Maoni ya Biblia
Je, Uhofu Wafu?
TAJA habari kuhusu wafu, na watu wengi wataepuka kuongea zaidi kuihusu. Hata hivyo, wengine hawajihisi kutostareheka na habari hiyo tu; wao hukumbwa na hofu. Kwa hiyo si jambo lisilo la kawaida kupata desturi na sherehe za ibada zinazohusiana na hofu ya wafu katika tamaduni kotekote ulimwenguni. Kwa kielelezo, ebu tutazame desturi zipatikanazo katika Afrika iliyoko kusini ya Sahara.
Mwanamke mmoja katika jiji fulani la Afrika Magharibi akumbuka vizuri sana kile kilichotukia baada ya mshiriki wa familia yake kufa. Yeye asimulia hivi: “Mtu wa ukoo alikuwa akitayarisha kwa ukawaida sahani ya chakula kwa ajili ya aliyekufa na kuiweka kwa uangalifu katika chumba chake cha kulala. Wakati hakuwepo, nilikuwa nikienda na kukila chakula hicho. Mtu huyo wa ukoo aliporudi, alifurahi sana! Aliamini kwamba yule mfu alikuwa amepata chakula hicho chenye kupendeza. Hilo liliendelea kwa muda fulani hadi nilipokuwa mgonjwa. Nilipoteza hamu yangu ya kula na singeweza kula chakula chochote. Hilo lilifanya niwe na wasiwasi! Wengi wa watu wangu wa ukoo walifikia mkataa kwamba ugonjwa wangu ulisababishwa na mtu wetu wa ukoo aliyekufa. Ni lazima amemkasirikia mtu fulani katika familia, waliwaza.”
Katika jiji lilo hilo, ikiwa familia ina mapacha na mmoja afa, hakuna yeyote atakayezungumza kuhusu aliyekufa katika hiyo nyumba. Mtu akiuliza kuhusu pacha aliyekufa, familia itajibu kidesturi: “Ameenda kununua chumvi.” Wanaamini kwa uthabiti kwamba pacha aliye hai atakufa kweli ikisemwa.
Kisha, wazia mandhari hii: Mwanamume aliyekuwa na wake watatu amekufa. Siku baada ya maziko, wake hao wanafanyiziwa mavazi ya kipekee meupe. Wakati uo huo, mahali pa kipekee panajengwa kwa mbao na nyasi karibu na nyumbani, ambapo wanawake hawa wataoga na kuvaa mavazi hayo meupe. Hakuna mtu apaswaye kuingia mahali hapo isipokuwa wao na mwanamke aliyechaguliwa kuwasaidia. Baada ya kutoka kwenye bafu hii ya kipekee, nyuso za wanawake hao zafunikwa. Wanawake hao pia wavalia sebe, mkufu wa kamba kwa ajili ya “ulinzi.” Uogaji huu wa kidesturi hufanywa kila Ijumaa na Jumatatu kwa siku 100. Katika kipindi hiki hawawezi kuchukua kitu chochote kutoka kwa mwanamume moja kwa moja. Ikiwa mwanamume ataka kuwapa kitu, ni lazima kwanza akiweke ardhini au mezani. Kisha mwanamke huyo atakichukua. Hakuna mtu aruhusiwaye kuketi au kulala katika kitanda cha wanawake hawa. Wanapoondoka nyumbani wakati wowote, ni lazima kila mmoja abebe kijiti cha kipekee. Wanafikiri kwamba kuwa na kijiti hiki kutamzuia mume wao aliyekufa kuwashambulia. Maagizo yaliyo juu yasipofuatwa, wanahisi kwamba mume aliyekufa aweza kukasirika na kuwadhuru.
Mambo hayo ni ya kawaida katika sehemu hiyo ya ulimwengu. Hata hivyo, aina hizi za desturi hazipo katika Afrika tu.
Hofu ya Wafu Imeenea
Ensaiklopedia moja, Encarta, hutaarifu yafuatayo juu ya jinsi jamii za watu wengi huona wazazi wao wa kale waliokufa: “Watu wa ukoo waliokufa . . . wanaaminiwa kuwa wamekuwa viumbe wa kiroho wenye nguvu mno au, mara chache zaidi, kuwa wamefikia hadhi ya miungu. [Dhana hii] inategemea itikadi kwamba wazazi wa kale ni washiriki watendaji wa jamii, bado wakipendezwa na mambo ya watu wao wa ukoo wanaoishi. Hilo limethibitishwa sana katika jamii za Afrika Magharibi . . . , katika Polynesia na Melanesia (Wadobu na Wamanu), miongoni mwa Wahindi-Wazungu (Waskandinavia wa kale na Wajerumani), na hasa katika China na Japani. Kwa ujumla, wazazi wa kale wanaaminiwa kuwa na mamlaka kubwa, wakiwa na nguvu za kipekee za kuwa na uvutano juu ya mwendo wa matukio au udhibiti juu ya hali-njema ya watu wao wa ukoo wanaoishi. Ulinzi wa familia ni mojapo mahangaiko yao makuu. Wanaonwa kuwa wapatanishi kati ya mungu mkuu zaidi, au miungu, na watu, na wanaweza kuwasiliana na wanaoishi kupitia ndoto na upagaaji. Mtazamo kuwaelekea ni wa woga na kicho. Wakipuuzwa, wazazi hao wa kale wanaweza kusababisha maradhi na mambo mengine mabaya. Upatanishi, dua, sala, na dhabihu ni njia tofauti-tofauti ambazo kwazo wanaoishi wanaweza kuwasiliana na wazazi wao wa kale.”
Kwa kweli, mapato ya familia yaweza kwisha kwa sababu ya hofu ya waliokufa. Mara nyingi, sherehe zenye mambo mengi zihitajizo chakula na kinywaji, wanyama walio hai kwa ajili ya dhabihu, na mavazi yaliyo ghali yanadaiwa na wale wanaoamini kwa uthabiti kwamba waliokufa wanapaswa kuhofiwa.
Lakini je, watu wa ukoo waliokufa au wazazi wa kale wako katika hali inayodai hofu na kicho? Neno la Mungu, Biblia, lasema nini?
Je, Wafu Waweza Kukudhuru?
Huenda ukapendezwa kujua kwamba Biblia hukubali kwamba kuna itikadi kama hizo. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, mazoea yanayohusiana na hofu ya wafu hutajwa. Hicho hutaarifu hivi: “Asionekane kwako . . . mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA.”—Kumbukumbu la Torati 18:10-12, italiki ni zetu.
Ona kwamba Yehova Mungu alishutumu sherehe hizo za ibada. Kwa nini? Kwa sababu zategemea uwongo. Uwongo wa kwanza unaohusiana na wafu ni kwamba nafsi yao huendelea kuishi. Kwa kielelezo, gazeti The Straight Path lilisema hili kuhusu kile kinachowapata wafu: “Kifo si kitu kingine ila kuondoka kwa nafsi. . . . Kaburi ni hifadhi ya mwili tu, si ya nafsi.”
Biblia haikubali. Jisomee mwenyewe Ezekieli 18:4: “Tazama, nafsi zote ni zangu; kama ilivyo nafsi ya baba, ndivyo pia nafsi ya mwana ni yangu: nafsi itendayo dhambi, hiyo itakufa.” (King James Version) Pia, hali ya wafu ilitajwa waziwazi katika Neno la Mungu kwenye Mhubiri 9:5: “Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote.” Hili laeleza kwa nini chakula kilichoachiwa wafu hakiliwi isipokuwa kiliwe na mtu fulani anayeishi.
Hata hivyo, Biblia haituachi bila tumaini kwa wale walio kaburini. Wao wanaweza kuishi tena! Biblia husema juu ya “ufufuo.” (Yohana 5:28, 29; 11:25; Matendo 24:15) Huo utatokea kwa wakati ufaao wa Mungu. Kwa wakati huu, wafu hulala bila fahamu kaburini, ‘wakilala,’ hadi wakati wa Mungu wa wao ‘kuamka.’—Yohana 11:11-14; Zaburi 13:3.
Kwa kawaida watu huhofu yasiyojulikana. Ujuzi sahihi waweza kumweka mtu huru kutokana na ushirikina huo usio na msingi. Biblia hutupa kweli juu ya hali ya wale walio kaburini. Ikisemwa kisahili, wewe huna haja ya kuhofu wafu!—Yohana 8:32.