Mbung’o—Laana ya Afrika?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA
MAJUZI tulikuwa tumehamia eneo la mashambani la Afrika Magharibi. Misitu ya kitropiki ilituzunguka. Alasiri moja mke wangu aliingia kwenye chumba cha faragha na kupiga kelele hivi: “Kuna nzi-mfyonza-damu humu!”
Huyo nzi akatoka chumbani upesi na kuingia kwenye bafu. Nikachukua kikebe cha kiuawadudu na kumfuata, nikiufunga mlango nyuma yangu. Huyo nzi hakuonekana popote. Kwa ghafula akanirukia usoni. Yuanishambulia! Nikitupa mikono huku na huku, nilijaribu kumpiga bila mafanikio. Aliruka kwenye dirisha. Kiwambo kilimzuia asitoroke. Nzi huyo akatua juu ya kiwambo.
Nilimlenga na kumpulizia kiuawadudu. Kwa kawaida mpulizo kama huo huua karibu kila mdudu papo hapo. Lakini si nzi huyo. Aliruka na kuendelea kuzunguka kwenye bafu.
Ni vigumu kumuua nzi huyu! Nilikuwa na hakika kuwa kiuawadudu kingefanya kazi na huyo nzi upesi angeanguka sakafuni. Lakini hakuanguka. Alipotua tena, nilimpulizia mara ya pili. Akaruka tena.
Huyu nzi ajabu ni wa aina gani? Mipulizo miwili ya ziada iliyomlenga ilimuua.
Nilivaa miwani yangu na kumtazama kiumbe huyo kwa uangalifu. Alikuwa mkubwa kuliko nzi wa kawaida, ingawa si mkubwa kama nzi-mfyonza-damu. Mabawa yake yalikuwa yamekingamana mgongoni, yakimfanya aonekane mwembamba kuliko nzi wa kawaida. Kifyonzeo kilicho kama sindano kilitokeza karibu na mdomo.
Nilimwita mke wangu: “Huyu si nzi-mfyonza-damu. Ni mbung’o.”
Pambano hilo lilinifanya nifikirie ule ugumu wa kujaribu kumwangamiza huyo nzi katika makao yake ya Afrika ya kilometa milioni 11.7 za mraba, eneo lililo kubwa kuliko lile la Marekani. Ni kwa nini watu hutaka kumwangamiza? Anashtakiwa mambo matatu. Shtaka la kwanza:
Yeye Hujilisha Damu
Kuna aina 22 tofauti za mbung’o. Aina zote hizo huishi katika sehemu ya Afrika iliyo kusini mwa Sahara. Wote, wa kiume na wa kike, hujivimbisha kwa damu ya wanyama wenye uti wa mgongo, wakifyonza kiasi kilicho mara tatu ya uzito wao kwa umo moja.
Wao hujilisha kutokana na wanyama walao nyasi wa aina nyingi tofauti-tofauti—wale wa Afrika na wasio wa Afrika. Wao huwauma watu vilevile. Umo ni la kina, la kufyonza damu, kali na chungu. Huwasha na kuuma wakati uleule. Huvimba.
Mbung’o waijua kazi yao sana. Hawapotezi wakati wakizunguka-zunguka kichwa chako. Waweza kuruka kuelekea mtu kama risasi na kwa njia fulani kupiga breki na kutua polepole sana usoni hivi kwamba hawahisiwi. Waweza kuwa kama wezi; wakati mwingine huna habari kuwa wameiba damu yako hadi wakati ambapo wameenda—wakati ambapo huna la kufanya ila kushughulikia madhara.
Kwa kawaida wao hushambulia sehemu za mwili zilizo wazi. (Yaonekana wanapendelea upande wa nyuma wa shingo yangu!) Hata hivyo, nyakati nyingine wao huamua kutambaa katika suruali au shati kabla ya kufyonza damu kutoka kwa mshipa wa damu. Wakipenda waweza kuuma kupitia mavazi—hilo si tatizo kwa mdudu awezaye hata kudunga ngozi ngumu ya kifaru.
Watu husema kwamba mbung’o si mwerevu tu bali pia ni mjanja. Wakati mmoja nilipojaribu kumuua mmoja kwa kutumia kiuawadudu, aliruka na kuingia chumba changu cha faragha na kujificha kwenye mavazi yangu ya kuogelea. Siku mbili baadaye nilipovaa hayo mavazi, aliniuma mara mbili! Kwenye pindi nyingine mbung’o alijificha kwenye kibeti cha mke wangu. Mke wangu alienda na kibeti hicho ofisini, na alipoingiza mkono wake ndani yacho, huyo mbung’o aliuuma mkono wake. Kisha mdudu huyo akaruka chumbani, akisababisha ghasia miongoni mwa wafanyakazi wa hiyo ofisi. Kila mtu aliacha kufanya kazi ili kujaribu kumuua.
Hivyo shtaka la kwanza dhidi ya mbung’o ni kwamba yeye ni mfyonza-damu mwenye umo kali. Shtaka la pili:
Huua Wanyama
Aina fulani ya mbung’o hupitisha maradhi yasababishwayo na vimelea vidogo sana viitwavyo trypanosomes. Mbung’o hao wafyonzapo damu ya mnyama aliye na ugonjwa huo, humeza damu yenye hivyo vimelea. Vimelea hivyo hukua na kugawanyika ndani ya mbung’o huyo. Mbung’o amuumapo mnyama mwingine, vimelea hutoka kwa mbung’o na kuingia kwenye mfumo wa damu wa mnyama wa pili.
Hayo maradhi ni trypanosomiasis. Aina ya maradhi hayo iwapatayo wanyama huitwa nagana. Vimelea vya nagana huishi vizuri katika damu ya wanyama wa Afrika, hasa paa, nyati, nguruwe-mwitu, funo, tohe, na ngiri. Vimelea haviwaui wanyama hawa.
Lakini vimelea hivyo huangamiza mifugo isiyo ya Kiafrika—ngamia, mbwa, punda, mbuzi, farasi, nyumbu, fahali, nguruwe, na kondoo. Kulingana na gazeti National Geographic, nagana huua ng’ombe milioni tatu kila mwaka.
Wachunga-ng’ombe, kama vile Wamaasai wa Afrika Mashariki, wamejifunza jinsi ya kuepuka maeneo ambayo yana mbung’o wengi, lakini ukame na ukosefu wa malisho nyakati nyingine hufanya hilo lisiwezekane. Wakati wa ukame wa majuzi, familia nne zilizoweka ng’ombe wao 600 pamoja zilikuwa zikinyang’anywa mnyama mmoja kila siku na mbung’o. Lesalon, mzee wa familia miongoni mwao, alisema: “Sisi Wamaasai ni watu wenye moyo mkuu. Sisi humchoma simba kwa mkuki na kukabiliana na nyati mwenye hasira. Sisi hupiga kwa rungu songwe-mweusi na kumkabili tembo aliye na hasira. Lakini orkimbai [mbung’o]? Hatuna la kufanya.”
Kuna dawa za kuponya nagana, lakini serikali fulani huruhusu zitumiwe chini ya uangalizi wa daktari wa wanyama tu. Kuna sababu nzuri ya kufanya hivyo, kwa kuwa kutumia madawa nusu-nusu hakumaanishi kifo kwa mnyama tu bali pia hutokeza vimelea viwezavyo kuyakinza madawa. Huenda ikawa vigumu kwa mchunga-ng’ombe aliye mwituni kumpata daktari wa ng’ombe kwa wakati ili aponye wanyama wake wanaokufa.
Mashtaka mawili ya kwanza dhidi ya mbung’o yamethibitishwa pasipo shaka lolote—yeye hujilisha damu na hueneza maradhi yauayo wanyama. Lakini kuna zaidi. Shtaka la tatu:
Huua Watu
Wanadamu hawadhuriwi na vimelea vya nagana. Lakini mbung’o hupitisha aina nyingine ya vimelea kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Aina hiyo huitwa malale. Usidhani kuwa mtu mwenye malale hulala sana tu. Maradhi hayo si usingizi wa kustarehesha. Hayo huanza na kujisikia vibaya, uchovu, na homa-homa. Baada ya hayo huja kusinzia kwa muda mrefu, homa kali, maumivu ya viungo, tishu zilizovimba, na kuvimba kwa ini na wengu. Kuelekea mwisho, vimelea viingiapo kwenye mfumo-neva mkuu, mgonjwa huugua kutokana na kupotewa na akili, kifafa, kuzirai, na kifo.
Mapema karne hii, mieneo ya malale iliikumba kontinenti ya Afrika. Kati ya 1902 na 1905, hayo maradhi yaliua karibu watu 30,000 karibu na Ziwa Viktoria. Miongo iliyofuata, hayo maradhi yalienea na kuingia Kamerun, Ghana na Nigeria. Katika vijiji vingi thuluthi ya watu iliambukizwa, na watu wengi walilazimika kuhama kutoka mabonde ya mito. Vikundi vyenye kuzunguka vilitibu maelfu ya watu. Mweneo huo uliendelea hadi 1930 wakati ambapo ulififia na kutoweka.
Leo hayo maradhi huwapata watu 25,000 hivi kila mwaka. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, zaidi ya watu milioni 50 katika nchi 36 za kusini mwa Sahara zimo hatarini mwa kupata hayo maradhi. Ingawa maradhi ya malale hufisha yasipotibiwa, kuna dawa za kuyatibu. Majuzi dawa iitwayo eflornithine iliundwa ili kuyatibu hayo maradhi—dawa mpya ya kwanza ya aina hiyo kwa muda wa miaka 40.
Wanadamu wamepiga vita kwa muda mrefu dhidi ya mbung’o na maradhi abebayo. Katika 1907, Winston Churchill aliandika juu ya kampeni ya kumaliza mbung’o hivi: “Jitihada nyingi sana zinafanywa ili kuzuia asiongezeke.” Tuangaliapo nyuma ni wazi kuwa “jitihada nyingi sana” za Churchill hazikufua dafu. Chasema kitabu Foundations of Parasitology: “Kufikia sasa, miaka 80 ya jitihada ya kumwangamiza mbung’o imekuwa na matokeo kidogo sana juu ya kuwepo kwa mbung’o.”
Jambo la Kumtetea
Mtunga-mashairi wa Marekani Ogden Nash aliandika: “Mungu kwa hekima Yake alimuumba mbung’o, na kisha akasahau kutupa sababu.” Ingawa ni kweli kuwa Yehova Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, kwa hakika si kweli kwamba yeye ni msahaulifu. Yeye huacha tujijulie mambo mengi. Namna gani basi juu ya mbung’o? Je, kuna lolote liwezalo kusemwa ili kumtetea mdudu huyo mwovu?
Huenda utetezi wenye nguvu zaidi kufikia sasa ni kuwa lile fungu lake katika kuangamiza ng’ombe limesaidia kulinda wanyama wa pori wa Afrika walioko bado. Maeneo makubwa ya Afrika hufanana na nyika za magharibi Marekani—nchi yenyewe ina uwezo wa kulisha wanyama wa kufugwa. Lakini kwa sababu ya mbung’o, wanyama wa kufugwa huuawa na vimelea ambavyo haviui wanyama walao nyasi katika asili yao.
Wengi huamini kuwa ikiwa si mbung’o, mbuga za wanyama kubwa-kubwa za Afrika zingekuwa zimetoweka muda mrefu uliopita, na mahali pao kuchukuliwa na makundi ya ng’ombe. “Naunga mkono mbung’o,” akasema Willie van Niekerk, mwongozi katika mbuga ya wanyama ya Botswana. “Mwangamizeni mbung’o nao ng’ombe watashambulia, na ng’ombe ndio huharibu Afrika, wakifanya hiyo kontinenti kuwa bara kubwa la jangwa tupu.” Aliongeza hivi: “Mbung’o lazima aendelee kuwapo.”
Bila shaka, si wote wanaokubaliana na hayo. Kusababu hivyo hakusadikishi mtu awaangaliaye watoto au ng’ombe wake wakiugua kutokana na vimelea hivyo. Wala hakusadikishi wale wabishao kuwa Afrika yahitaji ng’ombe ili ijilishe.
Licha ya hayo, hakuna shaka kuwa kuna mengi zaidi ya kujifunza juu ya fungu la mbung’o katika mambo ya asili. Ingawa mashtaka dhidi yake yaonekana kuwa na nguvu, labda ni mapema mno kutoa hukumu.
Tuzungumzapo juu ya nzi, mmoja ameingia sasa hivi chumbani. Niwieni radhi nihakikishe kuwa si mbung’o.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]
Mbung’o: ©Martin Dohrn, The National Audubon Society Collection/PR