Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kuwasiliana Asanteni kwa mfululizo ule mzuri ajabu “Kuwasiliana Katika Ndoa.” (Januari 22, 1994) Mimi nimekuwa katika ndoa kwa miaka 26. Miaka michache iliyopita, ndoa yangu ilipata kuwa yenye mikazo mingi kupindukia, nasi tulikuwa kwenye ukingo wa kupatwa na mgogoro mkubwa. Tatizo lilikuwa ukosefu wetu wa kuwasiliana. Nilipekua vichapo vya Watch Tower Society na kujaribu kutumia niliyoyasoma. Mume wangu pia alianza kujifunza Biblia. Lakini makala hizi zimenipa mambo ya ziada ya kujitahidi kurekebisha. Zinanisaidia kusitawisha utambuzi na zimenichochea kutenda kulingana na madokezo hayo.
Y. K., Japani
Vijana Huuliza Ile makala “Vijana Huuliza . . . Vipi Juu ya Kuzurura-zurura?” (Juni 22, 1993) ilinielekeza kikweli upande ufaao. Mimi naishi katika eneo ambamo ni kawaida sana kuzurura-zurura. Naamini kwamba vijana wengi kama mimi watanufaika na habari hizi.
T. S., Nigeria
Ile makala “Kwa Nini Wazazi Wangu Huwa na Hali ya Moyo Ibadilikayo Upesi?” (Novemba 8, 1993) ilinipendeza kwa njia ya pekee kwa sababu mimi nina baba ambaye hunitolea hasira kali kwa yale ndugu yangu afanyayo. Nyakati fulani mimi huenda kazini pamoja na baba yangu, na sasa natambua ni msongo wa kadiri gani ambao humpata yeye.
A. K., Marekani
Asanteni sana kwa zile makala “Je! Ninakua kwa Njia ya Kawaida?” na “Mbona Nakua Upesi Hivi?” (Septemba 22 na Oktoba 8, 1993) Mimi nina umri wa miaka 11, na watu fulani husema mimi ni mdogo mno kwa umri wangu. Makala hizo zilikuwa nzuri kwelikweli.
J. R. P., Ujerumani
Mimi nina umri wa miaka 11 na nimekuwa shabaha ya kufanyiwa-fanyiwa mizaha ya ukatili juu ya kimo changu. Asanteni kwa kunisaidia kuona kwamba si mimi peke yangu nipatwaye na jambo hili na kwamba mimi ni mtu wa kawaida. Ninakua upesi tu kuliko wengine. Nimesaidiwa kwelikweli na makala hizi.
E. Q., Uingereza
Laiti ningalikuwa na makala hii miaka kadhaa iliyopita wakati mmojapo wana wetu alipoanza kuingia katika ubalehe na kukua haraka sana kufikia kimo chake cha sasa cha sentimeta 206. Nashindwa kuwaeleza ni mara ngapi neno la kwanza kusemwa na watu lilikuwa, ‘Lo! si urefu huo!’ au, ‘Hali ya hewa ikoje huko juu?’ badala ya ‘Jambo, u hali gani?’ Ni wazi kwamba hayo yalimtatiza hata zaidi katika umri wake wa magumu. Twahitaji kusaidia vijana wahisi wamestareheka na miili ambayo wamerithi. Makala yenu ilithaminiwa sana.
M. D., Marekani
Baba Mwaminifu Asanteni kwa makala yenu yenye kutia moyo “Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu.” (Desemba 22, 1993) Baba yangu mwenyewe alikufa akiwa mwaminifu karibu miaka miwili iliyopita. Miguu yake ilikuwa imevimba sana hivi kwamba mwezi wa mwisho hangeweza kutembea. Lakini yeye alihubiria kila mtu aliyekuja kando ya kitanda chake mpaka siku yake ya mwisho. Alitumia karibu saa 20 akieleza wengine juu ya imani yake wakati wa mwezi wake wa mwisho. Makala hiyo ilinikumbusha kwamba ‘mambo yaleyale kwa njia ya mateso yanaupata ushirika mzima wa ndugu zetu.’—1 Petro 5:9, NW.
D. P., Marekani
Mitio ya Damu Mishipani Ningependa kutoa shukrani zangu kwa ajili ya ile makala “Mashahidi wa Yehova na Wastadi wa Tiba Washirikiana.” (Novemba 22, 1993) Ilionyesha hangaiko la Yehova kwa hali njema yetu ya kimwili na pia ya kiroho. Mimi nililazimishwa kutiwa damu mishipani karibu miaka 13 iliyopita kufuatia kuzaliwa kwangu. Kwa hiyo natambua umaana wa kuwa na wanaume Wakristo waliozoezwa kuja kututolea msaada uhitajiwapo. Natumaini na kusali kwamba wengine wataepushwa wasipatwe na lile lililonipata.
K. T., Marekani