Kiingereza, Kijerumani, na Kiitalia.
Maongezi na mwenendo usio wa adili wa vijana wengine ulinisumbua, kwa hiyo niliepuka ushirika wao. Lakini hii ilisababisha nihisi nikiwa mpweke sana. Nilipofika umri wa miaka 21, nilitakwa nifanye utumishi wa kijeshi, na wakati huo nikaendelea na funzo langu la lugha mbalimbali. Halafu, katika Machi 1964, baada ya mimi kuondoka jeshini, nilihamia Australia, nikalowea Melbourne.
Utafutaji wa Kidini Katika Bara Jipya
Upesi nilipata kazi, nikakutana na mhamiaji mwingine Mgiriki, jina lake Alexandra, na katika muda wa miezi sita baada ya kuwasili kwangu, tukafunga ndoa. Miaka kadhaa baadaye, katika 1969, mama mmoja mzee-mzee, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alitembelea nyumbani kwetu na kututolea Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Niliyaona magazeti hayo kuwa ya kupendeza, kwa hiyo nikayaweka mahali salama, nikimwagiza mke wangu asiyatupilie mbali. Mwaka mmoja baadaye Mashahidi wengine wawili walitembea na kunitolea funzo la Biblia nyumbani bila malipo. Nilikubali, na kile nilichojifunza kutokana na Maandiko ndicho kile hasa nilichokuwa nimekuwa nikitafuta ili kuujaza utupu uliokuwa umekuwa katika maisha yangu.
Mara tu mwanamke jirani yangu alipogundua kwamba nilikuwa nikijifunza na Mashahidi, alinielekeza kwa Waevanjelisti, akidai kwamba wao walikuwa dini nzuri zaidi. Tokeo ni kwamba, nilianza kujifunza na mzee mmoja kutoka Kanisa la Waevanjelisti pia. Upesi nikaanza kuhudhuria mikutano ya Waevanjelisti na pia ya Mashahidi, kwa maana nilikuwa nimeazimia kuipata dini ya kweli.
Wakati uohuo, nilianza kuichunguza sana dini ya Orthodoksi ili nitimize wajibu wangu wa malezi ya Kigiriki. Siku moja nilienda kwenye makanisa matatu ya Orthodoksi ya Kigiriki. Nilipoeleza kusudi la ziara yangu kwenye lile la kwanza, padri alinielekeza polepole mlangoni ili niende zangu. Alipokuwa akifanya hivyo, alieleza kwamba sisi ni Wagiriki, na kwa hiyo lilikuwa kosa kushirikiana ama na Mashahidi ama na Waevanjelisti.
Mtazamo wake ulinishangaza, lakini nilifikiri hivi: ‘Labda padri huyu hususa si mwakilishi mwema wa kanisa.’ Nikashangaa kuona padri kwenye kanisa la pili akitenda vivyohivyo. Hata hivyo, yeye aliniambia kwamba kila jioni ya Jumamosi darasa la funzo la Biblia liliongozwa na mwanatheolojia kwenye kanisa lake. Nilipojaribu kanisa la tatu, nilizidi kuzinduka.
Hata hivyo, niliamua kuhudhuria darasa la funzo la Biblia lililoendeshwa kwenye lile kanisa la pili, nikazuru huko Jumamosi iliyofuata. Nilifurahia kufuatana na usomaji kutoka katika kitabu cha Biblia cha Matendo. Kile kisehemu kihusucho Kornelio akipiga magoti mbele ya Petro kiliposomwa, yule mwanatheolojia alikatiza usomaji na kuonyesha kwamba Petro alikuwa amefanya ifaavyo kwa kulikataa tendo la ibada la Kornelio. (Matendo 10:24-26) Hapo basi nikainua mkono wangu nikasema kwamba nilikuwa na swali.
“Naam, ni nini utakalo kujua?”
“Sasa, ikiwa mtume Petro alikataa kuabudiwa, mbona tuna sanamu yake nasi huiabudu?”
Kwa sekunde kadhaa kukawa na kimya-a-a. Halafu ikawa kama kwamba kombora lilikuwa limeangushwa. Hasira ziliwaka, na mayowe yakapigwa, “Katoka wapi wewe?” Kwa muda wa saa mbili kulikuwa na majadiliano motomoto, kukiwa na makelele mengi. Mwisho, nilipokuwa nikiondoka, nikapokezwa kitabu niende nacho nyumbani.
Nilipokifungua, maneno ya kwanza niliyoyasoma yalikuwa: “Sisi ni Wagiriki, na dini yetu imemwaga damu ili kuhifadhi pokeo letu.” Mimi nilijua kwamba Mungu si wa Wagiriki peke yao, kwa hiyo nikakata mahusiano yangu na Kanisa la Orthodoksi la Kigiriki. Tangu hapo nikaendelea na funzo langu la Biblia pamoja na Mashahidi peke yao. Katika Aprili 1970, nilionyesha wakfu wangu kwa Yehova kwa ubatizo wa maji, na mke wangu akabatizwa miezi sita baadaye.
Kuonana na Padri wa Kijiji
Kuelekea mwisho wa mwaka huo, padri wa kutoka kijiji cha nyumbani kwangu katika Ugiriki alipeleka barua akiomba fedha za kusaidia kurekebisha kanisa la kijiji. Badala ya kupeleka fedha, nilimpelekea kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele, pamoja na barua ya kueleza kwamba sasa nilikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova na kwamba niliamini nilikuwa nimeipata kweli. Alipopokea barua yangu, alitangaza kanisani kwamba mtu fulani aliyehamia Australia alikuwa ameasi.
Baada ya hapo, akina mama waliokuwa na wana katika Australia wakafuliza kumwuliza padri kama mwana wao ndiye aliyefanya hivyo. Mama yangu hata alienda kwenye nyumba yake na kumsihi sana amwambie. “Kwa kusikitisha, ni mwana wako,” yeye akasema. Baadaye mama aliniambia kwamba angalipendelea padri huyo amwue kuliko kumwambia jambo hili juu yangu.
Kurudi Ugiriki
Baada ya ubatizo wetu, mke wangu na mimi tulitaka kurudi Ugiriki tukaambie familia na rafiki zetu mambo mema tuliyokuwa tumejifunza kutokana na Biblia. Kwa hiyo katika Aprili 1971, tukiandamana na binti yetu mwenye umri wa miaka mitano, Dimitria, tukarudi kwa likizo refu, tukikaa katika mji wa Kiparissia, karibu kilometa 30 kutoka kwenye kijiji cha nyumbani kwangu cha Karies. Tikiti za safari yetu ya ndege za kwenda na kurudi zilikuwa na uhalali wa kutuwezesha kukaa kwa miezi sita.
Katika usiku wa pili wa kuwa nyumbani, mama alizidiwa hisia akatoa machozi na kuniambia kwamba nilikuwa nimefuata mwendo wenye makosa na kuaibisha jina la familia. Huku akilia na kufanya sauti za kwikwi, alinisihi sana niache mwendo wangu “wenye makosa.” Halafu akazimia na kuanguka mikononi mwangu. Siku iliyofuata nilijaribu kusababu naye, nikieleza kwamba nilikuwa tu nimeongezea ujuzi wangu juu ya Mungu yule ambaye yeye alikuwa ametufundisha kwa upendo sana juu yake kuanzia utoto mchanga. Jioni iliyofuata ndipo nikawa na lile kabiliano maarufu na padri wa kwetu na meya wa kijiji.
Ndugu zangu wawili wachanga zaidi, walioishi Athens, walikuwa wamekuja kukaa kwa ajili ya Ista. Wote wawili waliniepuka kama kwamba nilikuwa mwenye ukoma. Hata hivyo, siku moja yule mwenye umri mkubwa zaidi kati ya hao wawili alianza kusikiliza. Baada ya saa kadhaa za mazungumzo, alisema kwamba alikubaliana na kila kitu nilichokuwa nimemwonyesha kutokana na Biblia. Kuanzia siku hiyo na kuendelea, alinitetea mbele ya washiriki wale wengine wa familia.
Baada ya hapo nilizuru Athens mara nyingi kukaa na ndugu yangu. Kila wakati nilipofanya hivyo, yeye alialika familia nyinginezo zije zisikie habari njema. Nilipata shangwe kubwa wakati yeye na mke wake, pamoja na familia nyingine tatu walizoongoza mafunzo ya Biblia pamoja nazo, zilipoonyesha wakfu wazo kwa Mungu kwa kubatizwa katika maji!
Majuma yalipita upesi, na kabla tu ya miezi yetu sita kumalizika, Shahidi mwenye kutumikia katika kutaniko moja karibu kilometa 70 kutoka kwenye kijiji chetu alizuru. Alionyesha msaada uliohitajiwa kuhusu kazi ya kuhubiri katika lile eneo na kuuliza kama mimi nilikuwa nimefikiria kukaa huko daima. Usiku huo nilizungumza na mke wangu juu ya uwezekano huo.
Sote wawili tulikubaliana kwamba ingekuwa vigumu kukaa. Lakini ilikuwa wazi kwamba kulikuwa na uhitaji mkubwa wa watu kusikia kweli ya Biblia. Mwishowe, tukaamua angalau tukae huko muda wa mwaka mmoja au miwili. Mke wangu angerudi Australia kuuza nyumba na gari letu na kurudisha mali zile ambazo angeweza. Tulipokwisha kufanya uamuzi wetu, tulienda mjini asubuhi iliyofuata tukakodi nyumba. Pia tuliingiza binti yetu katika shule ya msingi ya hapo.
Upinzani Walipuka
Upesi ikawa ni kama vita halisi imetangazwa juu yetu. Upinzani ulikuja kutoka kwa polisi, mkuu wa shule, na walimu. Dimitria alikuwa akikataa kufanya ishara ya msalaba shuleni. Maofisa wa shule waliita polisi ajaribu kumwogopesha kukubali, lakini yeye akasimama imara. Mimi nikaitwa kumwona mkuu wa shule, naye akanionyesha barua moja iliyotoka kwa askofu mkuu iliyoagiza kwamba nimchukue Dimitria na kuondoka. Hata hivyo, baada ya kufanya mazungumzo marefu na huyo mkuu wa shule, aliruhusiwa kubaki shuleni.
Baada ya muda nikapata kujua kwamba kulikuwako wenzi wa ndoa katika Kiparissia waliokuwa wamehudhuria kusanyiko la Mashahidi wa Yehova, nasi tukaweza kuwafanya wapendezwe upya. Mke wangu na mimi tulialika pia Mashahidi kutoka kijiji cha karibu kwenye mafunzo yetu ya Biblia nyumbani. Hata hivyo, muda mfupi baada ya hapo polisi walikuja wakatupeleka sote kwenye kituo cha polisi kuhojiwa. Mimi nilishtakiwa kutumia nyumba yangu kama mahali pa ibada bila leseni. Lakini kwa kuwa hatukufungwa gerezani, tuliendelea na mikutano yetu.
Ingawa nilipewa kazi, mara tu askofu alipopata habari, alitisha kuagiza duka la mwajiri wangu lifungwe asiponiondoa kazini. Duka fulani la ufundi wa mabomba na mabati ya kuezeka lilikuwa likiuzwa, nasi tukaweza kulinunua. Mara tu mapadri wawili wakaja na vitisho kutufungia kazi, na majuma machache baadaye yule askofu mkuu akaagiza kwamba familia yetu iondoshwe katika ushirika. Mtu yeyote aliyeondoshwa katika ushirika wa Kanisa la Orthodoksi la Kigiriki wakati huo alitendewa kama mkataliwa-na-jumuiya kabisa. Ofisa wa polisi aliwekwa awe akikaa nje ya duka letu kuzuia mtu yeyote asiingie. Hata ingawa hakukuwa na wanunuzi, sisi tulikaza shingo tukafungua duka kila siku. Upesi muhali wetu ukawa ndio maongezi ya mji.
Twakamatwa na Kufanyiwa Kesi
Jumamosi moja mtu mwingine na mimi tulifunga safari katika pikipiki yake tukatoe ushahidi katika mji wa karibu. Huko polisi wakatusimamisha na kutupeleka kwenye kituo cha polisi, ambako tulizuiliwa mwisho-juma wote. Asubuhi ya Jumatatu tulirudishwa Kiparissia kwa gari-moshi. Habari za kwamba tulikuwa tumekamatwa zikaenea, na umati ukakusanyika kwenye kituo cha reli kutuona tukiwasili pamoja na wasindikizi wetu polisi.
Baada ya kuchukuliwa alama za vidole, tulipelekwa kwa mshitaki wa serikali. Alianza hatua za kesi kwa kusema kwamba angeyasoma kwa sauti kubwa mashtaka yaliyokuwa yamekusanywa dhidi yetu kutoka kwa wanakijiji waliokuwa wamehojiwa na polisi. “Wao walituambia kwamba Yesu Kristo alikuwa amekuwa Mfalme katika mwaka 1914,” likawa ndilo shtaka la kwanza kusemwa.
“Mlitoa wapi wazo hili la kiajabu?” mshitaki akauliza kwa ugomvi.
Mimi nikapiga hatua mbele na kuichukua Biblia aliyokuwa nayo juu ya dawati lake nikaifungua kwenye Mathayo sura ya 24 na kudokeza kwamba aisome. Alisita kwa muda lakini akaichukua Biblia na kuanza kusoma. Baada ya kusoma kwa dakika chache, alisema hivi kwa kusisimka: “Lo, ikiwa hii ni kweli, basi napaswa kuacha mambo yote nijiunge na makao ya watawa!”
“La,” nikasema kwa utulivu. “Wapaswa kujifunza kweli ya Biblia halafu usaidie wengine kuipata kweli pia.”
Wanasheria wachache waliwasili, nasi tukaweza kuwapa ushahidi baadhi yao pia wakati wa mchana. Ajabu ni kwamba hii ilitokeza shtaka jingine—kugeuza msimamo wa watu!
Wakati wa mwaka huo, tulikuwa na kesi tatu mahakamani, lakini mwishowe tukaondolewa mashtaka yote. Ushindi huo ulionekana kuvunja ule ubaridi uliokuwa katika mtazamo wa watu kutuelekea. Kuanzia wakati huo na kuendelea wakaanza kutufikia kwa uhuru zaidi na kusikiliza tuliyokuwa tukisema juu ya Ufalme wa Mungu.
Hatimaye kile kikundi kidogo cha funzo nyumbani mwetu katika Kiparissia kikafanyizwa kuwa kutaniko. Mzee Mkristo alihamishwa kuletwa kwenye kutaniko letu jipya, nami nikawekwa kuwa mtumishi wa huduma. Punde si punde mikutano katika nyumba yetu ikawa ikihudhuriwa kwa ukawaida na Mashahidi watendaji 15.
Kurudi Australia
Baada ya miaka miwili na miezi mitatu kupita, tuliamua kurudi Australia. Miaka hapa imepita upesi. Binti yangu Dimitria amedumisha imani yake na ameolewa na mtumishi wa huduma katika kutaniko moja la Melbourne. Mimi sasa ninatumikia nikiwa mzee katika kutaniko moja la lugha ya Kigiriki katika Melbourne, ambako mke wangu na mimi na binti yetu mwenye umri wa miaka 15, Martha, huhudhuria.
Lile kutaniko dogo tuliloacha katika Kiparissia sasa limekua likawa kubwa zaidi, na watu wengi wa huko wenye kustahili wamefungua mioyo yao kwenye kweli za Biblia. Wakati wa kiangazi cha 1991, nilizuru Ugiriki kwa majuma machache na kutoa hotuba ya Biblia ya watu wote katika Kiparissia, na watu 70 walihudhuria. Jambo la kufurahisha ni kwamba dada yangu mwenye umri mdogo zaidi Maria amekuwa mtumishi wa Yehova kujapokuwa na upinzani wa familia.
Mimi nashukuru kwamba katika Australia nimekuwa na fursa ya kupata utajiri wa kweli—ujuzi na uelewevu juu ya Muumba wetu, Yehova Mungu, na juu ya serikali yake ya Ufalme. Maisha yangu sasa yana kusudi halisi, na familia yangu na mimi twaungojea wakati ujao ulio karibu tuzione baraka za serikali ya kimbingu ya Mungu zikitandaa juu ya dunia nzima.—Kama ilivyosimuliwa na George Katsikaronis.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kiparissia, nilikoishi baada ya kurudi kutoka Australia
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nikiwa na mke wangu, Alexandra