Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Wazee-Wazee Nahitaji kuwashukuru kwa makala ya Amkeni! ya Agosti 8, 1993, “Kuzeeka Ukiwa na Ufahamu.” Makala hiyo ilinifanya nitoe machozi. Yaani, mama yangu anakaribia miaka 90. Hivi karibuni aliamua kwenda nje peke yake, ijapokuwa hapaswi kufanya hivyo, naye akaanguka na akavunja mkono wake. Amepona vizuri lakini hawezi kuachwa peke yake. Nimekosa kuhudhuria mikutano kadhaa ya Kikristo, nami wakati mwingine nahisi kwamba nimemtamausha Yehova. Lakini mmenipatia tegemezo jingi sana. Ninaposhuka moyo, naifikiria makala hii.
B. T., Marekani
Msamaha Nimemaliza tu kusoma ile makala “Maoni ya Biblia . . . Msamaha wa Mungu ni Kamili Kadiri Gani?” (Desemba 8, 1993) Hiyo kwa kweli ndiyo niliyohitaji. Makala hiyo ilinisaidia nione kwamba Mungu wetu aondoapo dhambi, zimekwisha kufutwa kabisa, kuoshewa mbali. Ninapoandika barua hii, nahisi amani kwelikweli ya akili.
J. W., Marekani
Ilifariji kujua kwamba Yehova aona moyo na kwamba yu tayari kufuta dhambi zetu. Nilikuwa nikihisi kuwa sistahili msamaha wa Yehova hivi kwamba nikawa nimeshuka moyo. Hata nilifikiria juu ya kujiua. Marafiki wa karibu katika kutaniko wamenisaidia sana. Lakini bado nahitaji uhakikisho, na makala hii ilinisaidia.
K. H., Marekani
Miwani Asanteni sana kwa makala “Kuitazama Miwani.” (Julai 8, 1993) Nilijua nilikuwa na tatizo na macho yangu na kwamba nilipaswa kumwendea mstadi wa macho, lakini niliendelea kuahirisha kwenda kwangu. Baada ya kusoma makala yenu, nilifanya mpango. Nafurahi kwamba nilifanya hivyo. Makala hiyo ilikuja wakati ufaao kwangu.
J. W., Uingereza
Baba na Mwana Waaminifu Nilisoma simulizi la “Kielelezo cha Uaminifu cha Baba Yangu” bila kutua. (Desemba 22, 1993) Makala hii imenisaidia kufanya mengi katika utumishi wa Mungu. Azimio imara la akina Davey (wote wawili baba na mwana), cha kumtumikia Yehova hadi kifo, kimehuisha azimio nililokuwa nalo nilipobatizwa miaka miwili iliyopita nikiwa na umri wa miaka 18. Natumaini makala kama hizi zaweza kuwagusa mioyoni vijana wengine wengi ulimwenguni pote.
C. M., Italia
Vipepeo Ningependa kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa ajili ya makala “Siku Moja Katika Maisha ya Kipepeo.” (Oktoba 8, 1993) Mke wangu nami tulikuwa tukistarehe katika Mbuga ya Kitaifa ya Zion mwezi uliopita. Tulikuwa tukisoma makala hii pamoja wakati kwa ghafula kipepeo kilitua mchangani na kupanua mabawa yake tambarare. Hatukuwa tumejua kamwe ni kwa nini walifanya hivyo! Makala hiyo ilitusaidia tuthamini uumbaji wa ajabu wa Yehova.
C. B., Marekani
Wazazi Wenye Hali ya Moyo Ibadilikayo Upesi Nilithamini ile makala ya “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Wazazi Wangu Huwa na Hali ya Moyo Ibadilikayo Upesi?” (Novemba 8, 1993) Hivi karibuni mama yangu amekuwa na hali ya moyo ibadilikayo upesi. Makala hiyo ilinisaidia nielewe kwamba magumu ya kiuchumi, pamoja na madaraka mengineyo, ni mambo makubwa yanayochangia hali yake ibadilikayo upesi. Sasa nitasaidia nitakapoweza na kumkumbatia na kumwambia kwamba nampenda.
T. B., Marekani
Sisi ni wazazi wa wavulana wawili, wenye umri wa miaka 7 na 12. Masuala kadhaa mliyotoa katika toleo hili yametokea katika nyumba yetu hivi karibuni, nasi tumekuwa tukijaribu—bila mafanikio—kuelezea wana wetu mambo. Makala hii kwa kweli imekuwa jibu la sala zetu. Tayari imesaidia hali yetu.
R. P. na A. P., Marekani