Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/8 kur. 16-19
  • Tulipu—Ua Lenye Historia ya Fujo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tulipu—Ua Lenye Historia ya Fujo
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tulipu za Uholanzi Zenye Asili ya Mashariki
  • Kichaa cha Tulipu—Kipindi Chenye Fujo
  • Upendo Waendelea
  • Mitakawa Iliokoa Uhai Wao
    Amkeni!—2000
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • “Mwangaza Kamili”
    Amkeni!—2002
  • Unaweza Kuboresha Kumbukumbu Lako
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/8 kur. 16-19

Tulipu—Ua Lenye Historia ya Fujo

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UHOLANZI

“MASIKA yajapo Uholanzi, ni kana kwamba maelfu ya eka . . . yapata uhai,” yasema Ofisi ya Utalii ya Uholanzi. Kwa ghafula, kwa mchanuko wa rangi, mistari miangavu ya tulipu zenye kuchanuka huvuka mashamba, zikifanyiza urembo wa maua ambao huvutia watalii kutoka ulimwenguni kote. Kwa wageni wengi, maua hayo mazuri ya bustani na yenye kupendwa sana ni kawaida sana Uholanzi kama tu vinuupepo, jibini, na viatu vya mbao. Lakini, je, ulijua kwamba tulipu hasa zilianzia Uturuki?

Tulipu za Uholanzi Zenye Asili ya Mashariki

Madoido ya Uturuki ya kuanzia karne ya 12 yaonyesha tulipu, lakini fasihi za Ulaya zataja tulipu kwa mara ya kwanza mnamo miaka ya 1550, asema mtaalamu wa mimea Adélaïde L. Stork. Katika 1553 msafiri mmoja kutoka Ufaransa aliandika kwamba “watu kutoka nchi za kigeni wenye kushangaa” walikuwa wakinunua “lili nyekundu kubwa [zisizo za kawaida]” katika soko za Constantinople (Istanbul). Wenyeji waliita ua hilo dülbend, jina limaanishalo “kilemba” katika Kituruki, na neno hilo, aeleza Dakt. Stork, likawa “chanzo asili cha neno ‘tulipu.’”

Mmoja wa wageni waliovutiwa na maua hayo yenye kufanana na kilemba alikuwa Ogier Ghislain de Busbecq, balozi wa Austria nchini Uturuki (1555-1562). Alichukua baadhi ya tulipu kutoka Constantinople hadi Vienna, ambako zilipandwa katika bustani za Ferdinand 1, maliki wa Hapsburg. Huko tulipu zilisitawi chini ya utunzi stadi wa Charles de L’Écluse—mtaalamu wa mimea Mfaransa aliyejulikana zaidi kwa jina lake la Kilatini, Carolus Clusius.

Kabla ya muda mrefu kupita, umashuhuri wa Clusius ulivuta uangalifu wa Chuo Kikuu cha Leiden katika Uholanzi, ambacho kilimbembeleza awe msimamizi wa bustani ya mimea ya chuo hicho kikuu. Mnamo Oktoba 1593, Clusius—na “mzigo wa tulipu”—akafika Leiden. Miezi kadhaa baadaye, katika masika ya 1594, bustani mpya ya Clusius, ikawa mahali pa tulipu ya kwanza kabisa kuchanua maua katika Uholanzi.

Kichaa cha Tulipu—Kipindi Chenye Fujo

Rangi nyangavu na maumbo ya kigeni ya tulipu yalivutia Waholanzi. Hadithi zenye kuvutia za jinsi masultani wa Uturuki walivyothamini sana tulipu zilifanya zitamaniwe na kila mwananchi aliyetaka umashuhuri. Baada ya muda mfupi, kukuza tulipu kukawa biashara yenye kufana sana, na wakati mauzo yalipoanza kushinda ukuzi wa tulipu, bei za tulipu zikapanda haraka sana na kutokeza enzi yenye fujo ambayo wanahistoria Waholanzi wanaiita tulpenwoede, au kichaa cha tulipu.

Kichaa cha tulipu kilifikia upeo katika miaka ya 1630 wakati ambapo tulipu zilikuja kuwa bidhaa zenye kupendwa zaidi ya zote. Siku hizo, asema mwanahistoria wa sanaa Oliver Impey, ilikuwa afadhali kununua mchoro wa tulipu uliochorwa na Jan D. de Heem (mchoraji maarufu wa vitu visivyo na uhai wa Uholanzi wa karne ya 17) kuliko kununua tulipu zilizokuwa nadra sana kupatikana. Ua moja tu la tulipu lilikubalika kuwa mahari, tulipu tatu zilikuwa na bei ya nyumba iliyojengwa kando ya njia za maji, na tulipu moja tu aina ya Tulipe Brasserie ilibadilishwa na kiwanda cha kutengeneza pombe chenye ufanisi. Wafanya biashara wa tulipu waliweza kuchuma karibu dola 44,000 (za kisasa za Marekani) kwa mwezi mmoja. “Katika mikahawa na majumba ya umma kote Uholanzi,” chasema chanzo kimoja, “mazungumzo yalihusu kitu kimoja tu—tulipu.”

“Bei zenye kufuliza kupanda kwa utaratibu zilishawishi familia nyingi za kawaida zenye mapato ya kiasi na zilizo maskini kuhatarisha fedha zao katika soko la tulipu ili kupata faida,” huongezea The New Encyclopædia Britannica. “Nyumba, mitaa, na viwanda viliwekwa rehani ili tulipu zinunuliwe na kuuzwa kwa bei za juu zaidi. Tulipu ziliuzwa na kuuzwa tena mara nyingi sana hata bila hizo kutoka ardhini.” Utajiri uliongezeka upesi mno. Maskini wakawa matajiri; matajiri wakawa matajiri zaidi. Biashara ya tulipu ikawa soko la kuhatarisha fedha lenye fujo sana mpaka kwa ghafula, katika 1637, kulipokuwa na wauzaji wengi kuliko wanunuzi—nalo soko likaporomoka. Kwa karibu usiku mmoja tu, maelfu ya Waholanzi wakatoka kwenye utajiri hadi umaskini.

Upendo Waendelea

Hata hivyo, upendo kwa tulipu uliendelea hata baada ya matokeo ya kichaa cha tulipu, na biashara ya tulipu ikaanza kusitawi tena. Hata kufikia karne ya 18, tulipu za Uholanzi zilikuwa zimekuwa maarufu sana hivi kwamba sultani mmoja wa Uturuki, Ahmed 3, aliingiza nchini mwake maelfu ya tulipu kutoka Uholanzi. Basi baada ya safari ndefu, uzao wa tulipu za Uturuki zilizokuwa Uholanzi ukarudi nchi yao ya awali. Leo, kukuza tulipu Uholanzi kumekuwa biashara kubwa sana—au biashara maridadi sana, kama ambavyo wengine husema. Kati ya kilometa za mraba 34,000 za nchi hiyo, karibu hektari 7,700 hutumiwa kukuza tulipu. Kila mwaka, wakuzaji 3,300 katika nchi hiyo huuza karibu tulipu bilioni mbili katika zaidi ya nchi 80.

Ingawa tulipu imekuwa na historia yenye fujo, upendo wa binadamu kwa ua hilo lenye kupendwa la bustani umekuwa thabiti. Karibu karne hizo zote ua hilo maridadi limefanya wasanii, washairi, na wanasayansi kuhifadhi umbo lalo lenye urembo na rangi zalo zenye kuvutia kwenye michoro na mashairi. Baada ya mmoja wao, mwanasayansi wa karne ya 18 Johann Christian Benemann kuandika simulizi katika Kijerumani juu ya tulipu, aliita simulizi hilo Die Tulpe zum Ruhm ihres Schöpffers, und Vergnügung edler Gemüther (Tulipu kwa Utukufu wa Muumba Walo na Furaha ya Watu Wenye Akili ya Uelekevu). Kwake mwenyewe na kwa watungaji wengine wa vitabu, asema Adélaïde Stork, tulipu “si kitu cha kutumiwa tu na mtunza-bustani, bali hiyo huonyesha ukuu na utukufu wa Muumba.” Ukitazama ua hilo lenye urembo, bila shaka utakubaliana nao.

[Sanduku katika ukurasa wa18]

Jinsi ya Kukuza Tulipu Zako

MAADAMU kuna maji ya kutosha, karibu kila aina ya udongo yafaa. Hata hivyo, kuipanda kwaweza kurahisishwa kwa kuchanganya udongo wa juu pamoja na mchanga, majani yaliyooza, au mbolea.

Panda tulipu wakati wa vuli. Kuna njia mbili za kufanya hivyo: Unaweza kuchimba shimo kwa kila tulipu, au unaweza kutengeneza mahali pa kupandia tulipu zote mara moja.

Njia moja ya kupanda tulipu: Shimo lapaswa liwe lenye kina kinachoshinda shina la tulipu mara mbili. Hilo lamaanisha kwamba sehemu ya chini ya tulipu (sehemu bapa) yapaswa kuwa sentimeta 20 hivi chini ya uso wa ardhi. Panda tulipu sentimeta 12 hivi kutoka kwa nyingine.

Funika tulipu hizo kwa udongo uliochimbwa, na umwagilie maji mara hiyo ili ukuzi uanze. Wakati wa baridi kali tabaka ya majani yaliyooza au mbolea ya majani itakinga tulipu na kuzuia udongo usikauke. Ondoa majani hayo wakati wa masika ambapo chipukizi huanza kuonekana kwa mara ya kwanza.

Kata maua yaanzapo kunyauka; la sivyo, mmea huo utazaa mbegu na kuinyima tulipu chakula kinachohitaji mwaka ujao. Acha majani yanyauke yenyewe, na uyaondoe yageukapo rangi ya manjano.

Badala ya kupanda tulipu moja pindi kwa pindi hapa na pale, panda tulipu za aina moja na rangi moja pamoja katika vikundi. Kwa njia hiyo utafanyiza rangi tofauti-tofauti katika bustani yako na kufurahia kabisa urembo huo wa maua.—International Flower Bulb Centre, Holland/National Geographic.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Ukurasa 16 chini: Nederlands Bureau voor Toerisme; Juu kushoto, katikati, na juu kulia: Internationaal Bloembollen Centrum, Holland; Ukurasa 17 chini: Nederlands Bureau voor Toerisme/Capital Press

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki