Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kanisa Othodoksi Nikiwa Mkristo Mwothodoksi, fikira zangu zilivutwa na makala yenu “Kanisa Othodoksi la Kigiriki—Dini Iliyogawanyika.” (Januari 8, 1996) Wakati ujao mnapovunjia sifa Uothodoksi, mdhihirishe haki kwa kuzungumzia mafungu ambayo umechangia, kama vile jinsi ulivyohifadhi Ukristo wakati wa mnyanyaso wa Kiislamu na utawala wa Sovieti. Isitoshe, kutenganishwa kwa Kanisa na Serikali si jambo la Kibiblia. Je, serikali za Mfalme Daudi au Sulemani zilitenganishwa na Kanisa?
M. F., Marekani
Tulikazia tatizo ambalo wakati huu linakabili Kanisa Othodoksi—jambo ambalo limethibitishwa vyema sana na vyombo vya habari katika Ugiriki. Tatizo hili ni tokeo la ukosefu wa kanisa hilo kutii amri ya Yesu ya ‘kutokuwa sehemu ya ulimwengu’ na kutodumisha kutokuwamo kisiasa. (Yohana 17:16)—Mhariri.
Mishiko ya Hofu ya Ghafula Asanteni kwa makala “Kukabiliana na Mishiko ya Hofu ya Ghafula.” (Juni 8, 1996) Nimekuwa nikipatwa na mishiko hiyo kwa miaka 14 na kufikiri kwamba ni mimi tu niliyekuwa na tatizo hilo. Nyakati fulani hisia za hofu hata hunipata nikiwa kwenye Jumba la Ufalme. Ingawa huenda matatizo yangu yasiishe, makala hii imenisaidia kwelikweli.
C. C., Hispania
Nilisoma makala juu ya mishiko ya hofu ya ghafula kwa machozi mengi. Itanisaidia wakati ujao hisia za hofu zinijiapo tena. Nahisi kwamba makala hiyo ni jibu kwa sala zangu.
M. B., Scotland
Kwa karibu miaka 30, nimekuwa nikishindwa kupanda magari-moshi au basi au kuzungukwa na watu. Mikutano kwenye Jumba la Ufalme na mikusanyiko imekuwa tatizo kubwa. Kwa hiyo mwaweza kuelewa jinsi makala hii imekuwa chanzo cha kitia-moyo kikubwa na faraja kwangu. Nawashukuru kutoka ndani kabisa ya moyo wangu kwa kuandika kuhusu ugonjwa huu katika njia yenye kujenga na kufariji.
Y. T., Japani
Mimi ni mweneza-evanjeli wa wakati wote, na nimekuwa nikipatwa na mishiko ya hofu mibaya sana tangu 1994. Nilipoteza shangwe yangu na sikutaka kuondoka nyumbani kwangu. Nilifikiri hisia hizi zilisababishwa na ukosefu wa imani, lakini sasa najua kwamba mimi siye Mkristo pekee anayepitia hali hii.
S. A., Brazili
Waltzing Matilda Ule wimbo “Waltzing Matilda” huniletea kumbukumbu nizipendazo sana. Asanteni kwa makala hiyo (Juni 8, 1996) ambayo iliandaa habari ya msingi kuhusu wimbo huo. Kuisoma kumeamsha upendezi wangu katika kusoma makala zote katika Amkeni!
J. M., Germany
Adabu za Simu Asanteni kwa makala bora sana “Adabu Zako za Simu Zikoje?” (Juni 8, 1996) Nafanya kazi katika benki ambayo huandaa utumishi wa wateja kwa simu. Nilimpa msimamizi wangu makala hiyo, naye akaniambia kwamba aliiona ikiwa yenye manufaa sana, ya wakati ufaao, na yenye kutumika. Aliniomba niizungushe makala hiyo miongoni mwa maopareta wetu 32 wa simu.
N. J. S., Brazili
Tukiwa tumepata matatizo wakati uliopita na wapigaji simu wasiotakwa ambao walikuwa na nia za uhalifu, tumekuwa tukiendelea kufuata pendekezo la kampuni ya simu la kukata simu mpigaji akikataa kujitambulisha baada ya kumwomba mara tatu kwa heshima. Hilo limetokeza umizo la hisia mara kadhaa wakati rafiki amepiga na kucheza mchezo wa kisia ni nani huyu uliotajwa katika makala hiyo. Makala kama hizi huchochea fadhili na uelewevu hata katika maeneo kama hayo yasiyokuwa na umaana mkubwa.
G. A., Marekani