Majiji Makubwa ya Biashara
BABILONI la kale liliitwa ‘jiji la wachuuzi’ katika Biblia. (Ezekieli 17:4, 12) Maneno hayo yangalifaa Tiro la kale pia, ambalo leo latambuliwa kuwa Sur, mji wa bandari katika Bahari ya Mediterania kati ya Beirut (Lebanon) na Haifa (Israel).[2]
Kulingana na chanzo kimoja cha habari, Tiro lilikuwa “bandari kuu ya Foenike kutoka karibu 2000 KWK na kuendelea.”[3] Kufikia wakati Waisraeli walipotwaa Bara Lililoahidiwa karibu na mwaka 1467 K.W.K., Tiro ilikuwa bandari yenye nguvu sana kwa habari ya bahari. Wanamaji wayo na meli zayo za kibiashara zilikuwa maarufu sana kwa sababu ya kuabiri sehemu za mbali sana.—1 Wafalme 10:11, 22.[4]
Kikosi cha Meli Chenye Nguvu Zaidi
“Tawala, Uingereza, tawala baharini,” akaandika mshairi mmoja wa Skotland wa karne ya 18 James Thomson juu ya kikosi cha meli kilichofanya Milki ya Uingereza kuwa mojawapo milki kuu zaidi za kibiashara zilizopata kuwapo.[8] “Kuwa na mamlaka baharini kulihakikisha kwamba Uingereza haingeweza kushambuliwa kutoka baharini, usalama wa mali ya milki hiyo, na kukuza mapendezi yayo ya kibiashara ulimwenguni pote kwa amani.”—The Cambridge Historical Encyclopedia of Great Britain and Ireland.[9]
Milki ya Uingereza ilipopanuka, biashara yayo ilienea ulimwenguni pote. Kati ya 1625 na 1783, bidhaa za kuingizwa nchini humo ziliongezeka kwa asilimia yapata 400 na bidhaa za kupelekwa nje zikaongezeka kwa asilimia zaidi ya 300.[10] Kufikia 1870, viwanda vya Uingereza vilikuwa vikitokeza zaidi ya theluthi moja ya bidhaa zenye kutengenezwa katika ulimwengu wote mzima. Huku fedha yayo ya pauni kwa wazi ikithibiti biashara ya kimataifa, London likawa kitovu cha kifedha ulimwenguni kisicho na kifani.[11]
Leo London humaanisha mambo tofauti kwa watu tofauti. Wapenda muziki hufikiria jumba la muziki la Covent Garden au jumba la Royal Festival Hall, mashabiki wa michezo hufikiria stediamu ya Wembley na kiwanja cha Wimbledon, wapenda michezo ya kuigiza hufikiria eneo la West End. Wapendao mitindo ya mavazi hufikiria Savile Row au Carnaby Street, wanafunzi wa historia hufikiria Mnara wa London na Jumba la Hifadhi ya Ukumbusho la Uingereza, huku wapenzi wa wonyesho—kuongezea porojo na kashfa—huenda wakafikiria Bunge na Makao ya Kifalme ya Buckingham.
Kwa kushangaza, hakuna mojapo mavutio hayo ya watalii lililopo katika jiji lenyewe la London. Jiji lenyewe la London, likiitwa tu Jiji, hutumika likiwa kitovu cha kibiashara cha viunga vingi vinavyofanyiza eneo moja. Ndani ya ‘jiji lenyewe’ mna Benki ya Uingereza, ambayo imeitwa kwa upendo Old Lady of Threadneedle Street (Kibibi Kizee cha Barabara ya Threadneedle). Ilifanywa kuwa shirika halali kwa amri ya Bunge katika 1694 na ni mojapo benki kuu za ulimwengu za kale zaidi. Mashirika hayo yenye nguvu hutumika yakiwa benki za serikali, husimamia utendaji wa benki za kibiashara, na mara nyingi hayo huwa na uvutano mkubwa sana kwa sera za kiuchumi kwa kudhibiti ugavi wa fedha na deni. Ndani ya Jiji hilo pia mna Soko la Hisa na kampuni ya Lloyd’s ya London iliyoko karibu, ambayo ni kampuni ya kimataifa ya bima.[12][13]
Likiitwa London la Kisasa katika miaka ya 1960 kwa sababu ya mtindo wa maisha wa kutojali wa wakazi, Jiji hilo nalo limepata huzuni yalo katika kipindi cha karibu miaka 2,000 ya kuwapo kwalo. Katika 1665 ile Tauni Kuu—mweneo mkubwa wa tauni ya majipu ya kinenani—iliua watu wapatao 100,000, na mwaka mmoja baadaye ule Moto Mkuu karibu uangamize Jiji hilo kabisa. Na karibuni zaidi, mashambulizi ya ndege za kivita za Ujerumani zenye kutupa mabomu wakati wa Vita ya Ulimwengu 2 yaliua wakazi 30,000 wa London na kubomoa kabisa au kuharibu asilimia 80 ya nyumba zalo.[14]
Kapitwa na Kijana
Likilinganishwa na London, jiji la New York, lililoanzishwa katika 1624 na wahamiaji kutoka Uholanzi na kuitwa New Amsterdam, ni changa sana. Lakini leo hilo ni mojapo bandari kubwa zaidi na yenye shughuli nyingi zaidi ulimwenguni; ni kitovu cha viwanda, cha kibiashara, na cha kifedha; na ni makao ya benki nyingi zilizo kubwa zaidi na mashirika ya kifedha yaliyo makubwa zaidi ulimwenguni. Kikiwa kitovu cha kibiashara, kinashinda Amsterdam na London.[15] Na ikiwa kama ishara ya ukuu huo, ile minara miwili ya Kitovu cha Biashara cha New York, lililotikiswa katika 1993 na bomu la wavamizi, ingali imo juu zaidi ikiwa na orofa 110 juu angani.[16]
Kama lile taifa ambalo jiji hilo ndilo kubwa zaidi, New York lina mchanganyiko wa watu kutoka mataifa mbalimbali. Tangu 1886 Sanamu ya Uhuru katika bandari yalo imeita wahamiaji kwenda katika ulimwengu unaoahidi uhuru na fursa sawa kwa wote.[17]
Baadhi ya majina ya barabara za New York yana maana kubwa zaidi. Kwa kielelezo, Broadway inajulikana kwa vitumbuizo vya michezo ya kuigiza, ikiweka viwango na vigezo vinavyokuwa na uvutano katika ulimwengu wote mzima. Na vipi juu ya Wall Street? Katika 1792 kikundi cha wabadili hisa 24 kilikutana chini ya mti buttonwood ili kujadiliana kuanzishwa kwa Soko la Hisa la New York. Likiwa limeanzishwa rasmi katika 1817, hilo Soko la Hisa, likiwa soko kubwa zaidi la hisa za dhamana, siku hizi huitwa tu Wall Street.[19]
Broadway ina vitumbuizo vinavyosisimua sana, lakini haishindi Wall Street kwa vituko halisi. Mnamo Oktoba 1987, wakati Wall Street ilipoanguka vibaya sana na kwa haraka zaidi katika historia yayo, yale masoko mengine 22 ya hisa yaliyo maarufu zaidi kotekote ulimwenguni yalianguka vilevile. “Hisia ya kuharibika kwa mambo ilienea sana”—ndivyo alivyoandika mwandikaji fulani wa gazeti—iliyotokezwa na habari ya “kushuka sana kwa bei katika masoko yanayoanza kazi mapema: Tokyo, Hong Kong, London, Paris, Zurich.”[20]
Wall Street isiyo thabiti, Kitovu cha Kibiashara cha Ulimwengu kisicho thabiti—jambo hilo laashiria nini kwa ulimwengu wa biashara?
“Watu wa Ukuta kwa Ukuta”
Hong Kong limesongamana watu sana hivi kwamba pindi moja liliitwa “watu wa ukuta kwa ukuta.”[21] Wilaya ya Mong Kok ina watu 140,000 kwa kila kilometa ya mraba! Ardhi kubwa imetwaliwa kutoka baharini, na bado karibu asilimia 1 ya idadi ya watu wangali wanaishi kihalisi majini! Watu hao wanaoitwa Tanka na wenyeji huishi katika mashua, kama mababu zao waliokuwa wavuvi walivyofanya, ambao walitoka kaskazini mwa Uchina na kuanzisha kijiji kidogo cha uvuvi katika karne ya pili K.W.K.[22]
Kufikia katikati ya karne ya 19, Waingereza walikuja na kutambua mara moja kuwa Hong Kong lilikuwa katika mahali pafaapo na pazuri pa kibiashara. Bandari yalo bora sana ingeweza kufikiwa kutoka pande zote za mashariki na magharibi, na lilikuwa katika njia kuu ya kibiashara kati ya Ulaya na Mashariki ya Mbali. Yakiwa matokeo ya vile Vita vya Kasumba viwili (1839-42 na 1856-60), Uchina ililazimishwa kuachia Uingereza Kisiwa cha Hong Kong na sehemu fulani za Peninsula ya Kowloon, na hivyo hizo zikawa koloni za Uingereza. Katika 1898 eneo hilo lote, kutia ndani Maeneo Mapya katika sehemu za kaskazini, lilikodishwa kwa Uingereza kwa miaka 99. Katika 1997, wakati mkataba huo wa kodi utakapokwisha, Hong Kong litarudia Uchina.[23]
Kama inavyostahili jiji liitwalo na gazeti National Geographic kuwa “kitovu cha kibiashara cha namba tatu kwa ukubwa ulimwenguni na uchumi wa biashara wa namba kumi na moja ulimwenguni,” Hong Kong linashughulikia kutafuta fedha na kuzitumia. Salamu za kawaida katika sherehe za Mwaka Mpya ni “Na ubarikiwe na mali.” Na ni wazi kwamba wengi wa wakazi walo wamebarikiwa sana, jambo linalofanya gazeti hilo lidai kwamba “Hong Kong hutumia mvinyo zaidi kwa kiwango cha kila mtu mmoja-mmoja, na lina magari aina ya Rolls-Royce kwa kila ekari kuliko mahali pengine popote duniani.”[24]
Utajiri huo haungeweza kutabiriwa wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, wakati biashara katika Hong Kong ilipoathiriwa vibaya sana, na chakula kuwa haba, na wakazi wengi kukimbilia barani Uchina hivi kwamba idadi ya watu ikashuka kwa zaidi ya nusu.[25] Baada ya vita, jiji hilo lilianza kupata nguvu kiasi cha kwamba likawa mamlaka kuu ya kiuchumi katika Asia. Bidhaa zalo zauzwa sana katika masoko ya ulimwengu kwa sababu gharama ya chini ya kulipia kazi iliyofanywa na ya kupata mali ghafi hutokeza bei nafuu. Kufikia 1992 mauzo yalo ya nje yalikuwa yamepanda hadi karibu mara 45 kuliko yalivyokuwa katika 1971.[26]
Matokeo ya kibiashara, kisiasa, na kijamii yatakuwa nini wakati Hong Kong litakaporudia Uchina katika 1997? Wakazi fulani na biashara fulani wamekuwa na wasiwasi na wamehamia sehemu nyinginezo.[27] Wengine wamebaki, lakini huenda tayari wameficha fedha zao katika mahali ambapo wanafikiri kuwa pana usalama zaidi.
“Akiba ya Ulimwenguni Pote”
Katika kipindi cha karne ya 17, Uswisi ilichukua msimamo wa kutokuwamo, msimamo ambao haijadumisha kwa mafanikio nyakati zote. Hata hivyo, fedha zilizowekwa huko kuwa akiba huonwa kuwa salama kwa kadiri fulani. Mfumo wa benki za Uswisi huhakikisha kudumisha siri. Kwa hiyo watu wanaotaka kuweka mali zao kuwa siri—kwa sababu zao wenyewe—huweza kubaki bila kujulikana.[28]
Kitovu cha mambo hayo yote ya kifedha ni Zurich. Likiwa na idadi ya wakazi ipitayo 830,000, hilo ni jiji kubwa zaidi la Uswisi. Mahali palo pafaapo katika njia za biashara ya Ulaya pamelitumikia vizuri kwa karne nyingi, na leo jiji hilo linaongoza katika ulimwengu wa fedha.[29] Kwa kweli, Profesa Herbert Kubly anaiita barabara kuu ya Zurich kuwa “kitovu cha benki cha Bara la Ulaya na akiba ya ulimwenguni pote.”[30]
Zurich imechangia pia mambo ya kidini. Kasisi wa Katoliki aliyeitwa Huldrych Zwingli alihubiri kwa mfululizo huko katika 1519, jambo lililotokeza bishano na askofu wa Katoliki wa jiji hilo. Mijadala iliyofuata ilifanywa katika 1523, na Zwingli akashinda. Huku kikundi cha Waswisi wa Kiprotestanti Wenye Kutaka Mabadiliko kikiendelea kupata nguvu zaidi, majiji mengine makuu ya Uswisi yalimuunga mkono Zwingli na yakawa wateteaji wa namna yake ya Uprotestanti.[31]
“Mwana” wa karibuni zaidi wa Zurich alikuwa Albert Einstein, anayeonwa kuwa mmoja wa wasomi mashuhuri zaidi wa kisayansi katika historia. Ingawa alizaliwa katika Ujerumani, Einstein alijifunza fizikia na hesabu katika Zurich. Nadharia fulani aliyotangaza katika 1905 hata ilimwezesha kupata digrii ya Utalaamu wa Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Zurich. Matimizo yake yanafuatana na desturi ya muda mrefu ya Uswisi ya kufanya vizuri zaidi kisayansi, jambo ambalo Zurich limechangia sana. Taasisi ya Serikali ya Tekinolojia iliyoko huko imetokeza washindi wengi zaidi wa tuzo la Nobel kuliko shule nyingine yoyote katika ulimwengu.[32]
Lakini hata ingawa lina utajiri mwingi sana, na urithi wa kidini na kisayansi, Zurich lina matatizo yalo. Gazeti The European lilitoa upande usiopendeza wa jiji hilo mwezi wa Mei uliopita. Lilisema kwamba ingawa “bustani yenye sifa mbaya ya Needle Park iliyomo katika jiji hilo, ambayo wakati fulani ilikuwa uvutio wa watumizi wa dawa za kulevya,” imefungwa, watumizi wa dawa za kulevya wamehamia eneo liitwalo Kreis 5. Eneo hilo, ripoti hiyo yasema, “lina mambo ambayo Uswisi inajaribu sana kuficha—ukosefu wa kazi, ukosefu wa makao, ulevi, mtazamo wa kushindwa na hali, matatizo ya nyumba na, zaidi ya yote, matumizi ya dawa za kulevya.”[33]
Kwa kushangaza, tatizo la dawa za kulevya launganisha Zurich pamoja na New York na Hong Kong. Labda zaidi ya asilimia 80 ya heroini zote zinazoingizwa katika Jiji la New York kiharamu hutoka lile eneo linaloitwa Golden Triangle la kaskazini mwa Myanmar, Thailand, na Laos, ambako vikundi vya kisiri vya Hong Kong vinavyoitwa triads vinahusika sana katika ulanguzi wa dawa za kulevya.a Hivyo, dola nyingi zinazochumwa na vikundi hivyo vya triads vya Hong Kong kupitia mauzo ya heroini kwa wazoefu wa dawa za kulevya wa New York yaelekea huenda katika akiba za benki katika Zurich.[34]
Majiji makubwa ya biashara, yakiwakilishwa vizuri na London, Zurich, Hong Kong, na Jiji la New York, yafanana sana na jiji la kale la Tiro. Likitajirika kwa hasara ya wengine, ufanisi wa kibiashara wa Tiro ulitokeza majivuno ya kupita kiasi na kiburi kilichotokeza msiba.[36]
Je! vitovu vya kibiashara vya kisasa vitafanikiwa zaidi? Je! vina msingi bora zaidi? Uthibitisho waonyesha kwamba havitafanikiwa kuliko majiji yatakayozungumzwa katika sehemu itakayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Neno triad larejezea umbo la pembetatu uliotumiwa na mojapo watangulizi wao kuonyesha umoja uliopo kati ya mbingu, dunia, na mwanadamu. Vikundi vya kisiri vya Wachina vimekuwapo kwa miaka yapata 2,000; vikundi vya kisasa vimeanza katika karne ya 17. Zamani vilikuwa vikundi vya kisiasa, sasa vimekuwa magenge ya majambazi. Magenge hayo yanasemwa “kuwa na uanachama wa watu 100,000 au zaidi,” na gazeti Time lamnukuu mfanyakazi mmoja wa idara ya polisi ya Hong Kong akisema hivi: “Triads hutegemeza sana uhalifu wa magenge.”[35]
[Picha katika ukurasa wa 10]
Hong Kong