Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kuchezea-Chezea Ukosefu wa Adili Asanteni kwa ile makala “Vijana Huuliza . . . Kuchezea-Chezea Ukosefu wa Adili—Kuna Madhara Gani?” (Februari 8, 1994) Mimi nilikuwa nikifanya urafiki na mvulana, naye alikuwa akiniambia kwamba kama hangenibusu au kunigusa, hangeweza kuonyesha ni kadiri gani alinipenda. Tulivuka mipaka, na majuma mawili baadaye, alifuta arusi yetu. Nilihisi vibaya sana—na kuwa nimetumiwa. Laiti nisingalikuwa mpumbavu hivyo. Asanteni kwa kutokeza makala hizi, ambazo nilizihitaji sana.
N. R., Marekani
Safari moja nilihusika na upapasaji mzito, nami nikafikiri haukuwa na madhara mradi sikufikia hatua ya kufanya uasherati. Makala hii ilinisaidia kuthamini kwamba hatuwezi kumdhihaki Mungu na kwamba yeye ajua mambo yote.
T. J., Nigeria
Wakati wowote nikutanapo na washirika wa imani yenu, mimi hukubali nakala ya Amkeni! Ndivyo ilivyokuwa na lile toleo la Februari 8, 1994. Ile makala juu ya ukosefu wa adili ilinivutia. Vichapo vya Kanisa la Lutheri la Kievanjeli langu halizungumzii habari hizo, bali huhusika zaidi na habari za wagoni-jinsia-moja na Walawiti wa Kike. Katika magazeti yenu nyinyi hutoboa habari zilizo mwiko kwa wengine. Navutiwa na moyo mkuu na imani yenu yenye nguvu.
H. S., Ujerumani
Nawatolea asante kutoka moyoni kwa ile makala “Vijana Huuliza . . . ‘Kupita Kiasi’ Kwafikia Wapi?” (Oktoba 22, 1993) Mimi ninafanya urafiki na mwanamume kijana aliye Mkristo. Ingawa kupigana busu na kupapasana ni za kawaida katika jumuiya yetu, sisi tuliwekeana mipaka tangu palepale mwanzoni. Si rahisi kufuata viwango viadilifu vya Yehova, nami nina hakika makala hii itasaidia wengi.
P. S. F., Brazili
Ingawa nina miaka 26, zile makala “Vijana Huuliza . . . ” zina thamani kwangu. Nilikuwa nikijitahidi kutatua suala hususa hili. Naterema sana kwamba makala hii yasema kihususa na wazi sana juu ya ni wapi kupita kiasi kwafika!
V. V., Ubelgiji
Mabwawa Nilisukumwa kuandika kwa sababu ya ile makala “Mabwawa ya Ulimwengu—Hazina za Kimazingira Zinazoshambuliwa.” (Januari 22, 1994) Picha hizo zilisaidia kukazia wajibu wetu wa kudumisha uumbaji wa Yehova ubaki ukiwa na uzuri wao wote. Nafurahi kwamba karibuni Mungu ‘atawaangamiza wale wanaoangamiza dunia.’—Ufunuo 11:18, Zaire Swahili Bible.
Z. C. B. S., Brazili
Mimi ni mvulana tineja. Nilisoma makala hiyo na nikang’amua kwamba asili inamalizwa kwa wingi katika sehemu nyingi za ulimwengu. Sasa naweza kuona kwamba hata ingawa wanaume huongea juu ya kuwa wameungamana katika vitendo vyao, wao hawawezi. Kwa hiyo, nataka kufanya yote niwezayo nijifunze Biblia ili niweze kuwa katika Paradiso ya Mungu ya wakati ujao.
Y. K., Japani
Makala yenu ilikuwa kielelezo chema cha jinsi furaha ya kusoma Amkeni! huja si kutokana na yaliyomo tu bali pia kutokana na muundo na utolewaji wa habari zalo: picha ni bora kabisa, mipangilio ni maridadi na safi. Asanteni.
M. E., Kanada
Mwokokaji wa Kambi ya Mateso Nilitiwa moyo sana na ono la Feliks Borys, “Nililindwa na Imani Katika Mungu.” (Februari 22, 1994) Kulisoma kulinigusa hisia, na ilikuwa lazima nijitahidi kuzuia machozi. Limenipa nguvu ya kuvumilia chini ya jaribu.
A. C., Italia
Makala hiyo ilinisaidia kuuthamini hata zaidi uwezo wa Yehova wa kuwalinda wale wanaotia tumaini katika yeye. Niliguswa moyo kwelikweli kusoma juu ya njia nzuri ajabu ambayo kwayo Yehova alijibu sala za Feliks Borys!
E. F., Sweden