Ghadhabu za Barabarani—Waweza Kukabilianaje?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
KUWA na hasira na matokeo yanayofuata ya jeuri hutokea mara nyingi katika ripoti za ulimwengu. Kwa kuongezea ghadhabu za toroli (ambapo wateja wanaotumia matoroli, au mikokoteni ya kubebea chakula, huwakiana katika maduka makubwa) na ghadhabu za simu (zikiendelezwa na tekinolojia ambayo humruhusu yule unayempigia simu akufanye ungoje ili apokee simu nyingine), ni ghadhabu za barabarani ambazo zimevuta uangalifu wa watu katika Uingereza.
Ghadhabu za barabarani zimeenea sana kiasi cha kwamba katika mwaka wa 1996 ripoti kuhusu tabia za uendeshaji wa magari ilidai kwamba katika Uingereza ‘imefikia kiwango cha kutisha, nusu ya madereva wote wakipatwa na aina fulani ya shambulio au kutendwa vibaya katika mwaka uliopita’! Uchunguzi wa Shirika la Magari uliripoti kwamba ghadhabu za barabarani zilienea zaidi na uliripoti kwamba “madereva tisa kati ya kumi wadai kuwa wamekuwa wahasiriwa wa ghadhabu za barabarani.” Kwa kupendeza, uchunguzi huohuo ulionyesha kwamba “ni madereva sita tu kati ya kumi waliokubali kuwa na hasira waendeshapo.”
Jambo gani huchochea ghadhabu za barabarani? Ikiwa wewe ni mhasiriwa, waweza kufanya nini ili kujilinda? Ikiwa uendeshaji wa mtu mwingine wakufanya uwe na hasira, wapaswa kufanya nini? Kwa kweli, kwa vile ghadhabu za barabarani zimeenea ulimwenguni pote, waweza kukabilianaje?
Sababu na Matokeo
Kuwapo kwa madereva wenye hasira si jambo jipya. Mkosaji wa mapema ni mshairi Mwingereza Lord Byron. Katika mwaka wa 1817 aliandika barua ambayo katika hiyo alieleza tatizo alilolipata barabarani. Iliripotiwa kwamba, mtumiaji mwingine wa barabara alikuwa mwenye “ufidhuli” kwa farasi wa Byron. Likiwa tokeo mshairi huyo alimpiga ngumi mtu huyo sikioni.
Katika nchi nyingi, kadiri wingi wa magari uongezekapo, ndivyo kukatishwa tamaa kwa madereva huongezeka. Ilikuwa katika miaka ya 1980 kwamba magazeti ya Marekani yalifafanua jambo lililochochea jeuri katika matukio ya uendeshaji kuwa “ghadhabu za barabarani.” Ingawa kushikwa na hasira tu kwa dereva si uhalifu, ghadhabu za barabarani hufafanua vizuri sana hisia-moyo kuwa chanzo cha matendo mengi ya jeuri yafanywayo na madereva ambao huchokozeka na tabia za uendeshaji za watu wengine.
Mtazamo wa mimi-kwanza sasa waenea katika barabara zetu. Watafiti kuhusu mazoea ya uendeshaji wafikia mkataa kwamba “wafanya-jeuri au wachokozi mara nyingi huamini kwamba wao ni wahasiriwa wenye haki kutokana na tabia zisizo za kistaarabu za mtu fulani,” laeleza gazeti The Times la London. Bila kujali anaendesha gari ovyoovyo jinsi gani, dereva huhisi akiwa mwenye haki. Lakini wakati dereva mwingine afanyapo kosa dogo tu la barabarani, ghadhabu za barabarani hulipuka.
Kuongezeka kwa matumizi mabaya ya dawa za kulevya, kulikoenea sana miongoni mwa vijana, pia kumechangia ghadhabu za barabarani. Matumizi mabaya ya kokeini, kulingana na mshauri mmoja wa hospitali, “kwalingana na kuendesha gari ukiwa umelewa alkoholi.” Madereva ambao hutumia dawa za kulevya mara nyingi huwa na maoni ya kujikweza juu ya uwezo wao. Likiwa tokeo, wengine huendesha magari yao katika mwendo wa hatari. Watumiaji wengine wa dawa za kulevya huendesha magari kwa makosa, uwezo wao wa kufanya uamuzi ukiwa umeharibiwa.
Fikiria pia, matokeo ya mkazo kwa dereva. Profesa Cary Cooper wa Chuo Kikuu cha Manchester alaumu mikazo na ukosefu wa uhakika wa maisha ya kila siku katika miaka ya 1990 kuwa kisababishi cha ghadhabu nyingi za barabarani. “Madereva wanakuwa na mkazo zaidi na idadi ya matendo ya jeuri yanaongezeka,” asema msemaji wa Royal Automobile Club. Mtendaji mmoja mwenye shughuli nyingi wa mahusiano ya umma ambaye sasa hutumia muda wa saa nyingi akiendesha gari kwenda na kutoka kazini akubali kwamba sasa yeye si mstahimilivu kama alivyokuwa zamani. “Sasa ninakuwa mwenye haraka katika kutamka neno la ukali na kuwa na hasira kwa mambo madogo ambayo kamwe hayakunihangaisha hapo zamani,” gazeti la The Sunday Times lamripoti akisema hivyo. Labda wewe pia wahisi hivyohivyo. Ikiwa ndivyo, waweza kufanya nini?
Epuka Kuchochea Ghadhabu za Barabarani
Tambua kwamba madereva wengine si wakamilifu. Nyakati fulani-fulani, watavunja sheria. Uendeshapo fikiria jambo hili. Fikiri kimbele. Kwa kielelezo, uendeshapo katika barabara kuu yenye sehemu nyingi ndani yake, waweza kuendesha kando, au katika sehemu ya barabara ya waendao taratibu. Lakini kisha wakaribia njia panda ambapo barabara huungana, au barabara iingiayo katika barabara kuu, yaingiza magari polepole kuingia barabara kuu. Uangaliapo mbele, waona gari likaribialo katika barabara iingiayo barabara kuu. Je, wafikiri kwamba ulikuwa wa kwanza, hivyo basi una haki ya kuendesha katika barabara yako? Kwa nini uyapishe magari yaingiayo barabara kuu? Kwa nini uingie katika sehemu nyingine ya barabara, ikiwa kuna nafasi, ukimruhusu dereva mwingine aingie barabara kuu? Lakini fikiri, nini kitakachotokea ikiwa utasisitiza kubaki katika sehemu yako ya barabara na katika mwendo huohuo? Pengine dereva aingiaye barabara kuu atafikiri katika njia hiyohiyo. Ni lazima, mtu fulani apishe; kinyume cha hivyo, msiba utatokea.
Kwa busara, dereva ambaye ataka kuepuka kutokeza ghadhabu za barabarani ataangalia mbele na ataendesha kwa kufikiri kwa uangalifu. Yeye awapisha wenzake ikiwezekana, na hawi na hasira dereva mwingine ashindwapo kuthamini uungwana alioonyeshwa. Mwakilishi wa Institute of Advanced Motorists ya Uingereza akadiria kwamba dereva 1 katika madereva 3 ana tatizo la mtazamo wa hatari. Ingawa madereva hawa waweza kuendesha magari yao kwa ustadi, wanakosa uungwana. Aliwaita kuwa “madereva wazuri lakini wenye tabia mbaya.”
Nyakati nyingine madereva wengi hudharau watumiaji wengine wa barabara. Lakini hili halihalalishi kutenda katika njia hiyo. Fikiria matokeo yanayoweza kutokea. Bila shaka hutaki ushupavu wowote kwa upande wako utokeze foleni. Usiruhusu hisia-moyo zako zikudhibiti. Mtaalamu wa uendeshaji ashauri hivi: “Kamwe usitende au kuitikia dhidi ya uchokozi barabarani.” Kataa kujiunga na watu wenye ghadhabu-barabarani!
Je, Wewe Ni Mhasiriwa?
Kihalisi kila dereva wakati fulani amekuwa mhasiriwa wa ghadhabu za barabarani. Kunyoosha vidole, kutukana, hila zenye uchokozi yote haya yaweza kutisha na hutisha. Kwa hakika ulinzi bora ni kuepuka pambano. Mhasiriwa mmoja alihisi ametishwa sana na dereva wa gari jingine ambaye alitaka kuwa mbele yake. Hatimaye, dereva huyo mwenye hasira alimpita, alijiingiza kati, na kupunguza mwendo sana kiasi cha kumfanya mhasiriwa kuogopa kwamba magari yao yangegongana. Hali hii iliendelea kwa umbali fulani na iliisha tu wakati mhasiriwa huyo alipokata kona kuingia barabara nyingine.
Ikiwa waona madereva wengine wanataka kwenda mbele yako, fanya yote uwezayo kuwaruhusu wakupite. Epuka kushikilia haki yako ya kubaki mahali ulipo barabarani. Ikiwa umejua kwamba umewaudhi wengine, omba msamaha. Onyesha ishara ya mwili kwamba unasikitika kwa kufanya kosa bila kukusudia. Kumbuka kwamba neno la upole laweza kupooza ghadhabu.
Lakini ikiwa, kwa sababu yoyote, wewe ni mhasiriwa wa shambulio la ghadhabu barabarani, usilipize kisasi. “Usilipize kisasi,” gazeti Focus lashauri. “Usibebe vitu katika gari lako ambavyo vyaweza kutumiwa kuwa silaha za hatari.” Madokezo mengine: Wakati wote hakikisha kuwa milango na madirisha ya gari lako imefungwa kabisa. Epuka kutupiana jicho na mchokozi.
Madokezo yaliyo juu ya jinsi ya kukabiliana na ghadhabu barabarani si mapya. Yanapatana kabisa na shauri la zamani la Mfalme Daudi wa Israeli: “Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya,” alishauri. “Usiwahusudu wafanyao ubatili. Ukomeshe hasira, uache ghadhabu.”—Zaburi 37:1, 8.
Ingawa tatizo la ghadhabu barabarani linakua, usilikuze!
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
Kudhibiti Ghadhabu Barabarani
Shirika la Magari laeleza kwamba linapokuja suala la kumaliza ghadhabu za barabarani, “kubadili mitazamo ni muhimu kama vile hatua za uhandisi.” Kuwa na maoni halisi kuhusu ustadi wako katika uendeshaji na juu ya wale watumiaji wengine wa barabara ni muhimu katika kukabiliana na ghadhabu barabarani. Ingawa makosa ya wengine yanakuwa wazi kwako, usiachilie makosa yako katika uendeshaji. Kubali ukweli kwamba kuna madereva ambao huvunja sheria za barabarani. Uendeshapo, hakikisha uko chonjo kabisa. Uchovu huchangia mkazo. Kushindwa kukaza fikira mara moja kwaweza kuleta madhara ya kifo.
Fikiria pia shauri lifuatalo, na uangalie jinsi linavyohusiana na mithali za Mfalme Solomoni mwenye hekima.
• Je, abiria wako waona hasira zako? Labda washauri kwamba utulie. Usidharau shauri lao na kusema kwamba wao ni abiria watoao amri kwa dereva. Kumbuka, mtazamo wa upole huchangia kuwa na afya na kihalisi waweza kukusaidia kuishi zaidi! “Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili.”—Mithali 14:30.
• Fikiria kile ambacho madereva wengine waweza kufanya na uonyeshe ufikirio, na uepuke matatizo. “Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.”—Mithali 14:16.
• Poza hasira kwa ishara ya mwili au neno la kuomba msamaha. “Jawabu la upole hugeuza hasira.”—Mithali 15:1.
• Wengine waweza kuelekea kuwa na hasira za barabarani, lakini huna haja ya kuwaiga. “Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi.”—Mithali 22:24.
• Jiepushe na mabishano ya watu wengine. “Ondoka kabla ugomvi haujaanza.”—Mithali 17:14, NW.