Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 4/8 kur. 12-15
  • Unaweza Kuboresha Kumbukumbu Lako

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Unaweza Kuboresha Kumbukumbu Lako
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kukumbuka Majina ya Watu
  • Jinsi ya Kukumbuka Orodha Mbalimbali
  • Kukumbuka Usomayo
  • Unaweza Kuboresha Kumbukumbu Lako!
    Amkeni!—2009
  • Jinsi ya Kuboresha Kumbukumbu Lako
    Amkeni!—1995
  • Ubongo Wako Hufanyaje Kazi?
    Amkeni!—1999
  • Unaweza Kuboresha Kumbukumbu Yako
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 4/8 kur. 12-15

Unaweza Kuboresha Kumbukumbu Lako

“Nina kumbukumbu baya sana.” Je, umewahi kusema hivyo? Ikiwa ndivyo, usikate tamaa. Madokezo machache yaliyo rahisi pamoja na jitihada kidogo zaweza kuleta mabadiliko ya ajabu. Usiupuuze uwezo wa ubongo wako. Uwezo wao mbalimbali washangaza.

UBONGO hutimizaje kazi mbalimbali zilizo za ajabu? Katika miaka ya majuzi ubongo umechunguzwa kwa ukaribu kuliko wakati mwingine wowote. Lakini ingawa ufahamu wenye kina unakua, bado twajua machache sana juu ya jinsi ubongo hasa utimizavyo kazi mbalimbali.

Jinsi tujifunzavyo na kukumbuka mambo ni jambo ambalo halijafahamika wazi, lakini watafiti wanajaribu kufumbua fumbo hili. Zihusikazo katika kujifunza na kukumbuka ni nuroni zinazokisiwa kuwa bilioni 10 hadi bilioni 100, zilizo katika ubongo. Lakini kuna angalau miungano mara elfu kumi zaidi kati ya nuroni. Nadharia moja ni kwamba miungano, au sinepsia, ipatapo nguvu kwa kutumiwa, ndipo kujifunza kufanyikapo.

Tuzeekapo, uwezo wa ubongo huenda ukapungua; maitikio yetu huenda yakapungua. Seli za ubongo hazijifanyi upya zenyewe, na yaonekana kwamba watu wazima huendelea kupoteza kadhaa. Lakini kadiri tutumiavyo ubongo wetu, ndivyo tuwezavyo kuhifadhi uwezo wetu wa kiakili kwa muda mrefu zaidi.

Mwelekeo wetu wa kiakili huathiri ubongo wetu. Mtazamo wenye kutumainia mazuri, na wenye furaha huboresha utendaji wa ubongo katika umri wowote ule. Mkazo fulani waweza kunufaisha, lakini mkazo wa muda mrefu au mwingi sana waweza kuzuia utendaji wa ubongo. Mazoezi ya kimwili yaweza kusaidia kupunguza mkazo wa kiakili.

Hata hilo liwe jambo la kutia moyo jinsi gani bado huenda tukasahau mambo ya maana, licha ya umri wetu. Je, twaweza kufanya maendeleo? Eneo moja ambapo wengi hupata ugumu ni katika kukumbuka majina ya watu ambao sisi hukutana.

Kukumbuka Majina ya Watu

Madokezo machache rahisi yaweza kukusaidia sana ukumbuke majina vizuri zaidi. Kupendezwa na mtu husaidia. Jina la mtu ni la maana kwake. Mara nyingi huenda tusilikumbuke jina kwa kuwa hatukulielewa vizuri tulipolisikia kwa mara ya kwanza. Hivyo ujulishwapo kwa mtu, lifahamu jina vizuri. Mwombe huyo mtu alirudie au hata kuliendeleza herufi kwa herufi ihitajiwapo. Litumie mara kwa mara katika mazungumzo yako. Umuagapo, mwite kwa jina lake. Utashangazwa jinsi madokezo hayo machache yatakavyokusaidia.

Jambo jingine liwezalo kuongeza kumbukumbu lako la majina ni kuhusianisha jina la mtu na kitu uwezacho kupiga picha akilini mwako. Kuunganisha utendaji fulani katika picha hiyo kwaweza kusaidia hata zaidi.

Huenda majina mengi yasiwe na maana yoyote kwako, hivyo utahitaji kutumia neno lifananalo na jina hilo. Si lazima neno la badala unalotumia liwe sawa kabisa na jina lenyewe. Kumbukumbu lako litakumbuka hilo jina kwa kulihusianisha na neno la badala. Ufanyizapo maneno na picha zako mwenyewe, utakumbuka vizuri zaidi.

Wahitaji kujizoeza hilo kwa bidii kwa muda, lakini kwa kweli lina matokeo. Harry Lorayne aeleza hili katika kitabu chake How to Develop a Super-Power Memory, naye alikitumia pindi nyingi hadharani. Yeye asema: “Mara nyingi nimejulishwa kwa watu kati ya mia moja na mia mbili kwa muda wa dakika kumi na tano au unaopungua huo, bila kusahau jina hata moja!”

Jinsi ya Kukumbuka Orodha Mbalimbali

Waweza kuboreshaje uwezo wako wa kukumbuka orodha ya vitu visivyohusiana? Njia rahisi ni ile ya kuunganisha vitu. Hivi ndivyo ifanyavyo kazi: Ona akilini kila kitu katika orodha kisha uhusianishe picha ya kitu cha kwanza katika orodha na picha ya kitu cha pili, kisha fanya vivyo hivyo kwa kitu cha pili na cha tatu, na kuendelea.

Kwa kielelezo, wahitaji kununua vitu vitano kutoka kwa duka: maziwa, mkate, globu, vitunguu, na aisikirimu. Anza kwa kuhusianisha maziwa na mkate. Wazia kuyamwaga maziwa kutoka kwenye mkate. Ingawa picha hiyo huenda ikawa ya kipuuzi, itasaidia kuliweka jambo hilo wazi kwenye kumbukumbu lako. Pia, jaribu kutia utendaji fulani kwenye picha ya akilini unaokuhusisha katika kuyamwaga maziwa.

Baada ya kuhusianisha maziwa na mkate, songa mbele hadi kwenye kitu kifuatacho, globu. Waweza kuhusianisha mkate na globu kwa kuwazia ukijaribu kuuweka ule mkate kwenye soketi ya umeme. Kisha husianisha globu na kitunguu kwa kujiona mwenyewe ukiambua globu kubwa na wakati ule ule ukitoa machozi. Bila shaka, ni afadhali ukihusianisha vitu hivyo wewe mwenyewe. Je, waweza kuhusianisha vile vitu vya mwisho, vitunguu na aisikirimu? Labda waweza kujiwazia ukila aisikrimu ya kitunguu!

Jaribu kuona ikiwa waweza kukumbuka hiyo orodha. Kisha tahini kumbukumbu lako kwa kutumia orodha yako mwenyewe. Ifanye iwe ndefu utakavyo. Kumbuka, ili kufanya mahusianisho yawe yenye kukumbukika, waweza kuyafanya yawe yenye ucheshi au hata ya kipuuzi au yasiyo ya kawaida. Jaribu kutia ndani utendaji katika picha, na uweke kitu kimoja mahali pa kingine.

Huenda wengine wakapinga kwamba njia hii inachukua muda mrefu kuliko kuikumbuka orodha yenyewe tu. Hata hivyo, inachukua muda mrefu zaidi kuieleza kuliko inavyochukua kuitumia. Ukiwa umefanya mazoezi, utafanya mahusiano upesi zaidi, na kumbukumbu lako, pamoja na uharaka wako wa kujifunza, utakuwa bora zaidi kuliko ukijaribu kujifunza bila kutumia njia fulani. Watu 15 walipoombwa kukumbuka orodha ya vitu 15 mbalimbali bila kutumia njia yoyote, wastani wa matokeo yao ulikuwa 8.5. Wakitumia ile njia ya kuunganisha picha za mahusiano katika orodha nyingine, kikundi hichohicho kilikuwa na wastani wa 14.3. Bila shaka, ukikumbuka kubeba orodha iliyoandikwa ya vitu hivyo uendapo kununua vitu, ungekuwa na alama 15—asilimia 100!

Kukumbuka Usomayo

Katika wakati huu wenye habari nyingi, eneo jingine tuhitajilo msaada ni kusoma kwa njia yenye mafanikio. Kujifunza ni jambo muhimu shuleni, kwenye biashara, kwa ajili ya maendeleo ya kibinafsi, na katika kujitayarisha ili kusema hadharani. Kwa kuongezea, Mkristo lazima aweke kando wakati kwa ajili ya funzo la Biblia la kibinafsi.—Yohana 17:3.

‘Lakini mimi hupata ugumu wa kukumbuka yale ambayo nimejifunza,’ huenda ukasema. Ni nini liwezalo kufanywa? Kujifunza kufanya wakati wako wa funzo uwe wenye manufaa kwaweza kukusaidia kukumbuka uliyosoma. Hapa pana madokezo kadhaa.

Ujifunzapo, mpango wa kibinafsi ni muhimu. Uwe na vitabu, kalamu, na karatasi karibu. Jaribu kusoma mahali penye kupendeza pasipo na vikengeusha-fikira na penye nuru ya kufaa. Zima redio na televisheni.

Uwe na wakati wa kawaida kwa ajili ya funzo. Kwa wengine, kujifunza kila siku kwa vipindi vifupi kwaweza kuwa na matokeo badala ya kutumia wakati mwingi kwenye funzo moja. Ni vizuri kugawanya wakati wako uwe vipindi. Badala ya kujifunza kwa muda wa saa mbili bila kuacha, ingekuwa afadhali kugawanya wakati huo uwe vipindi vya dakika 25 hadi 40 kila kimoja, kukiwa na dakika chache katikati ya vipindi. Utafiti umeonyesha kwamba hili huchangia kiwango cha juu zaidi cha kukumbuka.

Amua habari unayotaka kusoma wakati wa kipindi cha kujifunza. Hili husaidia kukaza fikira. Kabla ya kuanza kusoma kitabu, chukua dakika chache kukipitia. Tazama kichwa. Chunguza yaliyomo, ambayo hutoa muhtasari wa kitabu chote. Kisha usome dibaji au utangulizi. Hapa kusudi au maoni ya mwandishi yaweza kutajwa.

Kabla ya kuanza kusoma sura fulani, ipitie. Tazama vichwa vidogo, picha, chati, mihtasari, mafungu ya kwanza na ya mwisho. Tupia jicho mstari wa kwanza wa kila fungu. Sentensi hizi kwa kawaida huwa na mambo makuu. Elewa habari kwa ujumla. Jiulize maswali: ‘Mwandishi alikusudia kuthibitisha nini? Naweza kufaidikaje na habari hii? Ni nini yaliyo mambo makuu?’

Kukaza fikira ni kwa maana sana. Wapaswa kujihusisha kabisa. Siri ni kufanya wakati wako wa funzo uwe wenye kupendeza iwezekanavyo. Chochea idili kwa kufikiria sehemu zenye faida maishani za habari hiyo. Ona mambo akilini. Tumia hisia zako kwa kuwazia harufu, ladha, na mguso ikiwa habari yapatana na mambo haya.

Baada ya kuelewa kusudi la habari, sasa uko tayari kunakili mambo machache. Kuandika muhtasari mzuri kwaweza kuongeza ufahamu wako na kumbukumbu la habari hiyo. Maandishi hayahitaji kuwa sentensi nzima nzima lakini yapaswa kuwa maneno au mafungu ya maneno makuu ambayo yatakusaidia kukumbuka mawazo makuu.

Kufahamu habari hakumaanishi kwamba utakumbuka mambo yote wakati ujao. Ukweli ni kwamba katika muda wa saa 24 za kwanza baada ya kujifunza, karibu asilimia 80 ya habari hiyo huenda ikasahaulika, angalau kwa muda fulani. Hilo laonekana lenye kuvunja moyo, lakini kiwango fulani au sehemu kubwa ya ile asilimia 80 yaweza kukumbukwa kwa kurudia habari ile. Baada ya kila kipindi cha kujifunza, pitia habari kwa dakika chache. Ikiwezekana, pitia tena siku moja baadaye, kisha juma moja baadaye, na kisha mwezi mmoja baadaye. Kutumia madokezo haya kwaweza kukusaidia kufaidika zaidi kutokana na wakati wako wenye thamani sana wa kujifunza na kukumbuka uliyokuwa umejifunza.

Kwa hiyo usiupuuze uwezo wa ubongo wako. Uwezo wako wa kukumbuka mambo waweza kuboreshwa. Mwanasayansi mmoja aliurejezea ubongo kuwa “kitu kigumu zaidi kufahamika katika ulimwengu wote mzima ambacho bado twakivumbua.” Ni sifa kwa hekima yenye kutisha na nguvu za Muumba wao, Yehova.—Zaburi 139:14.

[Mchoro katika ukurasa wa 15]

Ili kukumbuka orodha mbalimbali, tumia ile njia ya kuunganisha vitu: Fanyiza picha akilini ya kila kitu. Kisha husianisha picha ya kitu cha kwanza na picha ya kitu cha pili na kuendelea

Orodha ya vitu vya kununuliwa:

1. Maziwa 1 na 2 vimeunganishwa

2. Mkate 2 na 3 vimeunganishwa

3. Globu 3 na 4 vimeunganishwa

4. Vitunguu 4 na 5 vimeunganishwa

5. Aisikirimu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki