Ethiopia Yenye Kupendeza
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ETHIOPIA
KWA miaka mingi Ethiopia iliitwa milki iliyojificha. Na ijapokuwa zile karne ilipojitenga zimekwisha, ni watu wachache leo wanaojua historia yayo yenye kupendeza, watu wayo wa tamaduni za namna mbalimbali, na hali zayo za kijiografia zisizo za kawaida. Ikiwa na wakazi zaidi ya milioni 50—karibu idadi kama ya Ufaransa—ni nchi isiyopasa kupuuzwa kamwe.
Kwa wazi ni Wagiriki wa kale waliotunga neno “Ethiopia,” limaanishalo “Eneo la Nyuso Zilizochomeka.” Hata hivyo, historia yayo ya mapema ya kisiasa imefunikwa kwa fumbo na hekaya. Mapokeo yadai kwamba Ethiopia ilikuwa sehemu ya Sheba ya kale yenye sifa ya Kibiblia na kwamba malkia wayo alikuwa yule tajiri mwenye cheo kikuu aliyemtembelea Mfalme Sulemani. Hivyo, watawala kadhaa wa zamani wa Ethiopia walidai kuwa wazao wa mwanamume aliyeitwa Menelik, anayedhaniwa kuwa mwana aliyezaliwa katika mahaba kati ya Sulemani na huyu malkia.
Hata hivyo, yaelekea sana kwamba Sheba kwa kweli ilikuwa kusini-magharibi mwa Arabia.a Biblia hutaja Ethiopia katika sehemu zayo zote mbili za Kiebrania (“Agano la Kale”) na Kigiriki (“Agano Jipya”). Kwa mfano, Matendo sura ya 8, hutuambia juu ya “towashi” Mwethiopia, au mkuu wa serikali, ambaye aligeuka kwa Ukristo. Lakini kulingana na mipaka ya siku ya kisasa, Ethiopia ya Kibiblia hasa ilikuwa eneo linaloitwa sasa Sudan.
Kufikia karne ya tatu ya Wakati Wetu wa Kawaida, ufalme wa Aksum ulikuwa umesimamishwa katika Ethiopia. Ulifikia kilele chao chini ya Mfalme ‛Ēzānā katika karne ya nne. Mwenyewe akiwa mgeuka, ‛Ēzānā aligeuza milki yake yote kuwa ya “Ukristo.” Ethiopia iliwasiliana na ulimwengu wa Magharibi kwa muda, lakini uhusiano huo uliharibika kufikia karne ya saba. The Encyclopedia Americana hueleza: “Kwa karibu miaka 1,000 baadaye, Ethiopia ilikuwa imetengwa kutoka sehemu nyingine za Kikristo katika jitihada zayo za kujitetea dhidi ya Waislamu wenye kujipenyeza kutoka kaskazini na mashariki, na vilevile wavamizi wa kipagani kutoka kusini.” Hasa ushindi wa Waislamu juu ya Misri na Nubia ulitenganisha Ethiopia kutoka sehemu nyingine za Jumuiya ya Wakristo.
Tofauti na nchi nyingine za Afrika, Ethiopia haikutawaliwa kwa muda mrefu na wakoloni wa Ulaya, isipokuwa kuwapo kwa Waitalia kwa muda mfupi karibu na mwanzo wa karne hii na kutoka 1935 hadi 1941. Katika 1974 mapinduzi ya kijeshi yalikomesha miliki hiyo ya zamani. Tangu 1991 serikali mpya ilileta mabadiliko katika kufanya nchi hii iwe huru zaidi. Kwa hiyo, sasa inawezekana kujua vizuri nchi hii iliyokuwa imejificha.
Watu na Utamaduni Wao
Ni vigumu kujumlisha habari kuhusu Waethiopia kwa sababu wanatofautiana sana. Kuna Waafar wenye kuhamahama ambao huzunguka-zunguka Jangwa la Danakil lenye joto kali sana. Upande wa magharibi kuna Wanailo wenye ngozi nyeusi. Upande wa kusini huishi hasa Waoromo. Nao Waamhara hukaa katika milima ya kati, ambapo hufanya ukulima kwenye vilele vya milima vyenye upepo mwingi. Basi, si jambo la kushangaza kwamba Ethiopia ina lugha karibu 300. Vikundi vya kikabila vina mitindo yao ya nywele, mitindo ya nguo, na ujenzi. Ujenzi huo hutia ndani vibanda vya mianzi viitwavyo tukuls vilivyo vya kawaida kusini hadi nyumba za matofali ya udongo katikati ya Ethiopia na majengo ya mawe ya ghorofa upande wa kaskazini.
Pia kuna namna-namna ya majina yenye kupendeza. Zaidi ya kuwa majina ya utambulishi tu, majina haya ya kigeni yana maana ambazo sikuzote hujulikana huko. Wasichana huenda wakaitwa Fikre (Mpenzi wangu), Desta (Shangwe), Senait (Wema), Emnet (Imani), Ababa (Ua), au Trunesh (Wewe U Mwema). Baadhi ya majina ya wanaume ni Berhanu (Nuru), Wolde Mariam (Mwana wa Mariamu), Gebre Yesus (Mtumishi wa Yesu), Haile Sellassie (Nguvu ya Utatu), au Tekle Haimanot (Mmea wa Dini).
Mengi ya majina haya hutoa uthibitisho ulio wazi wa athari ya dini ya Othodoksi. Kwa kweli, dini imepenya katika karibu kila utamaduni wa Ethiopia! Kalenda ya miezi 13 imejaa sherehe za kidini. Iliyo mashuhuri kati yazo ni Meskel, “Msherehekeo wa Msalaba,” na Timkat, yenye mwandamano wa kusherehekea ubatizo wa Kristo. Na haishangazi kwamba nyingi ya sanaa ya kitamaduni ya Ethiopia ina asili ya kidini.
Sehemu za Kijiografia
Tazamo lako la kwanza la Ethiopia lapaswa pia kutia ndani jiografia yenye kustaajabisha. Sehemu moja mashuhuri ni Bonde Kuu la Ufa, linalogawanya nchi hiyo mara mbili likielekea Kenya. Kandokando yalo kunapatikana chemchemi nyingi za maji-moto na mapango. Maziwa saba yenye kupendeza hutapakaa katika hili bonde. Milima yenye kimo cha zaidi ya meta 2,000 imeinuka pande zote mbili, ikifikia kaskazini kwenye Milima ya Simyen. Hii huitwa Paa la Afrika ikiwa na kilele cha zaidi ya meta 4,600! Nguzo ndefu sana na mabonde yenye kushangaza ya eneo hili ni vyenye kutazamisha kweli. Ziwa Tana, chanzo cha mto Naili Buluu halipo mbali kutoka hapo. Mto huu nao una mabonde yenye kupendeza yenye kuelekea magharibi kuelekea Sudan. Karibu na Ziwa Tana, Naili Buluu pia huandaa mandhari yenye kupendeza—yale Maporomoko ya Tisissat, ambayo huporomoka juu ya majabali kama nakili ndogo ya Maporomoko ya Victoria yajulikanayo sana. Upande wa kaskazini-mashariki, mabonde ya chumvi yenye rangi mbalimbali yamepamba Danakil, jangwa ambalo ni sehemu ya nchi yenye kina cha chini kabisa ya Afrika. Liko chini ya usawa wa bahari.
Ethiopia hutoa mazao mbalimbali yenye kuvutia, kama ngano, shayiri, ndizi, mahindi, na pamba vilevile zabibu, machungwa na wingi wa vikolezo. Ethiopia pia hudai kuwa mwanzilishi wa awali wa mkahawa, na hata leo ndiye mtokezaji mkubwa wa buni. Kisha kuna nafaka isiyo ya kawaida iitwayo tefi. Hufanana na nyasi, na mbegu zake ndogo sana husagwa ili kuandaa injera, chakula kikuu cha Ethiopia na mlo wa kitaifa. Injera hutengenezwa katika tanuu ya pekee na mara nyingi hupakuliwa ikiwa ndani ya kikapu kikubwa cha mviringo kilichopambwa, mesob. Kikiwekwa sakafuni mwa nyumba nyingi za Waethiopia, mesob hutumika kwa mambo mengi na pia ni sehemu muhimu ya pambo!
Wanyama-Pori
Ethiopia ina nini kwa habari ya wanyama-pori? Ina namna mbalimbali za wanyama-pori. Kwa kweli, Ethiopia ina idadi ya mbuga zilizo mbali zilizojaa namna mbalimbali za swala na simba. Zaidi ya aina za ndege 830 zaishi katika nchi hii, baadhi yazo zapatikana Ethiopia pekee.
Miongoni mwa wanyama wasio wa kawaida ni mbuzi-mwitu walia ibex mwenye kutokeza, huyo ni mbuzi wa mlimani mwenye fahari ambaye hubaki tu katika vilele vya juu vya Milima Simyen. Mamia machache bado huishi miongoni mwa majabali yasiyofikika. Wanaweza kuruka shimo refu sana bila kuteleza. Pia kuna yule gelada maridadi. Kwa sababu ya nywele zake ndefu na doa jekundu lenye kutokeza kifuani pake, pia ameitwa tumbili-simba na nyani mwenye moyo uvujao damu. Huhitaji kusafiri mbali ili uone wanyama. Kwani, barabara za Ethiopia mara nyingi hujaa ngamia, nyumbu, ng’ombe, na punda!
Ni kweli kwamba, nchi hiyo haikosi matatizo. Jiji kuu liitwalo Addis Ababa, ni jiji kubwa la kisasa lenye watu zaidi ya milioni moja. Lakini lina upungufu wa nyumba na ukosefu wa kazi. Ukame na vita vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisha ukosefu wa makao, vilema, na idadi kubwa ya wajane na mayatima. Mashahidi wa Yehova katika nchi hii wanajitahidi zaidi kusaidia Waethiopia waelewe kwamba suluhisho pekee kwa matatizo yao ni Ufalme wa Mungu kupitia Kristo Yesu.—Mathayo 6:9, 10.
Kwa wakati huu, Ethiopia ni nchi inayostahili kujulikana. Twatumaini tazamo hili la kwanza limeamsha hamu yako, ili labda siku moja, uwe na tazamo jingine kwa macho yako mwenyewe, katika nchi hii yenye kupendeza.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi, ona makala “Sheba” katika Insight on the Scriptures, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 18]
“Mesob” hutumiwa kupakulia “injera,” mlo wa kitaifa wa Ethiopia