Mwenendo wa Kushurutisha—Je, Huo Hudhibiti Maisha Yako?
“Mimi huamka saa 12 kila asubuhi,” asema Keith.a “Saa yangu yenye kengele imewekwa sikuzote ipige kengele saa 12. Mimi najua kwamba imewekwa hivyo. Siibadili kamwe. Hata hivyo, ni lazima niichunguze tena na tena. Kila usiku ninaiangalia angalau mara tano kabla ya kulala. Na vidude vya kuwashia jiko—ni lazima nihakikishe kwamba kila kimoja kimezimwa. Naweza kuona kwamba vimezimwa, lakini ni lazima nirudi na kuangalia mara moja, mara mbili, mara tatu—ili kuhakikisha tu. Kisha ni lazima nichunguze mlango wa friji, tena na tena, ili kuhakikisha umefungwa. Kisha kuna kufuli la mlango-wavu wa kuzuia wadudu, na yale makufuli mawili kwenye mlango wa mbele wa nyumba . . .”
KEITH ana ugonjwa uitwao obsessive-compulsive disorder (misukumo na mishurutisho ya kupita kiasi) (OCD), unaofasiliwa kuwa hali inayodhoofisha yenye mawazo (misukumo ya kupita kiasi) na matendo (mishurutisho) yasiyodhibitika.b Mtu mwenye OCD huhisi kwamba misukumo na mishurutisho hiyo ya kupita kiasi inatokea bila kukusudiwa. Ni kana kwamba inajilazimisha ndani yao na kuwadhibiti.
Pindi kwa pindi kila binadamu hupatwa na mawazo na misukumo wasiyotaka. Lakini mtu akiwa na OCD hiyo huendelea na kurudia-rudia sana hivi kwamba inavuruga maisha ya kawaida na kusababisha usumbufu mwingi, nyakati nyingine ikitokeza mshuko-moyo. “Lile pigano la akilini la daima lilinifanya nifikirie kujiua,” asema mtu mwenye ugonjwa huo. Angalia baadhi ya dalili za ugonjwa huu wa ajabu.
Kuona Si Kuamini
Bruce aendeshapo gari lake juu ya mwinuko, yeye hupatwa na hofu kuu. ‘Vipi ikiwa nimemkanyaga mwenda-kwa-miguu?’ yeye hujiuliza. Hisia hiyo huongezeka mpaka ni lazima tu arudi tena mahali pa “uhalifu” huo na kuchunguza—si mara moja tu bali tena na tena! Bila shaka, Bruce hapati mwenda-kwa-miguu ambaye amejeruhiwa. Bado, yeye hana uhakika! Basi afikapo nyumbani, yeye atazama habari ili kuona kama kuna ripoti za aksidenti ya mtu aliyegongwa na gari na mwenye gari kutoroka. Yeye hata hupigia polisi simu ili “kuungama.”
Kama vile Bruce, wengi wenye OCD wanakumbwa na shaka: ‘Je, nilimuumiza mtu fulani? Je, nilizima jiko nilipoondoka nyumbani? Je, niliufunga mlango kwa kufuli?’ Nyakati nyingine watu walio wengi waweza kuwa na mawazo kama hayo, lakini mtu mwenye OCD atachunguza na kuchunguza tena na bado hatatosheka. “Wagonjwa wangu wenye kuchunguza-chunguza mambo huonekana kana kwamba wasema ‘jambo la hakika hutokana na ufahamu tu,’” aandika Dakt. Judith Rapoport. “Kwa hiyo ni lazima kifundo cha mlango kizungushwe tena na tena; taa iwashwe na kuzimwa, iwashwe na kuzimwa. Vitendo hivyo hutoa habari mara iyo hiyo, hata hivyo habari hiyo haiwasadikishi.”
Kuwa Safi Si Safi vya Kutosha
Mvulana mwenye umri wa miaka 14 aitwaye Charles alikuwa na msukumo wa kupita kiasi wa kuhofu kuambukizwa viini vya ugonjwa. Mama yake alilazimika kusafisha kila kitu ambacho huenda angegusa kwa kutumia alkoholi ipakwayo. Zaidi ya hayo, Charles aliogopa kwamba wageni wangeleta ambukizo kutoka barabarani.
Fran alihofu alipokuwa akifua nguo zake. “Ikiwa nguo zingegusa upande wa mashine ya kufulia nilipokuwa nikizitoa,” yeye asema, “ilikuwa lazima zioshwe mara nyingine tena.”
Kama vile Charles na Fran, wengi wenye OCD wana misukumo ya kupita kiasi inayohusiana na viini vya ugonjwa na kuambukizwa. Hilo laweza kutokeza hali ya kuoga au kunawa mikono kupita kiasi, nyakati nyingi kufikia hatua ya kusababisha malengelenge—hata hivyo mwenye ugonjwa huo bado hajihisi kuwa safi.
Kuteswa na Akili
Elaine anakumbwa na mawazo yasiyokusudiwa yenye kukosa staha kumwelekea Mungu. “Hayo ni mambo ambayo nisingeweza kamwe kukusudia na ingekuwa afadhali nife badala ya kuyakusudia,” yeye asema. Hata hivyo, mawazo hayo huendelea. “Nyakati nyingine kwa sababu ya kushindana nayo kila siku, ninakuwa nimechoka kihalisi usiku.”
Steven humwekea Mungu “nadhiri” zinazochochewa na hisia za hatia juu ya makosa yake. “Mwelekeo huo hunihuzunisha kwa sababu huonekana kuja bila mimi kutaka,” yeye asema. “Baadaye, dhamiri yangu hunichoma kutimiza kile nilichoahidi. Kwa sababu ya hiyo, wakati mmoja nilishurutishwa kuharibu kitu fulani nilichopenda sana.”
Elaine na Steven pia wana misukumo ya kupita kiasi inayotokea akilini hasa. Ingawa dalili zao hazionekani waziwazi, wale wenye mawazo ya kupita kiasi wanafungiwa katika hali inayorudia-rudia ya kuwa na hisia za hatia na hofu.
Hizi ni baadhi tu ya dalili nyingi za OCD.c Ni nini husababisha ugonjwa huu? Unaweza kuondolewaje?
Kudhibiti Hali Isiyodhibitika
Daktari mmoja afafanua mwenendo wa OCD kuwa tokeo la “mkato wa njia ubongoni” ambamo habari inayohusu ufahamu haifiki na “programu hiyo inarudiwa tena na tena.” Ni nini husababisha kurudia-rudia huko? Hakuna yeyote aliye na uhakika. Yaonekana kwamba kipunguza-ukubwa wa vifereji vya neva ya kupitisha habari kinahusika, lakini mambo mengine kuhusiana na ubongo yanafikiriwa pia. Wengine husema kwamba maono ya maisha ya mapema yaweza kutokeza OCD, labda yakiwa pamoja na maelekeo yaliyorithiwa.
Hata hivyo, kisababishi kiwe ni nini, jambo moja ni wazi: Ni yamkini kwamba kuwaambia tu wale wenye OCD waache kuoga-oga waache kuchunguza-chunguza mambo hakutafaulu. Zaidi yanahusika kuliko kuwa na uthabiti wa moyo na nia.
Dawa zimethibitika kuwa zenye msaada kwa wengi. Njia nyingine yahusisha kumweka mgonjwa katika hali fulani anayoogopa kisha kuzuia itikio la kawaida. Kwa kielelezo, mtu mwenye desturi ya kuoga-oga, angetakwa ashike kitu kichafu kisha asioge. Bila shaka, utibabu huo haumponyi mtu mara moja. Lakini kwa uendelevu, wengine huhisi kwamba wanaweza kuondoa hali hiyo.
Wataalamu wamechunguza pia uwezekano wa kwamba, angalau katika hali fulani, OCD waweza kuwa na msingi wao katika maono ya maisha ya mapema. Imeonwa kwamba watoto wengi waliotendwa vibaya hukua wakihisi hawafai kitu au ni wachafu kiasili, na baadaye baadhi yao wamedhihirisha desturi za mshurutisho wa kuoga.
Ondoleo la Misukumo na Mishurutisho ya Kupita Kiasi
Ikiwa una OCD, usihisi wewe ni tofauti au labda unapatwa na kichaa. “Isipokuwa hofu zao hususa,” aandika Dakt. Lee Baer, “watu wenye OCD huendelea kufahamu uhalisi wa mambo katika sehemu nyinginezo za maisha zao.” Wanaweza kusaidiwa! Kumbuka, OCD ni tokeo la kutokamilika. Si ishara ya udhaifu wa kiadili wala si kushindwa kiroho! Wala hauonyeshi kutopendelewa na Mungu. “BWANA amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”—Zaburi 103:8, 14.
Lakini namna gani ikiwa mawazo ya kupita kiasi yaonekana kutofaa au kuwa yenye kufuru? Kwa habari ya OCD, mawazo mabaya huchochea hisia za hatia, na hisia za hatia zaweza kuchochea hata mawazo mabaya mengine zaidi. “Hunifanya niwe mwenye kuudhika sana,” asema Elaine. “Hunifanya nifadhaike—nikifikiri sikuzote kwamba huenda Yehova amekasirika nami.” Wengine waweza hata kuhisi kwamba mawazo yao ni mamoja na kufanya dhambi isiyosameheka!
Hata hivyo, kwa wazi, maneno ya Yesu kuhusu dhambi isiyosameheka, dhambi dhidi ya roho takatifu ya Mungu, hayakuwa yakirejezea mawazo yasiyokusudiwa, ya kupita kiasi. (Mathayo 12:31, 32) Yesu alielekeza maneno yake kwa Mafarisayo. Yeye alijua kwamba mashambulio yao yalikuwa ya kimakusudi kabisa. Matendo yao ya kimakusudi yalitoka katika mioyo iliyojaa chuki.
Kwa kweli, kuhangaika kwa mtu kama amemchukiza Mungu kwaweza sana kuwa uthibitisho wa kwamba mtu huyo hakutenda dhambi isiyosameheka. (Isaya 66:2) Zaidi ya hayo, inafariji kujua kwamba Muumba aelewa ugonjwa huu. Yeye ni mwenye rehema na yu “tayari kusamehe.” (Zaburi 86:5; 2 Petro 3:9) Hata wakati mioyo yetu inatuhukumu, “Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote.” (1 Yohana 3:20) Yeye anajua kadiri ambayo mawazo na misukumo hutokana na ugonjwa ambao mtu hana uwezo mwingi wa kuudhibiti. Mtu mwenye OCD anayeng’amua jambo hili aweza basi kuacha kujisumbua na hisia za hatia za kadiri isiyofaa.
Twaweza kushukuru kama nini kwamba Yehova aahidi ulimwengu mpya ambao katika huo kutakuwa na ondoleo la taabu zote za kimwili, kiakili, na kihisiamoyo! (Ufunuo 21:1-4) Kwa sasa, wale ambao ni lazima wavumilie ugonjwa huu waweza kuchukua hatua zenye kusaidia ili kupunguza kuteseka kwao.
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina katika makala hii yamebadilishwa.
b Amkeni! haliungi mkono utibabu wowote hususa. Wakristo wenye ugonjwa huu wangetaka kuwa waangalifu kwamba utibabu wowote wanaofuatia haupingani na kanuni za Biblia.
c Chache kati ya dalili nyingine nyingi huhusisha kuhesabu au kuweka akiba ya vitu vingi mno au msukumo wa kupita kiasi kuhusu ulinganifu wa vitu.
[Sanduku katika ukurasa wa22]
Kuandaa Utegemezo
UKIWA rafiki au mshiriki wa familia, wewe waweza kufanya mengi ili kumtegemeza mtu anayepigana na ugonjwa wa misukumo na mishurutisho ya kupita kiasi (OCD).
• Kwanza, chunguza mtazamo wako mwenyewe. Ukiamini kwamba huyo mgonjwa ni dhaifu, mvivu, au mkaidi, sikuzote yeye atafahamu hilo naye hatachochewa kufanya maendeleo.
• Ongea na mgonjwa. Pata kujua hali ambayo yeye anashindana nayo. Kuwa na rafiki-msiri asemaye mambo waziwazi na aliye mnyoofu mara nyingi ni hatua ya kwanza ya mgonjwa kuelekea hali ya kudhibiti dalili za OCD.—Mithali 17:17.
• Usifanye milinganisho. OCD hutokeza misukumo yenye nguvu sana ambayo si kama ile inayohisiwa na wale ambao hawana ugonjwa huo. Kwa hiyo kwa kawaida haisaidii kusimulia jinsi wewe umekabiliana na misukumo yako.—Linganisha Mithali 18:13.
• Msaidie mgonjwa aweke na kutimiza miradi ya kihalisi. Chagua dalili fulani, na uonyeshe mfululizo wa miradi ya kuishinda. Anza na mradi ulio rahisi zaidi kufikia. Kwa kielelezo, mradi mmoja waweza kuwa kuoga kwa muda usiozidi kiasi hususa cha wakati.
• Toa pongezi kwa maendeleo. Sifa hutia nguvu mwenendo ufaao. Kila hatua ya maendeleo—hata iwe ni ndogo jinsi gani—ni ya maana.—Mithali 12:25.
Kuishi na mtu mwenye OCD kwaweza kudhoofisha kihisiamoyo washiriki wa familia. Kwa hiyo, marafiki wapaswa wawe wenye uelewevu na wenye kutegemeza katika njia zozote zile zenye kusaidia wawezavyo.—Mithali 18:24b.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Kuoga kupita kiasi na kuchunguza-chunguza mambo—dalili mbili za OCD