Kuutazama Ulimwengu
“Maangamizo ya Ukimya”
Kwa maoni ya Oxfam, shirika fulani mashuhuri la kufadhili usitawishaji, kule kuteseka kwa maskini wa ulimwengu ni kwingi mno hivi kwamba kunaweza kuitwa “maangamizo ya ukimya,” kulingana na gazeti la habari la Uingereza Guardian Weekly. Katika ripoti fulani ya kuanzisha kampeni ya miaka mitano ya kusaidia maskini wa ulimwengu, Oxfam ilipata kwamba mtu mmoja kwa kila watano ulimwenguni huishi katika mataifa 50 yaliyo maskini kuliko yote. Nchi hizohizo zimeona mapato yazo ya ulimwengu yakishuka kwa asilimia 2 tu. Mwanya kati ya matajiri na maskini katika nchi mbalimbali unakua pia. Kwa mfano, Mexico, imepatwa na matatizo mabaya ya kifedha na umaskini wenye kuenea bali kwa wakati uleule imeona ukuzi wa kasi mno katika idadi ya mabilionea. Akasema msemaji fulani wa kike wa Oxfam: “Kuna maoni kwamba viongozi wa ulimwengu na UM . . . wamekosa lengo lao. Tunahitaji kuanza upya kwa ajili ya mileani mpya.”
Yenye Kudhuru Zaidi Kuliko Sigareti
Huu ndio mkataa uliofikiwa na kamati ya kibunge katika India kuhusu bidi, pia inayoitwa sigareti ya watu maskini. Yakadiriwa kwamba zaidi ya wanaume, wanawake, na watoto milioni nne hutokeza bidi zaidi ya milioni 300 kwa siku, wakifunganya ugoro wa tumbaku katika majani ya tendu na kufunga hivyo visokoto kwa uzi. Kulingana na The Times of India, ripoti ya hivi majuzi huonyesha kwamba bidi ina uwezo wa mara mbili unusu kuweza kutokeza kansa kuliko sigareti, yaweza kusababisha ugonjwa wa silicosis na kifua kikuu, na huwa na lami kwa asilimia 47 na nikotini kwa asilimia 3.7 ikilinganishwa na sigareti ya kawaida ya India ambayo ina lami kwa asilimia 36 na nikotini kwa asilimia 1.9 ya nikotini. Si wavutaji peke yao ambao wako hatarini. Mamilioni ya watu ambao hutayarisha bidi kwa kawaida hupatikana wakifanya kazi kwa saa nyingi katika hali zisizo safi kiafya, wakipumua uvumbi wa tumbaku katika vibanda visivyopitisha hewa vizuri. Hasa watoto wafanyao kazi huugua.
Matokeo ya Kujua Kusoma kwa Akina Mama
Wataalamu wa afya ya umma kwa muda mrefu wameamini kwamba watoto katika nchi zinazositawi wana nafasi nzuri zaidi ya kuokoka ikiwa mama zao wajua kusoma na kuandika—lakini hawajaweza kamwe kuainisha kusoma kwenyewe kuwa jambo kuu. Kulingana gazeti New Scientist, uchunguzi uliofanyiwa katika Nikaragua “ulikuwa wa kwanza kuonyesha kwamba kuelimisha wanawake kuna matokeo ya moja kwa moja kwa afya ya watoto wao.” Huo uchunguzi ulichunguza wanawake wasiojua kusoma na kuandika ambao wakiwa watu wazima walishiriki katika programu kubwa ya kuelimishwa ya Nikaragua katikati ya 1979 na 1985. Katika miaka ya mwishoni mwa 1970, kiwango cha kifo cha watoto wa akina mama wasiojua kusoma na kuandika kilikuwa karibu vifo 110 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa wakiwa hai. Kufikia 1985, kiwango cha kifo cha watoto wa akina mama waliojifunza kusoma katika hiyo programu kilishuka hadi 84 kwa kila elfu. Watoto wao pia walikuwa wamelishwa vizuri zaidi. Wataalamu bado hawana uhakika kuhusu sababu inayofanya watoto wa akina mama wanaojua kusoma kuwa na afya nzuri zaidi na kuishi zaidi.
Imani Yadhoofika
Mji mdogo wa Chesterfield Inlet kwenye Hudson Bay katika Maeneo ya Kaskazini-Magharibi mwa Kanada umekumbwa na visa vya kutendwa vibaya kwa watoto wa shule kulikoenea sana. Kulingana na gazeti Maclean’s, ripoti fulani ya kujitegemea iliyotolewa hivi majuzi na serikali ilipata visa vya kutendwa vibaya kingono na kimwili kwa watoto wenyeji wa Inuit kwa kipindi cha miaka 17 katika miaka ya 1950 na 1960 kwenye Sir Joseph Bernier Federal Day School na kwenye makao jirani yanayoendeshwa na Kanisa Katoliki. Polisi walimaliza uchunguzi wa miezi 21 wa mashtaka 236 ya kutendwa vibaya wakaamua kutofikiliza hukumu—katika visa vingine kwa sababu muda uliowekwa kisheria kufikiliza hukumu ulikuwa umepita; katika vingine kwa sababu washtakiwa walikuwa wazee-wazee au hata wamekufa; katika vingine kwa sababu wanafunzi hawangeweza kuwatambulisha wakosaji kihususa. Likaonelea Maclean’s: “Ingawa kupita kwa wakati hakika kumefanya kuadhibiwa kwa wakosaji kuwe kugumu, huko hakujaondosha maumivu ya majeruhi.”
Maisha ya Familia Yanazorota
Maisha ya familia yananawirije siku hizi? Kulingana na Idara ya Habari ya Umma ya Umoja wa Mataifa, akina baba ulimwengu pote kwa wastani hutumia chini ya saa moja kwa siku moja wakiwa peke yao pamoja na watoto wao—katika Hong Kong wastani ni dakika sita tu. Familia za mzazi mmoja zaongezeka. Kwa kielelezo, katika Uingereza nusu ya watoto wote waliozaliwa katika 1990 walizaliwa na wanawake wasioolewa. Jeuri ya familia pia yaongezeka. Yakadiriwa kwamba kati ya watoto wanaoishi Marekani na Ulaya Magharibi, asilimia 4 hupatwa na jeuri mbaya katika nyumba kila mwaka. Walio wazee-wazee wanapatwa na matatizo pia. Hiyo ripoti ya UM ilitaarifu hivi: “Hata katika zile zinazoitwa eti nchi ‘zilizositawi’ za Muungamano wa Ulaya (MU), moja kati ya tano ya idadi ya wazee-wazee wanaishi katika umaskini wa kadiri, aghalabu wakitengwa katika mitaa michafu ya jijini bila utegemezo wa washiriki wa familia na watu wa karibu wa ukoo.”
Hatari ya Kuoanisha Kimataifa
Pamoja na uhuru uliongezeka wa kusafiri kutoka Ulaya Mashariki hadi Ulaya Magharibi kumekuwa na matokeo yasiyopendeza: kuoanisha kimataifa. Tangu 1991 wanawake wakadiriwao kuwa 15,000 wamesafiri kutoka Ulaya Mashariki hadi Ulaya Magharibi wakiwa mabibi-arusi walioagizwa. Wanawake wengi huishi katika umaskini na huota ndoto za maisha mazuri zaidi, hivyo wao hujibu tangazo la shirika la kuoanisha. Angalabu, hiyo ndoto hubadilika kuwa ogofyo mwanamke anapoishia mahali pa upweke katika nchi ya kigeni na katika hali ambayo mume mkatili ana umaliki kamili juu yake. Bibi-arusi mmoja kutoka Poland alicharazwa vibaya sana na mume wake katika Ujerumani hivi kwamba alitorokea vichakani akajificha huko kwa siku mbili katika halijoto zenye kuganda. Kama tokeo la baridi kali, wayo wake wa kushoto na mguu wake wa kulia ulihitaji kukatwa. Likaonelea hivi gazeti la habari Guardian Weekly la Uingereza: “Mengi ya mashirika ya kuoanisha huendesha pia ukahaba. Hayo hunasa wanawake ng’ambo na kisha kuwashurutisha kwenye madanguro. Kama kawaida wale wanaokataa huuliwa.”
Ugonjwa wa Kusafiri
Je, wewe hupatwa na ugonjwa wa kusafiri? Ikiwa ndiyo, hauko peke yako. Watu wapatao 9 kwa kila 10 hupatwa na ugonjwa wa mwendo kwa viwango vinavyotofautiana, laripoti International Herald Tribune. Mbwa, hasa wale wadogo, pia huelekea kupatwa. Hata samaki wakisafirishwa kwa mashua kwenye bahari ambayo si tulivu wanaweza kupatwa na ugonjwa wa baharini! Tiba ni nini? Watu wengi hutafuta kitulizo kwa madawa, ambayo yaweza kununuliwa katika maduka mengi ya dawa. Hapa pana madokezo mengine ambayo yaweza kusaidia: “Usisome ukiwa ndani ya gari lililo mwendoni. Keti mahali ambapo mwendo wahisika kuwa mdogo mno—kwa kielelezo, katika kiti cha mbele cha gari, au sehemu ya juu ya ubawa wa eropleni. Kaza macho kwenye vitu vilivyo mbali, kama vile upeo wa macho. Ikiwa hutaki kufanya hivyo, funga macho yako.
Uchafuzi wa Hewa Wazidi Kuwa Mbaya Katika Ufaransa
Licha ya jitihada nyingi za kuukomesha, uchafuzi wa hewa unaendelea kuwa mbaya zaidi na unatokeza tisho baya la afya kwa mamilioni ya watu waishio Paris na majiji mengine ya Ufaransa. Ingawa katika wakati uliopita kichafuzi kikuu kilikuwa viwanda vikubwa, leo magari yachangia asilimia 80 ya uchafuzi wa hewa jijini. Idadi ya magari katika Ufaransa imerudufika tangu 1970, ikipanda kutoka milioni 12 hadi milioni 24, kukiwa na milioni 3.2 katika eneo la Paris peke yalo. Gazeti la habari la Paris Le Monde lasema kwamba uchunguzi wa hivi majuzi wa serikali ulionyesha kwamba kwa kila ongezeko katika ukolevu wa gesi zenye sumu katika eneo la Paris, kulikuwa na ongezeko linalolingana katika idadi ya vifo na kulazwa hospitalini kwa sababu ya magonjwa ya upumuaji. Hatua madhubuti bado yahitaji kuchukuliwa. Kwa wazi, wanasiasa wahofu kwamba hatua zozote ambazo ni kali vya kutosha kuweza kuwa zenye matokeo hazitapendeza wapiga kura wao wanaoendesha magari.
Tatizo la Usemi Miongoni mwa Watoto
Watafiti kwenye Kliniki ya Matatizo ya Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Mainz, Ujerumani, wamegundua kwamba kila mtoto mmoja kwa wanne wa umri wa kabla ya kwenda shule ana tatizo la usemi. “Singeweza kuamini hizo takwimu,” akaungama Profesa Manfred Heinemann, mkurugenzi wa hiyo kliniki. Wafanyakazi wa kitiba walifanyia uchunguzi kwa watoto wa umri wa miaka mitatu na minne na kupata kwamba kati ya asilimia 18 na 34 walikuwa na matatizo ya usemi. Takwimu zinazolingana katika 1982 zilikuwa asilimia nne tu. Kwa nini kuna hilo ongezeko? “Familia nyingi zinatazama televisheni mno na kuzungumza kidogo sana,” laripoti gazeti la habari la Ujerumani Der Steigerwald-Bote. Yaonekana kwamba vidio, televisheni, na michezo ya kompyuta yachukua fungu la wazazi katika familia nyingi. Watafiti walionelea kwamba baadhi ya watoto ambao hawangeweza kamwe kuzungumza hata hivyo walikuwa “wenye kasi kama umeme” walipocheza michezo ya kompyuta.