Wasiojiweza-Lakini Wawezao Kuendesha Gari
“NAWEZA kuendesha gari!” Huenda maneno hayo yasiwe na maana yoyote kwako, lakini yana maana sana kwangu. Mwanamume mwenye umri wa miaka 50 aliyetaja maneno hayo alikuwa chini mbele yangu. Kwa kuwa alipooza akiwa mtoto, miguu yake haikupata kamwe kukua. Miguu hiyo midogo na isiyotumika, ilikuwa imekingamana chini ya mwili wake. Licha ya hayo, alikuwa na mikono na mabega yenye nguvu kwa sababu ya kutembea kwa mikono yake kwa miaka mingi. Nako kukosa kwake kujisikitikia kuliniaibisha—hasa ile sauti ya kujisikia alipokuwa akisema kuwa anaweza kuendesha gari.
Waona, mimi mwenyewe nilipooza nikiwa na umri wa miaka 28. Nilivunjwa moyo sana na zile habari za kwamba singeweza kamwe kutembea bila kutumia mikongojo. Maneno sahili ya mwanamume huyu yalinisaidia kukabiliana na mshuko-moyo wangu. Nilisababu mwenyewe kuwa ikiwa yeye, ingawa hajiwezi zaidi yangu, aliweza kushinda tatizo lake, kwa nini mimi nisifanye vivyo hivyo? Nikaamua papo hapo kuwa mimi nami ningeendesha gari tena!
Haikuwa Rahisi
Hilo lilikuwa karibu miaka 40 iliyopita. Huko nyuma, kuendesha gari ukiwa mtu asiyejiweza kulihitaji kuwa na moyo mkuu. Gari langu lililorekebishwa lilikuwa ubuni kwelikweli! Kulikuwa na mkongojo chini ya kwapa langu la kushoto, ulioenda chini hadi kwenye kikanyagio cha klachi. Nilibadili klachi kwa kusogeza mbele bega langu la kushoto. Kichapuo kilikuwa wenzo uliotumiwa kwa mkono kutoka kwa Model T Ford ya awali, nayo breki pia ilifanya kazi kwa kutumia wenzo wa mkono. Je, waweza kuniwazia nikiendesha gari? Bega langu lilikuwa likisonga nyuma na mbele, mkono wangu wa kushoto ulikuwa ukiongoza gari na kupiga breki, na mkono wangu wa kuume ukiongoza gari, kuongeza mwendo, na kutoa ishara za mikono za barabarani! (Katika Australia sisi huendesha magari upande wa kushoto wa barabara.) Wakati huo magari hayakuwa na indiketa.
Nashukuru kwamba siku hizo za kuendesha magari kwa kutumia vitu vingi vyenye kuchosha zimepita. Leo, kukiwa na transmisheni ifanyayo kazi yenyewe, na indiketa za kubonyeza tu, kuendesha gari kumerahisishwa sana. Maendeleo ya kitekinolojia yamewezesha watu wengi wasiojiweza kuendesha magari. Vifaa fulani ambavyo hutumika kwa wingi vyaelezwa katika kisanduku kwenye ukurasa 14.
Mapendekezo Yangu Binafsi
Ikiwa wewe ni asiyejiweza na wafikiri juu ya kurekebisha gari ili uweze kuendesha, napendekeza kwa dhati kuwa umwendee mtaalamu katika uwanja huo. Aweza kupanga ili mashine zote zikaguliwe ili kukulinda ukiwa dereva na pia kulinda abiria wako. Kwa sababu ya uwezekano wa aksidenti, ni vizuri kuwa na bima iwezayo kulipia hasara zote kutoka kwa kampuni ya bima ijulikanayo.
Kwa ujumla, yaweza kuwa tahadhari ya kihekima kwenda pamoja na mwandamani wakati uendeshapo gari. Mithali ya kale ilishauri hivi kwa hekima: “Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa kuwa pamoja wao waweza kufanya kazi kwa matokeo zaidi. Mmoja wao akianguka chini, yule mwingine aweza kumsaidia ainuke. Lakini mtu akiwa peke yake na aanguke, ni vibaya kama nini, kwa sababu hakuna yeyote wa kumsaidia.” (Mhubiri 4:9, 10, Today’s English Version) Mwandamani aweza kuwa msaada mkubwa ukipatwa na aksidenti, gari likiharibika, au gurudumu likitoka pumzi. Baadhi ya madereva wasiojiweza huwa na simu kwenye gari. Hivyo wao waweza kuendesha gari wakiwa peke yao, ikiwa lazima, wakiwa na uhakika zaidi.
Pia ni jambo la kiakili kwa dereva asiyejiweza kujiunga na mashirika yatoayo utumishi wa barabarani kwa ajili ya waendeshaji wa magari ili asaidiwe upesi akipiga simu, iwe mchana au usiku. Ada ya mwaka mzima kwa kawaida ni ya kadiri—gharama ndogo ya kulipia amani ya akilini uwezayo kuandaliwa.
Ni wazi kwamba sisi ambao ni madereva wasiojiweza twapaswa kutambua mipaka yetu na kuendesha magari kupatana nayo. Hatupaswi kuendesha kwa fujo ili kuthibitisha kuwa twaweza kuendesha magari kama wengine. Badala ya hivyo, madereva wengi wasiojiweza wana maandishi kwenye magari yao yasemayo: “Dereva Asiyejiweza—Tahadhari,” au maneno kama hayo. Hii ni ilani kuwa dereva asiyejiweza aweza kuwa mwangalifu na kuendesha kwa mwendo wa pole kidogo kuliko wengine. Hili halimaanishi kuwa wengine wapaswa kuondokea hilo gari kabisa. Kwa hakika, katika kisa changu, karibu nyakati zote, mtu asiyejiweza hachukui muda mrefu kupiga breki kuliko dereva wa kawaida, hasa tangu kuanzishwa kwa vifaa vya kisasa.
Kuendesha au Kutoendesha Gari—Uamuzi Mzito
Ikiwa wewe ni asiyejiweza na ungependa kuendesha gari, wapaswa kulishughulikia hilo tatizo kwa uzito. Kwanza zungumza na daktari wako na washiriki wa familia yako. Huenda ukafikiria pia maswali kama haya: Je, ni lazima niendeshe gari? Je, naweza kukabiliana na aksidenti ikitokea? Je, naweza kushinda woga wowote nilio nao? Faida ni zipi? Je, uwezo wangu wa kuendesha utaniwezesha kufanya kazi tena? Je, waweza kunisaidia kushirikiana zaidi na watu wengine?
Kujua wakati wa kuacha pia kwaweza kuwa jambo la maana. Siku yaweza kumjia dereva yeyote, asiyejiweza au wa kawaida, utambuzi na maitikio yapunguapo na kufanya iwe lazima kufanya uamuzi kama huo. Wakati huo ukikufikia, kukumbuka una wengi kuliko wewe upaswao kuwafikiria. Namna gani wale uwapendao—familia yako na pia jirani yako, mwanadamu mwenzako njiani? Je, uwezo wako wa kuendesha uliopunguka waweza kuwahatarisha?
Katika nchi fulani, kama kwetu, Australia, kila dereva asiyejiweza mwenye umri wa zaidi ya miaka 65 aweza tu kupata upya leseni ya kuendesha magari kwa mwaka mmoja kila pindi—na hilo ni baada ya kupata cheti cha daktari kionyeshacho kuwa hana tatizo lolote la kitiba ambalo laweza kupunguza uwezo wake wa kuendesha gari zaidi.
Gari Langu na Huduma Yangu
Katika kizazi hiki kilicho mbioni, gari limekuwa kitu cha lazima kuwa nacho kwa Wakristo katika nchi fulani. Magari yamewasaidia kufikia maelfu, labda hata mamilioni ya watu wakiwa na habari njema za Ufalme wa Mungu. (Mathayo 24:14) Hivyo ndivyo ilivyo hasa kwa wenye vizuizi kama mimi. Gari langu, ambalo limerekebishwa lifae mahitaji yangu ya kibinafsi, huniwezesha kuwaambia wengine imani yangu ya kuwa kuna ulimwengu mpya utakaokuja karibuni ambao hautakuwa na aksidenti, magonjwa, na kutojiweza kokote. (Isaya 35:5, 6) Watu fulani wasiojiweza hata wameweza kutumikia wakiwa waevanjeli wa wakati wote.
Mmoja wa Mashahidi wa Yehova ambaye hutumia kiti cha kusukumwa katika Iowa, Marekani, ameweza kufanya hivi kwa miaka mingi. Yeye aeleza kuwa gari lake limemsaidia sana; Shahidi mwenzake alibuni vifaa vyalo vya pekee vya kuliongoza, kama vile kifaa kimwinuacho na kumwingiza garini. Akiwa ndani, yeye hutoka kwenye kiti cha kusukumwa na kuketi kwenye kiti cha dereva. Yeye asema: “Kwa njia hii nimeweza kuondoka na kuwatembelea watu kwa ukawaida nyumbani mwao, nami kwa kawaida naweza kuongoza mafunzo ya Biblia kadhaa.”
Katika kisa changu, ingawa siwezi kuhubiri kwa wakati wote katika huduma, hata hivyo gari langu lililorekebishwa limekuwa lenye thamani sana katika kazi yangu ya kuhubiri. Kwa miaka mingi nilienda mlango kwa mlango kwa kutumia mikongojo, lakini kadiri muda ulivyozidi kupita, kule kutumia mikono na mabega yangu kuliniathiri vibaya. Hivyo nikalazimika kuvumbua njia nyingine isiyo ya kuchosha sana. Niwe nahubiri mjini au mashambani, mimi huchagua nyumba zenye barabara za magari ili niweze kuendesha gari hadi karibu na mlango.
Kwenye ziara yangu ya kwanza, kwa kawaida mimi huliacha gari, na kutembea hadi kwenye mlango wa mbele kwa kutumia mikongojo, na kwa ufupi kueleza kusudi la ziara yangu. Mwenye nyumba akionyesha upendezi fulani katika ujumbe, mimi hujaribu kuanzisha urafiki ili kwamba ziara zitakazofuata naweza kuwa huru kupiga honi ili kumjulisha nimefika—kisha wao huja.
Mfikio huo una matokeo. Badala ya kuhisi kwamba wanasumbuliwa, wenye nyumba wengi hukubali kuketi kwenye gari pamoja nami kwa kipindi fulani ili tuweze kuzungumza kwa starehe, bila kutatizwa na hali-hewa. Sikosi kamwe kuwa na wenye nyumba kadhaa wanaokaribisha ziara yangu na wanaotazamia kuzungumza ujumbe wa Biblia wenye kutia moyo na kupata magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! ya karibuni zaidi.
Bila shaka, hali ya kila mtu asiyejiweza ni tofauti. Lakini huenda kuendesha gari kutakuletea manufaa kama yale ambayo kumeniletea—uhakika mpya, kujitegemea, fursa ya kusaidia wengine, na furaha kubwa itokanayo na kuweza kusema, “Naenda kuendesha gari!”—Kama ilivyosimuliwa na Cecil W. Bruhn.
[Sanduku katika ukurasa wa14]
Jinsi Magari Hurekebishwa Yawafae Wasiojiweza
MADEREVA walio wengi wasiojiweza hutumia mikono yao kufanya yale ambayo miguu yao haiwezi kufanya. Aina moja ya kifaa cha mkono cha kuongoza gari hasa ina manufaa. Hiyo ni wenzo utosheao vizuri chini ya usukani nao hutokeza kwenye nguzo ya usukani. Ufito wa feleji hutoka kwenye wenzo hadi kwenye kikanyagio cha breki. Kuusukuma wenzo mbele hushika breki.
Kwenye mfumo uo huo, kuna waya iliyounganishwa na kichapuzi. Wenzo una mwendo wa aina mbili: mwendo wa mbele ili kushika breki na mwendo wa juu ili kuongeza mwendo. Hiyo haihitaji nguvu nyingi. Faida hususa ya mwongozo wa aina hii wa mkono wa gari ni kwamba hauwazuii wengine kuendesha hilo gari kwa njia ya kawaida. Kwa kuongezea, mfumo huo wote waweza kuhamishwa kwa urahisi kwa magari mengine.
Kwa ajili ya wale wasio na nguvu za kutosha mikononi, aina tofauti ya kifaa hicho cha mkono hupatikana. Hicho hufanya kazi kwa njia hiyohiyo, kikiwa na mwendo wa mbele ili kushika breki, na kuelekea chini ili kuongeza mwendo wa gari hivi kwamba uzito wa mkono tu hulichapua gari.
Namna Gani Kiti cha Kusukumwa?
Tatizo la ziada humkumba dereva asiyejiweza: Apaswa kufanya nini na kile kiti cha kusukumwa? Madereva wengi wachanga hununua magari yenye milango miwili yanayowawezesha kuweka kiti cha kusukumwa nyuma ya kiti cha dereva. Bila shaka, hilo huhitaji nguvu nyingi kwenye mikono na mabega. Wasio na nguvu za kutosha hulazimika kusubiri mpita njia mwenye urafiki awaingizie kiti ndani ya gari.
Njia moja iwezayo kutumika ni ile ya kipandisha-kiti cha kusukumwa ambacho ni sanduku kubwa lililotengenezwa kwa nyuzi na kioo ambalo huwekwa juu ya gari. Kwa kubonyeza kibonyezo tu, mota ndogo huinamisha lile sanduku hivi kwamba kiti cha kusukuma chaweza kuingizwa kwa kutumia roda. Baada ya kukiweka, hilo sanduku hujilainisha tena. Kipandishi kama hicho kipatikanacho Australia hupata nguvu za umeme kwa kuingia kwa njia nzuri katika kiwasha-sigareti.
Jambo moja lisilo zuri juu ya kipandisha kiti cha kusukumwa ni kwamba hicho hupunguza mwendo wa gari kwa sababu ya upepo uvumao, jambo ambalo huongeza matumizi ya mafuta kwa asilimia 15 hadi 20. Kwa kuongezea, gharama yacho yenyewe yaweza kuwa ya juu sana. Hata hivyo, wengi bado huona vichukuzi hivyo kuwa vyenye mafaa kwa sababu hivyo humfanya mtu ajitegemee. Mwanamke mmoja asiyejiweza alisema: “Sasa naweza kwenda popote mwenyewe bila kuhitaji mtu kuwa pamoja nami mwishoni mwa safari yangu ili asaidie kushusha kile kiti cha kusukumwa.”
[Picha katika ukurasa wa 13]
Naweza kutoa ushahidi nikiwa kwenye gari langu