Kutoka Kisiwa Kidogo Hadi Kuwa Uwanja wa Ndege Wenye Shughuli Nyingi
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Hong Kong
“LAZIMA tuwe tunagonga antena za televisheni zilizo juu ya paa!” akasema kwa mshangao abiria aliyeshtuka alipotazama nje ya dirisha la ndege ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hong Kong, Kai Tak. Huko chini mwanamke mmoja aliyekuwa akianika nguo zake kwenye paa ya nyumba yake katika Kowloon City iliyo karibu, alijikunyata, akivumilia kelele kubwa sana kwenye masikio yake wakati ndege ilipokuwa ikinguruma juu yake.
“Tatizo ni milima,” asema John, rubani ambaye ametua hapo mara nyingi licha ya hatari. “Tukitua kutokea upande wa kaskazini-magharibi, itamaanisha kukata kona hatari kabla tu ya kufika kwenye barabara ya ndege. Milima husababisha pia mikondo ya hewa iliyo hatari ambayo hutokezwa na badiliko la ghafula la mwendo wa upepo.”
Kwa abiria waliokuwa na wasiwasi, marubani, na hasa watu wa Kowloon City, siku ambayo ndege ya mwisho ingetua katika Kai Tak ilingojwa kwa hamu. Na siku hiyo ilifika, kwani katika Julai 1998, Hong Kong ilianza kutumia uwanja mpya wa ndege.
Uwanja wa Ndege Kwenye Kisiwa
Katika miaka ya 1980, uwanja wa ndege wa Kai Tak ulijaa pomoni. Sehemu mpya ya kujenga uwanja wa ndege ilitafutwa kwa kuwa hakukuwa na uwezekano wa kupanua uwanja huo. Ardhi iliyo tambarare na kubwa vya kutosha uwanja wa ndege haikupatikana katika Hong Kong. Mbali na hivyo, watu hawakutaka makelele yatokayo kwenye uwanja wa ndege katika maeneo ya nyumba zao. Suluhisho lilikuwa gani? Chek Lap Kok, kisiwa kidogo kilicho upande wa kaskazini ya Lantau, kisiwa kikubwa, ambacho hakijajengwa sana. Ulikuwa mradi mgumu ambao wahandisi ujenzi wangependelea.
Ili kujenga uwanja huo wa ndege, kisiwa kidogo kilihitaji kusawazishwa na kingine kidogo kilicho karibu na kutwaa ardhi yenye ukubwa wa kilometa tisa na nusu za mraba kutoka baharini. Ili kuunganisha uwanja wa ndege na jiji la Hong Kong, reli ya kilometa 34 na barabara kuu zilijengwa, zote zikiwa juu na kuvuka visiwa na milangobahari, zikipitia kati ya jiji la Kowloon, na kuvuka Bandari ya Victoria. Hii ilimaanisha kujenga madaraja, mitaro, na daraja ndefu zinazovuka bonde. Huo ukawa mojawapo wa miradi mikubwa zaidi ya ujenzi kupata kufanywa.
Madaraja ya Kipekee ya Kuvuka Visiwa
Maelfu ya watu huenda kwenye Maeneo Mapya ya Hong Kong ili kujionea mnara mashuhuri ulimwenguni, uitwao Lantau Link, unaounganisha Kisiwa cha Lantau na bara. Umetengenezwa kwa daraja la kamba nene za waya inayounganisha Kisiwa cha Lantau na Kisiwa Kidogo Ma Wan, daraja linalovuka Ma Wan, na daraja la kuning’inizwa lenye upana wa meta 1,377, linalounganisha Kisiwa cha Ma Wan na kisiwa cha tatu, Tsing Yi. Madaraja hayo ya orofa ndiyo marefu zaidi ulimwenguni kati ya madaraja ya aina hiyo, yakiwa na barabara ya magari kwenye orofa ya juu na barabara mbili za magari kwenye sehemu ya chini iliyozingiwa.
Ukiwa mbali nyaya zenye kushikilia daraja la kuning’inizwa huonekana kuwa dhaifu. Mtu hustaajabu ikiwa wahandisi waliipima vizuri au ikiwa daraja litaporomoka majini. Hata hivyo, unapotazama kwa ukaribu utaona kwamba nyaya hizo si dhaifu. Nyaya hizo zenye unene wa meta 1.1 zina nyaya ndogondogo ndani yake zipatazo kilometa 160,000, zinazotosha kuizunguka dunia mara nne. Nyaya hizo zapaswa kuwa na unene wa kiasi hicho kwa sababu zinashikilia sehemu zilizojengwa kimbele zenye tani 500 ambazo hufanyiza daraja hilo. Nyaya hizo zilipomaliza kutengenezwa, sehemu zilizojengwa kimbele zilibebwa na mashua kubwa hadi kwenye eneo hilo na kufungwa juu kutoka majini.
Wakazi wa hapo karibu walivutiwa kuona minara inayotegemeza nyaya za kuning’inizwa ikiinuliwa. Minara hiyo iliinuliwa bila jukwaa ambalo kwa kawaida hutumiwa katika miradi ya ujenzi. Wajenzi walitumia njia ya kuinua bamba la saruji na huku wakimwaga sementi wakati uleule. Kwa kutumia njia hii fremu ya dirisha ambamo saruji humwagwa huinuliwa polepole bila kuzibomoa na kuzijenga upya katika kila hatua. Kwa kutumia uvumbuzi huu, wajenzi walijenga mnara wa daraja wenye meta 190 kwa miezi mitatu tu.
Hong Kong iko katika ukanda wa tufani. Pepo zenye nguvu zitaathirije wanaovuka? Katika mwaka wa 1940 daraja la awali la Tacoma Narrows, Washington, Marekani, liliharibiwa na upepo uliokuwa ukisafiri kwa mwendo wa kilometa 68 kwa saa na kulikunja daraja hilo kana kwamba lilitengenezwa kwa mwanzi. Tangu wakati huo, mbinu za kujenga madaraja zimeboreka sana. Madaraja haya yametengenezwa na kujaribiwa ili kustahimili dhoruba zenye kusafiri kwa mwendo wa kilometa 300 kwa saa.
Kutoka Kwenye Uwanja wa Ndege Hadi Jijini kwa Dakika 23!
Inachukua muda mfupi kufika kwenye Kisiwa cha Hong Kong kutoka kwenye uwanja mpya wa ndege kuliko kutoka kwa ule wa hapo awali katika Kai Tak, hata ingawa ni mbali zaidi kwa mara nne. Kwa nini? Magari-moshi yanayosafiri kwa mwendo wa kilometa 135 kwa saa huhudumia watu hadi kwenye eneo la kati la biashara la Hong Kong, linaloitwa kwa kufaa Eneo la Kati. Kwanza, waweza kuona vizuri milima tambarare ya Lantau. Kisha, baada ya gari-moshi kuvuka visiwa viwili zaidi hadi kwenye bara, linapitia bandari kubwa zaidi ya shehena ulimwenguni katika Kwai Chung. Kilometa 5 zaidi, linafika Mong Kok, makao ya watu 170,000. Kisha, linaendelea hadi kwenye kituo cha watalii, Tsim Sha Tsui, na kwenye handaki inayopitia chini ya bandari, na hivyo gari-moshi lafikia kituo cha mwisho katika Eneo la Kati kwa dakika 23 tu baada ya kuondoka kwenye uwanja wa ndege!
Uwanja wa Ndege kwa Ajili ya Wakati Ujao
Katika Desemba 1992, Chek Lap Kok kilikuwa kisiwa chenye mawemawe chenye ukubwa wa hekta 302. Kufikia Juni 1995, kikawa jukwaa la uwanja mpya wa ndege, wenye hekta 1,248 na bara la Hong Kong likawa na ukubwa wa asilimia 1. Kisiwa cha awali kilipokuwa kikisawazishwa kwa kutumia baruti kali zenye uzito wa tani 44,000, kundi kubwa la meli za kuzoa takataka zilileta mchanga kwenye kisiwa kutoka katika sakafu ya bahari. Wakati ujenzi ulipofikia kilele, zaidi ya hekta mbili kwa siku zilikuwa zikitwaliwa kutoka kwenye bahari. Kwa wastani, tani kumi za vifaa vya ujenzi zilikuwa zikisongezwa kwa kila sekunde kwa miezi yote 31. Mara tu wenye kandarasi ya kusawazisha ardhi walipoanza kuondoka, wengine walianza kujenga uwanja wa ndege hasa.
Steve aliyehusika sana na mradi huu wa ujenzi aandaa mambo makuu fulani: “Ndege kubwa za kisasa zaweza kuharibu njia ya ndege iliyojengwa vibaya. Kwa sababu hiyo, mashine kubwa za kushinikiza zilitumiwa kushinikiza mchanga kabla ya kutandaza lami juu yake. Inakadiriwa kuwa wakati mashine hizi zilipomaliza kutandaza barabara ya kwanza ya ndege na mahali pa kuegeshea ndege, zilikuwa zimekimbia-kimbia umbali wa kilometa 192,000, unaotoshana na kuzunguka ulimwengu mara tano.
“Kampuni yetu ilipewa kandarasi ya kujenga kituo; tulijenga na kuezeka trasi za paa zilizotengenezwa kwa feleji. Kila moja ina uzito wa tani 150. Tulitumia kreni kubwa sana ili kuziinua, na kuziingiza ndani ya trela zenye magurudumu mengi ambazo zilisafiri kwa mwendo wa kilometa mbili kwa saa hadi kwenye kituo.”
Kituo hiki hakijajengwa kwa saruji. Badala ya hivyo, ilitakikana ijengwe kwa mazingira maangavu na yenye hewa ambayo ingependeza wafanyakazi na abiria vilevile. Mbali na hivyo, uwanja wa ndege ulijengwa ili kushughulikia abiria kwa haraka wanapokuwa safarini bila kuwachelewesha sana. Abiria waweza kuketi ndani ya ndege baada ya kufika dakika 30 tu kwenye sehemu za kukaguliwa. Ili kurahisisha mwendo, kigari kisichokuwa na dereva husafirisha abiria kutoka kituo kimoja cha mwisho hadi kingine. Kwa kuongezea, njia za kusonga zenyewe zenye urefu wa kilometa 2.8 hufanya iwe rahisi kwa abiria kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Steve aendelea: “Ni badiliko lililoje kutoka Kai Tak, uwanja ambao ulihudumia abiria zaidi ya milioni 27 katika mwaka wa 1995! Uwanja huu mpya wa ndege waweza kuhudumia abiria milioni 35 na kushughulikia shehena za tani milioni tatu kwa mwaka. Hatimaye utaweza kuhudumia abiria milioni 87 na kushughulikia tani milioni tisa za shehena!”
Hong Kong inatumia pesa nyingi sana kwa mradi huu—dola zipatazo bilioni 20, au karibu dola 3,300 kwa kila wakazi milioni 6.3 wa Hong Kong. Inatumainiwa kwamba uwanja wa ndege wa Chek Lap Kok utasaidia Hong Kong kudumisha ufanisi wake wa kisasa. Kama itakuwa hivyo au sivyo, twaweza kuwa na uhakikisho kamili wa jambo moja: Kutua katika Hong Kong kutakuwa jambo litakaloendelea kukumbukwa.
[Ramani katika ukurasa wa 12]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Reli ya Uwanja wa Ndege
Uwanja wa Ndege katika Chek Lap Kok
Kisiwa cha Lantau
Barabara pana ya Lantau Kaskazini
Lantau Link
Daraja la Kap Shui Mun
Daraja la Tsing Ma
Barabara pana ya Kowloon Magharibi
Kowloon
Uwanja wa Ndege katika Kai Tak
Kisiwa cha Hong Kong
[Picha katika ukurasa wa 13]
Kujenga daraja la Tsing Ma
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]
New Airport Projects Co-ordination Office