Ndege Mpweke Zaidi Ulimwenguni
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI
IKIWA unafikiri kwamba bundi-madoadoa na furukombe wamo hatarini mwa kutoweka, basi hujasikia hadithi ya kasuku-mkia wa Spix. Ndege huyu wa Brazili hutoa maana mpya kabisa ya lile wazo “aina-kiumbe iliyo hatarini mwa kutoweka.” Hata hivyo, ili kukupa hadithi kamili ya ndege mpweke zaidi ulimwenguni, tutaanza katika karne ya 17.
Wakati huo, George Marc Grav, Mholanzi aliyeishi Brazili, alirekodi kwa mara ya kwanza kuwepo kwa na sifa za ndege huyu. Kabla ya muda mrefu, watu wa huko wakamwita ararinha azul, au kasuku-mkia mdogo wa buluu—jina sahili lakini lenye kumfaa sana. Huyo ndege ana rangi ya buluu na ya kijivu kidogo-kidogo. Akiwa na kipimo cha sentimeta 55, kutia ndani mkia wake wenye urefu wa sentimeta 35, yeye ndiye mdogo zaidi kati ya kasuku-mkia wa buluu wa Brazili.
“Baadaye, katika 1819,” aeleza mwanabiolojia Carlos Yamashita, mstadi wa kasuku aliye mashuhuri zaidi wa Brazili, “wanasayansi walimpa huyo ndege jina rasmi: Cyanopsitta spixii.” Cyano humaanisha “buluu” na psitta ni “kasuku.” Namna gani spixii? Nyongeza hiyo, aeleza yule mwanabiolojia, humtolea sifa mtafiti wa mambo ya kiasili Mjerumani Johann Baptist Spix. Yeye alikuwa wa kwanza kujifunza juu ya aina hizi za ndege katika makao yazo ya kiasili yaliyo hori kadhaa zenye miti kaskazini-mashariki mwa Brazili.
Kutoweka Kwaanza
Ni wazi kwamba, makundi ya kasuku-mkia wa Spix hawajapata kamwe kuwa wengi. Hata katika siku za Spix, idadi yao iliyohesabiwa ilikuwa 180 pekee, lakini tangu wakati huo, hali yao imeendelea kuwa mbaya. Masetla waliharibu misitu mingi ambamo ndege walikuwa wakiishi hivi kwamba kufikia katikati ya miaka ya 1970, kasuku-mkia wanaopungua 60 ndio waliokuwapo bado. Ingawa hilo lilikuwa baya sana, kutoweka kulikuwa ndipo tu kumeanza.
Kilichowashinda masetla kutimiza kwa karne tatu, wanasa-ndege walifaulu kufanya kwa miaka michache—walifagilia mbali karibu idadi yote ya kasuku-mkia wa Spix. Katika 1984, ni ndege 4 tu kati ya 60 waliokuwa hai mwituni, lakini kufikia wakati huo wafuga-ndege walikuwa tayari kulipa “pesa nyingi sana” kwa ajili ya ndege ambaye huenda ni wa mwisho wa aina yake—hata kufikia dola 50,000 kwa ndege mmoja. Haishangazi kwamba katika Mei 1989 gazeti Animal Kingdom lilitangaza kwamba mwaka mzima ulikuwa umepita tangu watafiti waone ndege wa mwisho walio huru wakiruka. Miezi michache baadaye, iliripotiwa kwamba wanasaji walikuwa wamenyakua ndege wote waliosalia. Kasuku-mkia wa Spix, likaomboleza Animal Kingdom, alikuwa amepata “pigo la mwisho.”
Mshangao na Tumaini
Wanabiolojia walikuwa wamekata kauli kuwa kasuku-mkia wa Spix alikuwa ametoweka wakati ambapo watu waliokuwa wakiishi kwenye ujirani wa makao ya hao ndege waliposema kuwa walikuwa wamemwona ararinha azul. Ripoti zaidi ya kuonekana kwake zikafuata. Je, kungeweza bado kuwako ndege aliyesalia? Ili kupata jibu, katika 1990 watafiti watano wakafunganya vitu vyao vya kupiga kambi, darubini, na vijitabu vya kuandikia na kuelekea eneo la kasuku-mkia wa Spix.
Baada ya kupekua kwa uangalifu hilo eneo kwa miezi miwili bila kufanikiwa, watafiti waliona kundi la papagaios maracanãs wenye rangi ya kijani-kibichi, au kasuku-mkia wa Illinger, lakini wakaona kitu kisicho cha kawaida. Mmoja wa washiriki wa kundi hilo alikuwa tofauti—mkubwa zaidi na wa buluu. Alikuwa kasuku-mkia wa Spix wa mwisho aliyekuwa porini! Walimchunguza kwa juma moja na kugundua kwamba huyo Spix, mwenye urafiki kiasili, alikuwa akifuatana na wale wa Illinger ili kukabiliana na upweke wake na pia ili apate mwenzi. Na ndege hao wa kijani-kibichi walimkubali ndege huyo wa buluu mwenye kuwafuata kuwa rafiki yao—lakini namna gani kujamiiana naye? Bila shaka ingawa kasuku-mkia wa Illinger ni wapole, kuna mipaka kwa yale waliyo tayari kufanya!
Hivyo, kwa sababu ya kukataliwa, kasuku-mkia wa Spix aliwaacha waandamani wake wakati wa mshuko-jua kila siku na kuruka hadi kwenye mti ambapo yeye na aliyekuwa mwenzi wake kasuku-mkia wa Spix walipoishi pamoja kwa miaka mingi—kufika 1988, mwaka ambao wanasaji walipomnyakua rafiki wake wa maishani na kumuuza utekwani. Tangu wakati huo, yeye hulala huko peke yake—ndege mdogo na mwenye manyoya ya buluu juu ya tawi refu lililonyauka. Sasa, labda tu muujiza utukie, kutoweka kwa kasuku-mkia wa Spix wa mwisho mwenye ujuzi wa kusalimika porini ni dhahiri—isipokuwa mtu amtafutie mwenzi. Jambo hilo lilifuatiwa, na katika 1991 ule Projeto Ararinha-Azul (Mradi wa Kasuku-Mkia wa Spix) ulianzishwa. Kusudi lao lilikuwa nini? Kumhifadhi ndege aliyesalia, kumtafutia mwenzi, kuwaambatanisha, na kutazamia wazaane kwenye huo ujirani. Je, hilo lafanikiwa?
Maendeleo yamefanywa. Ofisi ya Posta ya Brazili ilitangaza hali ya ndege huyo aliyehatarishwa zaidi kwenye sayari kwa kutoa stampu kwa sifa yake. Wakati huohuo, wanabiolojia waliwaunganisha wakazi 8,000 wa Curaçá, mji ulio karibu na makao ya huyo ndege katika kaskazini mwa Bahia, ili wamtegemeze kasuku-mkia wa Spix aliyesalia. Watu wa mji huo wamchungapo ndege “wao,” ambaye wanamwita Severino, wanasaji sasa wamo hatarini mwa kunaswa. Jambo hili linafanikiwa. Severino angali anaruka huku na huku. Kizuizi cha pili kimeshughulikiwa ifaavyo—kuwasihi wafugaji watoe mmoja kati ya ndege sita walionaswa ambao bado wanaishi Brazili. (Ona kisanduku.) Mfugaji mmoja alikubali, na katika Agosti 1994 ndege mdogo wa kike, aliyenyakuliwa na wanasaji akiwa kifaranga, alisafirishwa kwa eropleni hadi Curaçá ili aachiliwe na kuishi katika makao yake ya kiasili tena.
Kufaana na Kufahamiana na Hali
Kasuku-mkia huyu wa kike aliwekwa katika kitundu kikubwa kilichowekwa katika makao ya ndege wa kiume na kupewa chakula cha kawaida cha kasuku-mkia wa porini. Ili kumfanya afaane na hali kwa ajili ya maisha ya kiasili, watunzi wake walimwachisha kula mbegu za alizeti—chakula chake cha kawaida alipokuwa akifugwa—na kumlisha mbegu za msunobari na matunda ya huko yenye miiba yameayo porini. Tumbo lake lilibadilikana ifaavyo.
Mazoezi ya kila siku yakawa sehemu ya programu—kwa sababu nzuri. Kutarajia ndege aliyekuzwa katika kizimba, mara moja tu aweze kufuatana na mwenzi apendaye kuruka kilometa 50 hivi kwa siku ni sawa na kumwomba mraibu wa televisheni kukimbia mbio za marathoni. Ili kuijenga misuli yake, wanabiolojia waliokuwa wakimtunza huyo ndege mfungwa walimchochea kuruka kwenye kile kitundu kwa kadiri ambayo angeweza.
Haikuchukua muda mrefu kabla ya Severino kukigundua hicho kitundu. Baada ya kumwona ndege wa kike, alitoa mlio kwa nguvu, akamwita, na kuja karibu meta 30 kutoka kwa hicho kitundu. “Yule wa kike,” asema Marcos Da-Ré, mwanabiolojia anayefanya kazi katika huo mradi, aliitikia na “kuonyesha mchachawo mkuu” alipomwona mgeni wake wa kiume. Mchachawo wake, yeye asema, “ulitupa tumaini.”
Mwalimu na Baba . . .
Hatimaye, siku ya siku zote ikafika: milango ya kitundu ikafunguliwa. Baada ya kusitasita kwa nusu saa, yule ndege wa kike akaruka nje na kutua juu ya mti karibu meta 300 kutoka kwenye kitundu. Lakini Severino alikuwa wapi? Alikuwa kilometa 30 toka hapo akiwafuata kasuku-mkia wa Illinger tena. Kwa nini alikuwa ameondoka? Baada ya kungoja kwa miezi miwili, majira ya kujamiiana yalipofika, yule ambaye angekuwa mwenziwe alikuwa bado amefungiwa. Lazima awe alifikiri, akasema mwanabiolojia Da-Ré, “Hamadi kibindoni, ni silaha iliyo mkononi.” Wakati huu kufuatia kwake Severino kulikuwa na matokeo. Kasuku-mkia mmoja wa Illinger wa kike alimkubali kuwa mwandamani wake.
Hata hivyo, majira ya kujamiiana yaishapo, wanabiolojia watazamia kwamba Severino atamaliza uchumba wake, arudi kwenye makao yake mwenyewe, na kugundua kuwepo kwa yule kasuku-mkia wa Spix aliye huru, na kumchukua akiwa mwenziwe. Baada ya hilo, yeye atarajiwa kutimiza mafungu mawili—mwalimu na baba. Kwa kuwa yeye ndiye kasuku-mkia wa Spix wa pekee ulimwenguni pote ajuaye jinsi ya kusalimika porini, ahitaji kumfundisha mwenzake jinsi ya kupata chakula na makao na kuendelea kuishi katika mojawapo maeneo ya Brazili yaliyo makame sana.
. . . Na Mfanya Historia
Hivyo majira ya kujamiiana yaanzapo tena, wanabiolojia wa Mradi wa Kasuku-Mkia wa Spix watakuwa wakitarajia kwamba Severino ataacha kufuata kasuku-mkia wa Illinger na kujishughulisha na kutafuta mti wenye mwanya uwezao kutumika kuwa kiota kwa mwenzake. Mambo yote yakienda sawa, kasuku-mkia wa Spix wa kike atataga mayai mawili madogo, na miezi michache baadaye, Severino atakuwa akifunza darasa la watatu mbinu za kusalimika. Je, lengo hilo litafanikiwa?
“Itachukua muda kujua jibu,” asema mwanabiolojia Yamashita, “lakini mradi huu waweza kuwa ndio njia ya pekee ya kuepuka kutoweka kwa kasuku-mkia wa Spix kutoka katika historia.” Sasa ni juu ya Severino kufanya mwanzo mpya. Hilo likifanikiwa, wapenda mambo ya asili—na kasuku-mkia wa Illinger—watapata kitulizo.
[Sanduku katika ukurasa wa24]
Ndege Vizuizini
Kasuku-mkia wa Spix wanaokadiriwa kuwa 30 wanaishi kwa kufungiwa. Idadi fulani ya ndege hao wa Brazili walizalishwa na mkuza ndege wa Ufilipino nao bado huishi katika nchi hiyo ya Asia. Ndege waliosalia ambao wamefungiwa wanaishi Brazili, Hispania, na Uswisi. Hata hivyo, ndege hao wote walio vizuizini wanakosa jambo ambalo Severino peke yake ndiye aliye nalo—ujuzi wa kusalimika porini.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Alihifadhiwa—angalau kwenye stampu
[Hisani]
Empresa Brasileira de Correios e Telégrafos