Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 8/8 kur. 21-23
  • Uchovu—Mtego Usiotambuliwa na Madereva wa Lori

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uchovu—Mtego Usiotambuliwa na Madereva wa Lori
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Visababishi vya Uchovu
  • Kutambua Hatari
  • Kuzuia Hatari
  • Aksidenti za Magari Je, U Salama?
    Amkeni!—2002
  • Je! Wewe Ni Dereva wa Hatari Sana?
    Amkeni!—1991
  • Ghadhabu za Barabarani—Waweza Kukabilianaje?
    Amkeni!—1997
  • Je, Wewe Ni Dereva Salama?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 8/8 kur. 21-23

Uchovu—Mtego Usiotambuliwa na Madereva wa Lori

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI

KADIRI saa zizidivyo kupita, mvumo wenye kukinaisha wa injini yenye nguvu na mlio mkali wa magurudumu 14 barabarani huungana na kufanya pambano la dereva wa lori dhidi ya uchovu kuwa gumu. Alama za barabarani zaonwa zikipita kwa ukimya katika nuru ya taa za mbele. Kwa ghafula, trela yayumba kutoka upande mmoja hadi mwingine; imeanza kuacha barabara.

Kwa kuzungusha usukani kwa nguvu sana dereva afaulu kurudisha barabarani gari lake la tani 40. Akiwa ameamshwa kabisa, atambua kwamba hakumbuki yaliyotukia katika sekunde chache zilizopita. Anaugua uchovu.

Yeyote apambanaye na uchovu akiendesha aweza kupatwa kwa urahisi na usingizi mfupi kwa muda. Kwa kufikiria barabara za leo zilizosongamana, kupatwa na usingizi mfupi kwaweza kuwa hatari sana—hata kwa watumizi wengine wa barabara. Mathalani, katika Afrika Kusini, kati ya aksidenti zote zilizohusisha magari ya kubebea shehena nzito zilizotukia kati ya Januari 1989 na Machi 1994, zaidi ya asilimia 35 zilisababishwa na madereva waliolala wakiendesha.

Profesa G. Stöcker, mtafiti wa mwenendo wa madereva, alisema katika gazeti la Ujerumani Fahrschule kwamba uchovu unaoongezeka unaongoza kwenye usinziaji na una athari zinazofanana na zile zisababishwazo na alkoholi. Bila shaka, maelezo yake yanafaa kwa madereva wa magari yote, si wa lori tu.

Visababishi vya Uchovu

Kwa nini aksidenti zinazohusiana na uchovu hutukia mara nyingi sana, wakati katika nchi nyingi sheria hupendekeza, au hata kuweka sharti, idadi ya juu ya saa ambazo dereva wa lori hapaswi kupitisha? Kwanza, ni lazima tutazame jumla ya saa za kufanya kazi za madereva wa lori, ambazo hutia ndani wakati uliotumiwa si katika kuendesha tu bali katika kufanya kazi nyinginezo vilevile. Saa hizi za kazi mara nyingi ni za muda mrefu na zisizo za kawaida.

Madereva wengi wa lori hufurahia kumaliza kazi yote, jambo linalomaanisha kusafirisha mizigo hadi kwa mteja katika kila halihewa. Utendaji bora hupimwa kwa umbali uliosafiriwa na shehena iliyosafirishwa. Saa za kazi zaweza kuwa nyingi kupita za wastani. Katika Ujerumani watu wengi hufanya kazi chini ya saa 40 kwa juma, lakini madereva wengi wa lori hufanya kazi mara mbili ya hiyo.

Katika nchi nyinginezo hali iko vivyo hivyo. Katika Afrika Kusini ujira ni kidogo, kwa hiyo madereva hujaribu kuongezea mapato yao kwa kuendesha muda mrefu zaidi. Ripoti kutoka India zaonyesha kwamba ingawa mashirika ya usafirishaji huwapa madereva wakati wa kutosha kumaliza safari yao, madereva wengi huongezea mapato yao kwa kupeleka shehena ya ziada mahali pengi, hilo likihitaji wakati zaidi wa kuendesha. Wanahitaji kupunguza saa za kulala ili warudi kwa wakati kwenye shirika lililowaajiri.

Katika maeneo ya Muungano wa Ulaya, kwa kutumia idadi ya juu zaidi ya saa zilizoruhusiwa na sheria, dereva wa lori aweza kutumia muda wa saa 56 akiendesha kwa juma. Lakini katika juma lifuatalo, saa zake za juu zaidi za kuendesha hupunguzwa hadi 34. Saa zake za kazi, kutia ndani wakati uliotumiwa kupakia na kupakua, hurekodiwa na kidude cha kufuatilia. Rekodi hii hufanya iwezekane kujua ikiwa kila dereva anafuata maagizo.

Jambo jingine ambalo huathiri kiasi cha wakati kilichotumiwa kuendesha ni maoni ya bwana-mkubwa. Lori yake ni kitega uchumi kilicho ghali ambacho ni lazima kitumiwe kwa faida, ikiwezekana saa 24 kwa siku ikibeba bidhaa kila wakati. Mashindano miongoni mwa mashirika ya usafirishaji yanaongezeka, na mameneja wanawakaza madereva wafanye kazi muda mrefu zaidi kwa hiari.

Uchovu huja wakati ambapo saa za kazi ni za muda mrefu lakini pia wakati zianzapo katika nyakati zisizo za kawaida. Mathalani, ni jambo la kawaida kuanza kazi kati ya saa saba na saa kumi usiku wa manane. Huu ndio wakati ambapo madereva wako katika hali ya kudhoofika kabisa na ukazaji-fikira wao ni dhaifu zaidi. Msongo huongezeka wakati ambapo shirika lipelekewalo bidhaa huweka ugavi wa chini sana, likidai uwasilishi wa bidhaa ‘kwa wakati barabara.’ Hilo lamaanisha kwamba ni lazima dereva afike kwenye jengo la mteja na shehena kwa wakati barabara uliokubaliwa. Msongamano mkuu wa magari, halihewa mbaya, na marekebisho ya barabara yaweza kusababisha kuchelewa ambako dereva kwa njia fulani atahitaji kulipia.

Japo vizuizi vya idadi ya saa iruhusiwayo kuendesha, uchunguzi wa hapa na pale bado hufunua kuvunjwa kwa sheria. Kulingana na gazeti Polizei Verkehr & Technik, “karibu dereva 1 kati ya 8 wa lori, mabasi, na wasafirishaji wote wa shehena hatari hawafuati idadi ya saa zilizowekwa za kuendesha na kupumzika.” Wakati wa uchunguzi wa magari katika Hamburg, polisi waligundua dereva mmoja wa lori aliyekuwa ametumia saa 32 kuendesha bila kupumzika.

Kutambua Hatari

Dereva mmoja wa mwendo mrefu ambaye alisafirisha shehena ya kimataifa kwa miaka 30 aliulizwa kuhusu tatizo la uchovu. Yeye alionelea hivi: “Kiburi na kujiamini kupita kiasi kwaweza kumfanya dereva apuuze uchovu. Hivyo ndivyo aksidenti hutukia.” Ishara za uchovu zimeorodheshwa katika sanduku kwenye ukurasa wa 22.

Kutambua ishara za kuonya za mapema kwaweza kuokoa uhai. Uchunguzi katika Marekani uliofanywa na National Transportation Safety Board ulifunua takwimu zenye kushangaza: Kati ya madereva 107 waliosalimika aksidenti zisizohusisha magari mengine, 62 zilihusiana na uchovu. Hivyo, biashara ya usafirishaji huweka umaana wa usitawishaji wa misaada ya kiufundi ambao hutoa onyo wakati wowote dereva aanzapo kulala.

Shirika moja la Japani linatengeneza mfumo wa kielektroni utumiao kamera ya vidio ambayo hutazama ni mara nyingi kadiri gani dereva anapesa macho. Dereva akipesa macho kwa uchovu mara nyingi, sauti iliyorekodiwa tayari humwonya juu ya hali yake iliyo hatari. Kampuni moja ya Ulaya inatengeneza kidude ambacho hupima jinsi gari liendeshwavyo kwa utaratibu. Lori iyumbapo, sauti ya onyo hutokea. Hata hivyo, itachukua muda fulani kabla ya misaada yenye matokeo kutokezwa.

Kuzuia Hatari

Uchovu umekuwa abiria asiyealikwa na asiyekaribishwa katika karibu kila gari. Swali ni, jinsi ya kuuondoa. Madereva fulani hunywa vinywaji vingi sana vyenye kafeni, lakini bado uchovu huwapata bila kuacha. Wengine hugeukia visisimuaji vinginevyo. Bila shaka hivyo huhusisha hatari kwa afya. Katika Mexico, madereva fulani hula vipande vya pilipili hoho ili kubaki wakiwa macho.

Kabla ya kuanza mapema, ni vyema kupata usingizi wa kutosha. Na, kama kanuni, mtu apaswa kudumisha idadi iliyowekwa ya saa za kuendesha. Katika Afrika Kusini, wataalamu hupendekeza pumziko baada ya muda wa saa tano za kuendesha. Katika barabara zilizonyooka sana bila kupinda, dereva apaswa kuweka akili yake ikiwa tendaji na ikiwa imekazwa. Madereva fulani husikiliza redio au kuzungumza na madereva wengine kwenye CB radio. Dereva mmoja, ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, husikiliza kaseti zenye vichwa vya Biblia, kama vile Mnara wa Mlinzi na Amkeni! na mafungu kutoka kwenye Biblia. Madokezo mengine yaweza kupatikana katika sanduku lililo kwenye ukurasa huu.

Kuchuma pesa za kutosha kushughulikia gharama ya maisha kunaendelea kuwa jambo gumu, kwa hiyo kuwa na usawaziko si rahisi. Mashirika au mameneja fulani hupuuza hatari ambayo mtego wa uchovu huwekea madereva. Basi, kila mtu ahusikaye na biashara ya usafirishaji, apaswa kukumbuka kile ambacho tumejua kufikia hapa kuhusu uchovu. Kwa kuongezea, madereva mara nyingi huwa na madokezo yenye msaada kutokana na waliyojionea wenyewe ambayo yaweza kuwasaidia wengine kupambana na kusinzia.

Bila shaka njia nzuri zaidi ya kubaki ukiwa chonjo, ni kukubali madai ya mwili: Ukigundua ishara za kuonya, simama mahali pa kupumzikia pafuatapo na ulale. Baadaye, anza kuendesha tena. Usiangukie mtego usiotambuliwa wa uchovu!

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Ishara za Kuonya Zihitajizo Hatua ya Mara Moja

• Je, macho yako yanawasha au kope zako ni nzito?

• Je, unawazawaza kuhusu mambo au kujipata ukiota ndoto za mchana?

• Je, barabara yaonekana ikiwa nyembamba zaidi, ikikufanya uendeshe kwenye laini ya katikati?

• Je, unashindwa kukumbuka sehemu fulani za safari?

• Je, unatumia usukani na breki kwa mshtuko-shtuko kuliko ilivyo kawaida?

Kujibu ndiyo kwa moja tu ya maswali yaliyo juu kwamaanisha kwamba unahitaji kupumzika mara hiyo

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Kwenye Safari za Mwendo Mrefu

• Pata usingizi wa kutosha

• Usitegemee visisimuaji

• Pumzika kwa ukawaida, ukifanya mazoezi ya mwili ili kuulainisha

• Kumbuka kwamba barabara zilizonyooka sana bila kupinda ndizo hatari hasa

• Usianze safari ukiwa na njaa. Jizoeze kula vizuri: mlo mwepesi na wenye afya

• Kunywa viowevu vingi, lakini epuka alkoholi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki