Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/22 kur. 21-24
  • Uwezo Wako wa Kusikia—Zawadi ya Kuthaminiwa Sana

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uwezo Wako wa Kusikia—Zawadi ya Kuthaminiwa Sana
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sikio Lako la Nje Lenye Umaana
  • Sikio Lako la Kati—Ufundi wa Ajabu
  • Sikio Lako la Ndani Lenye Kustaajabisha
  • Ubongo Wako na Kusikia
  • Zawadi Inayopasa Kuthaminiwa Sana
  • Sikio Lako—Yule Mwasiliani Mkubwa
    Amkeni!—1991
  • Linda Uwezo Wako wa Kusikia!
    Amkeni!—2002
  • Thamini Uwezo Wako wa Pekee
    Amkeni!—2011
  • Zawadi ya Mungu ya Usawaziko
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/22 kur. 21-24

Uwezo Wako wa Kusikia—Zawadi ya Kuthaminiwa Sana

JIONI tulivu mashambani, mbali na kelele za ustaarabu, huandaa fursa ya kufurahia sauti nyororo za usiku. Upepo mwanana wapigapiga majani kwa utaratibu. Wadudu, ndege, na wanyama waongeza sauti zao za mbali. Ni hisi yenye kufurahisha kama nini kusikia sauti nyororo kama hizo! Je, waweza kuzisikia?

Uwezo wa mfumo wa kusikia wa binadamu unastaajabisha sana. Tumia muda wa nusu saa katika chumba ambacho hakirudishi mwangwi—chumba cha pekee chenye kuta zilizotengenezwa maalumu kufyonza kelele zote—na uwezo wako wa kusikia utaongezeka kiasi cha kukufanya ‘usikie sauti ambazo si za kawaida’ zinazotoka katika mwili wako. Mwanasayansi wa akustika F. Alton Everest aeleza ono hili katika kitabu The Master Handbook of Acoustics. Kwanza, mapigo yako mwenyewe ya moyo yaanza kusikiwa kwa sauti. Baada ya kukaa katika chumba hicho kwa karibu muda wa saa moja, wasikia damu yako ikipita katika mishipa yake. Hatimaye, ikiwa una masikio makali, “uvumilivu wako wa kuwa katika chumba hicho utathawabishwa kwa kusikia sauti isiyo ya kawaida ya zii kati ya ‘mapigo ya moyo’ na mmwagiko wa damu. Hiyo ni nini? Hiyo ni sauti ya visehemu vya hewa vikipiga dhidi ya viwambo vya masikio yako,” aeleza Everest. “Msogeo wa kiwambo cha sikio unaotokezwa na mapigo ya visehemu vya hewa ni mdogo sana—ni 1/100 tu ya sehemu ya milioni ya sentimeta!” Hiki “ndicho chanzo cha kusikia,” kiwango chako cha chini kabisa cha kugundua sauti. Uwezo wa juu zaidi ya hapo wa kusikia usingekuwa na faida yoyote, kwa sababu sauti ndogondogo zingemezwa na sauti ya mwendo tu wa vipande vya hewa.

Kusikia kunawezekana kwa sababu ya ushirikiano wa sikio la nje, la kati, na la ndani pamoja na uwezo wa mfumo wetu wa neva na ubongo wa uainishaji na utambuzi. Sauti husafiri kupitia hewa kwa namna ya mawimbi ya mtikisiko wa kanieneo. Mawimbi haya husukuma kiwambo chetu cha sikio mbele na nyuma, na mwendo huu, hatimaye huhamishwa kutoka sikio la kati hadi sikio la ndani. Hapo mwendo huo hubadilishwa kuwa mipwito ya neva, ambayo ubongo hufasiri kuwa sauti.a

Sikio Lako la Nje Lenye Umaana

Sehemu ya nje ya sikio yenye kunyumbulika na ambayo imevingirika inaitwa pina. Hiyo pina hukusanya sauti, lakini hufanya zaidi ya hilo. Je, umepata kujiuliza ni kwa nini sikio lako lina mikunjo yote hiyo midogo-midogo? Mawimbi ya sauti yafikayo katika maeneo tofauti ya pina hurekebishwa kwa ustadi mwingi kulingana na jinsi ilivyofikia. Ubongo una uwezo wa kufasiri tofauti hizo ndogondogo na kujua mahali pa chanzo cha sauti. Ubongo hufanya hivyo kwa kuongezea kulinganisha wakati na uzito wa sauti kadiri iingiavyo katika masikio yako.

Ili kutoa kielezi cha jambo hili, piga vidole vyako upelekapo mkono juu na chini mbele tu ya mtu ambaye amefunga macho. Ingawa vidole vyabaki katika umbali ulio sawa kutoka kila sikio, ataweza kusema ikiwa sauti yatoka juu, chini, au mahali pengine popote katikati. Kwa hakika hata mtu mwenye sikio moja linalosikia vizuri aweza kutambua sauti vizuri sana.

Sikio Lako la Kati—Ufundi wa Ajabu

Kazi ya msingi ya sikio la kati ni kuhamisha mitetemeko ya kiwambo chako cha sikio kwenda kwa umajimaji ambao hujaza sikio lako la ndani. Umajimaji huo ni mzito sana kuliko hewa. Hivyo, kama ilivyo kweli kwa mwendesha-baiskeli anayeenda juu ya kilima chenye mwinuko mkali, ‘gia ifaayo’ inatakiwa ili kuwasilisha nishati ya sauti vizuri kadiri iwezekanavyo. Katika sikio la kati, mitetemeko ya kiwambo cha sikio husafirishwa na mifupa mitatu midogo, ambayo kwa kawaida huitwa nyundo, kifuawesikio, na stapi kwa sababu ya miundo yao. Mwungano huu mdogo wa kiufundi wafikia ‘gia ifaayo’ ambayo inafaa kabisa sikio la ndani. Inakadiriwa kwamba bila hii, asilimia 97 ya nishati ya sauti ingepotea!

Kuna misuli midogo miwili laini iunganishwayo kwa kiunzi hiki katika sikio lako la ndani. Katika muda wa sehemu ya mia ya sekunde baada ya sikio lako kusikia kitu chenye sauti ya juu, misuli hii hujikaza yenyewe, ikizuia sana mwendo wa kiunzi hiki na hivyo ikizuia uwezekano wowote wa jeraha. Tendo hili jepesi ni la haraka sana kiasi cha kukukinga kutokana na sauti kubwa ambazo hutokea katika asili, ingawa si kutokana na zote ambazo hutokezwa na mitambo na kifaa cha kielektroni. Zaidi ya hilo, misuli hiyo midogo yaweza kubaki hivyo ikiwa imelinda kwa dakika kumi tu. Lakini hili lakupa nafasi ya kukimbia kutoka kwenye kelele hiyo. Kwa kupendeza, uongeapo, ubongo wako hupeleka ishara kwa misuli hii ili kupunguza uwezo wako wa kusikia, ili kwamba sauti yako mwenyewe isiwe kubwa sana kwako.

Sikio Lako la Ndani Lenye Kustaajabisha

Sehemu ya ndani ya sikio lako ihusikayo na kusikia imo ndani ya koa, huitwa hivyo kutokana na umbo lake la konokono. Kasha lenye kulinda mitambo yake iliyo laini ni mfupa ulio mgumu sana katika mwili wako. Katika sikio la ndani kuna basilar membrane, ambayo ni moja kati ya tishu kadha zinazogawanya urefu wa koa katika mifereji. Kando ya basilar membrane ipo ogani ya Korti, ambayo hutegemeza hair cells—ambazo ni chembe za neva ambazo zina miisho kama nywele zinazosambaa hadi katika umajimaji ambao hujaza koa.

Mwendo wa mtikisiko wa mifupa ya sikio la ndani utikisikapo dirisha duaradufu la koa, husababisha mawimbi katika umajimaji huo. Mwendo huu husukuma tando, kama vile viwimbi katika kidimbwi husukuma majani yaeleayo juu na chini. Mawimbi hukunja basilar membrane katika sehemu inayolingana na kasimawimbi ihusikayo. Zile hair cells katika sehemu hizo husugua dhidi ya tectorial membrane iliyofunika. Mgusano huu huchochea hair cell, nazo hutokeza mipwito na huituma katika ubongo wako. Kadiri sauti iwavyo kubwa, ndivyo hair cells zichochewavyo na zinachochewa na pia kwa haraka zaidi. Hivyo, ubongo hutambua sauti kubwa.

Ubongo Wako na Kusikia

Ubongo wako ndiyo sehemu muhimu zaidi katika mfumo wa kusikia. Una uwezo wa kutisha wa kugeuza habari nyingi sana inazozipokea katika umbo la mipwito ya neva kuwa hisi ya akili ya sauti. Kazi hii kubwa ya ubongo huonyesha kwa wazi kiungo maalumu kati ya mawazo na kusikia, kiungo kinachosomwa katika taaluma ijulikanayo kuwa psychoacoustics. Kwa mfano, ubongo wako wakuwezesha kusikia mazungumzo fulani hususa kati ya mengi katika chumba chenye msongamano. Maikrofoni haina uwezo huu mrekodio wa kanda uliofanywa katika chumba hicho hauwezi kueleweka.

Kero isababishwayo na kelele zisizotakiwa huonyesha upande mwingine wa kiungo hiki. Bila kujali sauti ni ndogo kiasi gani, ikiwa waweza kuisikia hata kama ni kidogo wakati usipoitaka, yaweza kukera. Kwa mfano, uzito wa sauti itokezwayo na bomba la maji lenye kuvuja ni kidogo sana. Lakini waweza kupata kwamba inaudhi kabisa ikiwa, katika usiku wa manane, itaendelea kukufanya uwe macho!

Kwa kweli, hisia-moyo zetu zimefungamanishwa karibu sana na hisi zetu za kusikia. Fikiria tu matokeo yenye kuambukiza ya kicheko chenye uchangamfu, au shauku ifanyizwayo na neno litolewalo kwa moyo mweupe la shauku au kusifu. Hali kadhalika, kiasi kikubwa cha kile tujifunzacho kwenye akili chapatikana kupitia masikio yetu.

Zawadi Inayopasa Kuthaminiwa Sana

Siri nyingi zenye kuvutia sana za kusikia kwetu bado hazijagunduliwa. Lakini uelewevu wa kisayansi ambao umepatikana waongeza uthamini wetu kwa akili na upendo uonyeshwao katika hilo. “Katika kuchunguza mfumo wa kusikia wa kibinadamu kwa kina,” aandika mchunguzi wa akustika F. Alton Everest, “mtu avutwa kufikia mkataa kwamba kazi zake na miundo yake tata huonyesha kwamba mtu fulani mwenye akili aliubuni.”

Mfalme Daudi wa Israeli la kale hakuwa na ujuzi wa kisayansi ambao unapatikana leo juu ya utendaji wa masikio yetu. Hata hivyo, alifikiria kwa makini mwili wake na zawadi zake nyingi na alimwimbia Mfanyi wake hivi: “Nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu.” (Zaburi 139:14) Uchunguzi wa kisayansi juu ya maajabu na mafumbo ya mwili, kutia ndani kusikia, waongeza uthibitisho kwamba Daudi alikuwa sahihi—tulibuniwa na Muumba mwenye hekima na upendo!

[Maelezo ya Chini]

a Ona Amkeni! la Januari 22, 1990, ukurasa wa 18-21 la Kiingereza.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Msaada kwa Walioharibika Masikio

Kuwa mahali penye makelele sana kwa muda mrefu husababisha kuharibika kwa uwezo wa kusikia. Kujiweka kwenye muziki wenye makelele au kufanya kazi mahali penye kifaa chenye kelele bila ya kuwa na kitu cha kuzuia kelele hakustahili uharibifu kama huu. Visaidizi vya kusikia vyaweza kuandaa kwa kiasi fulani msaada kwa wale wenye matatizo ya kusikia, au hata kwa baadhi ya watu waliozaliwa viziwi. Kwa watu wengi, vifaa kama hivyo vyaweza kuwarudishia uwezo wa kusikia sauti tofauti-tofauti. Baada ya kuwekewa vifaa vya kusaidia kusikia kwa mara ya kwanza, mwanamke mmoja aligundua sauti isiyo ya kawaida nje ya dirisha la jiko lake. “Walikuwa ndege!” alisema kwa mshangao. “Sikuwa nimewasikia hao ndege kwa miaka kadhaa!”

Hata bila ya kuharibika sana, uzee mara nyingine hupunguza uwezo wetu wa kugundua sauti kali. Kwa kusikitisha, hii yatia ndani kasimawimbi za konsonanti—sauti ambazo mara nyingi ni muhimu sana katika kuelewa usemi. Kwa hiyo, watu waliozeeka, waweza kupata kwamba kuwasiliana kwa mdomo kwaweza kuvurugwa na sauti za kawaida za nyumbani, kama zile zitokezwazo na maji au kukunja karatasi, kwani hizo huwa na kasimawimbi za juu ambazo huvuruga konsonanti. Vifaa vya kusaidia kusikia vyaweza kuandaa kitulizo kwa kiasi fulani, hata hivyo pia vina hasara zake. Jambo moja ni kwamba, vifaa bora vya kusaidia kusikia vyaweza kuwa ghali sana—ghali kiasi cha kwamba haviwezi kununuliwa na mtu wa kawaida katika mabara mengi. Kwa vyovyote, hakuna kifaa cha kusaidia kusikia kinachoweza kukurudishia kwa ukamili uwezo wako wa kusikia. Hivyo basi, kitu gani kinaweza kufanywa?

Kuonyesha ufikirio kwaweza kusaidia sana. Kabla ya kuongea na mtu aliyepoteza uwezo wa kusikia, hakikisha kwamba ajua uko karibu kusema kitu fulani. Jaribu kumwangalia mtu huyo. Hilo humruhusu kuona miendo ya mwili wako na ya midomo yako ili aweze kusikia vizuri kabisa konsonanti zilizo katika maneno yako. Ikiwezekana, mkaribie zaidi huyo mtu, ongea kwa utaratibu na kwa wazi; usipige kelele. Kwa kweli, sauti kubwa huumiza sana wengi wenye matatizo ya kusikia. Ikiwa sentensi haikueleweka, jaribu kuiunda tena badala ya kuirudia. Hali kadhalika, ikiwa kusikia kwako si kuzuri kama kulivyokuwa, waweza kufanya iwe rahisi kwa wengine wawasiliane nawe kwa kumkaribia zaidi mtu anayeongea na kuwa mwenye subira. Jitihada hizi za ziada zaweza kutokeza maendeleo katika mahusiano na zaweza kukusaidia upatanishwe ifaavyo na mazingira.

[Picha]

Uongeapo na mtu aliyepoteza uwezo wa kusikia, mwangalie na uongee kwa utaratibu na kwa wazi

[Michoro katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sikio Lako

Pina

Mfereji sikivu

Kiwambo cha sikio

Nyundo

Kifuawesikio

Stapi

Dirisha duara

Dirisha duaradufu

Koa

Neva sikivu

Ogani ya Korti

Neva sikivu

Hair cells

Tectorial membrane

Nyuzi za neva

Basilar membrane

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki