Jinsi ya Kuboresha Kumbukumbu Lako
WEWE una kumbukumbu zuri mno! Je, unaona hilo likiwa gumu kuamini? Fikiria kwa muda mfupi mambo mengi ambayo unakumbuka mara moja: mandhari za utotoni, majina ya marafiki na watu wa ukoo—hata wahusika wa kutungwa katika vitabu na televisheni, melodia na maneno ya nyimbo uzipendazo sana, alfabeti, jinsi ya kuhesabu, maelfu ya maneno. Ndiyo, tayari umeonyesha uwezo wa kukumbuka mamilioni ya mambo!
‘Lakini ikiwa kumbukumbu langu ni ajabu kubwa hivyo,’ huenda ukajiuliza, ‘kwa nini mimi husahau mambo? Kwa nini mara kwa mara mimi hupoteza vitu? Kwa sababu gani nifikapo dukani husahau nilichoenda kununua? Na vibaya zaidi, kwa nini huwa vigumu kwangu kukumbuka majina—bila kutaja nambari za simu na miadi?’ Haya ni mahangaiko ya kawaida. Hata hivyo, kumbukumbu lako ni bora zaidi sana kuliko uwezavyo kutambua—na linaweza kuboreshwa.
Sababu Inayofanya Tusahau
Mungu alituumba tukiwa na uwezo wa ajabu wa kukumbuka. Kwa kufaa, ubongo hukaa katika kile kirejezewacho kishairi katika Biblia kuwa “bakuli la dhahabu”—kiwekeo chenye thamani cha kumbukumbu. (Mhubiri 12:6) Kwa nini, basi, kumbukumbu letu huelekea kukosa kufanya kazi nyakati fulani? Mara nyingi ni kwa sababu ya ukosefu wa upendezi. Mwongoza kwaya ajulikanaye sana Arturo Toscanini aliongoza nyimbo zote kutoka kumbukumbu. Mwanabiashara tajiri Charles Schwab angeweza kukumbuka majina ya wafanyakazi 8,000. Lakini walikumbuka mambo hivyo kuhusiana na habari isiyohusisha maeneo yao ya upendezi? Yaelekea sivyo. Basi, haidhuru hata kumbukumbu lako liwe zuri kadiri gani, itakuwa vigumu mno kwako kujifunza na kukumbuka mambo yasiyokupendeza.
Jambo jingine ambalo laweza kusababisha tusahau ni badiliko la hali au mahali. Mambo hukumbukwa vyema zaidi katika mahali ambapo mtu alijifunza. Mwanamume mmoja aliyekuwa akitembelea mahali ambapo alilelewa alisalimiwa na mwanamke asiyemjua. Kiasili, yeye alidhani kwamba lazima alikuwa mtu aliyekua pamoja naye katika ujirani wake wa zamani. Hata hivyo, akatambua ghafula kwamba alikuwa mtu ambaye alikuwa akimwona kila siku—mfanyakazi mwenzake wa wakati huo! Bila kujua yeye pia alikuwa akizuru sehemu hiyo hiyo. Kumwona katika kikao tofauti kulimfanya amsahau kwa muda.
Kwa uzuri, huhitaji kukumbuka mamilioni ya habari ndogo-ndogo zinazoingia akilini mwako kila siku; nyingi zazo ni mambo yasiyokuwa na maana. Hata hivyo, jambo liwapo la maana, waweza kujifunza kulikumbuka. Jinsi gani? Kwa kulitolea uangalifu wa pekee.
Jinsi ya Kukumbuka
Tuseme unahitaji kupiga simu ya maana leo usiku. Ikiwa hutafanya zaidi ya kufikiria akilini upesi tu, yaelekea utasahau. Kwa hiyo tua na ufikiri juu ya kupiga hiyo simu. Kitabu Instant Recall—Tapping Your Hidden Memory Power, kilichoandikwa na Jeff Budworth, hupendekeza kuchukua “dakika kadhaa, si sekunde kadhaa,” ili kukazia habari ya maana katika kumbukumbu. Jiambie kwamba unanuia kikweli kupiga hiyo simu. Ukiwa umetoa uangalifu wa pekee kwa jambo hili, hutaelekea kulisahau.
Ingawa hivyo, ni zipi baadhi ya njia nyingine, ambazo kwazo waweza kutoa uangalifu wa pekee kwa vitu usivyotaka kusahau? Madokezo yafuatayo, yakitumiwa, yaweza baada ya muda mfupi kuwa ya kawaida kwako.
Pata habari yako katika njia yenye kueleweka: Kompyuta haiwezi kuhifadhi habari kwa usahihi isipokuwa kwanza habari hiyo iliingizwa ifaavyo. Kwa kadiri kubwa, ndivyo ilivyo na kumbukumbu letu. Kwa kielelezo, fikiria kuhusu kujifunza majina. Dakt. Bruno Furst aonelea hivi katika kitabu chake Stop Forgetting: “Tusipolishika jina vizuri na kwa usahihi, hatuwezi kusema juu ya kukumbuka au kusahau. Hatuwezi wala kukumbuka wala kusahau jambo ambalo hatukulijua kamwe. Kwa hivyo hatua yetu ya kwanza yapasa kuwa kulishika jina katika njia ambayo hakuna shaka lolote linalobaki kuhusu matamshi yalo au mwendelezo walo.” Mtu akinong’ona jina lake wakati wa kujulishwa kwako, usisite kumuuliza mtu huyo kulirudia. Uliza jinsi jina hilo huendelezwa.
Ona akilini: Jaribu kuwazia kile unachojaribu kukumbuka. Kuna kazi fulani usiyopaswa kusahau? Basi jiwazie ukiifanya. Kadiri uongezavyo habari katika picha hii ya akilini, ndivyo utakavyokumbuka kwa urahisi zaidi.
Kuona akilini kwaweza pia kukusaidia kushirikisha mambo yasiyohusiana. Kwa kielelezo, wazia kwamba ni lazima ukumbuke kununua maziwa na dawa ya kusugulia meno. Huenda ukajaribu kubuni picha ya akilini ya ng’ombe anayesugua meno yake. Hii si picha ambayo yaelekea utasahau, hata ujaribu jinsi gani!
Taja kwa maneno: Kujisemea kwa sauti kubwa, ‘lazima nimpigie simu John leo usiku,’ ni njia nyingine ya kukusaidia kukumbuka kufanya jambo hilo. Kwa upande ule mwingine, je, wewe husahau kama umefunga mlango au kuzima jiko la kuokea? Kitabu How to Improve Your Memory, kilichoandikwa na Dakt. James D. Weinland, chasema hivi: “Tatizo laweza kutatuliwa kwa kutaja kwa maneno kazi tuzifanyapo . . . Unapotia saa majira na kuweka wakati wa kulia kwa kengele, sema, ‘nimetia saa majira na kuweka wakati wa kulia kwa kengele.’ Unapofunga mlango jisemee, ‘nimefunga mlango.’” Huenda ukahisi unafanya upuzi, lakini yaweza kukusaidia kukumbuka.
Kuza upendezi katika mada yako: Huenda usivutwe kiasili kwa mada fulani, lakini ikiwa unajikumbusha kwamba unahitaji kujifunza hiyo habari na matokeo ya kukosa kuikumbuka, kujifunza kutakuwa rahisi. Isitoshe, kadiri unavyojifunza zaidi kuhusu mada yoyote, ndivyo izidivyo kuwa yenye kukupendeza. Yasema Biblia: “Maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.”—Mithali 14:6.
Hesabu: Tuseme unahitajika kwenda na vitu kadhaa kazini kesho asubuhi. Kwa kutambua idadi hususa ya vitu upaswavyo kuchukua, hutaelekea kuacha chochote.
Panga: Ikiwa wataka kununua vitu kadhaa katika duka la chakula, jaribu kuviweka katika mpangilio. Kwa kielelezo, huenda ukaamua kwamba unahitaji kununua vitu vitatu vinavyotokana na maziwa ya ng’ombe, vitu viwili kutokana na nyama, na vitu vingine viwili. Kupanga vitu kwa njia hii hukusaidia kutoa uangalifu zaidi.
Utumie na uurudie: Sikuzote utakumbuka jina lako mwenyewe, alfabeti, au jinsi ya kutumia uma au penseli. Kwa nini? Kwa sababu umetumia ujuzi huo tena na tena. Utumizi wa mara kwa mara hutia nguvu kumbukumbu, ukilifanya likumbukwe kwa urahisi. Basi, muda fulani fulani, rudia au tumia kiakili mambo unayotaka kukumbuka. Baada ya kujulishwa kwa mtu fulani, jaribu kutumia jina lake mara kadhaa. Au baada ya kujifunza habari mpya, jaribu kuitumia katika mazungumzo yako, ukiangalia usisikike kama kwamba unajigamba.
Thamani ya Kukumbuka
‘Lakini kwa nini kujiingiza katika taabu yote hii?’ huenda ukauliza. ‘Je, haingekuwa rahisi kuandika tu?’ Kalenda, orodha, saa zenye kengele, maandishi uliyojiandikia—yote haya hutumikia kusudi nzuri. Hata hivyo, nyakati fulani ni jambo lisilotumika kuandika, kama vile wakati unapokutana na watu katika kikao cha watu wengi. Na wakati orodha yako ya ununuzi iliyofikiriwa vizuri inahitaji kufanyiwa marekebisho, mara nyingi penseli haiwi karibu. Isitoshe, orodha zaweza kupotea kwa urahisi. Na namna gani ukisahau kuangalia kalenda yako? Hivyo basi kuzoeza kumbukumbu lako ni jitihada inayostahiki.
Kadiri ufanyavyo mazoezi, ndivyo utakavyozidi kuhitaji jitihada kidogo kukariri. Kwa kweli, baada ya muda mfupi utapata kwamba unapendelea kukariri mambo kuliko kuyaandika. Ingawa hivyo, usihofu kwamba huenda kwa njia moja au nyingine ukavuruga akili yako na kuiacha ikiwa haina matokeo sana au isiyoweza kubuni. Akili, kama vile msuli, hupata nguvu zaidi na kuwa yenye matokeo zaidi kwa kutumiwa. Asema Dakt. Joan Minninger: “Watu walio wengi wanafikiri juu ya kumbukumbu la muda mrefu kuwa kabati kubwa ya kuwekea nguo ambayo yahitaji kufanywa tupu baada ya muda ili kutokeza nafasi kwa vitu vipya. Hilo ni kosa. Hakuna mipaka ijulikanayo ya uhifadhi katika kumbukumbu lako. Unaweza kujifunza na kukumbuka mambo mapya katika maisha yako yote.”
Dakt. Furst vivyo hivyo ataja kwamba “lingekuwa kosa kufikiria kwamba ili kutunza chembe zetu za ubongo ifaavyo twapaswa kuzihifadhi kutokana na kila jitihada na kuziweka bila kutumiwa. Kinyume cha hilo ndiyo kweli.” Kumbukumbu lako litakuwa na nguvu kupitia utumizi. (Linganisha Waebrania 5:14.) Wengine, kama vile Harry Lorayne, aliyesaidia kuandika The Memory Book, hata huamini kwamba “kumbukumbu laweza hasa kuwa bora uzidipo kuzeeka.”
Iwe ndivyo ilivyo au la, hutapoteza chochote bali utapata mengi kwa kutumia zawadi ya kupewa na Mungu ya kumbukumbu. Manufaa zaweza kuwa zisizosahaulika.