Hii Inaweza Kuwa Nchi Gani?
Watu katika mataifa ambayo yamesitawi huona hongo, ufisadi na umaskini kuwa zimeenea sana katika nchi za Kiafrika na za Amerika ya Latini. Basi nukuu lifuatalo lahusu nchi gani?
“Mawaziri wa serikali husema uwongo, wafanya biashara hufungwa gerezani kwa sababu ya ufisadi, watumishi wa serikali hushikwa wakichukua hongo, siasa hudunishwa, na [wanasiasa] huonwa kuwa wenye kutilika shaka, wanywaji wa kupindukia, na wenye tamaa ya kupita kiasi ya ngono. . . . Nchini kote, unyang’anyi katika barabara kuu umerudi. . . . Uhalifu wa kawaida umeandamana na ongezeko kubwa la ufisadi katika biashara, mambo ya kifedha, na katika utumishi wa umma. . . . Watu milioni 11 sasa wanakosa mambo matatu au zaidi ya mahitaji ya msingi ya maisha, . . . na idadi ya wanaoishi katika umaskini kabisa—wanaokosa mambo saba au zaidi yaliyo muhimu—imeongezeka kutoka milioni 2.5 hadi milioni 3.5.”—Phillip Knightley, The Australian Magazine.
Je, ulipata jibu? Jibu ni Uingereza. Lakini ni jambo la kuhuzunisha katika nyakati zetu kwamba mambo yaliyotajwa yanaweza kuhusu makumi ya nchi nyinginezo. Sisi sote twahitaji kama nini utawala mnyoofu, mzuri, na wenye kufuata haki! Ndiyo, twahitaji utawala wa Mungu kupitia Ufalme ule ambao Yesu alifundisha wafuasi wake wasali hivi kuuhusu, “Ufalme wako uje.”—Mathayo 6:9.