Uwanja wa Ndege wa “Kanku”—Huonekana Lakini Hausikiki
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAPANI
UKIKARIBIA Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kansai kutoka hewani, utaona kisiwa chenye maandishi “Kansai” katika Kiingereza.a Kisiwa hiki cha Japani kiko kilometa zipatazo tano kutoka pwani katika Ghuba ya Osaka. Hakuna kitu kingine kiwezacho kuonwa isipokuwa huo uwanja wa ndege na majengo yao. Kwa hakika, hicho kisiwa kilitengenezwa kwa ajili ya kuwa uwanja wa ndege. Kikifunguliwa katika Septemba 1994, uwanja huo wa ndege umepewa jina la lakabu, Kanku, kifupi cha jina lao la Kijapani, Kansai Kokusai Kuko.
Daraja la barabara kuu, lenye urefu wa kilometa 3.75, huunganisha uwanja huo wa ndege wa kisiwa na bara, ikifanya uweze kufikiwa kwa barabara na reli. Hicho kisiwa kina vifaa vya bandari kwa ajili ya huduma za meli na feri. Lakini kwa nini kujenga kisiwa kizima kipya kwa ajili ya uwanja wa ndege?
Uwanja wa Ndege Usiosikika
Idadi inayoongezeka ya watalii na wageni kwa eneo la Kansai ilisababisha kuongezeka kwa idadi ya ndege zenye kuvuma juu ya eneo la ukazi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Osaka. Ili kuwaondolea kelele watu wanaoishi hapo, kafiu kutoka saa 3:00 usiku hadi saa 1:00 asubuhi iliwekwa. Hakuna ruhusa imetolewa ya kuongeza safari za ndege za kimataifa tangu 1974. Hivyo, uwanja wa ndege wa kushughulikia wasafiri na mizigo yenye kuongezeka bila kusikiwa barani ukawa uhitaji muhimu.
Uwanja wa ndege ambao ungeweza kutumiwa mchana na usiku bila kusababisha udhiko—hilo lilikuwa tatizo kubwa kwa wale waliohusika katika huo mradi. Suluhisho pekee lililojitokeza lilikuwa kujenga kisiwa mbali na mahali wanapoishi watu na kukifanya kuwa uwanja wa ndege. Mradi mkubwa kwelikweli!
Serikali ya kitaifa na za kimtaa pamoja na wafanyabiashara wa mahali hapo waligharimia huo mradi wa dola bilioni 15, kukianzishwa kampuni ya kibinafsi kujenga na kuendesha uwanja huo mpya. Bw. Keisuke Kimura, naibu msimamizi wa Kampuni ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kansai, aliambia Amkeni! hivi: “Tukiwa kampuni ya kibinafsi, hatungeweza kutumia wakati mwingi katika kufanyiza hicho kisiwa. Ilibidi kazi hiyo ifanywe haraka.”
“Kufanyiza Kisiwa”
Ni vigumu kupata bara kandokando ya pwani, lakini ni vigumu hata zaidi kufanyiza kisiwa kilometa tano kutoka pwani. Ili kufanyiza huo uwanja wa ndege wa hektari 511, mchanga na udongo meta za kyubiki 180,000,000 zilitumiwa kuijaza bahari. “Hiyo yatoshana na piramidi 73—namaanisha kubwa kuliko zote zilizotengenezwa na Mfalme Khufu,” aeleza Bw. Kimura.
Kwenye sakafu ya bahari, kwa wastani wa kina cha meta 18, ulikuwa utando wa udongo laini ambao kutoka kwao maji yalipasa kutolewa. “Miimo milioni moja ya mchanga, yenye kipenyo cha sentimeta 40, iliingizwa katika utando huo ili kuvuta maji kutoka kwao na kuimarisha msingi. Kwa uzito wa mchanga huo, maji yalikamuliwa kutoka utando wa mchanga laini wenye meta 20, ukiukunjamanisha hadi meta 14,” aeleza Bw. Kenichiro Minami, ambaye alisimamia mradi wa kujaza bahari mchanga. “Tulichohofia zaidi kilikuwa kutulia kusiko sawia kwa udongo wa chini. Tulitumia kompyuta ili kukadiria barabara mahali ambapo pangejazwa mchanga ili kutulia kwa udongo kuwe sawia.”
Kwa ujumla, kina cha mchanga kilifika meta 33, sawa na jengo la orofa kumi. Hata hivyo, chini ya uzito wa mchanga, sakafu ya bahari imezama na yaendelea kuzama. Inakadiriwa kwamba sakafu ya bahari itazama meta 1.5 zaidi katika miaka 50, ikiacha hicho kisiwa kikiwa meta nne juu ya usawa wa bahari.
Katika 1991, hata kabla ya kisiwa chote kumalizika kufanyizwa, kazi katika jengo la mahali wanakoshukia abiria na mnara wa kudhibitia ndege ilikuwa imeanzwa. Baada ya zaidi ya miaka saba ya kazi ngumu, ujenzi wa hicho kisiwa, uwanja wa ndege, na majengo yanayohusiana nao ulikuwa umemalizika.
Kubwa Lakini Lililoshikamana
Abiria wanaofika hushangaa mno. “Kufikia wakati tulifika katika eneo la kuchukua mizigo, masanduku yetu yalikuwa yamefika,” asema msafiri mmoja kutoka Marekani. Ni nini hutokeza utaratibu huo mwepesi? “Jengo la kushukia abiria ni kubwa lakini limeshikamana,” asema Bw. Kazuhito Arao, ambaye husimamia jengo la kushukia abiria. “Abiria hawahitaji kuzunguka-zunguka kwenye vipitio vingi, ambavyo ni kawaida ya nyanja za ndege za kimataifa.”
Muundo wa jengo la kushukia abiria ni sahili lakini wa kipekee. Jengo kuu limeundwa ili kusaidia abiria kutokana na kutembea kusiko kwa lazima. Abiria wa safari za nchini wanaweza kutoka kwenye stesheni ya gari-moshi moja kwa moja hadi kwenye mahali pa kuonyeshea tikiti na kisha kuelekea kwenye lango la kuingilia ndege bila kupanda na kushuka ngazi zozote.
Kutoka jengo kuu, ambapo kuna mahali pa kuonyesha tikiti, ofisi za idara ya uhamiaji, na forodha, majengo ya nyongeza ya meta 700 huelekea kaskazini na kusini, yakiongoza hadi kwenye malango 33 ya kuingilia ndege. Abiria wanaotumia malango yaliyo mbali na jengo kuu wanaweza kuchukua mfumo wenye kujiendesha wa uchukuzi, uitwao Kichukuzi cha Majengo ya Nyongeza. Hicho huchukua abiria hadi kwenye lango wanalotaka kwa muda wa dakika tano—kutia ndani wakati uliotumiwa kungojea hicho kichukuzi.
Uwanja wa Ndege wa Kuonwa
“Ukiwa uwanja wa ndege ulio baharini kabisa, hauna vizuizi vyovyote,” asema Bw. Arao. “Ndiyo, sisi husikia kwamba marubani husema ni uwanja wa ndege ulio rahisi kutua juu yao,” akubali Bw. Kimura.
Wengine pia huthamini sura ya huo. Muundo tata wa jengo la kushukia abiria lenye umbo la mabawa ya ndege umevutia watalii wengi kuelekea Kanku. Wao pia hufurahia kutazama ndege zikiondoka na kutua kwenye uwanja wa ndege wa kisiwa usio wa kawaida. “Tulilazimika kujenga mahali pa utazamaji juu ya mahali pa udumishaji kwa ajili ya wale wanaozuru uwanja huo, ingawa hatukunuia kufanya hivyo mwanzoni,” asema Bw. Kimura. Wastani wa watu 30,000 kwa siku huzuru uwanja huo ili kuutazama.
Ukizuru Japani karibu na eneo la Kansai, kwa nini usiende kwa ndege kuingia au kutoka Kanku—uwanja wa ndege ambao waweza kuonwa lakini usiosikiwa na majirani wao.
[Maelezo ya Chini]
a Kansai ni eneo la jumla magharibi mwa Japani ambalo hutia ndani majiji ya kibiashara ya Osaka na Kobe na majiji ya kihistoria ya Kyoto na Nara. Kukosai kuko “humaanisha uwanja wa ndege wa kimataifa.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Kansai International Airport Co., Ltd.