Je, Wewe Ni Dereva Salama?
MTAZAMO wako unapokuwa kwenye usukani wa gari waweza kuathiri sana uwezo wako wa kuendesha gari. Uchunguzi uliofanywa na British Automobile Association ulifunua kwamba kila mwaka asilimia 22 ya wanaume Waingereza walio kati ya umri wa miaka 17 na 20 huhusika katika angalau aksidenti moja ya barabarani.
Ni nini visababishi vikuu katika mazoea yao ya uendeshaji gari usio salama? Mbali na alkoholi, kubadilika-badilika kwa tabia-moyo, na muziki wa sauti kubwa, naibu mkurugenzi mkuu wa Automobile Association, Kenneth Faircloth, aandika hivi: “Wengi mno huathiriwa na marika wao ili waendeshe kwa njia hatari.” Kama tokeo, Automobile Association lapendekeza kwamba mazoezi ya kufunza yakaze fikira nyingi zaidi juu ya mitazamo ya dereva na chache zaidi juu ya mbinu za uendeshaji gari.
Kwa kielelezo, jiulize hivi: ‘Je, mimi hujaribu kuwavutia abiria katika gari langu kwa kujasiria mambo hatari kwa kujionyesha? Je, tabia-moyo yangu ndiyo huamua mwenendo wangu kwenye usukani? Je, mimi huwaona madereva wengine barabarani kuwa vipingamizi tu ambavyo ni lazima vishindwe?’ Majibu kwa maswali kama hayo yafunua wewe ni dereva wa aina gani.
Uwe u mwanamume au mwanamke, mchanga au mzee, kuza mtazamo wa kijirani unapoendesha gari. “Tendea watu wengine sawasawa na vile wewe ungependa kutendewa nao.” (Mathayo 7:12, Phillips) Kufanya hivyo kutakusaidia uendeshe gari kwa usalama.