Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 4/8 kur. 7-11
  • Kuthamini Wanawake na Kazi Yao

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuthamini Wanawake na Kazi Yao
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wanawake Wakiwa Watafuta-Riziki
  • Akina Mama na Walimu
  • Huruma Inayohitajika Sana
  • “Mpe Thawabu Aliyojipatia”
  • ‘Wanawake Wenye Bidii Katika Bwana’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Heshima na Staha Chini ya Utunzaji wa Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Wanawake Wana Wakati Ujao Gani?
    Amkeni!—1998
  • Cheo cha Wanawake Chenye Maendeleo Katika Nyakati za Kisasa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 4/8 kur. 7-11

Kuthamini Wanawake na Kazi Yao

MIAKA elfu tatu iliyopita, mwanamume aliyeitwa Lemueli aliandika ufafanuzi mwangavu wa mke mwema. Huo umerekodiwa katika Biblia katika kitabu cha Mithali sura ya 31. Mwanamke ambaye wema wake wahimidiwa kwa kweli alikuwa na shughuli nyingi. Aliitunza familia yake, alifanya biashara sokoni, alinunua na kuuza ardhi, aliishonea familia yake nguo, na alifanya kazi shambani.

Mwanamke huyu hakupuuzwa. ‘Watoto wake humwita mbarikiwa, na mume wake humsifu.’ Mke kama huyo ni hazina. Biblia husema, “Thamani yake yapita thamani ya yakuti.”—Mithali 31:10-28, New International Version.

Tangu wakati wa Lemueli, kazi ya wanawake imekuwa, kwa vyovyote, tata zaidi. Fungu lao katika karne ya 20 lawataka wawe wake, akina mama, wauguzi, walimu, watafuta-riziki, na wakulima—yote katika wakati uleule. Wanawake wengi hufanya dhabihu za kishujaa ili kuhakikisha kwamba watoto wao wamepata chakula cha kutosha. Je, wanawake hawa wote hawahitaji uthamini na sifa?

Wanawake Wakiwa Watafuta-Riziki

Leo wanawake wengi zaidi wanalazimika kufanya kazi nje ya nyumbani ili kusaidia kutegemeza familia au ndio pekee wanaotegemeza familia. Kitabu Women and the World Economic Crisis chataja ripoti iliyotaarifu kwamba: “Kazi za nyumbani si ndizo kazi pekee wanazofanya wanawake. Kuna wanawake wachache sana mahali popote ulimwenguni wanaoweza kudai kuwa wao ni ‘wake wa nyumbani tu.’” Na kazi ya wanawake ni yenye kupendeza kwa nadra sana. Ingawa magazeti na vipindi vya televisheni vya mfululizo huenda vikawaonyesha wanawake wakiwa wenye mamlaka katika ofisi kubwa, kwa kawaida uhalisi huwa tofauti kabisa. Wanawake walio wengi wa ulimwengu humenyeka kwa muda wa saa nyingi kwa ajili ya mshahara mdogo sana.

Mamia ya mamilioni ya wanawake hufanya kazi shambani, kulima, kutunza mashamba madogo ya familia, au kutunza mifugo. Kazi hii ya jasho—kwa kawaida ikilipiwa kidogo sana au kutolipiwa kabisa—hulisha nusu ya ulimwengu. “Katika Afrika, asilimia 70 ya chakula hukuzwa na wanawake, katika Asia tarakimu ni asilimia 50-60 na katika Amerika ya Latini ni asilimia 30,” charipoti kitabu Women and the Environment.

Wanawake wanapokuwa na kazi ya kuajiriwa yenye malipo, kwa kawaida wao huchuma kidogo zaidi ya wafanyakazi wa kiume, kwa sababu tu ni wanawake. Ubaguzi huu hasa ni mgumu kuukubali kwa mama ambaye ndiye mtafuta-riziki pekee wa familia, daraka linaloendelea kuwa la kawaida zaidi na zaidi. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa yakadiria kwamba kati ya asilimia 30 na 50 ya nyumba zote katika Afrika, Karibea, na Amerika ya Latini hutegemea mwanamke akiwa mtoa-riziki wao mkuu. Na hata katika nchi zilizositawi zaidi, idadi inayoongezeka ya wanawake wamelazimika kuwa watoa-riziki wakuu.

Umaskini katika sehemu za mashambani katika nchi nyingi zinazositawi waongezea mwendo huu. Mume anayepata kuwa ni mng’ang’ano kuendelea kuilisha familia yake aweza kuamua kuhamia jiji jirani au hata nchi nyingine ili kupata kazi. Anamwacha mke wake kuitunza familia. Ikiwa anafanikiwa kupata kazi, anatuma pesa nyumbani. Lakini licha ya makusudi yake mazuri, kwa kawaida hili haliendelei. Familia aliyoiacha yaweza kuingia ndani zaidi katika umaskini, na hali njema yao sasa yamtegemea mama.

Mzunguko huu wa mambo mabaya, ambao kwa kufaa waelezwa kuwa “kufanya umaskini kuwa wa kike,” huwatupia mamilioni ya wanawake mzigo mkubwa wenye kulemea. “Nyumba zinazosimamiwa na wanawake, zakadiriwa kuwa thuluthi moja ya jumla ya ulimwenguni pote, zina uwezekano wa kuwa maskini mara nyingi kuliko zinazosimamiwa na wanaume, na idadi ya nyumba kama hizo yaongezeka,” chaeleza kitabu Women and Health. Lakini kama ilivyo vigumu, kuandaa chakula si ndio ugumu pekee ambao wanawake wanakabili.

Akina Mama na Walimu

Mama pia anapaswa kutunza hali njema ya kihisia-moyo ya watoto wake. Ana fungu muhimu katika kumsaidia mtoto kujifunza kuhusu upendo na shauku—masomo ambayo yaweza kuwa ya maana kama kutimiza mahitaji yake ya kimwili. Ili kutokeza mtu mzima mwenye usawaziko mzuri, mtoto ahitaji mazingira yenye ujoto na usalama anapoendelea kukua. Mara nyingine tena, fungu la mama ni la maana.

Katika kitabu The Developing Child, Helen Bee aandika: “Mzazi mwenye shauku humjali mtoto, huonyesha shauku, mara nyingi au kwa kawaida hutanguliza mahitaji ya mtoto, huonyesha shauku kwa ajili ya utendaji wa mtoto, na huitikia hisia za mtoto kwa wepesi wa hisia na hisia-mwenzi.” Watoto ambao wamepokea shauku kama hiyo kutoka kwa mama mwenye kujali kwa hakika wanapaswa kuonyesha uthamini wao.—Mithali 23:22.

Kwa kunyonyesha, mama wengi huandaa mazingira yenye shauku kwa mtoto tangu kuzaliwa. Hasa katika nyumba maskini maziwa ya mama ni zawadi isiyo na kifani ambayo aweza kumpa mtoto wake aliyetoka tu kuzaliwa. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 10-11.) Kwa kupendeza, Biblia hutuambia kwamba mtume Paulo alifananisha shauku yake nyororo kwa Wakristo katika Thesalonike na ile ya “mama mwenye kunyonyesha” ambaye ‘huwatunza sana watoto wake mwenyewe.’—1 Wathesalonike 2:7, 8.

Mbali na kulisha na kutunza watoto wake, mara nyingi mama ndiye mwalimu mkuu. “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, wala usiiache sheria ya mama yako,” yashauri Biblia, ikidokeza sehemu kubwa inayofanywa na akina mama katika kuwaelimisha watoto wao. (Mithali 1:8) Hasa ni mama au nyanya ambaye humfunza mtoto kwa subira kuzungumza, kutembea, na kufanya kazi za kila siku za nyumbani na mambo mengine mengi.

Huruma Inayohitajika Sana

Zawadi moja kubwa zaidi ambayo wanawake wanaweza kupatia familia zao ni huruma. Wakati mshiriki wa familia awapo mgonjwa, mama huchukua fungu la muuguzi, huku akiwa angali anatunza madaraka yake mengine. “Kwa hakika wanawake hutoa utunzaji mwingi wa kiafya ulimwenguni,” chaeleza kitabu Women and Health.

Huruma ya mama yaweza kumfanya ale chakula kidogo ili kwamba watoto wake wasikose chakula. Watafiti fulani wamepata kwamba wanawake fulani huona ulaji wao kuwa watosha hata ingawa hawapati lishe ya kutosha. Wamezoea sana kuwapatia waume zao na watoto sehemu kubwa ya chakula hivi kwamba ikiwa wanaweza kuendelea kufanya kazi, wanajiona kuwa wanalishwa vizuri.

Nyakati nyingine huruma ya mwanamke hujionyesha katika kuhangaikia kwake mazingira. Mazingira ni ya muhimu kwake, kwa sababu hata yeye huteseka wakati ukame, kufanywa jangwa, na kukata misitu kunapoiharibu nchi. Katika mji mmoja huko India, wanawake walikasirika walipojua kwamba kampuni moja ya miti ilitaka kukata miti karibu 2,500 katika msitu uliokuwa karibu. Wanawake hao waliihitaji miti hiyo kwa chakula, fueli, na chakula cha mifugo. Wakataji-miti walipofika, wanawake hao tayari walikuwa wamefika, wakiwa wameshikana mikono, wakiizunguka miti kwa kuilinda. ‘Itawabidi kuvikata vichwa vyetu ikiwa mwataka kuikata miti,’ wanawake hao wakawaambia wakataji-miti. Msitu uliokolewa.

“Mpe Thawabu Aliyojipatia”

Awe katika fungu la mtafuta-riziki, mama, mwalimu, au chemchemi ya huruma, mwanamke astahili staha na utambulishi, sawa na kazi yake. Mtu mwenye hekima Lemueli, aliyezungumza kwa kustahi sana mke mwema, alithamini kazi na shauri la mwanamke. Kwa kweli, Biblia yaeleza kwamba ujumbe wake hasa ulikuwa umetoka kwa maagizo aliyopewa na mama yake. (Mithali 31:1) Lemueli alisadiki kwamba mke na mama mwenye kudhamiria hakupasa kupuuzwa. “Mpe thawabu aliyojipatia,” akaandika. “Kazi zake zamletea sifa.”—Mithali 31:31, NIV.

Hata hivyo, wakati Lemueli aliporekodi maoni hayo, hayakuwa tu mrudisho wa fikira za mwanadamu. Yamerekodiwa katika Biblia, ambayo ni Neno la Mungu. “Andiko lote limepuliziwa na Mungu.” (2 Timotheo 3:16) Mawazo hayo yanadhihirisha maoni ya Mungu Mweza Yote kuhusu wanawake, kwani Mungu alipulizia vifungu hivi katika Biblia ili kutuongoza.

Zaidi, Neno la Mungu lililopuliziwa lataarifu kwamba waume wapaswa kuwa ‘wakiwapa wake zao heshima.’ (1 Petro 3:7) Na katika Waefeso 5:33, mume aambiwa: “Acheni kila mtu mmoja-mmoja kati yenu ampende hivyo mke wake kama yeye mwenyewe.” Kwa kweli, Waefeso 5:25 husema: “Waume, endeleeni kuwapenda wake zenu, kama vile Kristo pia alivyolipenda kutaniko na kujikabidhi mwenyewe kwa ajili yalo.” Ndiyo, Kristo alionyesha upendo wa namna hiyo kwa wafuasi wake hivi kwamba alikuwa tayari kufa kwa ajili yao. Aliweka kielelezo bora, na kisicho na ubinafsi kama nini kwa wanaume! Na viwango ambavyo Yesu alifunza na kuishi kulingana navyo vilidhihirisha viwango vya Mungu, ambavyo vimerekodiwa katika Biblia kwa faida yetu.

Lakini, ijapokuwa kazi yao ngumu katika sehemu nyingi, wanawake wengi hupata sifa kwa nadra sana kwa yale wanayofanya. Wanaweza kuboreshaje hata sasa sehemu yao katika maisha? Pia, je, kuna nafasi yoyote kwamba mtazamo kuwaelekea utabadilika? Kuna matumaini gani ya wakati ujao kwa wanawake?

[Sanduku katika ukurasa wa 10]

Njia Tatu Ambazo Kupitia Hizo Mwanamke Aweza Kuboresha Hali Yake

Elimu. Kuna karibu wanawake milioni 600 ambao hawajui kusoma wala kuandika ulimwenguni—wengi wao hawajawahi kupata nafasi ya kwenda shuleni. Labda wewe mwenyewe ulipata elimu kidogo tu, lakini hilo halimaanishi kuwa huwezi kujielimisha. Si rahisi, lakini wanawake wengi wamefaulu. “Sababu za kidini zaweza kuwa na sehemu kubwa katika kuwachochea watu wazima kupata ustadi wa kujua kusoma na kuandika,” chaeleza kitabu Women and Literacy. Ukiwa waweza kujisomea Biblia ni thawabu bora ya kujifunza kusoma. Lakini kuna faida nyingi zaidi.

Si kwamba tu mama anayejua kusoma na kuandika ana nafasi bora zaidi kiuchumi, bali anaweza pia kujifunza kuhusu mazoea mazuri ya kiafya. Jimbo la India la Kerala latolea kielezi chenye kutazamisha cha manufaa za kujua kusoma na kuandika. Hata ingawa eneo hili liko chini ya wastani kwa habari ya mapato, asilimia 87 ya wanawake wake wanajua kusoma na kuandika. Kwa kupendeza, katika jimbo hilohilo vifo vya watoto ni mara tano chini zaidi ya sehemu nyingine zote za India; kwa wastani, wanawake huishi miaka 15 zaidi; na wasichana wote huenda shuleni.

Kiasili, mama anayejua kusoma na kuandika huchochea hatua za kusoma katika watoto wake—tendo la ujasiri lisilotambuliwa sana. Kuelimisha wasichana ni kitega-uchumi bora kabisa. Hakuna kitu kingine kilicho na uwezo wa kuboresha afya ya familia na kuboresha afya ya wanawake wenyewe, chataja kichapo cha Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) The State of the World’s Children 1991. Hakuna shaka kuhusu hilo, stadi za kusoma na kuandika zitakusaidia uwe mama na mtoa-riziki bora zaidi.a

Afya. Ukiwa mama, wahitaji kujitunza, hasa ikiwa u mjamzito au wanyonyesha. Je, waweza kuboresha ulaji wako? Karibu thuluthi mbili za wanawake wajawazito katika Afrika vilevile kusini na magharibi mwa Asia wanaugua kutokana na upungufu wa damu. Mbali na kukumaliza nguvu, upungufu wa damu huongeza hatari zinazohusiana na kuzaa na hufanya iwe rahisi kushambuliwa na malaria. Ingawa nyama na samaki zaweza kuwa zapatikana kwa shida au ni ghali, mayai na mboga au matunda yenye wingi wa chuma yaweza kupatikana. Usiruhusu mapokeo yakuzuie usile vyakula vyenye lishe, wala usiruhusu desturi za kwenu zikuzuie usipate sehemu ya chakula cha familia.b

Kunyonyesha kwa kufaa wewe na mtoto wako pia. Maziwa ya matiti si ghali, ni safi zaidi kwa afya, na yenye lishe zuri zaidi kuliko kibadala kingine chochote kiwezacho kutumiwa. UNICEF yakadiria kwamba vifo vya watoto milioni moja kila mwaka vyaweza kuzuiwa ikiwa akina mama waliwanyonyesha watoto wao wachanga kwa miezi ya kwanza minne hadi sita ya maisha zao. Bila shaka, ikiwa mama ana ugonjwa wa kuambukiza ambao wajulikana kupitishwa kwa maziwa yake, basi kibadala salama chapasa kutumiwa.

Hakikisha kwamba una hewa ya kutosha unapopika ndani ya nyumba yako kwa moto ulio wazi. “Kufunuliwa kwa moshi na gesi zenye sumu za moto huenda kukawa hatari kubwa zaidi ya kiafya ya kikazi inayojulikana leo,” chatahadhari kitabu Women and Health.

Usivute tumbaku, hata msongo uwe mkubwa kadiri gani. Matangazo yenye kupotosha ya sigareti katika nchi zinazositawi yawalenga wanawake, yakijaribu kuwasadikisha kwamba kuvuta sigareti ni ustaarabu. Hili bila shaka si kweli. Kuvuta sigareti huwaumiza watoto wako na kwaweza kukuua. Inakadiriwa kwamba robo ya wavutaji-sigareti wote huuawa na uraibu wao wa tumbaku hatimaye. Zaidi ya hilo, wataalamu wanaonya kwamba uwezekano wa mvutaji-sigareti kwa mara ya kwanza kuwa mraibu wa tumbaku ni wa juu sana.

safi wa Kiafya. Kielelezo chako na shauri lako kuhusu usafi wa kiafya ni muhimu kwa afya ya familia yako. Kichapo Facts for Life chaorodhesha hatua za msingi kwa usafi wa kiafya mzuri zifuatazo:

• Nawa mikono yako kwa sabuni na maji baada ya kugusa kinyesi na kabla ya kugusa chakula. Hakikisha kuwa watoto wako wananawa mikono kabla ya kula.

• Tumia msala, na uuweke ukiwa safi na kuufunika. Ikiwa hili haliwezekani, enda choo mbali iwezekanavyo na nyumba yako, na ufunike kinyesi mara hiyo.—Linganisha Kumbukumbu la Torati 23:12, 13.

• Jitahidi kutumia maji safi kwa nyumba yako. Kwa ajili ya hili, weka visima vikiwa vimefunikwa na utumie vyombo safi kubebea maji.

• Ikiwa huwezi kupata maji salama yaliyo safi ya kunywa, chemsha maji na uyaache yapoe kabla ya kuyanywa. Ingawa maji yasiyochemshwa yaweza kuonekana kuwa safi, bado yaweza kuwa yamechafuliwa.

• Kumbuka kwamba chakula kisichopikwa kina uwezekano mkubwa zaidi wa kupitisha ambukizo. Chakula kipasacho kuliwa kibichi chapasa kusafishwa kabla ya kuliwa na kuliwa haraka iwezekanavyo. Vyakula vingine vyapasa kupikwa kikamili, hasa nyama na kuku.

• Weka chakula kikiwa safi na kikiwa kimefunikwa ili wadudu au wanyama wasikichafue.

• Choma au ufukie takataka za nyumbani.c

[Maelezo ya Chini]

a Mashahidi wa Yehova hupanga madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika bila malipo kama sehemu ya programu yao yenye kuenea sana ya elimu ya Biblia.

b Katika nchi nyingine, mapokeo hushikilia kwamba wanawake hawapaswi kula samaki, mayai, au kuku wakati wa ujauzito, kwa kuogopa kumwumiza mtoto asiyezaliwa bado. Wakati mwingine desturi hudai kwamba mwanamke ale chakula kilichobakia, mara baada ya wanaume na wavulana wanapomaliza kula.

c Ona Amkeni! la Aprili 8, 1995, ukurasa wa 6-11, kwa habari zaidi.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Wanawake wengi katika nchi za Magharibi hufanya kazi ofisini

[Picha katika ukurasa wa 9]

Wanawake wengi ni lazima wafanye kazi katika hali mbaya

[Hisani]

Godo-Foto

[Picha katika ukurasa wa 9]

Akina mama ni walimu nyumbani

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki