Usalama Barabarani kwa Ajili ya Wanyama wa Pori
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
MBWEHA laki moja na kadiri iyo hiyo ya nungunungu na sungura hufa katika barabara za Uingereza kila mwaka, kama wafavyo melesi 40,000, bundi 5,000 na vyura zaidi ya milioni moja. Ukungu wa majira ya kipupwe na giza huchangia mauaji ya wanyama wa pori yasababishwayo na magari yaendayo kasi katika barabara kuu. Mara nyingi madereva huenda upande ili kuepuka kuua mnyama lakini wao huharibu magari yao au hugongana na magari yanayokuja. Hili nyakati nyingine hutokeza kupoteza uhai wa kibinadamu. Baada ya aksidenti imhusishayo mnyama, madereva wengi hupatwa na kiwewe, na kulingana na ripoti za polisi, mamia ya madereva hawawezi kuendelea na safari zao.
Katika baadhi ya barabara kuu katika Uingereza, wenye mamlaka wameweka viakisi maalumu vya kuwaogopesha dia kutoka barabarani. Nuru kutoka taa za mbele za magari zifikiapo viakisi, hutoa mwonekano wa macho ya mbwa-mwitu! Mahali pengine, miti imepandwa mbali zaidi ya kawaida kutoka barabarani ili kuwasaidia madereva waone vizuri mnyama wa pori yeyote aliye mbele. Katika Marekani, baadhi ya madereva wamewekea magari yao filimbi ambazo hutokeza sauti ya juu ya kasimawimbi gari linaposafiri mwendo wa zaidi ya kilometa 55 kwa saa. Hewa ipitapo katika filimbi hutokeza sauti ya desibeli 60 katika kasimawimbi ambayo haiwezi kusikiwa na sikio la binadamu lakini inasikiwa kwa wazi na wanyama wa pori. Kifaa hicho kimethibitika kuwa cha kufaa sana kwa wanyama wenye masikio yanayoelekea mbele. Polisi waliripoti kwamba migongano na dia ilipungua kwa asilimia 50 katika majaribio ya kutumia hiyo filimbi.
Unaweza kuepukaje hatari na uharibifu usio wa lazima kwa wanyama wa pori barabarani? Uendeshapo, hasa wakati wa kipupwe au usiku, punguza mwendo na utii ishara za barabarani zinazokutahadharisha kuhusu kuwapo kwa wanyama.