Ni Nani Alindaye Wanyama wa Pori wa Afrika?
NA MLETA HABARI ZA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI
MANENO fulani yasiyo ya fadhili yamesemwa kuhusu jinsi Waafrika huuona urithi wao wa wanyama wa pori. ‘Hawauthamini sana; wao huuona kuwa tu chanzo cha chakula na fedha,’ wageni fulani husema. Ni kwa nini wao hufikia mikataa hiyo? Kwa kawaida mbuga za wanyama hujaa watalii kutoka nchi za Magharibi na wenyeji wachache sana. Lakini wakati mmoja chifu mmoja wa Zulu katika Afrika Kusini alieleza hivi: “Kuna magumu yanayowazuia weusi wasizuru mbuga za wanyama. Kwetu sisi hifadhi za wanyama wa pori ni anasa ambayo ni weusi wachache sana wawezao kufurahia kwa sababu ya kuwa na hali nzuri ya kiuchumi.”
Waafrika wengi leo, tofauti na babu zao, hulelewa katika mitaa ya hali ya chini ya mijini, ambako wanakuwa mbali sana na wanyama wa pori. Mara nyingi wakazi wa mashambani vilevile huwa ni maskini na kupuuzwa. “Ni wale tu walio na chakula cha kutosha ndio wanaoweza kuhifadhi wanyama hasa kwa sababu ya uzuri, tamaduni na elimu,” akaeleza mlinzi wa wanyama wa nchi moja ya Afrika Magharibi.
Yajapokuwa mambo hayo yasiyofaa, wanyama wa pori wanapendwa sana katika sanaa za Kiafrika, kama vile utakavyoona ukizuru maduka ya vinyago. Akiolojia yafunua wanyama wa pori kuwa kitu kikuu cha sanaa za Kiafrika kutokea nyakati za kale. Je! hilo si uthibitisho wa kuthamini uzuri wa wanyama wa pori?
Ebu fikiria hali ya Abel na Rebecca, ambao wametumia likizo kadhaa kuzuru hifadhi za wanyama wa pori za kusini mwa Afrika. Lakini, wote wawili walilelewa katika vijiji vya weusi vya Afrika Kusini. Upendezi wa Rebecca kwa wanyama wa pori ulianzishwa na makao ya wanyama ya kutembelewa na umma katika Johannesburg na Pretoria. “Nikiwa mtoto,” aeleza, “wakati pekee tulioona wanyama wa pori ulikuwa pindi tulipozuru makao hayo ya wanyama.”
Upendezi wa Abel kwa wanyama wa pori ulianza kwa njia tofauti. Mara nyingi alitumia likizo za shule katika sehemu za mashambani akiwa na babu na nyanya. “Babu yangu,” akumbuka, “alikuwa akitaja wanyama tofauti-tofauti na kueleza tabia zao. Nakumbuka akinieleza juu ya mnyama nyegere na yule ndege mdogo mwenye akili, mlembe (kiongozi-asali), anayeaminiwa kuwa huongoza wanyama kwenye mizinga ya nyuki.” Abel asimulia ono hili lenye kushangaza lililompata akiwa mvulana mwenye umri wa miaka 12.
“Siku moja, tulipokuwa tukitembea vichakani, babu yangu alinionyesha ndege mmoja mdogo aliyeonekana kama anatuita. Alikuwa mlembe. Kwa hiyo tulimfuata ndege huyo alipokuwa akiruka mbele yetu kutoka kichaka kimoja hadi kingine. Jambo hilo liliendelea kwa muda unaozidi nusu saa. Hatimaye ndege huyo alitua kwenye tawi na kuacha kulia. Babu yangu akasema kwamba ni lazima sasa tutafute mzinga wa nyuki. Na kwa kweli, upesi tuliona nyuki wakiingia ndani ya shimo moja chini ya mwamba. Babu akatenga kwa uangalifu asali kiasi fulani. Kisha akachukua kipande kidogo cha sega yenye mabuu na kukiweka juu ya mwamba. Hiyo ilikuwa njia yake ya kushukuru ndege huyo kwa kutuongoza kwenye mzinga wa nyuki.”
Uhusiano huo wenye kutokeza sana kati ya binadamu na mlembe umeandikwa katika vitabu vingi na wastadi wa ndege. “Sitasahau kamwe ono hilo,” Abel aendelea kusema. “Lilinifanya nitake kujua mengi zaidi juu ya wanyama wa pori.”
Solomon ole Saibull, aliyekuwa zamani moran wa Masai kutoka Tanzania na ambaye baadaye alifuzu kuwa mhifadhi wa wanyama wa pori, alielewesha mambo alipoeleza mwandikaji mmoja wa vitabu kutoka nchi za Magharibi hivi kwa upole: “Najua idadi kubwa ya Waafrika ambao huthamini uchumi wa hifadhi ya wanyama wa pori, na vilevile kuthamini mazuri yasiyoleta faida . . . Hao ni watu—Waafrika—wawezao kuketi na kutazama Asili ikijionyesha yenyewe katika njia nyingi ndogo-ndogo. Kutua kwa jua juu ya milima yenye rangi ya urujuani, mandhari yenye kusitawi ya mito na mabonde, ule unamna-namna na wingi wa viumbe wakiwa na uhuru wao kamili—yote hayo yakifanyiza mwono mkubwa wa ajabu wenye kuvutia. Kwa kweli, hisi hiyo ya uzuri haipatikani katika Ulaya na Amerika pekee?”
Naam, kutokea wakazi wa vijiji wa maisha ya kawaida hadi wanasayansi waliosoma sana—ni nani hawezi kuvutiwa na urithi wa Afrika wa wanyama wa pori? Mwanafunzi mmoja wa tiba ya wanyama kutoka Ujerumani ambaye hivi karibuni alizuru Afrika Kusini na Mbuga yayo ya Kitaifa ya Kruger alisema hivi: “Niliona asili na wanyama wa pori kuwa vitu vya kupendeza zaidi katika nchi hii. Sisi tukiwa na unamna-namna mdogo wa wanyama wakubwa na ukosefu wa nafasi katika Ujerumani, sijui kabisa kuhusu tafrija ya mambo ya asili na hifadhi inayofikia kiwango hiki.”
Watalii huvutiwa pia na hifadhi kubwa-kubwa za wanyama wa pori katika Botswana, Namibia, na Zimbabwe. Lakini labda mkusanyo ulio mkubwa zaidi wa wanyama wakubwa wa pori katika Afrika wapatikana katika Mbuga ya Kitaifa ya Serengeti katika Tanzania na Hifadhi ya Wanyama ya Masai Mara katika Kenya. Mbuga hizo mashuhuri hushikana, na wanyama hawajafungwa ndani. “Zikiwa pamoja,” laeleza gazeti International Wildlife, “Serengeti na Mara hutegemeza mojapo idadi kubwa zaidi ya wanyama wa pori ulimwenguni pote: nyumbu milioni 1.7, swala 500,000, pundamilia 200,000, pofu 18,000, kutia na idadi kubwa ya ndovu, simba na duma.”
John Ledger, mhariri wa jarida la Afrika Kusini Endangered Wildlife, alizuru Kenya kwa mara ya kwanza katika 1992 na kueleza kuwa hapo ni ‘ma-hali pafaapo na pa ajabu.’ Masai Mara, yeye aliandika, “ni lazima iwe kama mandhari ya nchi ya wakati uliopita ambayo Cornwallis Harris [mwandikaji na mwindaji wa karne ya 19] aliona, alipokuwa akivumbua sehemu ya ndani ya Afrika Kusini katika miaka ya 1820. Nyika kubwa-kubwa, michongoma ya hapa na pale, na wanyama wengi sana wa pori, kufikia upeo wa macho!”
Wonyesho Mdogo wa Utukufu Uliopita
Kwa kusikitisha, leo katika sehemu kubwa ya Afrika, sisi huona wanyama wachache zaidi kuliko wanyama walioonwa na Wazungu walowezi katika karne zilizopita. Kwa kielelezo, katika 1824 mzungu wa kwanza aliishi katika ile sehemu iliyokuja kuwa koloni ya Uingereza ya Natal (sasa ni mkoa wa Afrika Kusini). Koloni hiyo ndogo ilifurika sana kwa wanyama wa pori hivi kwamba kuwinda wanyama kwa ajili ya sehemu fulani zao na vitu vingine vinavyotokana na wanyama wa pori ilikuwa biashara yayo kubwa. Katika mwaka mmoja, ngozi zipatazo 62,000 za nyumbu na za pundamilia zilisafirishwa kutoka bandari ya Durban, na katika mwaka mwingine wenye kuvunja rekodi, zaidi ya tani 19 za pembe za ndovu zilisafirishwa. Upesi, idadi ya wazungu ilikua kufikia zaidi ya 30,000, lakini wengi wa wanyama wa pori tayari walikuwa wameangamizwa. “Ni wanyama wachache sana ambao wamebaki,” akaripoti hakimu mmoja wa Natal katika 1878.
Masimulizi hayo yenye kuhuzunisha yaweza kusemwa pia katika sehemu nyinginezo za Afrika ambako serikali za kikoloni ziliruhusu uangamizo wa wanyama wa pori uendelee mpaka kufikia karne ya 20. Ebu fikiria Angola, iliyopata uhuru kutoka kwa Ureno katika 1975. “Rekodi ya utawala wa awali wa kikoloni,” aandika Michael Main katika kitabu chake Kalahari, “haivutii. Ili kufungua Wilaya ya Huila kwa ajili ya kufuga ng’ombe, ile sheria yenye sifa mbaya iliyoitwa Diploma Legislativo ya Nambari 2242 ya mwaka 1950 ilitangaza eneo hilo kuwa sehemu ya kuwinda bila kizuizi. Matokeo yakawa ni machinjo makubwa sana ya wanyama . . . Karibu kila mnyama mkubwa alitoweshwa. Imekadiriwa kwamba machinjo hayo yalitia ndani vifaru 1,000, maelfu kadhaa ya twiga, na makumi ya maelfu ya nyumbu, pundamilia, na nyati. Sheria hiyo ya Diploma haikubatilishwa kwa karibu miaka miwili na nusu, ambapo kufikia wakati huo tayari hasara kubwa ilikuwa imetokea, na hakukuwa na wanyama waliobaki.”
Lakini hali ikoje leo, na ni wakati ujao wa aina gani unaongojea wanyama wa pori wa Afrika?
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Hifadhi za Wanyama wa Pori Zenye Kuleta Fedha
Hifadhi za wanyama na mbuga za wanyama za Afrika zimetawanyika huku na huku katika kontinenti hii kubwa na zakadiriwa kuwa na mweneo wa kilometa za mraba 850,000. Mweneo huo watoshana na sehemu ambayo ni kubwa zaidi ya Uingereza na Ujerumani zikiwa zimeunganishwa pamoja.
Katika hifadhi nyingi za wanyama wa pori kati ya hizo, waweza kuona wale waitwao wakuu-watano—ndovu, kifaru, simba, chui, na nyati. Kutokea tai wenye fahari wanaopaa angani hadi mendemilia wadogo wanaoviringisha mipira yao ya samadi kuvuka barabara, kuna viumbe vingi vya kustaajabisha macho.
Maelfu ya watalii kutoka ng’ambo huthamini wanyama hao wa pori. Kila mwaka wao huingiza zaidi ya dola bilioni moja katika nchi zinazoshughulikia watu hao wenye kupenda wanyama wa pori. Naam, hifadhi za wanyama wa pori huleta fedha.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Muda usio mrefu uliopita, maelfu yasiyohesabika ya wanyama wa pori waliuawa kila mwaka katika Afrika Kusini kwa ajili ya sehemu zao za mwili na ngozi
[Hisani]
Kwa hisani ya Africana Museum, Johannesburg