Je, Tuyakumbuke Yaliyopita?
“JE, WAYAHUDI waweza kusahau yale Maangamizi Makubwa?” Swali hili lilizushwa na Virgil Elizondo, msimamizi wa Kituo cha Utamaduni wa Kimexico na Kimarekani katika San Antonio, Texas. Linatukumbusha kwamba ukatili ambao umefanywa katika karne hii unaweza kuacha kumbukumbu zisizoweza kusahaulika katika akili za watu kwa ujumla. Yale maangamizi ya Waarmenia (1915-1923) na mauaji makubwa ya Wakambodia (1975-1979) ni lazima pia yatiwe ndani ya ukatili ambao umefanywa katika karne ya 20. Na bado kuna mengine.
Wakijaribu kupatanisha watu walioathiriwa na watesi wao, viongozi wa kidini na wa kisiasa wamewaomba watu mara nyingi wasahau ukatili waliotendwa. Kwa mfano, jambo hilo lilitendeka Athens, Ugiriki, mwaka wa 403 K.W.K. Jiji hilo lilikuwa limetoka tu kutawalwa kimabavu na wale walioitwa Wakatili Thelathini, ambao ulikuwa utawala wa wachache ulioondolea mbali, hata kihalisi, karibu maadui wake wote. Magavana wapya walijaribu kurudisha utengamano wa raia kwa kuamuru kusamehewa kwa watu waliounga mkono utawala uliopita.
Je, Inawezekana Kusahau kwa Sababu ya Amri ya Kusamehe?
Inaweza kuwa rahisi kujaribu kufuta kwa amri kumbukumbu za ukatili waliotendwa watu wasio na hatia. Watawala waweza kuamua kufanya hivyo kwa faida yao ya kisiasa, kama ilivyofanyika katika Ugiriki ya kale na katika nchi kadhaa za Ulaya mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Kwa mfano, nchini Italia amri moja katika mwaka wa 1946 ilitangaza kuachiliwa kwa zaidi ya raia 200,000 ambao “walikuwa na hatia ya kushiriki, kwa njia moja au nyingine, katika maovu ya utawala wa Kifashisti,” likasema gazeti la habari La Repubblica.
Ni rahisi kwa serikali au mashirika ya umma kufanya maamuzi. Lakini ni vigumu kuondoa hisia za watu mmoja-mmoja. Haiwezekani kuweka sheria ya kushurutisha raia mmoja-mmoja—labda watu wasio na kinga walioathiriwa na vita vikatili, mauaji, au ukatili mwingine wowote—wasahau jinsi walivyoteseka wakati uliopita.
Zaidi ya watu milioni mia moja wamekufa vitani katika karne hii pekee, wengi wakafa baada ya kuteseka vibaya sana. Tukiongezea wale wote ambao wamekufa katika mauaji ya wakati wa amani, ukatili huo ungekuwa mwingi usiweze kuhesabika. Watu wengi hujitahidi sana kuhakikisha kwamba hata jambo moja halisahauliki.
Wale Ambao Wangependa Kufuta Kumbukumbu Hizo
Watu wanaowahimiza wale walioathiriwa na ukatili au wazao wao wasahau na kusamehe mara nyingi husisitiza kwamba kukumbuka yaliyopita husababisha tu mgawanyiko, hasa ikiwa miongo mingi imepita. Wao husema kwamba kusahau huleta muungano, na kukumbuka ni kama maji yaliyokwisha kumwagika, hayawezi kuzoleka hata kama kuteseka kulikuwa msiba ulioje.
Lakini wakijaribu kuwafanya watu wasahau, wengine wamefikia hatua ya kukana uhalisi wa uhalifu mbaya zaidi waliofanyiwa wanadamu. Wakiungwa mkono na watu wanaojiita eti wasahihishaji wa historia, wengine hudai, kwa mfano, kwamba yale Maangamizi Makubwa hayakutokea kamwe.a Hata wamepanga safari za kuzuru kambi za mauaji, kama Auschwitz au Treblinka, nao wamewaambia wageni kwamba vyumba vya kuulia watu kwa gesi havikuwapo kamwe katika kambi hizo—na wanasema hayo japo uthibitisho mwingi ajabu wa mashahidi waliojionea na hati nyingi sana.
Inakuwaje kwamba mawazo ya wasahihishaji hao bandia wa historia yanakubaliwa na watu fulani? Kwa sababu watu wengine hutaka kusahau hatia zao na za watu wao. Kwa nini? Kwa sababu ya uzalendo, dhana zao wenyewe, au uhasama dhidi ya Wayahudi au uhasama mwingine kama huo. Wasahihishaji hao wa historia wakata kauli kwamba mara ukatili huo usahauliwapo, hatia huisha. Lakini watu wengi huwapinga sana wasahihishaji hao wasiowajibika, ambao wameitwa na mwanahistoria mmoja Mfaransa “wauaji wa kumbukumbu.”
Hawasahau
Bila shaka ni vigumu sana kwa waokokaji kusahau wapendwa wao waliokufa vitani au katika ukatili. Lakini, wengi wa wale wanaotaka kukumbuka yale mauaji na maangamizi wanafanya hivyo kwa sababu wanatumaini kwamba somo linalotokana na kuteseka kwao na kuteseka kwa wapendwa wao litasaidia kuepusha kurudiwa kwa ukatili kama huo.
Basi, serikali ya Ujerumani imeamua kuadhimisha siku ya kugunduliwa kwa ukatili wa Wanazi katika kambi ya mateso ya Auschwitz. Kulingana na rais wa Ujerumani kusudi ni kwamba “kukumbuka kutakuwa onyo kwa vizazi vya wakati ujao.”
Vivyo hivyo, kwenye mwadhimisho wa mwaka wa 50 wa mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, papa John Paul wa Pili alisisitiza: “Miaka ipitapo, kumbukumbu za Vita hazipaswi kudidimia; badala yake, zinapasa kuwa somo kali kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.” Lakini, ni lazima itajwe kwamba si kawaida kwa Kanisa Katoliki kukumbuka ukatili uliofanywa na vilevile waathiriwa wa miaka hiyo.
Ili vizazi vipya pia vipate somo na maonyo kutokana na maangamizi ya jamii katika karne hii na nyinginezo, majumba kadhaa ya makumbusho yamefunguliwa—kama vile Jumba la Makumbusho la Maangamizi Makubwa katika Washington, D.C., na Beit Hashoah Museum of Tolerance katika Los Angeles. Kwa sababu iyo hiyo, sinema za mambo halisi zenye kugusa moyo zinazohusu habari hii zimefanyizwa. Hayo yote yamefanywa ili kujaribu kuzuia wanadamu wasisahau watu walioteswa na wengine.
Kwa Nini Tukumbuke?
“Wale ambao hawawezi kukumbuka yaliyopita ni sharti watarudia kuyafanya,” akaandika mwanafalsafa mmoja Mhispania aliyezaliwa Marekani, George Santayana. Kwa kusikitisha, inaonekana kwamba katika maelfu ya miaka mwanadamu husahau haraka wakati wake uliopita, na kuyafanya tena na tena makosa yaleyale yenye msiba.
Mfululizo mrefu wa mauaji ya kikatili yaliyofanywa na wanadamu wakazia kwamba binadamu ameshindwa kabisa kumtawala binadamu. Kwa nini? Kwa sababu wanadamu wamerudia daima kufanya kosa lilelile la msingi—wamemkataa Mungu na sheria zake. (Mwanzo 3:1-6; Mhubiri 8:9) Na leo, kama ilivyotabiriwa katika Biblia, “kizazi kilichopotoka” kinafanya kosa ilo hilo na kuvuna tufani.—Wafilipi 2:15; Zaburi 92:7; 2 Timotheo 3:1-5, 13.
Kwa kuwa tumemhusisha Muumba, Yehova, katika mazungumzo yetu, yeye ana maoni gani? Yeye husahau nini, naye hukumbuka nini? Je, historia yenye uchungu wa ukatili unaofanywa na wanadamu unaweza kusahaulika? Je, ‘ubaya wao wasio haki utakoma’?—Zaburi 7:9.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari juu ya uwongo wa hoja za wasahihishaji hao wa historia, tafadhali ona makala “Lile Teketezo la Umati—Ndiyo, Kwa Kweli Lilitukia!” iliyochapishwa katika Amkeni! la Novemba 8, 1989, ukurasa wa 4-8.
[Blabu/Picha katika ukurasa wa 7]
“Wale ambao hawawezi kukumbuka yaliyopita ni sharti watarudia kuyafanya.”—George Santayana
Tanuu ya kuchomea maiti na joko katika kambi ya mateso ya Auschwitz
[Hisani]
Oświęcim Museum