Kujifunza Biblia—Katika Hifadhi ya Wanyama!
WAKATI fulani uliopita tulichagua mahali ambapo si pa kawaida sana kwa ajili ya mazungumzo ya Biblia ya familia ya kila juma—Hifadhi ya Wanyama ya Emmen—karibu na nyumbani kwetu Uholanzi tukiwa na sababu nzuri sana, ambayo itakuwa wazi kwako upesi.
Sawa na familia nyingi za Kikristo ulimwenguni pote, sisi tuna funzo la Biblia la kila juma. Mara nyingi wakati wa funzo hili tunajifunza juu ya wanyama wanaotumiwa katika Biblia kufananisha sifa njema na mbaya. Tulijiuliza ikiwa tungeweza kuwafahamu hawa wanyama vizuri zaidi nasi tukaamua kuufanya mradi wa familia. Kila mshiriki wa familia alipewa mgawo wa mnyama hususa na kuombwa atafute habari juu ya mnyama huyo katika vichapo kama vile Insight on the Scriptures na mabuku yaliyojalidiwa ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni!
Tunapokaribia lango la Hifadhi ya Wanyama ya Emmen, macho ya watoto wetu, Mari-Claire, Charissa, and Pepijn, yang’aa kwa mtazamio. Twaenda kuona mamba, dubu, punda-milia, chungu, na huenda wengi hata zaidi wa wanyama ambao tumesoma juu yao kwenye Biblia. Lakini kwanza, acha tukueleze juu ya hifadhi hii ya kipekee ya wanyama.
Hakuna Vizimba, Hakuna Vizuizi
Noorder Dierenpark, kama iitwavyo Hifadhi ya Wanyama ya Emmen katika Kiholanzi, ni mbuga ya wanyama ya pekee sana, ambayo imetengenezwa kulingana na kanuni za kisasa. Hapa hutapata wanyama wowote katika vizimba au vizuizi. Badala ya hivyo, katika Emmen kila kitu kimefanywa ili kuwaweka wanyama katika mazingira yanayofanana sana na makao yao ya kiasili. “Ni mgeni aliyezuiliwa kwa ua, wala si mnyama,” mmoja wa wanabiolojia wa mbuga hiyo Wijbren Landman, asema kwa kutabasamu.
“Wanyama hao hawajapangwa kulingana na aina zao mbali-mbali bali kulingana na mahali walipotoka. Hiyo ndiyo sababu katika hii mbuga kubwa ya Kiafrika unayoiona hapa, wanyama wengi iwezekanavyo wanaoishi pamoja mwituni wamewekwa pamoja.” Ndiyo, nasi twawaona pale—wale wanyama warefu zaidi ulimwenguni, twiga wenye shingo ndefu, wawezao kukua kufikia urefu wa meta sita. Wako pamoja na paa, kulungu, punda-milia, nyumbu, kuro, na hata vifaru wachache.
Lakini Wijbren angali ana mengi ya kutueleza kuhusu mbuga ya Emmen: “Wanyama wana nafasi kubwa sana hapa hivi kwamba hawahisi kwamba wanazuiwa. Hata hivyo, tumeandaa njia za kutorokea. Je, wayaona yale mawe makubwa pale? Katikati yayo paa aweza kujificha ili vifaru wasiwasumbue. Nacho kilima kile pale chawawezesha wanyama wasionane. Lakini mara nyingi sana wanyama hata hawaonani. Hili kwa kweli halishangazi, kwa kuwa wameishi pamoja kwenye makao yao katika Afrika kwa maelfu ya miaka.”
Punda-Milia Wenye Kiu
“Tazama! Punda-milia!” Charissa anasisimuka sana. Yeye alifanya utafiti wa kupendeza kuhusu punda-milia. “Ile mistari inapotosha sana umbo na mwili wa punda-milia hivi kwamba hata wenyeji wenye macho makali mara nyingi hawatambui kuwepo kwa punda-milia wakiwa umbali wa meta 40 hadi 50. Ule uwezo mkubwa wa punda-milia wa kuona na kunusa pamoja na uwezo wao wa kukimbia kasi—hata zaidi ya kilometa 60 kwa saa—humlinda kutokana na wanyama walao nyama. Kama vile Zaburi 104:11 hutaja, punda-milia ‘huzima kiu yao.’ Hiyo ndiyo sababu ni mara chache sana wanapatikana zaidi ya kilometa nane kutoka majini.” Kisha akaongeza: “Sisi nasi ni lazima tuzime kiu yetu ya kiroho kwa ukawaida kwa kuwa karibu na kutaniko, kujifunza Biblia, na kuhudhuria mikutano.”
Twaiacha mbuga ya Kiafrika na kutembea kuelekea upande alioko mmoja wa wanyama wawindaji walio wakubwa zaidi duniani, yule dubu-kodiak. Dubu huyu aliye mkubwa zaidi ya dubu wote anaweza kukua kufikia urefu wa meta tatu na kuwa na uzito wa kilogramu 780. Ili ile sehemu wanakofungiwa iwe ya kiasili iwezekanavyo, mawe makubwa na vijito yamepangwa kwa njia ya kupendeza. Dubu-kodiak ni ndugu mkubwa wa dubu-kahawia wa Siria aliyeishi katika Israeli nyakati za Biblia. Kama alivyogundua Mari-Claire, dubu huishi kwa kula vyakula mbalimbali. Wao hula majani na mizizi ya mimea pamoja na matunda, beri, kokwa, mayai, wadudu, samaki, wanyama wagugunao, na vitu kama hivyo, nao wanapenda sana asali. Katika Israeli la kale wakati mboga zilipopungua katika chakula cha dubu, wachungaji walihitaji kulinda dubu wasiwanyang’anye wanyama. Katika ujana wake Daudi alilazimika kukabiliana na shambulizi la dubu ili alinde mifugo ya baba yake.—1 Samweli 17:34-37.
“Moshi Hutoka Katika Mianzi ya Pua Yake”
Lakini kuna wanyama wengine ambao kwa hakika tunataka kuona. Siku nyingine katika funzo letu la Biblia, tulisoma juu ya “Leviathani,” mamba. Mara ya kwanza Pepijn alimfafanua kuwa ‘aina ya samaki, lakini aliye mkubwa sana!’ Kwa kuwa mamba huathiriwa haraka sana na mabadiliko ya halijoto, wanaishi katika Africa House, ambapo hali-hewa ya kitropiki inadumishwa. Mara tunapoingia, tunakumbwa na lile joto na unyevunyevu, unaofanya miwani zetu ziwe na mvuke. Kwa kuongezea hilo, lazima tuzoeane na giza. Tukitembea juu ya daraja la mbao, kwa ghafula tunakutana uso kwa uso na mamba kadhaa wakubwa wanaoonekana kana kwamba wanalinda yale matope ya kugaagaa katika pande zote mbili. Wanakaa pale bila kutikisika hivi kwamba Pepijn analazimika kusema: “Hawa si mamba halisi.”
Mamba ni baadhi ya wanyama-watambaazi waliopo duniani leo walio wakubwa zaidi. Wengine wanaweza kufikia urefu wa meta sita na kuwa na uzito hata kufikia kilogramu 900. Nguvu ya taya zao inashangaza—hata mamba mdogo kwa kulinganishwa mwenye uzito wa kilogramu 50 ana uwezo wa kutoa nguvu inayotoshana na kilogramu 700. Wakati mamba wanapoelea tena baada ya kupiga mbizi kwa muda fulani majini, kule kutoa hewa upesi kupitia mianzi ya pua hufanyiza mpulizo ambao wakati wa mwangaza wa asubuhi waweza kuwa kama ‘mmweko wa nuru’ (NW) na ‘moshi unaotoka katika mianzi ya pua yake’ ambao kitabu cha Ayubu huelezea.—Ayubu 41:1, 18-21.
“Busara Kama Nyoka”
Mara tuwaachapo mamba twaona katika hilo giza—kwa kufaa, nyuma ya vioo—violezo kadhaa vya kiumbe anayetumika katika Biblia kama mfano wa sifa zenye kupendeza na zisizopendeza. Tunazungumza juu ya nyoka, mnyama wa kwanza anayetajwa kwa jina katika Biblia. (Mwanzo 3:1) Yesu alitumia busara ya nyoka kama kielelezo alipokuwa akiwaonya wanafunzi wake kuhusu mwenendo wao kati ya wapinzani walio kama mbwa-mwitu. (Mathayo 10:16) Lakini, bila shaka, nyoka kwa kawaida hutambulishwa kuwa “nyoka wa zamani” Shetani Ibilisi, ambaye katika 2 Wakorintho 11:3 anatajwa kuwa mdanganyi na mwenye hila kama nyoka.—Ufunuo 12:9.
“Mwendee Chungu,. . . Ukapate Hekima”
Mwono usiotazamiwa katika mbuga ya wanyama ni kile kichuguu kikubwa tunachoona, chenye makao ya jamii tatu za chungu wafyeka-majani. Kati ya chungu wengine wafyeka-majani ni wakulima. Twaweza kuona makao hayo nyuma ya kioo; hili hutuwezesha kuchunguza tabia halisi za viumbe hawa wadogo. Chungu hutupendeza kwa kuwa wanatumika katika Biblia kufananisha bidii na hekima ya kisilika.—Mithali 6:6.
Wijbren Landman ni mtaalamu wa wadudu. Anaeleza hivi: “Idadi ya chungu inayokadiriwa kuwa milioni moja mara bilioni moja inafanya kazi ngumu katika uso wa dunia, ikimaanisha kwamba kwa kila binadamu kuna chungu wasiopungua 200,000! Kati ya zile aina tofauti 15,000 zinazopatikana zimesambaa kwenye mabara yote isipokuwa kwenye ncha ya kaskazini na kusini, hakuna aina mbili za chungu zinazofanana. Wote wanajenga nyumba zilizo tofauti, na wanakula aina tofauti za vyakula, lakini wamepangwa vizuri katika njia iliyo karibu sawa.
“Chungu wafyeka-majani hukuza kuvu zinazolika, kama vile tu wanadamu hukuza viyoga. Kama tuonavyo, ukuzaji huu huendelea chini ya ardhi, lakini chakula cha kuvu hutoka juu ya ardhi. Mchana kutwa, chungu wafanya-kazi hushughulika kusafirisha majani hadi kwenye viota vyao. Wanapanda mti au kichaka na kuchagua jani. Kisha, kwa kutumia taya zao zilizo kama makasi, upesi wanakata vipande nusu-duara kutoka kwenye jani kwa msafara wanavibeba hadi kwenye viota vyao, wakivibeba kama mwavuli juu ya vichwa vyao, ikieleza sababu ya jina lao la pili, chungu-miavuli. Kule kukatakata majani huendelea kwa uharaka sana hivi kwamba katika Amerika ya Kusini na ya Kati, wanamaliza majani yote kwenye vichaka au miti kwa muda wa saa chache tu. Si ajabu kwamba hawapendwi huko! Katika kiota wafanya-kazi wengine wanasafisha vile vipande vya majani kwa uangalifu kabla ya kuvitafuna. Baadaye, majani yaliyotafunwa yanachanganywa na vimeng’enya na asidi-amino ambavyo chungu hunya. Sasa ndipo majani hayo yaliyotafunwa yako tayari kutumiwa kama chakula cha kuvu, hivyo ikihakikisha kuwepo kwa kuvu za kutosha kwa ajili ya jamii nzima.”
Tukiwa tumevutiwa sana na hekima ya uumbaji inayoonekana katika unamna-namna usiokoma wa viumbe, twaondoka kwenye mji wa chungu. Ni jioni, na lazima turudi nyumbani. Lakini kuna mengi ambayo hatujaona. Bado hatujatembelea bundi (Isaya 13:21), pomboo (Kutoka 35:23), viboko (“Behemothi,” Ayubu 40:15, NW), mbuni (Yeremia 50:39), au wale wanyama wengine wengi wanaoishi hapa wanaotajwa katika Biblia. Kila mmoja wao anastahili kuchunguzwa. Bila shaka tutarudi tena kwenye Hifadhi ya Wanyama ya Emmen!—Imechangwa.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Mbuni: Yotvatah Nature Reserve