Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 3/22 kur. 25-27
  • Zawadi ya Mungu ya Usawaziko

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zawadi ya Mungu ya Usawaziko
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Huo Ni Nini? Nao Hufanya Kazi Namna Gani?
  • Kasoro za Utendaji wa Mfumo wa Ukumbi
  • Visababishi na Maponyo
  • Sikio Lako—Yule Mwasiliani Mkubwa
    Amkeni!—1991
  • Uwezo Wako wa Kusikia—Zawadi ya Kuthaminiwa Sana
    Amkeni!—1997
  • Ubongo Wako Hufanyaje Kazi?
    Amkeni!—1999
  • Thamini Uwezo Wako wa Pekee
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 3/22 kur. 25-27

Zawadi ya Mungu ya Usawaziko

“UNAKOSA usawaziko kwa sababu ya kuwa baharini kwa muda mrefu,” rafiki yangu akaniambia, “nao waweza kuendelea kwa siku kadhaa.” Ilikuwa mwezi wa Oktoba 1990, nami nilikuwa nimetoka tu kwenye meli na kuingia nchi kavu baada ya safari ya siku saba katika Karibea. Hata hivyo, jambo ambalo nilifikiri lingepita baada ya siku chache, limeendelea sasa kwa zaidi ya miezi mingi. Ilikuwa ni kana kwamba sikupata kamwe kushuka kutoka meli hiyo. Mfumo wangu wa ukumbi ulikuwa umeharibika, ule mfumo tata wa usawaziko wa sikio la ndani pamoja na miungano yao ya katikati kwenye ubongo.

Huo Ni Nini? Nao Hufanya Kazi Namna Gani?

Kitovu kinachokusawazisha kinapatikana sehemu ya chini ya ubongo wako inayoitwa shina la ubongo. Wakati u mwenye afya, unadumisha usawaziko wako kwa sababu ya ile mipwito inayopokewa kutoka kwa macho yako, misuli yako, na mfumo wako wa ukumbi.

Macho yako huliandalia shina la ubongo mfululizo wa habari zinazotolewa na hisi kuhusu mazingira yako ya nje. Hisi pokezi katika misuli yako huingiza katika ubongo wako habari juu ya aina ya sehemu unayotembea juu yayo au unayogusa. Lakini mfumo wako wa ukumbi ndio unaofanya kazi ukiwa mfumo wa kindani wa kukuongoza unaojulisha ubongo wako mahali mwili wako ulipo kwa uwiano na dunia na nguvu zayo za uvutano.

Mfumo wa ukumbi umefanyizwa kwa sehemu tano zinazoshughulika na usawaziko: mifereji tata ya nusu-duara na vifuko viwili. Ile mifereji ya nusu-duara huitwa mfereji mkuu, mfereji-lala, na mfereji mdogo (wa nyuma). Vile vifuko vidogo-vidogo viwili huitwa utricle na saccule.

Ile mifereji ya nusu-duara hulala ikielekeana ikifanyiza pembe, kama vile kuta na sakafu hukutana katika pembe ya nyumba. Hiyo mifereji ni mapito yafanyizayo mzingile uliofichwa katika mfupa mgumu wa fuvu la kichwa uitwao mfupa wa kulalia. Ndani ya mzingo huo wa mfupa kuna mzingile mwingine, uitwao mzingile wenye viwambo. Mwishoni mwa kila kifereji nusu-duara chenye viwambo, kuna kile ambacho kingeonekana kama uvimbe, kiitwacho ampulla. Katika sehemu ya ndani ya mzingile wenye viwambo kuna umaji-maji wa pekee uitwao limfundani. Na katika sehemu ya nje ya kiwambo, kuna umaji-maji ulio na muundo wa kikemikali ulio tofauti, uitwao perilimfu.

Sehemu hii iliyofura ya kifereji ina seli-nywele za pekee zilizo kama mafundo yaliyo juu ya masi gelatini iitwayo cupula. Unaposogeza kichwa chako upande wowote, ule umaji-maji wa limfundani hukawia kusonga pamoja na ile mifereji yenyewe; na hivyo umaji-maji huo hukunja ile sehemu iliyofura na yale mafundo ya nywele yaliyo ndani. Kusonga kwa yale mafundo ya nywele hutokeza mabadiliko katika tabia-umeme za seli-nywele, nako hupeleka ujumbe kwenye ubongo wako kupitia seli-neva. Jumbe husafiri si kutoka seli-nywele moja-moja hadi kwenye ubongo kupitia neva zinazokusanya habari tu bali pia kutoka kwenye ubongo hadi kwenye seli-nywele moja-moja kupitia neva zinazoeneza habari ili kutoa habari fidiaji wakati hilo lihitajiwapo.

Ile mifereji ya nusu-duara hubainisha mwendo wenye pembe au wa kuzunguka wa kichwa chako upande wowote, kama vile kukiinamisha mbele au nyuma, kukilaza upande mmoja au mwingine, au kukizungusha kushoto au kuume.

Kwa upande ule mwingine, hubainisha mchapuko nyoofu; hivyo huitwa vibaini vya nguvu za uvutano. Hivyo pia vina seli-nywele katika kile kiitwacho macula. Kwa mfano, kile kifuko kidogo aina ya succule, kingeweza kupelekea ubongo wako habari ambayo ingekupa hisia ya mchapuko wa kuelekea juu unapoinuliwa katika lifti. Kifuko cha aina ya utricle ndicho kibaini kikuu ambacho huitikia unaposafiri ndani ya gari na kuongeza mwendo kwa ghafula. Hupelekea ubongo wako habari ili kukupa ile hisia ya kusukumwa mbele au nyuma. Kisha ubongo wako huunganisha jumbe hizi pamoja na mipwito mingine ili kufanya maamuzi, kama vile jinsi ya kupepesa macho yako na kusogeza viungo mbalimbali vya mwili ili kuitikia mwendo wako. Hilo hukusaidia kudumisha mwelekeo wako.

Ni mfumo wa ajabu unaoheshimu Mbuni wao, Yehova Mungu. Hata wanasayansi watafiti hawawezi kuepuka kuvutiwa na muundo wao. A. J. Hudspeth, profesa wa biolojia na fisiolojia, aliandika katika gazeti Scientific American: “Kazi ya ziada, hata hivyo, yaweza tu kutia nguvu hisia ya mshangao juu ya unyetivu na utata wa chombo hiki kidogo cha kibiolojia.”

Kasoro za Utendaji wa Mfumo wa Ukumbi

Katika kisa changu tatizo la sikio langu la ndani lilichunguzwa na kupatikana kuwa otospongiosis au otosclerosis. Hii ni hali ambayo mfupa ambao katika huo mfumo wa ukumbi wa mtu hukaa, unakuwa mwororo au kama sponji. Kwa kawaida mfupa huu hudumu ukiwa mgumu sana, hata mgumu zaidi ya mifupa mingine ya mwili wako. Wakati unapoendelea kuwa mwororo, yadhaniwa kuwa kimeng’enya hutokezwa ambacho hupenya ndani ya umaji-maji wa sikio la ndani na kuliharibu kikemikali au kihalisi kuutia sumu umaji-maji huo. Hili laweza kusababisha ile hisia isiyo ya kawaida ya kuwa mwendoni kwa kuendelea ingawa waweza kuwa umesimama au umelala bila kusonga.

Kwangu mimi ilifanya sakafu iliyo chini yangu ionekane kana kwamba ilikuwa ikisonga kwa mwendo wa mawimbi nyakati nyingine hata kufikia theluthi moja ya meta juu. Nilipolala chini nilihisi kana kwamba nilikuwa nikilala katika sakafu ya mashua katikati ya bahari yenye mawimbi ya meta moja. Hisia hiyo haikuja na kutoweka kama nyakati za kuwa na kizunguzungu, lakini ilinipata na kuendelea muda wa saa 24 kila siku kwa miezi kadhaa mfululizo. Kitulizo pekee kilipatikana nilipokuwa sina fahamu nikiwa nimelala.

Visababishi na Maponyo

Kisababishi cha otospongiosis/otosclerosis bado hakijulikani, ingawa chaweza kuhusianishwa na urithi. Hiyo hali imekuwa ngumu kuchunguzwa na sayansi ya kitiba kwa sababu hiyo huonekana kuwa isiyo ya kawaida kwa wanadamu. Ni mara chache sana, ikitukia, hali hii inapowapata wanyama. Otospongiosis yaweza kutokeza mlio kama wa kengele katika sikio, kuhisi kichwa kikiwa kimejaa, kichwa kuwa chepesi, kuhisi ukosefu wa usawaziko, au aina mbalimbali za kizunguzungu. Hali hiyohiyo yaweza kusababisha kivumishi kilichoko katika sikio la kati kisisonge na kusababisha kupoteza uwezo wa kusikia. Ikiwa otospongiosis yafika kwenye kokilea, yaweza kusababisha upoteze uwezo wa kusikia kwa kuharibu utendaji wa neva.

Kuna maponyo kwa hali hii. Mengine yatia ndani upasuaji (ona Amkeni! la Julai 8, 1988, ukurasa 19, Kiingereza); mengine hujaribu kuzuia kuharibika kwa huo mfupa kwa kuuongezea kalsiamu na floridi. Kula vyakula visivyo na sukari hupendekezwa kwa kuwa sikio la ndani huhitaji sana damu yenye sukari. Kwa hakika, sikio la ndani huhitaji sukari iliyo mara tatu zaidi ya ile ihitajiwayo na sehemu ya ubongo ya ukubwa huo ili kulipa nguvu. Sikio lisilo na kasoro hushughulika na mabadiliko ya kawaida ya sukari katika damu kwa kufaa; lakini mara sikio linapoharibika, mabadiliko haya yaweza kukufanya uwe na kizunguzungu. Kafeini na alkoholi huonekana kuwa zenye madhara ikiwa sikio lako la ndani halifanyi kazi sawasawa. Ingawa kuwa katika ile meli, iliyotajwa mwanzoni mwa makala hii, hakukusababisha kikweli tatizo hili, mabadiliko katika halijoto, unyevu, na kawaida za kula vilianzisha ukosefu huo wa usawaziko.

Sikio lako la ndani hufanya mengi zaidi ya kufanya usikie. Kwa njia ya ajabu na ya kushangaza, hilo hukusaidia udumishe usawaziko wako. Muundo walo wapaswa ufanye tustaajabie kazi ya Mfanyi wetu, nayo yapasa iongeze uthamini kwa ajili ya Uumba wake.—Imechangwa.

[Michoro/Picha katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mfumo Wako wa Ukumbi Ulio wa Ajabu

Mwono wa Nje

MFEREJI MKUU

DIRISHA UMBO-YAI

KOKILEA

DIRISHA MVIRINGO

MFEREJI MDOGO

MFEREJI LALA

Mwono wa Ndani

MFUPA WA KULALIA

MZINGILE-VIWAMBO

AMPULLA

SACCULE

Kibaini mwendo wa ulalo

KOKILEA

Kiungo cha kusikia

MACULA

UTRICLE

CRISTA

Kibaini mwendo wa ulalo

Hupima mwendo wenye pembe

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki