Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/22 kur. 19-21
  • Miaka 100 ya Sinema

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Miaka 100 ya Sinema
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Enzi ya Ukimya
  • Sauti na Rangi
  • Propaganda za Wakati wa Vita
  • Matatizo
  • Uvutano wa Kijamii
  • Je! Kuna Ubaya Hata Kama Ni Sinema Zipi Nionazo?
    Amkeni!—1991
  • Utatazama Sinema Zipi?
    Amkeni!—2005
  • Naweza Kuchaguaje Sinema ya Adabu?
    Amkeni!—1992
  • Ni Sinema Gani Zitakazoonyeshwa Msimu Huu?
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/22 kur. 19-21

Miaka 100 ya Sinema

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA

SINEMA haikuwa hasa tokeo la uvumbuzi fulani bali ilikuwa tokeo la utafiti na majaribio ya kimataifa kwa miaka ipatayo 75. Katika 1832, phenakistoscope, iliyovumbuliwa na Mbelgiji Joseph Plateau, ilifanyiza kwa mafanikio miendo kutokana na michoro mingi. Katika Ufaransa, kwa msaada wa Joseph Niepce na Louis Daguerre, mfumo wa kupiga picha wa kubadili uhalisi kuwa picha ukaweza kupatikana kufikia 1839. Mfaransa Emile Reynaud alisitawisha jambo hilo hata zaidi, akionyesha sinema zenye kusonga ambazo zilionwa na mamia ya maelfu ya watu kati ya 1892 na 1900.

Maendeleo makubwa ya sinema yalifanywa muda uzidio kidogo tu miaka 100 iliyopita. Katika 1890, Thomas Edison, yule mvumbuzi maarufu Mmarekani, na msaidizi wake Mwingereza, William Dickson, walibuni kamera yenye ukubwa na uzito wa piano ndogo, na mwaka uliofuata Edison aliomba haki ya kumiliki kinetoscope ya kuonwa na mtu mmoja. Hizo sinema, zikiwa zimerekodiwa katika filamu za milimeta 35 za seluloidi yenye mashimo, zilifanyizwa katika studio ya kwanza ya filamu ulimwenguni, iliyoitwa Black Maria, katika West Orange, New Jersey. Sinema hizo zilionyesha maonyesho, michezo ya kuigiza, sarakasi, mambo ya magharibi mwa Marekani na vilevile mandhari za michezo ya kuigiza yenye mafanikio ya New York. Mahali pa biashara ya kwanza ya kinetoscope palifunguliwa katika New York mwaka wa 1894, na mwaka uo huo mashine kadhaa zilisafirishwa Ulaya.

Ingawa hapo awali Edison hakuwa amependezwa na kuonyesha sinema kwenye kiwambo, alilazimika kutengeneza projekta ili kushinda ushindani aliopata. Ilikuwa katika Aprili 1896 ndipo vitascope yake ilipoanza kufanya kazi kwa mara ya kwanza katika New York. Ushindani wa haki ya umilikaji ambao alianzisha ulitokeza kuanzishwa kwa shirika la kudhibiti kabisa biashara ya sinema.

Ni nakala moja ya kinetoscope ya Edison iliyowachochea Auguste na Louis Lumière, wenye viwanda katika Lyons, Ufaransa, wabuni kamera ya kuendeshwa kwa mikono ambayo iliweza kupiga picha na pia kutokeza filamu katika kiwambo. Hiyo cinématographe (kutokana na Kigiriki kinema, linalomaanisha “mwendo,” na graphein, linalomaanisha “kuonyesha”) ilipata haki za umilikaji mnamo Februari 1895, na mnamo Desemba 28 “wonyesho rasmi wa kwanza wa sinema ulimwenguni ulifanywa,” kwenye Grand Café, 14 Boulevard des Capucines, Paris. Siku iliyofuata, wakazi wa Paris 2,000 walimiminika kwenye Grand Café wajionee ajabu hii ya majuzi zaidi ya sayansi.

Upesi akina Lumière ambao ni ndugu walikuwa wakifungua majumba ya sinema na kupeleka wapiga picha ulimwenguni pote. Kwa miaka michache tu, walifanyiza sinema zipatazo 1,500 za sehemu au matukio ya maana ulimwenguni, kama vile kutawazwa kwa Maliki Nicholas 2 wa Urusi.

Enzi ya Ukimya

Georges Méliès, mchawi na mwenye jumba moja la sinema Paris, alivutiwa na yale aliyoona. Alijitolea kununua cinématographe. Yaonekana alijibiwa hivi: “La, cinématographe haiuzwi. Na unishukuru, kijana; uvumbuzi huu hautafanikiwa.” Hata hivyo, bila kutishika Méliès akaanza kupiga picha za sinema akitumia vifaa vilivyoletwa kutoka Uingereza. Kwa kuongeza sauti na mandhari za pekee, Méliès aligeuza ufundi wa sinema kuwa ustadi. Katika 1902 sinema yake Le Voyage dans la lune (Safari ya Mwezini) ilipata mafanikio ya kimataifa. Katika studio yake kule Montreuil, kiungani cha Paris, alifanyiza zaidi ya filamu 500—nyingi zazo zikiwekewa rangi kwa mkono.

Kufikia karibu 1910, asilimia 70 ya sinema zilizopelekwa ulimwenguni pote zilikuwa za Kifaransa. Hiyo hasa ilitokezwa kwa kufanyizwa kwa sinema nyingi na akina Pathé waliokuwa ndugu, ambao walikuwa na mradi wa kwamba sinema iwe “wonyesho, gazeti, na shule za siku zijazo.”

Katika 1919, Charlie Chaplin, Douglas Fairbanks, David W. Griffith, na Mary Pickford walianzisha shirika la United Artists ili kuvunjilia mbali udhibiti wa shirika lile jingine. Katika 1915, sinema ya Griffith Birth of a Nation ikawa sinema ya kwanza ya Hollywood iliyopata mafanikio makubwa. Sinema hiyo iliyobishaniwa sana iliyohusu Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Marekani ilisababisha fujo na watu kadhaa hata wakafa ilipoanzishwa rasmi kwa sababu ya mambo yaliyomo yenye ubaguzi wa rangi. Hata hivyo, ilifanikiwa sana ikitazamwa na watu zaidi ya milioni 100, ikiifanya iwe mojayapo sinema zenye faida kubwa zaidi katika historia.

Baada ya vita ya ulimwengu ya 1, sinema “zilionyesha Marekani nzima ulimwengu wa vilabu vya usiku, vilabu vya mashambani, vilabu haramu na uovu wa kiadili wenye kuandamana navyo.” Sinema za kigeni karibu zipotee Marekani, huku sinema za Marekani zikifanyiza toka asilimia 60 hadi 90 za programu nyinginezo zote ulimwenguni. Sinema ilitumiwa kutukuza njia ya maisha ya Kimarekani na bidhaa za Marekani. Kwa wakati uo huo, “mfumo mpya wa wahusika wakuu” ulifanya watu kama Rudolph Valentino, Mary Pickford, na Douglas Fairbanks kuwa kama miungu.

Sauti na Rangi

“Mama, ebu sikiliza hili!” Kwa maneno hayo Al Jolson, katika sinema The Jazz Singer, ya 1927, alimaliza enzi ya sinema zisizo na sauti na kuingiza ulimwenguni sinema zenye sauti.” Majaribio pamoja na sauti inayoambatanishwa kwa kinanda yalifanywa tangu mwanzo kabisa wa sinema, lakini haikuwa mpaka miaka ya 1920, kwa kutokea kwa kurekodi kielektroni na kutumia vikuza sauti vya vali, ndipo sauti ikaweza kutumika. Kuingizwa kwa sauti kulikuwa na matatizo.

Awali rangi ilitumiwa katika sinema kupitia filamu zilizotiwa ukungu. Baadaye, stensili zikaanza kutumiwa. Filamu zilitiwa ukungu kwa sababu hakukuwa na mfumo mzuri wa kuweka rangi. Njia nyingi zilitumiwa mpaka mafanikio ya shirika la Technicolor lenye mfumo wa rangi tatu katika 1935. Hata hivyo, ni baada tu ya kupendwa sana kwa sinema Gone With the Wind katika 1939 ndipo rangi ilionwa kuwa kitu cha kuleta ufanisi mkubwa.

Propaganda za Wakati wa Vita

Wakati wa mshuko wa kiuchumi wa miaka ya 1930, sinema ilitumika ikiwa “kikengeushi cha watu.” Lakini ulimwengu ulipoelekea vitani, kazi ya sinema ikawa ya kutumia habari vibaya na propaganda. Mussolini aliita sinema “l’arma più forte,” au “silaha yenye nguvu zaidi,” na chini ya Hitler, sinema ikawa msemaji wa Nazi, hasa ili kufundisha wachanga. Sinema kama vile Der Triumph des Willens (Ushindi wa Nia) na Olympia zilitukuza sana viongozi wa Nazi kwa mafanikio. Kwa upande mwingine Jud Süss, iliendeleza uhasama dhidi ya Wayahudi. Na katika Uingereza, sinema ya Laurence Olivier Henry V ilitumika ikiwa kichocheo katika kujitayarishia siku kubwa ya vita na hasara ambazo zingetokea.

Matatizo

Baada ya vita ya ulimwengu ya pili, televisheni zilipopatikana kwa wingi zaidi, watu walikaa nyumbani badala ya kwenda kuona sinema. Hudhurio la sinema katika Marekani likashuka, likipunguka kwa nusu kwa miaka kumi tu. Maelfu ya majumba ya sinema yalilazimika kufungwa, na utokezwaji wa sinema ukapunguka kwa thuluthi, japo kuletwa kwa viwambo vikubwa vya sinema na sauti za stirio katika miaka ya 1950. Sinema zenye kufanikiwa sana zilizochuma mamilioni ya dola, kama vile Ten Commandments (1956) ya Cecil B. de Mille, zilitokezwa ili kujaribu kukinza mashindano ya televisheni. Sinema za Ulaya pia zilipatwa na upungufu katika hudhurio.

Uvutano wa Kijamii

Sinema imeitwa kioo cha jumuiya. Hivyo, sinema nyingi katika miaka ya 1970 zilionyesha “hangaiko, kutoridhika, kuvunjika moyo, wasiwasi, na ukichaa” wa wakati huo, kama iwezavyo kuonwa katika kurudishwa kwa sinema zenye kuogofya na “uvutio usio na kifani kwa ibada ya Shetani na mambo ya kifumbo.” Sinema za msiba zilitumika zikiwa “kikengeushi kutoka kwa misiba halisi ya maisha.” (World Cinema—A Short History) Kwa upande mwingine, miaka ya 1980 ikawa na kile ambacho mwandikaji wa magazeti Mfaransa alikiita “jaribio la kimakusudi la kufanya upotovu uwe jambo la kawaida.” Kati ya sinema zilizoonyeshwa kwenye Sherehe za Sinema Katika Cannes mwaka wa 1983, nusu ya sinema hizo zilikuwa na vichwa vya ugoni-jinsia-moja au ngono ya maharimu. Ujeuri umekuwa jambo kuu, au jambo la kurudiwa-rudiwa, la sinema za wakati huu. Katika 1992, asilimia 66 kati ya sinema za Hollywood zilikuwa na mandhari zenye ujeuri. Na ingawa jeuri katika siku zilizopita ilikuwa na kusudi, sasa inafanywa kiholela tu.

Matokeo ya kufunuliwa kwa mambo hayo yamekuwa nini? Mnamo Oktoba 1994, mwanamume mmoja na mwanamke mmoja wachanga ambao awali hawakuwa wahalifu walipovamia Paris, wakiua watu 4, sinema Natural Born Killers, ambamo wenzi wa ndoa waliua watu 52, ilihusika moja kwa moja. Zaidi na zaidi, wanasosholojia wanahangaikia uvutano ambao ujeuri unao—hasa juu ya vijana, ambao kwao mandhari kama hizo huwafanyizia vigezo vya tabia. Bila shaka, si sinema zote hutukuza ujeuri au ukosefu wa adili. Sinema za karibuni kama vile The Lion King zilivunja rekodi za awali za kutazamwa kwa wingi.

Mtengenezaji mmoja mashuhuri wa sinema aliye pia mchezaji wa kuigiza alipoulizwa na gazeti la Paris Le Monde jinsi ambavyo sinema imekuwa na uvutano katika jamii kwa miaka 100 ambayo imepita alijibu kwamba japo “imetukuza vita, kuwafanya majambazi waonekane mashujaa, kutokeza masuluhisho rahisi yasiyo ya kweli na hali za kimungu za kijuu-juu, kutokeza matumaini bandia, na kupendekeza ibada ya utajiri, mali, urembo mno wa kimwili, na miradi mingine mingi isiyo ya kihalisi na isiyofaa,” sinema imewapa mamilioni ya watu kikengeushi kutoka kwa mambo halisi yaliyo machungu katika maisha ya kila siku.

Taa zizimapo na sinema ianzapo, nyakati nyingine huenda tukahisi ile hisia ya ajabu ambayo iliwavutia sana watu zaidi ya miaka 100 ambayo imepita.

[Sanduku katika ukurasa wa21]

Ile “Photo-Drama of Creation”

Kufikia mwisho wa 1914, watu wapatao milioni tisa katika Australia, Ulaya, New Zealand, na Amerika Kaskazini walikuwa wameona sinema ya Watch Tower Society iitwayo “Photo-Drama of Creation” bila malipo. Programu hiyo ya muda wa saa nane yenye sehemu nne ilifanyizwa kwa picha zenye kusonga na za slaidi, ikiambatanishwa na sauti na muziki. Zote mbili slaidi na sinema ziliwekewa rangi kwa mkono. Hiyo “Photo-Drama” ilikusudiwa “ijenge ufahamu wa Biblia na kusudi la Mungu kama litajwavyo ndani yayo.” Mambo makuu yalitia ndani kufumuka kwa ua na kuanguliwa kwa kifaranga, kulikopigwa picha kwenye sinema kwa kutumia njia ya picha ya wakati. Angalau seti 20 zenye sehemu nne-nne zilitayarishwa, ikifanya iwezekane kwa sehemu moja ya “Photo-Drama” kuonyeshwa katika majiji tofauti-tofauti 80 kila siku na Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, kama Mashahidi wa Yehova walivyokuwa wakiitwa wakati huo.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Ile “Cinématographe Lumière,” iliyopata haki ya umilikaji mnamo Februari 1895

[Hisani]

© Héritiers Lumière. Collection Institut Lumière-Lyon

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

© Héritiers Lumière. Collection Institut Lumière-Lyon

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki