Ni Nani Awezaye Kuleta Amani Yenye Kudumu?
“Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.”
ANDIKO hili lililoko juu latoka katika Isaya sura ya 2, mstari wa 4. Ile Human Development Report 1994, iliyotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), ilinukuu maneno hayo na kisha ikaongeza hivi: “Ilionekana kwamba unabii huu ulikuwa umetimia wakati vita baridi ilipokwisha [katika 1990]. Lakini kufikia wakati huu hilo limethibitika kuwa tumaini lenye kuhepa.”
Kupunguza Wanajeshi
Kisababishi kimoja kinachodhoofisha tumaini la amani ni kwamba badiliko katika hali ya kimataifa ya kisiasa halijaambatana na mapunguzo makubwa katika matumizi ya kijeshi. Ni kweli, kumekuwa na mapunguzo fulani. Kulingana na tarakimu za UM, matumizi ya duniani kote ya kijeshi yalishuka kutoka kilele cha dola bilioni 995 katika 1987 hadi dola bilioni 815 katika 1992. Bado, dola bilioni 815 ni tarakimu kubwa mno. Kwa kadirio inatoshana na jumla ya mapato ya nusu ya idadi ya watu ulimwenguni!
Kisababishi kingine kilicho dhidi ya kupunguza silaha ni maoni ya kwamba uwezo wa kijeshi huleta usalama. Hivyo, hata ingawa Vita Baridi imekwisha, wengi katika nchi zilizovuvumuka kiviwanda husababu kwamba matumizi ya kijeshi ya kitaifa yapaswa kubaki yakiwa katika viwango vya juu. James Woosley, alipokuwa mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani, aliliambia Bunge katika Februari 1993: “Tumechinja joka kubwa [Muungano wa Sovieti], lakini sasa twaishi katika msitu uliojaa aina zenye kutia wasiwasi za nyoka wenye sumu.”
Katika nchi zinazositawi matumizi ya juu ya kijeshi pia hutolewa udhuru kuwa njia ya kuzuia shambulizi kutoka nchi zinazoonwa kuwa ziwezazo kuwa majoka na nyoka wenye sumu. Lakini kwa uhalisi, UNDP likaonelea, “nchi zinazositawi zimepigana vita vichache vya kimataifa, na nyingi zimetumia majeshi yazo kukandamiza watu wazo.” Kwa hakika, ripoti ya UNDP ilieleza hivi: “Katika nchi zinazositawi, uwezekano wa kufa kutokana na kupuuzwa kwa jamii (kutokana na utapia-mlo na maradhi yawezayo kuzuiwa) ni mkubwa mara 33 zaidi kuliko uwezekano wa kufa katika vita inayotokana na shambulizi la nje. Hata hivyo, kuna uwiano wa wanajeshi 20 kwa kila tabibu. Kwa vyovyote, wanajeshi waelekea zaidi kupunguza usalama wa kibinafsi kuliko kuuongeza.”
Biashara ya Kimataifa ya Silaha
Wakati wa Vita Baridi, yale mataifa mawili yenye nguvu zaidi yaliuza silaha kwa washirika wayo ili kuimarisha miungano, kupata vituo vya shughuli za kijeshi, na kudumisha uwezo. Majeshi ya mataifa mengi yakawa na uwezo. Kwa kielelezo, kwa wakati huu, kuna nchi 33 ambazo kila moja ina vifaru vya kivita zaidi ya 1,000.
Sasa kwa kuwa Vita Baridi imekwisha, udhuru wa kisiasa na mbinu za kivita kwa mauzo ya silaha umedidimia. Hata hivyo, vichocheo vya kiuchumi vyabaki imara. Faida nyingi zaweza kupatwa! Kwa hiyo, huku uhitaji wa silaha wa ndani ya nchi ukizidi kupungua, watengenezaji wa silaha wanahimiza serikali zao kwamba njia ya kuhifadhi kazi na kudumisha uchumi ukiwa bora ni kuuza silaha ng’ambo.
Gazeti World Watch laeleza hivi: “Kwa kinyume, kama tu vile mataifa makuu zaidi yaondoavyo makombora yayo makubwa ya nyuklia, ndivyo yanavyotafuta kwa uharaka njia za kuuza mabomu na bunduki zisizo za kinyuklia kwa karibu mtu yeyote atakayenunua.” Tarakimu ni zipi? Kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm, thamani ya silaha zisizo za kinyuklia zilizouzwa katika soko la kimataifa katika miaka ya 1988 hadi 1992 ilikuwa dola bilioni 151. Muuzaji-nje mkubwa zaidi alikuwa Marekani, ikifuatiwa na zile nchi zilizokuwa Muungano wa Sovieti.
Tisho la Nyuklia Labaki
Namna gani juu ya tisho la nyuklia? Marekani na Muungano wa Sovieti (au mataifa-andamizi yao) yalitia sahihi Mkataba wa Silaha za Kinyuklia za Masafa Mafupi katika 1987 na Mikataba [miwili ya] Kupunguza Silaha Muhimu (START) katika 1991 na 1993.
Mikataba ya START ilipiga marufuku makombora ya barani yenye vilipukaji zaidi ya kimoja na ikaagiza kuondoshwa, kufikia mwaka wa 2003, kwa karibu robo tatu ya vilipukaji vya nyuklia vilivyo kwenye vifaa vinavyobeba vilipukaji. Lakini ingawa tisho la Vita ya Ulimwengu 3 ya nyuklia limefifia, kunabaki maghala mengi makubwa ya silaha za nyuklia—zinazotosha kuharibu uhai wote duniani mara kadhaa.
Kuachanisha silaha hizi huongeza fursa za wizi wa nyuklia. Kwa kielelezo, Urusi inabomoa na kuhifadhi vilipukaji 2,000 hivi kila mwaka, ikitoa kutokana navyo tufe za plutoniamu zenye ukubwa wa ngumi ziitwazo piti. Piti ya kilipukaji, ambayo huhitaji gharama kubwa mno na tekinolojia ili kuitengeneza, ndiyo kichanganyiko kikuu cha bomu la nyuklia. Kwa kuwa piti kwa kawaida hufunikwa katika tabaka la chuma ambayo huzuia unururifu, yaonekana mwizi angeweza kubeba moja mfukoni mwake. Haramia aliyepata piti iliyotengenezwa tayari angeweza kuifunika kwa kifaa cha kuifanya ilipuke ili kutengeneza tena bomu lenye nguvu mno.
Hangaiko jingine ni tisho la kuenea kwa silaha za nyuklia kwa nchi nyingi zaidi. Mataifa matano yanajulikana kuwa mataifa yenye silaha za nyuklia—China, Marekani, Ufaransa, Uingereza, Urusi—na nchi nyinginezo kadhaa pia zafikiriwa kuwa na uwezo wa kueneza silaha za nyuklia kwa haraka.
Kadiri mataifa mengi zaidi yapatavyo silaha za nyuklia, ndivyo uwezekano wa kwamba mtu fulani atazitumia uongezekavyo. Watu wana haki ya kuhofu silaha hizi zenye kutisha. Kama kitabu The Transformation of War kinavyoeleza, “silaha hizo zina nguvu nyingi mno hivi kwamba hufanya silaha zisizo za kinyuklia kuonekana kuwa duni.”
Kupunguza Silaha na Amani
Lakini namna gani ikiwa mataifa yangeharibu silaha zayo za uharibifu zilizo tata? Je, hilo lingehakikisha ulimwengu wenye amani? Sivyo hata kidogo. Mwanahistoria wa kijeshi John Keegan aonelea hivi: “Silaha za kinyuklia hazijaua mtu yeyote tangu Agosti 9, 1945. Wale 50,000,000 ambao wamekufa vitani tangu tarehe hiyo, hasa, wameuawa na silaha za bei ya chini na risasi za mizinga midogo, inayogharimu kidogo kuliko redio za transista na betri za seliumeme kavu ambazo zimejaa ulimwenguni kwa wakati mmoja.”
Kielelezo cha hivi majuzi cha utumizi wa silaha za tekinolojia ya hali ya chini ni machinjo katika Rwanda, nchi ambayo kuihusu The World Book Encyclopedia (1994) husema: “Watu walio wengi ni Wakatoliki wa Kiroma. . . . Makanisa ya Katoliki ya Kiroma na mengine ya Kikristo huendesha nyingi za shule za msingi na sekondari.” Hata hivyo, katika Rwanda watu wapatao nusu milioni waliuawa na watu waliokuwa na panga. Kwa wazi, ili kuleta amani ya ulimwengu, jambo zaidi ya kupunguza silaha za nyuklia na zisizo za nyuklia lahitajiwa. Pia, jambo jingine lahitajiwa zaidi ya mafundisho yanayotolewa na dini za ulimwengu.
Uadui wa Kikabila Waongezeka
Sadako Ogata, kamishna mkuu wa tume ya UM inayoshughulikia wakimbizi, alisema majuzi hivi: “Mara tu baada ya Vita Baridi, tulifikiri kwamba matatizo yote yangelisuluhishwa. Hatukutambua kwamba Vita Baridi ilikuwa na sehemu nyingine—kwamba mataifa yenye nguvu zaidi yalitoa agizo au kulazimisha agizo kwa maeneo yazo hususa ya uvutano. . . . Kwa hiyo sasa, baada ya Vita Baridi, twaona mlipuko wa vita ya kidesturi ambayo haikuendelea, labda ya aina za kabla ya Vita ya Ulimwengu 1.”
Arthur Schlesinger, mshindi wa tuzo la kila mwaka kwa waandishi bora, ambaye ni mwanahistoria na mwandishi, atoa hoja inayofanana na hiyo: “Aina moja ya chuki huchukua mahali pa nyingine. Kuondoa mshiko wenye nguvu mno wa ukandamizaji wa dhana tofauti katika Ulaya Mashariki na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti huachilia uadui uliokandamizwa wa kikabila, kitaifa, kidini, na kilugha uliokazwa imara katika historia na katika kumbukumbu. . . . Ikiwa karne ya 20 imekuwa karne ya vita vya dhana tofauti, karne ya 21 yaanza ikiwa karne ya vita vya kikabila.”
Kati ya 1989 na 1992, kulingana na kadirio la Umoja wa Mataifa, kulikuwa na vita 82 vyenye silaha, vingi vyavyo vikipiganwa miongoni mwa nchi zinazositawi. Katika 1993, nchi 42 zilikuwa na vita kubwa na nchi nyinginezo 37 zilipatwa na jeuri ya kisiasa. Wakati huohuo, Umoja wa Mataifa—bajeti yalo ikiwa imetanuka kufikia ukomo wayo—lilijikakamua bila mafanikio mengi kuleta amani katika opereshani 17 tu. Kwa wazi, ni lazima wanadamu watafute amani ya ulimwengu mahali kwingineko.
Matatizo Yanayotisha Kutokea
Kwa njia yenye kuongezeka, badala ya kutazama wakati ujao wakitazamia mazuri, wengi hutazamia mabaya. Jalada la toleo la Februari 1994 la The Atlantic Monthly hufupisha moja ya matabiri ya miongo inayokuja: “Mataifa yataangamia kwa sababu ya ongezeko lenye kupanda pindi kwa pindi la wakimbizi kutokana na msiba wa kimazingira na kijamii. . . . Vita vinapiganwa juu ya rasilimali chache sana, hasa maji, nayo vita yenyewe yaendelea kwa uhalifu, huku vikundi vyenye silaha vya watekaji wasio na taifa vikipigana na majeshi ya kibinafsi ya usalama ya watu mashuhuri.”
Je, hili lamaanisha kwamba amani yenye kudumu haiwezi kufikiwa? Sivyo hata kidogo! Makala ifuatayo yaonyesha sababu zinazofanya tutazame wakati ujao tukiwa na uhakika.
[Sanduku katika ukurasa wa5]
Dini—Uvutano wa Kuleta Amani?
Mataifa yaendapo vitani, dini za ulimwengu huacha mafundisho ya amani na udugu. Kuhusu hali ya wakati wa Vita ya Ulimwengu 1, brigedia-jenerali Mwingereza Frank P. Crozier alisema: “Makanisa ya Kikristo ndiyo wachochezi wakuu wa umwagikaji wa damu ulioko, nasi tumewatumia kwa uhuru.”
Fungu la dini katika vita limekuwa lilelile kotekote katika mihula yote. Mwanahistoria Mkatoliki E. I. Watkin alikubali hivi: “Hata ingawa ni jambo lenye kuumiza kukiri jambo hilo, hatuwezi kwa ajili ya kuelimisha kwa uwongo au kwa uaminifu-mshikamanifu usiofuatia haki kukataa au kupuuza uhakika wa kihistoria kwamba Maaskofu wameunga mkono kwa kuendelea vita vyote vilivyopiganwa na serikali ya nchi yao.” Na uhariri katika gazeti Sun la Vancouver, Kanada, ulionelea hivi: “Ni udhaifu wa labda dini zote mashuhuri kwamba kanisa hufuata bendera . . . Ni vita gani iliyopata kupiganwa ambamo Mungu hakudaiwa kuwa katika kila upande?”
Kwa wazi, badala ya kuwa uvutano wa kuleta amani, dini za ulimwengu zimeunga mkono vita na uuaji—kama ilivyoonyeshwa kwa dhati na machinjo katika Rwanda.
[Sanduku katika ukurasa wa6]
Ubatili wa Vita
Katika kitabu I Found No Peace, kilichotangazwa katika 1936, mleta-habari wa kigeni Webb Miller aliandika hivi: “Kwa kushangaza, ogofyo la kimsiba la [Vita ya Ulimwengu 1] halikunipiga likiwa na ubaya na ubatili mwingi sana hadi miaka minane kamili baada ya vita hiyo kwisha.” Katika pindi hiyo yeye alizuru tena uwanja wa pigano wa Verdun, ambapo alidai kwamba wanaume 1,050,000 walikuwa wamekufa.
“Wakati wa vita nilikuwa nimedanganywa, pamoja na mamilioni ya watu wengine,” akaandika Miller. “Vita ya Ulimwengu ilikuwa imefaulu katika kutokeza vita vipya tu. Watu milioni nane na nusu walikuwa wamekufa bure, makumi ya mamilioni yalikuwa yamepatwa na ogofyo lisiloelezeka, na mamia ya mamilioni yalikuwa yamepitia huzuni, hasara, na ukosefu wa furaha. Na yote haya yalikuwa yametukia chini ya madanganyo makubwa mno.”
Miaka mitatu baada ya kitabu hicho kutangazwa, Vita ya Ulimwengu 2 ikaanza. Gazeti The Washington Post lilionelea hivi: “Vita vyetu vya karne ya 20 vimekuwa ‘vita kamili’ dhidi ya wanajeshi na raia pia. . . . Vita vya ujahili vya karne zilizopita kwa ulinganifu vilikuwa vidogo na visivyotokeza kamwe.” Kulingana na kadirio moja lililofanywa na mtaalamu mmoja, watu milioni 197 wamekufa tangu 1914 katika vita na maasi dhidi ya serikali.
Hata hivyo, vita vyote na maasi ya kibinadamu dhidi ya serikali hayajaleta amani na furaha. Kama The Washington Post lilivyosema, “hakuna mfumo wowote wa kisiasa au kiuchumi ambao kufikia wakati huu umepatanisha au kutosheleza mamilioni yasiyotulia.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mama huyu ni mmoja wa mamia ya maelfu ya watu waliochinjwa katika Rwanda—wengi wakiuawa na watu wa dini yao wenyewe
[Hisani]
Albert Facelly/Sipa Press