‘Tofaa Moja Kila Siku, Huleta Afya’
TAZAMA yale matofaa mekundu yenye kuvutia. Je, hayatamanishi? Kwa hakika ndiyo—na bila shaka kwa sababu nzuri. Matofaa yalifanyizwa ili yachangie hali njema yako na afya nzuri. Miongoni mwa aina nyingi za matunda yafaayo kwa chakula, tofaa ni mojawapo muhimu zaidi. Hivyo, hayo hukushawishi ujinufaishe kwa kuyala.
Mtofaa ni miongoni mwa jamii ya darabi (Rosaceae), na vilevile mpea, mpera wa kizungu, whitethorn, na mti service. Utomvu wa miti hii yote una sukari nyingi sana. Matunda yayo yenye kunukia yana rangi mbalimbali za kijani kibichi, manjano, na nyekundu yakiwa na ladha kuanzia kali hadi tamu.
Pishi zipatazo bilioni 32 za matofaa hutokezwa kila mwaka—kati ya tani milioni 17 na 18. Katika Marekani, karibu nusu ya matofaa hayo huliwa yakiwa tayari. Yaliyobaki hutumiwa kutengeneza vitu kama vile siagi ya tofaa, maji ya tofaa, mchuzi wa tofaa, ute wa tofaa, mvinyo wa tofaa, kinywaji cha tofaa kilichoshindikwa, pai za tofaa, na vinyunya vingine, siki ya tofaa, na divai ya tofaa. Katika Ulaya sehemu kubwa zaidi ya zao hilo hutumika kwenye kinywaji kilichoshindikwa, divai, na mvinyo. Ipatayo robo moja ya jumla ya matofaa yatokezwayo ulimwenguni hutumika kwa kinywaji kilichoshindikwa.
Lakini muda mrefu kabla ya tunda hilo kuwa tamu kwenye ulimi wetu, mtofaa uliochanua kamili ni wenye kupendeza machoni petu. Umepambwa kwa machanuo yenye pindo nyekundu-nyeupe kwa wingi hivi kwamba kama yote yangekuwa matofaa, mti huo haungeweza kustahimili uzito huo. Dhoruba ya mapema ya kiangazi kwa kawaida husababisha baadhi ya machanuo kupeperushwa.
Ukuzaji wa Tofaa
Mtofaa humea vizuri katika Sehemu za Dunia Zenye Kiangazi cha Ukame. Na umekuwa ukikuzwa tangu zamani za kale. Mitofaa na matofaa yatajwa mara sita katika Biblia.a Waroma waliyafurahia, na katika ushindaji wao kadhaa wa kivita, walianzisha ukuzaji wa aina mbalimbali za matofaa kotekote Uingereza na sehemu nyingine za Ulaya. Wakoloni wa mapema Wamarekani walileta mbegu za tofaa na mitofaa kutoka Uingereza.
Kwa kufanya majaribio mengi, vizazi vya wakuzaji vimefanyia maendeleo ubora wa matofaa kupitia uzalishaji. Hata hivyo, hili si tendo la kasi. Kutokeza aina mpya ya tofaa yenye kuuzwa sana huenda kukachukua urefu wa miaka 20. Lakini leo, kwa sababu ya uvumilivu wa wakuzaji, tuna aina mbalimbali za matofaa yenye utamu zaidi na yenye rangi mbalimbali tuwezayo kuchagua.
Kuvuna
Majira ya tofaa huanza Julai au Agosti katika Kizio cha Kaskazini. Lakini aina za kwanza kuiva, kama vile aina ya James Grieve au Transparent, hayawezi kuwekwa kwa muda mrefu. Yapaswa kuliwa upesi, yawe yameiva au yamepikwa. Hata hivyo, hayo huongeza hamu yetu ya kula yale yatakayofuata: Summerred, Gravenstein, Cox’s Orange, Jonathan, Boskop, Red Delicious, Golden Delicious, McIntosh, Granny Smith—kutaja machache tu ya aina mbalimbali za maelfu ya matofaa.
Matofaa yapaswa kuvunwa wakati wa halihewa ya ukavu. Yapaswa kuchumwa kwa uangalifu ili kwamba mimea mipya na majani yayo yasidhuriwe. Matofaa yakiiva kabisa, kuligeuza tunda kidogo kutaling’oa kwa urahisi kutoka kwenye tawi. Ni jambo la maana kuangalia bua lisivunjike kutoka kwenye tofaa, kwa kuwa hili litasababisha madhara, likiharibu kudumu kwa tunda hilo.
Aina zinazoiva baadaye zapasa kuachwa mtini kadiri iwezekanavyo—halihewa ikiruhusu. Ikiwa kwa sababu ya baridi kali ya mapema matofaa yagandamana mtini, kuyachuma kwaweza kuahirishwa hadi yayeyuke. Matofaa yanaweza kuvumilia halijoto zenye digrii chache chini ya kiwango cha barafu, ikitegemea kadiri yayo ya kuiva na kiasi cha sukari, lakini yanapogandamana na kuyeyuka, hayawezi kuhifadhiwa. Yanapasa kutengenezwa haraka kuwa maji ya matunda, matunda yaliyopikwa kwa mvuke, au siki; hayawezi kukaushwa.
Kuhifadhiwa
Jambo lenye kupendeza la matofaa ni kwamba hayo hupumua. Hayo huvuta oksijeni kutoka hewani na kutoa kabonidioksidi pamoja na maji. Kwa hiyo, kadiri mazingira yawavyo yenye joto, ndivyo yanyaukavyo na kufinyaa upesi. Kupitia kupumua hayo pia huvuta harufu kutoka kwa mazingira yayo. Kwa hiyo, ni vema kuyahifadhi peke yayo kwenye halijoto ya digrii Selsiasi 5 hivi.
Kuhifadhi matofaa katika ghala pamoja na viazi kutafanya matofaa yapoteze ladha yayo ya awali. Isitoshe, aina tofauti-tofauti zapasa kuwekwa kando. Na ni vema kuyafunga matofaa kwenye karatasi yakiwa moja-moja. Kufanya hivi hupunguza kunyauka na hatari ya kuambukizwa na mengine yanayooza.
Thamani kwa Afya
Kuna msemo usemao, ‘tofaa moja kila siku, huleta afya.’ Ijapokuwa sivyo ilivyo sikuzote, tofaa lina sifa hii yenye kupendeza. Kwa sababu gani? Kwa sababu ya vitu lililo navyo viwezavyo kufanya afya ya mtu kuwa nzuri.
Kila tofaa moja ni ghala ndogo ya lishe za maana. Linapoiva, lina vitamini B1, B2, B6, C, na E. Pia hilo hutoa aina mbalimbali za sukari, kama vile dekstrosi, fruktosi, na sukrosi. Mchanganyiko wa asidi ndani yalo hutokeza ladha hiyo. Kwa kuongezea, huwa na hesabu fulani ya madini, kama vile kalsiumu, magnesi, potasiamu, na nyingine, pia pektimu na makapi. Asilimia 85 hivi ya tofaa ni maji.
Kitu kingine kipatikanacho katika tofaa ni ethilene, inayotumika hasa kama kichocheaji cha asili cha ukuzaji ambacho huchochea uivaji wa tunda. Kitu hiki chenye gesi chaweza kutumiwa vizuri ikiwa una nyanya za kijani kibichi au parachichi (avokado) ngumu. Ziweke kwenye mfuko wa karatasi pamoja na matofaa machache yaliyoiva, nayo yataiva haraka zaidi.
Kwa kuwa matofaa ni yenye thamani kwa afya, ni jambo la maana kujua lini na jinsi ya kuyala. Kwanza, lazima yawe yameiva. Na ni vema kutoyala matofaa baridi; yaache yawe kwenye halijoto ya chumba kwa muda fulani. Ni jambo la maana pia kuyatafuna vizuri.
Kwa kupendeza, matofaa yana vitu vinavyosemwa kuwa vyenye manufaa kwa kusafisha mfumo wa umeng’enyaji. Vitu vivyo hivyo husaidia kuponya uyabisi wa tumbo na kuhara.
Jambo la Kutahadhari
Matofaa, na vilevile matunda mengineyo, yanaweza kuwa na kuvu. Kwa sababu hii, inafaa kutahadhari. Sumu zitokeazo zaweza kusababisha matatizo na kichefuchefu. Kwa hiyo, linda dhidi ya kuvu, na uondoe si sehemu yenye kuvu tu, bali sehemu izungukayo sehemu iliyoharibika pia, kwa kuwa sumu huelekea kuenea kote.
Hata hivyo, matofaa huchangia afya nzuri yako. Kwa hiyo ikiwa wataka ‘kuwa na afya,’ basi jaribu kula tofaa moja kila siku!
[Maelezo ya Chini]
a Mtofaa: Wimbo wa Solomono 2:3; 8:5; Yoeli 1:12, Zaire Swahili Bible. Matofaa: Mithali 25:11, NW; Wimbo wa Solomono 2:5; 7:8, ZSB.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mtofaa ukiwa umechanua kabisa hupendeza macho