Viviringamavi wa Afrika Watoa Msaada!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI
KARNE mbili zilizopita, wakati ng’ombe walipoingizwa Australia, ni nani angeweza kuona kimbele matatizo makubwa ambayo yangetokea kwenye hiyo nchi?
Kadiri muda ulivyozidi kupita, malisho yakawa yamefunikwa-funikwa kwa samadi, ikizuia ukuzi wa nyasi katika sehemu mbalimbali au kuzifanya zisiweze kuliwa na ng’ombe. Marundo ya samadi hatimaye yakawa sehemu za kuzalia za nzi wanaotaabisha. Kwa hakika, kulingana na jarida Africa—Environment & Wildlife, kufikia miaka ya 1970 jambo hilo lilikuwa limefikia “tatizo kubwa sana la kiuchumi na kimazingira.” Ilikadiriwa kwamba “zaidi ya ekari milioni tano za malisho zilikuwa zikiacha kutoa mazao kila mwaka . . . , viwango vya juu vya nitrojeni havikuwa vinarudishwa mchangani kwa sababu ya samadi ambayo haikuzikwa, nayo idadi ya nzi ilikuwa imekuwa kubwa sana.”
Tatizo lilitokea wapi? Katika Afrika viviringamavi wangeondoa samadi hiyo upesi na ifaavyo. Samadi iliyozikwa na wadudu hao ingefanyiza mbolea kwenye udongo na kuufanya uwe mwepesi, na hivyo ikiboresha ukuzi wa mimea. Kwa njia hiyo, aina ya nzi wenye madhara wangedhibitiwa nayo mayai ya vimelea yangeharibiwa, hilo likizuia kuenea kwa magonjwa ya bakteria.
Hata hivyo, jambo ambalo wakazi wa Australia hawakutambua ni kwamba viviringamavi wa Australia huviringisha tu samadi ndogo, ngumu, iliyo kama vidonge ya wanyama wenye asili yao huko nao hawakuweza kukabiliana na samadi kubwa na laini ya ng’ombe.
Ni nini kilihitaji kufanywa? Kuleta viviringamavi kutoka nchi nyingine! Kwa kielelezo, wale wapatikanao Afrika (ambao ni zaidi ya aina 2,000), hukabiliana na kiasi kikubwa cha samadi laini, kama ile ya ndovu. Kuondoa samadi ya ng’ombe, hakutokezi tatizo lolote kwa viviringamavi hawa. Lakini jinsi ilivyo kuu idadi ya viviringamavi inayohitajiwa kutimiza kazi hiyo! Africa—Environment & Wildlife laripoti kwamba katika mbuga moja ya wanyama ya kitaifa, “viviringamavi 7,000 wameonekana kwenye rundo moja la samadi ya ndovu,” na katika mbuga nyingine, “kwa muda wa saa 12 viviringamavi 22 746 . . . walikusanywa kutoka kwenye rundo la kilo 7 la samadi ya ndovu.” Hebu wazia tu idadi iliyo kubwa sana ya viviringamavi wanaohitajiwa kushughulikia tatizo lenye kuleta msiba la Australia!
Kwa kufurahisha, hali hiyo inarekebika kwa kiasi fulani—shukrani kwa viviringamavi wa Afrika.