Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/22 kur. 4-8
  • Idadi Yenye Kuongezeka ya Wakimbizi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Idadi Yenye Kuongezeka ya Wakimbizi
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Tatizo Hilo Lazidi Kuwa Baya?
  • Mamilioni Yasiyotakikana
  • Ni Nini Kifanyacho Mambo Yawe Magumu?
  • Chuki na Hofu
  • Kuwasaidia “Wakaaji Wageni” ‘Wamtumikie Yehova kwa Kushangilia’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2017
  • Suluhisho Ni Nini?
    Amkeni!—1996
  • Ulimwengu Ambao Kila Mtu Atafurahia
    Amkeni!—2002
  • Watu Wanaotafuta Usalama
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/22 kur. 4-8

Idadi Yenye Kuongezeka ya Wakimbizi

SEHEMU kubwa ya historia ya mwanadamu imeharibiwa na vita, njaa kuu, na mnyanyaso. Likiwa tokeo, sikuzote kumekuwa na watu wanaohitaji mahali pa kimbilio. Katika nyakati zilizopita, mataifa na watu wamepatia wale wenye uhitaji mahali pa kimbilio.

Sheria zenye kuandaa kimbilio ziliheshimiwa na Waazteki wa kale, Waashuru, Wagiriki, Waebrania, Waislamu, na wengineo. Plato, mwanafalsafa Mgiriki, aliandika hivi zaidi ya karne 23 zilizopita: “Mgeni, akiwa ametengwa kutoka watu wa nchi yake na familia yake, apasa kuonyeshwa upendo mwingi na wanadamu na miungu. Kwa hiyo uangalifu wapasa kutolewa ili wageni wasitendewe mabaya.”

Katika karne ya 20, idadi ya wakimbizi imeongezeka kwa kutazamisha. Katika jitihada ya kutunza wakimbizi milioni 1.5 waliobakia baada ya Vita ya Ulimwengu 2, Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR) ilianzishwa katika 1951. Ilifikiriwa kwamba tume hiyo ingedumu kwa miaka mitatu, kutegemea wazo kwamba muda si muda wakimbizi waliokuwapo wangechangamana katika jamii waliyopata kimbilio. Ilifikiriwa kwamba baada ya hilo, shirika hilo lingekomeshwa.

Hata hivyo, kwa kipindi cha miongo mingi, idadi ya wakimbizi iliongezeka sana. Kufikia 1975 idadi yao ilikuwa imefika milioni 2.4. Katika 1985 tarakimu hiyo ilikuwa milioni 10.5. Kufikia 1995 idadi ya watu wenye kupokea ulinzi na msaada kutoka kwa UNHCR ilikuwa imeongozeka kwa kutazamisha hadi milioni 27.4!

Wengi walitumaini kwamba enzi ya baada ya Vita Baridi ingefungua njia ya kutatua tatizo la duniani pote la wakimbizi; haikulitatua. Badala ya hivyo, mataifa yamegawanyika kwa kufuata historia na ukabila, ikitokeza mapambano. Vita vilipokuwa vikiwaka, watu walitoroka, wakijua kwamba serikali zao hazingeweza kuwalinda. Kwa kielelezo katika 1991, karibu Wairaki milioni mbili walitoroka kwa idadi kubwa kuingia katika nchi za ujirani. Tangu wakati huo, wakimbizi wakadiriwao kuwa 735,000 wametoroka ile iliyokuwa Yugoslavia. Kisha, katika 1994 vita ya wenyewe kwa wenyewe katika Rwanda ikalazimisha zaidi ya nusu ya watu wa nchi hiyo milioni 7.3 kutoroka makao yao. Warwanda milioni 2.1 hivi walitafuta kimbilio katika nchi za karibu za Afrika.

Kwa Nini Tatizo Hilo Lazidi Kuwa Baya?

Kuna sababu kadhaa ambazo zachangia idadi yenye kuongezeka ya wakimbizi. Katika mahali fulani, kama vile Afghanistan na Somalia, serikali za kitaifa zimeporomoka. Hilo limeacha mambo mikononi mwa wanamgambo wenye silaha ambao hupora nchi bila kuzuiwa, wakisababisha wasiwasi na kufanya watu watoroke.

Mahali penginepo, mapambano husababishwa na tofauti tata sana za kikabila na kidini, kusudi kuu la vikundi vyenye kupigana likiwa kuondosha raia. Kuhusu vita katika ile iliyokuwa Yugoslavia, mwakilishi wa UM aliomboleza hivi katikati mwa 1995: “Kwa watu wengi ni vigumu sana kufahamu visababishi vya vita hii: ni nani anayepigana, sababu za kupigana. Watu wengi mno wanatoka upande mmoja na kisha majuma matatu baadaye watu wengi wanatoka upande ule mwingine. Ni vigumu sana kufahamu hata kwa watu ambao eti wanafahamu.”

Silaha za kisasa haribifu mno—roketi zenye kurushwa kwa mfuatano, makombora, mizinga, na silaha kama hizo—huongezea machinjo na kupanua mweneo wa mapambano. Tokeo: wakimbizi wengi hata zaidi. Katika nyakati za hivi majuzi asilimia 80 hivi ya wakimbizi wa ulimwenguni imetoroka kutoka nchi zenye kuendelea hadi nchi za ujirani ambazo zinaendelea pia na zisizo na vifaa vya kutunza wale wanaotafuta kimbilio.

Katika mapambano mengi ukosefu wa chakula huchangia tatizo hilo. Watu wanapokufa njaa, labda kwa sababu msafara wa ugavi wa kutuliza wazuiwa, watu walazimika kuhama. Gazeti The New York Times lataja: “Katika mahali kama vile Pembe ya Afrika, ukame na vilevile vita vimeharibu bara hilo hivi kwamba haliwezi kuandaa riziki tena. Iwe hayo mamia ya maelfu yanatoroka kufa njaa au vita si jambo la maana.”

Mamilioni Yasiyotakikana

Ingawa lile wazo la kimbilio linaheshimiwa kikanuni, idadi kubwa ya wakimbizi hutamausha mataifa. Hali hiyo yapatana na ile ya Misri ya kale. Wakati Yakobo na familia yake walipokimbilia Misri ili kutoroka baa la njaa kuu ya miaka saba, walikaribishwa. Farao aliwapa “palipo pema pa nchi” ili waishi hapo.—Mwanzo 47:1-6.

Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita, Waisraeli wakawa wengi, “ile nchi ilikuwa imejawa na wao.” Sasa Wamisri wakaanza kuitikia kwa ukali, lakini “kadiri [Wamisri] walivyowatesa ndivyo [Waisraeli] walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichuki[z]wa kwa sababu ya wana wa Israeli.”—Kutoka 1:7, 12.

Vivyo hivyo, mataifa leo ‘huchukizwa’ kadiri idadi ya wakimbizi iendeleavyo kuongezeka. Sababu kubwa ya hangaiko lao ni ya kiuchumi. Hugharimu fedha nyingi kulisha, kuvisha, kulipia makao, na kulinda mamilioni ya wakimbizi. Kati ya 1984 na 1993, utumizi wa kila mwaka wa UNHCR ulipanda kutoka dola milioni 444 hadi dola bilioni 1.3. Nyingi za fedha hizo huchangwa na mataifa yaliyo tajiri zaidi, baadhi yayo yakiwa yanang’ang’ana na matatizo yayo yenyewe ya kiuchumi. Mataifa yenye kusaidia nyakati nyingine hulalamika: ‘Tunang’ang’ana kusaidia wasio na makao katika mitaa yetu wenyewe. Twaweza kuwaje na daraka kwa wasio na makao wa dunia nzima, hasa wakati ambapo tatizo laelekea kuongezeka badala ya kupungua?’

Ni Nini Kifanyacho Mambo Yawe Magumu?

Wale wakimbizi ambao hufika kwenye nchi tajiri mara kwa mara hupata kwamba hali yao imekuwa ngumu kwa sababu ya maelfu mengi ya watu ambayo yamehamia nchi iyohiyo kwa sababu za kiuchumi. Wahamaji hawa wa kiuchumi si wakimbizi wanaotoroka vita au mnyanyaso au njaa kuu. Badala ya hivyo, wanakuja wakitafuta maisha bora zaidi—maisha yasiyo na umaskini. Kwa sababu mara nyingi wao hujifanya kuwa wakimbizi, wakitaabisha mashirika ya kutoa kimbilio kwa madai yasiyo ya kweli, wanafanya iwe vigumu zaidi kwa wakimbizi wa kweli kupata kusikiwa kwa haki.a

Kuingia kwa wakimbizi wengi na wahamiaji kumefananishwa na mito miwili ambayo imetiririka kando kwa kando ikiingia katika nchi tajiri kwa miaka mingi. Hata hivyo, sheria za uhamiaji zenye kuzidi kuwa ngumu zimezuia mto wa wahamaji wa kiuchumi. Hivyo, wamekuja kuwa sehemu ya mto wa wakimbizi, na mto huu umefurika kupita kiasi.

Wakijua kwamba huenda ikachukua miaka kadhaa kuchunguza maombi yao ya kimbilio, wahamaji wa kiuchumi husababu kwamba wako katika hali itakayowaboresha licha ya matokeo ya maombi yao ya kimbilio. Maombi yao ya kimbilio yakikubaliwa, wanaboresha hali yao, kwa kuwa wanabaki katika mazingira yenye ufanisi zaidi kiuchumi. Maombi yao yakikataliwa, wanaboresha hali yao pia, kwa kuwa watakuwa wamepata fedha na kujifunza stadi fulani za kwenda nazo kwenye nchi ya kwao.

Huku idadi yenye kuongezeka ya wakimbizi, pamoja na wakimbizi wasio wa kweli, ikitiririka katika nchi nyinginezo, nchi nyingi hazikaribishi wala kukubali tena wakimbizi. Nyingine zimefungia wale wanaotoroka mipaka yao. Nchi nyinginezo zimeanzisha sheria na taratibu ambazo hukataa kuingia kwa wakimbizi. Na bado nchi nyingine zimewarudisha wakimbizi kwa lazima hadi kwenye nchi walikotoka. Kichapo kimoja cha UNHCR chataja hivi: “Ongezeko lisilokoma katika idadi—ya wakimbizi wa kweli na wahamaji wa kiuchumi—limeweka mkazo mbaya juu ya desturi ya uandaaji wa kimbilio ambayo imefuatwa kwa miaka 3,500, likifanya ikaribie kuporomoka.”

Chuki na Hofu

Kuongezea matatizo hayo ya wakimbizi ni hali yenye kusumbua ya xenophobia—kuhofu na kuchukia wageni. Katika nchi nyinginezo watu huamini kwamba watu kutoka nje hutisha utambulisho wao wa kitaifa, utamaduni, na kazi. Nyakati fulani hofu hizo husababisha jeuri. Gazeti Refugees lasema: “Kontinenti ya Ulaya hupatwa na shambulio moja la kijamii kwa kila dakika tatu—na makao ya muda kwa wanaotafuta kimbilio mara nyingi sana ndiyo shabaha.”

Bango moja katika Ulaya ya kati huonyesha uhasama wenye kina, uhasama ambao unaendelea kuonekana katika mabara mengi ya dunia. Ujumbe walo wenye nia ovu humlenga mgeni: “Wao ni jipu lichukizalo na lenye maumivu kwenye mwili wa taifa letu. Kikundi cha kikabila kisicho na utamaduni, viwango vya kiadili au kidini, kikundi cha watu wenye kuhama-hama chenye kunyang’anya na kuiba tu. Wakiwa wachafu, waliojaa chawa, wao hukaa barabarani na kwenye vituo vya gari-moshi. Na wakusanye matambara yao machafu na kuondoka milele!”

Bila shaka wakimbizi wengi wangetaka sana “kuondoka milele.” Wao wanatamani kwenda nyumbani. Mioyo yao yatamani kwa maumivu kuishi maisha yenye amani, ya kawaida pamoja na familia na marafiki. Lakini hawana nyumbani pa kwenda.

[Maelezo ya Chini]

a Katika 1993, serikali za Ulaya Magharibi pekee zilitumia dola bilioni 11.6 kuwashughulikia na kuwapokea wanaotafuta kimbilio.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Hali Mbaya ya Wakimbizi

“Je, ulijua kwamba mamia ya maelfu ya watoto wakimbizi hulala njaa kila usiku? Au kwamba ni mtoto mmoja wa mkimbizi kati ya wanane ambaye amepata kwenda shuleni? Wengi wa watoto hawa hawajapata kamwe kwenda sinemani, au bustanini, acha kwenda hata kwenye jumba la hifadhi ya vitu vya kale. Wengi hukua katika kambi zilizozingirwa kwa seng’enge au katika kambi zilizotengwa. Hawajapata kamwe kuona ng’ombe au mbwa. Watoto wengi sana wa wakimbizi hufikiri kwamba nyasi za kijani kibichi ni kitu cha kula, si kitu cha kuruka-ruka na kukimbia juu yacho. Watoto wa wakimbizi ndio sehemu yenye kuhuzunisha zaidi ya kazi yangu.”—Sadako Ogata, Kamishna Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi.

[Hisani]

Picha ya U.S. Navy

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Yesu Alikuwa Mkimbizi

Yusufu na Mariamu walikaa Bethlehemu pamoja na mwana wao, Yesu. Wanajimu kutoka Mashariki walikuja na zawadi za dhahabu, manukato, na manemane (NW). Baada ya wao kuondoka malaika alimtokea Yusufu, akisema: “Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.”—Mathayo 2:13.

Haraka hao watatu wakakimbilia nchi ya kigeni—wakawa wakimbizi. Herode alikasirika kwamba wale wanajimu hawakumripotia mahali pa Yule aliyetabiriwa kuwa mfalme wa Wayahudi. Katika jaribio la kumuua Yesu lisilokuwa na matokeo, yeye aliamuru wanaume wake wawaue wavulana wote wachanga katika Bethlehemu na viunga vyao.

Yusufu na familia yake walibaki Misri hadi malaika wa Mungu alipomtokea tena Yusufu katika ndoto. Malaika huyo alisema hivi: “Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.”—Mathayo 2:20.

Inaonekana kwamba Yusufu alinuia kukaa katika Yudea, ambapo walikuwa wakiishi kabla ya kukimbilia Misri. Lakini alionywa katika ndoto kwamba ingekuwa hatari kufanya hivyo. Hivyo tisho la jeuri liliathiri maisha yao tena. Yusufu, Mariamu, na Yesu walisafiri kaskazini hadi Galilaya na kukaa katika mji wa Nazareti.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Katika miaka ya majuzi mamilioni ya wakimbizi wamekimbilia nchi nyinginezo ili kuokoa uhai wao

[Hisani]

Juu kushoto: Albert Facelly/Sipa Press

Juu kulia: Charlie Brown/Sipa Press

Chini: Farnood/Sipa Press

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

Mvulana aliye kushoto: UN PHOTO 159243/J. Isaac

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki