Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 6/8 kur. 24-26
  • “Waltzing Matilda”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Waltzing Matilda”
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Waltzing Matilda” Humaanisha Nini?
  • Umashuhuri wa “Matilda” Waongezeka
  • Je, Wimbo Huo Una Ujumbe?
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Shiriki Kuimba Wimbo wa Ufalme!
    Mwimbieni Yehova
  • Shiriki Kuimba Wimbo wa Ufalme!
    ‘Mwimbieni Yehova kwa Shangwe’
  • Shiriki Wimbo wa Ufalme!
    Mwimbieni Yehova Sifa
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 6/8 kur. 24-26

“Waltzing Matilda”

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

WIMBO wa Australia “Waltzing Matilda” wajulikana sana ulimwenguni kote. Upendezi mwingi wa ghafula wa huo wimbo ulitokea mwaka jana katika msherehekeo wao wa miaka mia moja tangu uimbwe kwa mara ya kwanza hadharani katika Aprili 6, 1895.

Wimbo sahili huo ulio na maneno ya kifumbo ulikujaje kupendwa na wengi, si katika Australia yote tu bali katika nchi nyingi za ulimwengu? Kuna masimulizi yenye kupingana juu ya chanzo halisi cha wimbo huo. Hata hivyo, linalokubaliwa na wengi ni kwamba mtungaji wa wimbo huo alikuwa A. B. (Banjo) Paterson, ambaye mashairi yake yalikuja kuuzwa zaidi Australia mwishoni mwa miaka ya 1800 na mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Maneno ya “Waltzing Matilda” hutofautiana, lakini kwa wazi hadithi ni juu ya mbeba-shanta. Shanta ni mfuko wa kubebea vitu vya kibinafsi, naye mbeba-shanta ndiye abebaye hiyo shanta asafiripo. Katika wimbo huo huyo mbeba-shanta amepiga kambi kando ya kijito kidogo cha mto, kiitwacho billabong kilichoko mashambani mwa Australia. Alipokuwa akichemsha maji katika sufuria yake juu ya moto, kondoo aliyelishwa vizuri, aitwaye jumbuck, akaja kunywa maji katika billabong iyo hiyo. Huyo mbeba-shanta akamshika huyo kondoo, akamuua, na kuweka nyama yake kwenye mfuko wake wa chakula. Mara tu alipomaliza kufanya hivyo, skwota mwenye shamba hilo akaja kwa farasi wake. (Maskwota walikuwa wakulima waliokuwa wamepata kibali cha kumiliki kwa “kukaa” huko. Baadaye, waliweza kusajili maeneo makubwa ya ardhi kuwa yao.) Skwota huyo aliambatana na polisi watatu waliokuwa wamepanda farasi. Ashtakiwapo kumwiba yule kondoo, na bila shaka akabiliwa na kifungo au mabaya hata zaidi, mbeba-shanta ambaye mambo yamemwendea mrama, aruka na kujitumbukiza katika billabong, na kufa-maji.

Ni kwa nini hadithi hii isiyowezekana inawavutia watu wengi hivyo? Elezo moja la sababu ni lile la Bruce Elder katika utangulizi wake wa kitabu Favourite Poems of Banjo Paterson cha Rex Newell. Adokeza kwamba huo wimbo ni taarifa ya jinsi Waaustralia watakavyo kujiona: “Unahusisha mengi zaidi ya hadithi tu ya mbeba-shanta anayeiba kondoo. Ni wonyesho jinsi tunavyochukia dhuluma na wenye mamlaka. Yule mbeba-shanta hufananisha kila Mwaustralia aliyewahi kutaka kukaidi wenye mamlaka ndogo . . . Ni afadhali kujitumbukiza katika billabong kuliko kuacha watu hao waongoze maisha yetu.” Lakini hata sababu ya kupendwa kwa wimbo huo iwe nini, “Waltzing Matilda” umekuwa wimbo wa mfano wa Australia kwa zaidi ya miaka 100.

“Waltzing Matilda” Humaanisha Nini?

Wimbo huo una mafungu manne, au beti nne fupi. Baada ya kila fungu korasi hufuata, ikianza na mistari isemayo:

Waltzing Matilda, Waltzing Matilda,

You’ll come a-waltzing Matilda with me.

Hiyo hufuatwa na mistari miwili ikirudia yale yaliyosemwa katika fungu lililotangulia. Huo wimbo hupata jina lao kutoka kwa korasi hiyo.

Ukosefu wa uhakika, hata ubishi, umetokea juu ya maana halisi ya “matilda” ni nini hasa na ni nani afanyaye “waltzing.” Elezo sahili litolewalo na watafiti huonekana kuwa lenye kutosheleza zaidi. Mwandikaji mmoja asema: “Paterson alikuwa . . . amependezwa na wabeba-shanta waliokuwa wakihama kutoka shamba moja hadi jingine wakiwa wamebeba vitu vyao vyote katika mfuko uliobebwa mabegani mwao. Alipenda lugha ya usemi waliyotumia wabeba-shanta hao. Kubeba shanta kuliitwa ‘kuweka kifurushi kwenye nundu’, ‘kuweka mfungo begani’, ‘kubeba laana’, au ‘waltzing Matilda.’”

Fasili dhahiri kwa maneno machache ya waltzing matilda iliyotolewa na Sydney May katika kitabu chake The Story of “Waltzing Matilda” husomeka: “Mavazi na vitu vya kibinafsi vilikuwa vimefunganywa pamoja na kisha kufungwa katika blanketi ambalo halikuwa limekunjwa. Kisha blanketi hilo lilifungwa kwenye kila pembe ya furushi, uzito ukiwa katikati, na kubebwa shingoni pembe ambazo hazikufungwa zikiwa zinaning’inia pande zote mbele na mkono mmoja kwa kawaida ukionekana kushikilia pembe moja.”

Umashuhuri wa “Matilda” Waongezeka

Sydney May afikia mkataa wa kwamba kule kuabiri kwa majeshi ya Australia hadi nchi nyinginezo wakati wa vita ya kwanza na ya pili za ulimwengu ndiko kulikoleta umashuhuri mkubwa jinsi hiyo wa huo wimbo “Waltzing Matilda” nje ya nchi ulikoanzia. Yeye atoa vielelezo hivi: “Mwaka wa 1941 katika Tel Aviv okestra za mkahawa ziliucheza wimbo huo mara tu Mwaustralia alipoingia mlangoni pa mkahawa; Kikosi cha Tisa kiliuimba kilipoingia Libya baada ya kuinyakua tena; meli ya vita ya Australia iliyojiunga na manowari za Uingereza, mapema katika 1917, ilikaribishwa na bendi ya Meli ya Kamanda iliyokuwa ikicheza ‘Waltzing Matilda’ na kabla ya Mwaustralia kuanza kutangaza redioni wimbo huo huchezwa.” Kati ya pindi zenye kuheshimiwa sana ambapo huo wimbo uliimbwa zilikuwa zile gwaride za kisherehe za Kutawazwa kwa Kikosi cha majeshi ya Australia katika Buckingham Palace, London, juma lililotangulia kutawazwa kwa Malkia Elizabeth 2.

Ripoti yenye kupendeza ya gazeti pia hutoa wazo fulani juu ya kupendwa sana kwa “Waltzing Matilda” na watu wa tabaka mbalimbali. Hiyo ripoti ya gazeti yasema: “Jioni moja baada ya [waziri mkuu wa Australia] Bw. Menzies kula pamoja na [waziri mkuu wa Uingereza] Bw. Churchill katika The Chequers na pamoja na kiongozi wa Wapiganaji Wafaransa Jenerali de Gaulle, walienda kwenye moja ya vile vyumba vingine. Sir Winston aliashiria nayo rekodi ya ‘Waltzing Matilda’ ikachezwa. Akiimba kwa furaha nyingi na hata akikaribia kucheza dansi chumbani, alitua kidogo na kumwambia Jenerali: ‘Huo ni mojawapo nyimbo nzuri zaidi ulimwenguni.’”

Akithibitisha zaidi kupendwa sana kwa “Matilda,” Richard Magoffin katika kitabu chake Waltzing Matilda—The Story Behind the Legend asema: “Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, ule wimbo wa billabong ulipelekwa mbali zaidi ulimwenguni, kokote majeshi ya Australia yalikoenda. Ulikuwa wimbo ulioamsha kumbukumbu za nyumbani kwa urahisi nao ulitambuliwa kwa urahisi kuwa wimbo wa Australia.” Yeye pia amnukuu mtayarishi wa sinema, Kramer, aliyechagua “Waltzing Matilda” uimbwe mara nyingi katika sinema On the Beach. Kramer alisema: “Huu ni wimbo ubadilikanao kwa njia nzuri sana. Waweza kuimbwa kama wimbo wa kitamaduni, wimbo wa kusawazisha mwendo wa askari, wimbo wa mapenzi au aina yoyote nyingine ya wimbo, nasi tumeutumia kwa njia nyingi tofauti-tofauti katika sinema ‘On the Beach’. Niliamua mara moja kwamba ‘Waltzing Matilda’ wapaswa kuwa wimbo mkuu katika nyimbo za hiyo sinema.”

Je, Wimbo Huo Una Ujumbe?

Watu fulani huamini kwamba Banjo Paterson alikuwa akitoa ujumbe kwa wale waliousoma au kuuimba wimbo wake. Kwa kielelezo, William Power aliandika makala katika Yale Review Marekani akionyesha mawazo fulani ya ndani yahusianayo na ujumbe uwezao kupatikana katika huo wimbo. Ni wazi kwamba si watu wote walikubaliana na maoni yake, hata hivyo, maelezo yake hufanyiza umalizio ufaao wa mchanganuo huu mfupi wa “Waltzing Matilda.” Alisema:

“Waaustralia wamelazimika kung’ang’ana si na nguvu za asili tu, bali pia na makosa ya asili ya kibinadamu. . . . Mivutano hiyo huelezwa katika ‘Waltzing Matilda’, washindani wakiwa watu wawili walio tofauti kabisa, skwota na mbeba-shanta. Katika pambano kama hilo, wengi wangesema kwamba skwota alistahili kushinda. Uchumi wa Australia hutegemea sana ustadi wake akiwa mfuga kondoo au ng’ombe. Yeye ni mwenye bidii, mwenye kuwajibika, mjasiri; ikiwa alikosa zozote za sifa tuhusianishazo na wa kwanza kukaa mahali hapo, hangefaulu. . . . Mbeba-shanta pia ni binadamu. . . . Yeye pia ni sehemu ya jamii. Wabeba-shanta wachache walifikia kuwa maskwota; wengi zaidi walifikia kiwango cha chini kidogo lakini chenye kuridhisha cha kuwa wakulima, wafanyakazi katika mashamba makubwa ya kondoo au ng’ombe huko Australia, mekanika, wafanyakazi wa majijini; wengine wakabaki bila mashamba na makao mpaka walipokufa na kutozikwa huku wakizurura kwenye vijia vya mashambani. Huenda jamii ikataka kwamba skwota amshinde mbeba-shanta, lakini haki za mbeba-shanta akiwa binadamu hazipaswi kamwe kusahauliwa.”

Sasa, zaidi ya miaka 100 imepita tangu wimbo huu sahili wa mashambani uandikwe. Banjo Paterson hakuwazia kwamba shairi lake lililofanywa kuwa wimbo lingekuwa wimbo wa Australia upendwao sana hivyo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki