Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/22 kur. 6-9
  • Uhuru wa Kusema Je, Unatumiwa Vibaya?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uhuru wa Kusema Je, Unatumiwa Vibaya?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ponografia ya Kompyuta
  • Maoni Yenye Kupinga
  • Usitawi wa Kihistoria wa Uhuru wa Kusema
    Amkeni!—1996
  • Ponografia—Je, Ina Madhara?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Kwa Nini Ponografia Imeenea Sana?
    Amkeni!—2003
  • Madhara Yanayosababishwa na Ponografia
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/22 kur. 6-9

Uhuru wa Kusema Je, Unatumiwa Vibaya?

MLANGO wa karne ya 21 uko karibu kufunguka wazi. Hakuna shaka kwamba karne hiyo mpya italeta matumaini, miradi, mitazamo ya kiadili, dhana za tekinolojia zenye kushangaza, na madai ya kutaka uhuru zaidi. Tayari maoni ya kidesturi ya serikali, dini, na watu yanashindwa na maoni na madai mapya. Katika mahali pengi kuna madai yenye kusisitiza kuondolewa kwa vizuizi vya uhuru wa kusema na kujieleza, hata matokeo yawe nini!

Kile ambacho wakati mmoja hakikukubaliwa na kilikatazwa na watangazaji wa redio na televisheni na wachujaji—lugha chafu na mandhari na ishara za mwili za kiponografia—sasa ni jambo la kawaida katika nchi nyingi, likikubaliwa kwa kudai eti ni haki ya uhuru wa kusema!

Wenye ustadi katika kutumia kompyuta, watu wazima na vilevile watoto, sasa wanaweza kupitisha picha zilizo wazi za vitendo vichafu vya ngono hadi mabara mengine kwa sekunde chache tu na kuzungumza na wakosaji wa kingono na wenye kutendea watoto vibaya kingono wanaojulikana ambao huomba majina na anwani kwa ajili ya mikutano ya kisiri. Maneno ya muziki ambayo hudokeza na kutia moyo ujiuaji kimakusudi na kuua wazazi, polisi, na maofisa wa serikali sasa husikiwa kila siku kwenye redio na televisheni au kwenye mirekodi inayochezwa na watoto.

Wachache wa hao wanaodai uhuru wa kusema usiozuiwa wangekosa kukubaliana na Hakimu wa Mahakama Kuu Zaidi Oliver Wendell Holmes, Jr., ambaye nusu karne iliyopita aliandika uamuzi wa maana sana kuhusiana na uhuru wa kusema: “Uhuru wa kusema haungempa mtu haki ya kupaaza sauti kwa udanganyifu kwamba kulikuwa na moto katika jumba la maonyesho na kusababisha wasiwasi.” Matokeo ya kitendo hicho ni wazi. Basi ni kukosa kusababu vizuri kama nini, kwamba watu hawa wanaodai uhuru wa kusema usiozuiwa wasithamini adhabu itakayofuata ya uamuzi huohuo wa mahakama na kutenda kwa fujo kwa kuupinga. “Suala katika kila kisa,” akasema Holmes, “ni kama maneno yaliyotumiwa hutumiwa katika hali kama hizo na ni za asili ya kusababisha hatari ya wazi na ya kuendelea hivi kwamba maneno hayo yatatokeza maovu ambayo Bunge lina haki ya kuzuia.”

Ponografia ya Kompyuta

“Ngono iko kila mahali siku hizi,” likaripoti gazeti Time, “katika vitabu, magazeti, filamu, televisheni, vidio za muziki na matangazo ya manukato ya vibanda vya kungojea basi. Hiyo huchapwa katika kadi za biashara za huduma za kiponografia zipatikanazo kwa simu ambazo huingizwa chini ya vipanguso vya kioo cha gari. . . . Wamarekani wengi wamekuja kuzoea sana wonyesho wa wazi kabisa wa uamshaji wa ashiki—na wamezoea kutetea sababu za wonyesho wa wazi wa uamshaji wa ashiki kuwa na hadhi ya kipekee katika Marekebisho ya Kwanza [uhuru wa kusema]—hivi kwamba ni vigumu sana kwao kutambua kwamba ponografia iko.” Hata hivyo, kuna jambo fulani kuhusu kuchanganywa kwa ngono ya wazi kabisa na kompyuta ambalo limeleta hali na maana mpya kwa ulimwengu wa “ponografia.” Imekuja kupendwa na wengi, kuenea sana, na kuwa na mweneo wa ulimwenguni pote.

Kulingana na uchunguzi mmoja, waandikishaji wa mifumo ya kompyuta ya jumbe za ngono, ambao wako tayari kulipa ada za kila mwezi kuanzia dola 10 hadi 30, walipatikana katika majiji “zaidi ya 2,000 katika majimbo yote 50 ya Marekani na nchi 40, maeneo na mikoa ulimwenguni pote—kutia ndani nchi kama vile China, ambapo kupatikana na ponografia kwaweza kuwa kosa la kustahili adhabu ya kifo.”

Gazeti Time lilifafanua aina moja ya ponografia ya kompyuta kuwa “kifuko cha mambo ya siri chenye vitu ‘vyenye tabia iliyopotoka’ ambavyo hutia ndani raha ya kingono, kupata raha kutokana na kujitia au kutia wengine maumivu, ukojoaji, unyaji, na vitendo vya kingono pamoja na wanyama wengi tofauti.” Kuonekana kwa vitu kama hivi kwenye mfumo wa umma wa kompyuta, unaoweza kufikiwa na wanaume, wanawake, na watoto ulimwenguni kote, hutokeza maswali mazito kuhusu kutumiwa vibaya kwa uhuru wa kusema.

“Mara tu watoto waunganishwapo kwenye mfumo wa kompyuta,” likaonelea gazeti moja la habari la Uingereza, “ponografia zenye ngono halisi hazipatikani tu mahali ambapo itakuwa vigumu kwa watoto kufikia, bali zapatikana kwa utayari kwa mtoto yeyote, na hilo lamaanisha katika usiri wa chumba cha kulala.” Inatabiriwa kwamba asilimia 47 ya nyumba zote za Uingereza zenye kompyuta zitaunganishwa kwa mifumo ya kompyuta kufikia mwisho wa 1996. “Wazazi wengi wa Uingereza hawafahamu vidude vya kitekinolojia kama watoto wao. Katika miezi 18 ambayo imepita ‘kupitia-pitia mfumo wa Internet’ kumekuwa moja ya vipitisha-wakati vya matineja vipendwavyo sana,” gazeti hilo likasema.

Kathleen Mahoney, profesa wa sheria kwenye Chuo Kikuu cha Calgary, Kanada, pamoja na mtaalamu katika masuala ya kisheria yanayohusu ponografia, walisema: “Umma wapaswa kujua kwamba kuna njia isiyodhibitiwa kikamili ambayo kupitia kwayo watoto wanaweza kutendewa vibaya na kutumiwa vibaya.” Ofisa mmoja wa polisi wa Kanada alisema: “Ishara ziko wazi kwamba ongezeko kubwa katika visa vya ponografia ya watoto inayohusiana na kompyuta liko karibu kutukia.” Vikundi vingi vya kushauri familia husisitiza kwamba ponografia ya kompyuta inayoonwa na watoto na uvutano inayoweza kuwa nao juu yao “huwakilisha hatari ya wazi na iliyopo.”

Maoni Yenye Kupinga

Watetezi wa uhuru wa kiraia wanakasirishwa na jitihada zozote za Bunge kuzuia mambo kama vile ponografia ya kompyuta, sawa na uamuzi uliotolewa na Hakimu Holmes na Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani. “Ni shambulizi la moja kwa moja kwa Marekebisho ya Kwanza,” akatangaza profesa wa sheria wa Harvard. Hata waongoza-mashtaka wa muda mrefu waliudhihaki, likataja gazeti Time. “Hautastahimili uchanganuzi mwingi hata katika mahakama inayoshughulikia uhalifu mdogo-mdogo,” akasema mmoja. “Ni sawa na uchujaji wa serikali,” akasema ofisa mmoja wa Electronic Privacy Information Center. “Marekebisho ya Kwanza yapasa kutumiwa kuhusu Internet pia,” Time likamnukuu akisema. “Kwa wazi huo ni kukiuka uhuru wa kusema,” akatangaza mbunge mmoja wa Marekani, “ni uasi dhidi ya haki ya watu wazima kuwasiliana.

Profesa mmoja kwenye Shule ya Kisheria ya New York asababu kwamba kuna manufaa katika njia kadhaa za kujieleza kuhusu ngono, nje ya mweneo wa haki za kiraia na uhuru wa kusema. “Ngono kwenye Internet yaweza hasa kuwa nzuri kwa vijana,” Time likaripoti juu ya maoni yake. “[Ulimwengu wa kompyuta] ni mahali salama pa kuvumbua mambo yaliyokatazwa na yaliyo mwiko . . . Huandaa uwezekano wa mazungumzo ya kikweli bila haya kuhusu picha za akilini za kifantasia zilizo sahihi za ngono,” yeye akasema.

Wenye kuteta pia dhidi ya vizuizi vyovyote vya ponografia kwenye mifumo ya kompyuta ni vijana wengi, hasa wanafunzi wa chuo kikuu. Wengine wameandamana kwa kupinga kile wanachoona kuwa kunyimwa haki za uhuru wa kusema. Ingawa hakuwa mwanafunzi, maoni ya mtu mmoja yaliyonukuliwa katika The New York Times bila shaka hukubaliana na maoni ya wengi ambao hupinga dokezo lolote ambalo lingekataza ponografia kwenye kompyuta: “Nashuku hilo litachekelewa kwa ujumla na watumizi wa Internet wa nchi hii na kupuuzwa, na kwa habari ya watumizi wengine wa ulimwenguni wa Internet, litafanya Marekani ichekelewe.”

Katika kuripoti taarifa kutoka kwa ofisa wa kikundi cha kutetea uhuru wa kiraia, U.S.News & World Report lilisema: “Huenda ulimwengu wa kompyuta [mifumo ya kompyuta] ukaimarisha zaidi uhuru wa kusema kuliko Marekebisho ya Kwanza yafanyavyo. Kwa hakika, huenda tayari ‘limekuwa jambo lisilowezekana kihalisi kwa serikali kunyamazisha watu.’”

Katika Kanada, mabishano yanapamba moto juu ya kile kiwezacho kuvunja maandalizi ya uhuru wa kujieleza katika Mwafaka wa Haki na Uhuru. Wachoraji wameshikwa ambao michoro yao imetokeza hasira ya wahakiki na polisi, ambao huiweka katika kikundi cha “mambo machafu.” Wachoraji na watetezi wa usemi huru wameungana ili kupinga na kukataa kushikwa wakiona huko kuwa kuingiliwa kwa uhuru wao wa kusema. Hadi miaka minne hivi iliyopita, kanda za vidio za ponografia zilikamatwa na polisi kikawaida chini ya sheria ya Kanada ya mambo machafu, na kesi zilifanywa na wafanya biashara walioziuza kuadhibiwa.

Hata hivyo, yote hayo yalibadilika katika 1992, wakati Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada ilipotoa uamuzi katika kesi yenye umaana sana kwamba bidhaa hizo hazingeshtakiwa kwa sababu ya uhakikisho wa uhuru wa kusema katika Mwafaka wa Haki na Uhuru. Uamuzi wa mahakama “umeleta mabadiliko ya maana kwa jamii ya Kanada,” likaandika gazeti Maclean’s. “Katika majiji mengi sasa ni kawaida kupata magazeti na vidio za ponografia zenye ngono halisi katika maduka ya barabarani,” gazeti hilo likataja. Hata zile ambazo mahakama imetoa uamuzi kwamba zaweza kupigwa marufuku bado zapatikana kwa wateja.

“Najua ukienda ndani pale utapata vitu ambavyo huenda vikawa kinyume cha sheria,” akasema ofisa mmoja wa polisi. “Hivyo ndivyo vitu ambavyo tungeweza kuviwekea mashtaka. Lakini . . . hatuna wakati huo.” Pia hawana uhakikisho kwamba mashtaka hayo yataonwa kuwa yenye kusadikisha na halali. Katika muhula huu wa kuruhusu kila jambo, uhuru wa kibinafsi unapewa uangalifu wa kipekee usio na mipaka, na mara nyingi maoni ya umma huwa na uvutano juu ya mahakama. Lakini hata msingi uwe nini, mjadala utaendelea kutokeza hisia za kina na zenye kugawanya pande zote mbili—zenye kuunga mkono na zenye kupinga.

Hapo zamani za kale, Japani ilijikuta yenyewe chini ya vizuizi vizito vya uhuru wa kusema na wa vyombo vya habari. Kwa kielelezo, tetemeko la dunia lililokuwa 7.9 kwenye kipimo cha Richter na kuua watu zaidi ya elfu moja halingeweza kuripotiwa waziwazi. Visa vya ufisadi na wapenzi kuuana katika miafaka ya ujiuaji kimakusudi havingeweza kuripotiwa. Wahariri wa magazeti ya habari walishindwa na vitisho vya serikali huku udhibiti ukiongezeka juu ya mambo ambayo watu fulani waliyaona kuwa yasiyo na maana. Hata hivyo, kufuatia Vita ya Ulimwengu 2, vizuizi viliondolewa na Japani ikapata uhuru zaidi wa kusema na wa vyombo vya habari.

Kwa hakika, mabadiliko yakapita kiasi wakati magazeti na vitabu fulani vya ucheshi vya watoto vilipojawa na michoro yenye kuamsha ashiki na iliyo michafu. Gazeti kuu la Tokyo, The Daily Yomiuri, lilionelea hivi wakati mmoja: “Labda moja ya ono lenye kushtua zaidi kwa mgeni aliyefika Japani karibuni ni wafanyabiashara wakisoma vitabu vya ucheshi vyenye upotovu wa kingono kwenye magari moshi ya Tokyo ya chini ya ardhi. Sasa yaonekana mwelekeo huo waathiri wanawake, huku ‘vitabu vya ucheshi vya wanawake vyenye picha za ngono halisi vikipatikana kwenye rafu za maduka ya vitabu na maduka makubwa.”

Katika 1995 gazeti la habari lenye kusifika Asahi Shimbun liliita Japani “Paradiso ya Ponografia.” Ingawa wahariri na watangazaji walitafuta suluhisho la hiari kwa vipingamizi kutoka kwa wazazi badala ya maagizo ya serikali, wasomaji wachanga walipinga. Mtu angeuliza, ‘Ni sauti ya nani itakayoshinda hatimaye?’

Uhuru wa kusema ni mada ya ubishi mwingi sana wakati huu katika Ufaransa. “Bila shaka lolote,” akaandika mtungaji wa vitabu Mfaransa Jean Morange katika kitabu chake juu ya uhuru wa kusema, “historia ya uhuru wa kusema haijakwisha, nayo itaendelea kusababisha migawanyiko. . . . Karibu kila mwaka kuna kutolewa kwa filamu au kipindi cha televisheni au kampeni ya utangazaji isababishayo itikio kali, lenye kuamsha upya mjadala wa kale usiokwisha kuhusu uchujaji.”

Makala moja iliyokuwa katika gazeti la habari la Paris Le Figaro iliripoti kwamba kikundi cha rapu kitwacho Ministère amer (Huduma Chungu) kinahimiza mashabiki wacho kuua polisi. Mojapo mafungu ya maneno yao husema: “Hakutakuwako na amani isipokuwa [polisi] wafe.” “Kwenye muziki wetu,” akatangaza msemaji wa hicho kikundi, “twawaambia wachome vituo vya polisi na kutoa dhabihu [polisi]. Ni nini kingekuwa cha kawaida zaidi ya hicho?” Hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa dhidi ya kikundi hicho cha rapu.

Vikundi vya rapu katika Marekani pia huunga mkono uuaji wa polisi na kutangaza haki ya kusema hivyo chini ya ulinzi wa uhuru wa kusema. Katika Ufaransa, Italia, Uingereza na mataifa mengineyo katika Ulaya na ulimwenguni kote, kilio chaweza kusikiwa kutoka sehemu zote kikidai kwamba uhuru wa kusema haupasi kuzuiliwa hata ikiwa usemi huo ni “wa asili ya kutokeza hatari ya wazi na iliyopo.” Je, ubishi huo utakoma lini, na ni upande wa nani utakaoondokea kuwa mshindi?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Ponografia ya kompyuta, “kifuko cha mambo ya siri chenye vitu ‘vyenye tabia iliyopotoka’”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki