Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/22 kur. 3-5
  • Usitawi wa Kihistoria wa Uhuru wa Kusema

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Usitawi wa Kihistoria wa Uhuru wa Kusema
  • Amkeni!—1996
  • Habari Zinazolingana
  • Uhuru wa Kidini Wamaanisha Nini Kwako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Watu Huru Lakini Wanaotakwa Watoe Hesabu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Usikose Kusudi la Uhuru wa Kupewa na Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Karibuni Kwenye “Wapendao Uhuru” Mikusanyiko ya Wilaya!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/22 kur. 3-5

Usitawi wa Kihistoria wa Uhuru wa Kusema

KATIKA historia yote watu wamepigania uhuru wa kusema. Sheria zimepitishwa, vita vimepiganwa, na uhai umepotezwa kwa sababu ya haki ya kueleza wazo hadharani.

Kwa nini haki hiyo ionekanayo kuwa ya kiasili imetokeza ubishi, hata kufikia hatua ya umwagikaji wa damu? Kwa nini jamii, za kale na vilevile za wakati huu, zimeona likiwa jambo muhimu kuzuia au hata kukataza kudhihirishwa kwa haki hii?

Mitazamo kuelekea uhuru wa kusema kwa watu imebadilika kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine katika historia yote. Nyakati fulani uhuru wa kusema umeonwa kuwa pendeleo la kufurahiwa. Nyakati nyingine umeonwa kuwa tatizo la kuchukuliwa hatua na serikali au dini.

Kwa kuwa historia imejaa habari za wale waliopigania haki ya kueleza maoni hadharani, jambo ambalo mara nyingi liliongoza kwenye kunyanyaswa kwao au kuuawa kijeuri, pitio la baadhi ya matukio haya lapasa kutupatia ufahamu wenye kina kuhusu tatizo hilo.

Yaelekea wanafunzi wa historia wanamkumbuka mwanafalsafa Mgiriki Socrates (470-399 K.W.K.), ambaye maoni na mafundisho yake yalionwa kuwa uvutano wenye kufisidi maadili ya vijana wa Athene. Hili lilisababisha mtamauko mkubwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa na kidini wa utawala wa Kigiriki na kuongoza kwenye kifo chake. Ombi lake mbele ya baraza la mahakama ambalo hatimaye lilimhukumu labaki likiwa mojapo matetezi bora zaidi ya uhuru wa kusema: “Ikiwa mngejitolea kuniacha huru wakati huu kwa masharti kwamba siruhusiwi tena kueleza maoni yangu katika utafutaji huu wa hekima, na kwamba nikipatikana nikifanya hivi tena nitakufa, napaswa kuwaambia, ‘Watu wa Athene, nitamtii Mungu badala ya nyinyi. Mradi nina uhai na nguvu sitakoma kamwe kufuata falsafa na kuhimiza na kusadikisha yeyote wenu ambaye nitakutana naye. Nitafanya hivi kwa sababu, kwa hakika, hili ndilo analoamuru Mungu . . . ’ Na, Waathene, napaswa kuendelea kusema, ‘Ama mniachilie huru au sivyo; lakini fahamuni kwamba sitatenda tofauti kamwe, hata ikiwa nitalazimika kufa mara nyingi kwa sababu hiyo.’”

Kadiri wakati ulivyosonga, historia ya mapema ya Roma ilikuwa na vizuizi vichache zaidi kwa uhuru wa kusema, lakini baadaye vizuizi zaidi viliwekwa kadiri milki hiyo ilivyopanuka. Hilo lilitia alama mwanzo wa kipindi chenye kuhuzunisha zaidi kwa uhuru wa kusema. Wakati wa utawala wa Tiberio (14-37 W.K.), wale walioeleza maoni yao kwa ujasiri dhidi ya serikali au sera zayo hawakuvumiliwa. Na si Roma pekee iliyopinga uhuru wa kusema; ulikuwa wakati huu ambapo viongozi wa Kiyahudi walilazimisha Pontio Pilato amuue Yesu kwa sababu ya mafundisho yake na kuamuru pia mitume wake waache kuhubiri. Hawa pia walikuwa tayari kufa kuliko kuacha.—Matendo 5:28, 29.

Katika vipindi vingi vya historia, haki za kiraia zilizokubaliwa na serikali mara nyingi zilibadilishwa au kuondolewa kulingana na alivyotaka mtu fulani, jambo ambalo liliongoza kwenye mapambano ya daima ya uhuru wa kusema. Kuanzia na Enzi za Kati, baadhi ya watu walidai taarifa iliyoandikwa haki zao waziwazi, zikiwa na mipaka iliyowekewa udhibiti wa serikali kwa haki hizo. Likiwa tokeo, miswada yenye umaana ya haki ilianza kutayarishwa. Miongoni mwa hii mlikuwa na Magna Carta, tukio la maana sana kwa upande wa haki za kibinadamu. Baadaye kukaja Mswada wa Haki wa Uingereza (1689), Tangazo la Haki la Virginia (1776), Tangazo la Ufaransa la Haki za Mwanadamu (1789), na Mswada wa Haki wa Marekani (1791).

Karne za 17, 18, na 19 zilisikia sauti za watu mashuhuri wakisema kwa ujasiri wakitetea uhuru wa kujieleza. Katika 1644 mshairi Mwingereza John Milton, ambaye huenda anakumbukwa kwa shairi Paradise Lost, aliandika kijitabu kijulikanacho sana kiitwacho Areopagitica kikiwa bishano dhidi ya vizuizi vya uhuru wa waandishi wa habari.

Karne ya 18 ilishuhudia usitawi wa uhuru wa kusema katika Uingereza, ingawa vizuizi vilibaki. Katika Marekani koloni zilikuwa zikisisitiza zipate haki ya uhuru wa kusema, katika usemi na vilevile katika chapa. Kwa kielelezo Katiba ya Jumuiya ya Madola ya Pennsylvania, Septemba 28, 1776, ilitaarifu hivi kwa sehemu: “Kwamba watu wana haki ya uhuru wa kusema, na wa kuandika, na wa kutangaza maoni yao, hivyo uhuru wa uandishi wa habari haupaswi kuzuiwa.”

Taarifa hii ilikuwa kichocheo kwa Marekebisho ya Kwanza kwa Katiba ya Marekani katika 1791, ambayo ilitangaza kuwaza kwa waanzilishi wa Katiba ya Marekani kuhusu haki zilizothaminiwa za watu: “Bunge halitafanya sheria yoyote kuhusiana na kuanzishwa kwa dini, au kukataza kufuata dini kwa uhuru; au kunyima uhuru wa kusema, au wa uandishi wa habari; au haki ya watu kukusanyika kwa amani, na kuomba Serikali kurekebisha ukosefu wa haki.”

Mwanafalsafa Mwingereza wa karne ya 19 John Stuart Mill alitangaza insha yake “Katika Uhuru” katika 1859. Hiyo hunukuliwa mara nyingi na imekuwa ikirejezewa kuwa moja ya taarifa za maana zaidi katika kutetea uhuru wa kusema.

Hata hivyo, mapigano ya haki ya kusema kwa uhuru hadharani, hayakumalizikia kwa kuja kwa miaka iliyoonekana kuwa ya mnurisho ya hii karne ya 20. Kwa kielelezo, sababu ya jitihada za kuzuia uhuru wa kusema katika Marekani, mbiu za kutetea uhuru huo zimerudiwa-rudiwa katika mahakama, katika mahakama za chini na vilevile katika Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani.

Hakimu Oliver Wendell Holmes, Jr., wa Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani, alitaarifu itikadi yake katika uhuru wa kusema katika maamuzi kadhaa ya mahakama. Akifafanua mtihani wa usemi huru, yeye alisema: “Ikiwa kuna kanuni yoyote ya Katiba ambayo hudai sana uaminifu kuliko yoyote ile ni kanuni ya uhuru wa mawazo—si uhuru wa mawazo wa wale wanaokubaliana nasi bali uhuru kwa maoni tunayochukia.”—United States v. Schwimmer, 1928.

Ni kutotambua kanuni hii ambako kumetokeza mapigano ya mahakama ambayo huleta mabadiliko kati ya kukubaliwa na kuzuiwa kwa uhuru. Mara nyingi sana watu wamefuata dhana ya “Uhuru wa kusema kwangu—lakini si kwako.” Katika kitabu chake chenye kichwa hicho, Nat Hentoff, arejezea visa ambavyo katika hivyo watetezi wenye bidii wa Marekebisho ya Kwanza wamebadili maoni yao haraka kulingana na hali iliyowafaa. Yeye arejezea visa ambavyo katika hivyo Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani ilitangua baadhi ya maamuzi yayo yenyewe, kutia ndani mengine yenye kuhusu kesi zilizohusisha Mashahidi wa Yehova na miaka yao ya kupigania haki ya kusema kwa uhuru juu ya itikadi zao za kidini. Kuwahusu, yeye aliandika: “Washiriki wa dini hiyo wamechangia sana kupanuliwa kwa uhuru wa dhamiri kupitia kesi za kikatiba katika miongo ambayo imepita.”

Wachanganuzi wengi wa kisheria na wanahistoria wa kisasa wameandika kwa wingi sana juu ya mapigano tofauti-tofauti ya mahakamani kwa ajili ya kulinda uhuru wa kusema mwishoni-mwishoni mwa karne hii ya 20, si katika Marekani tu bali katika nchi nyinginezo vilevile. Uhuru wa kusema hauhakikishwi kamwe. Ingawa huenda serikali zikajidai kuwa na uhuru zinazowapa watu wazo, huo waweza kupotea serikali inapobadilika au mahakimu kubadilika, kama ambavyo imeonwa. Mashahidi wa Yehova wamekuwa katika mstari wa mbele katika pigano la uhuru huu wenye kuthaminiwa.

Katika kitabu chake These Also Believe, Profesa C. S. Braden aandika: “Wao [Mashahidi wa Yehova] wameandaa utumishi usio na kifani kwa demokrasi kwa pigano lao la kuhifadhi haki zao za kiraia, kwa kuwa katika mapambano yao wamefanya mengi ili kupata hizo haki kwa ajili ya kila kikundi cha wachache katika Marekani. Wakati haki za kiraia za kikundi chochote zinaposhambuliwa, hakuna haki za kikundi kingine zilizo salama. Kwa hivyo wamechangia sana kwa uhifadhi wa baadhi ya mambo yenye thamani sana katika demokrasi yetu.”

Watu wapenda-uhuru wanashindwa kuelewa ni kwa nini serikali na dini fulani zingezuia watu uhuru huu. Ni kunyimwa kwa haki ya msingi ya binadamu, na watu wengi ulimwenguni pote huteseka chini ya kukandamizwa kwa uhuru huu. Je, mitazamo kuelekea uhuru wa kusema itaendelea kubadilika-badilika hata katika nchi ambazo zina haki hii ya msingi? Je, lile wazo la uhuru wa kusema litatumiwa kutetea lugha zisizo za adili au zilizo chafu? Tayari mahakama zinapambana na bishano hilo.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Socrates alitetea uhuru wa kusema

[Hisani]

Musei Capitolini, Roma

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki