Suluhisho Ni Nini?
HALI ya wakimbizi si yenye kukosa tumaini kabisa. Kotekote ulimwenguni, mashirika ya ubinadamu hujitahidi kusaidia wale waliohamishwa na vita na matatizo mengineyo. Njia kuu wanayosaidia nayo ni kwa kuwasaidia wakimbizi kurudi katika nchi zao za uzaliwa.
Wakimbizi huacha nyumba, jamii, na nchi kwa sababu huhofu watauawa kimakusudi, kuteswa, kubakwa, kufungwa gerezani, kufanywa watumwa, kunyang’anywa vitu, au kufanywa wafe kwa njaa. Kwa hiyo kabla ya wakimbizi kurudi nyumbani kwa usalama, matatizo yaliyowafanya watoroke ni lazima yatatuliwe. Hata wakati mapambano ya kisilaha yakomapo hatimaye, kutokuwa na sheria na utengamano mara nyingi huzuia watu kwenda nyumbani. Akasema Agnes, mkimbizi Mrwanda aliye mama wa watoto sita: “Kutupeleka [kuturudisha] Rwanda kutakuwa kama kutupeleka kwenye makaburi yetu.”
Hata hivyo, tangu 1989, zaidi ya wakimbizi milioni tisa wamerudi nyumbani kwao. Milioni 3.6 hivi wamerudi Afghanistan kutoka Iran na Pakistan. Wakimbizi wengine milioni 1.6 katika nchi sita wamerudi Msumbiji, taifa lililoharibiwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya miaka 16.
Kurudi si rahisi. Mara nyingi nchi ambazo wakimbizi hurudi ni vifusi—vijiji vikiwa vimeporomoka, madaraja kuharibiwa, na barabara na viwanja kujawa na mabomu ya kutegwa ardhini. Hivyo, wakimbizi wanaorudi ni lazima waanze marekebisho tangu mwanzo si kwa maisha yao tu bali pia kwa nyumba, shule, kliniki za afya, na kila kitu chao kingine.
Hata hivyo, hata wakati mapambano yakomapo mahali pamoja, yakiruhusu wakimbizi kurudi, hayo huanza mahali pengine, yakisababisha mitiririko mipya ya wakimbizi. Kwa hiyo kusuluhisha tatizo la wakimbizi, kwamaanisha kusuluhisha tatizo la vita, ukandamizaji, chuki, mnyanyaso, na visababishi vingine ambavyo hufanya watu watoroke ili kuokoa uhai.
Gazeti The State of the World’s Refugees 1995 hukiri hivi: “Kweli halisi . . . ni kwamba masuluhisho [kwa tatizo la wakimbizi] yategemea hasa mambo ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi ambayo hayawezi kusuluhishwa na shirika lolote la ubinadamu.” Kulingana na Biblia, masuluhisho pia hayawezi kufikiwa na shirika lolote la kidunia, la ubinadamu au jinginelo.
Ulimwengu Usio na Wakimbizi
Hata hivyo, kuna suluhisho. Biblia huonyesha kwamba Yehova Mungu hujali wale ambao wametenganishwa na nyumba zao na familia zao. Tofauti na serikali za dunia, yeye ana uwezo na hekima ya kusuluhisha matatizo yote magumu yanayokabili jamii ya kibinadamu. Atafanya hivyo kupitia Ufalme wake—serikali ya kimbingu ambayo karibuni itadhibiti mambo ya dunia.
Ufalme wa Mungu utachukua mahali pa serikali zote za kibinadamu. Badala ya kuwa na serikali nyingi duniani, kama tulizo nazo sasa, kutakuwa na serikali moja tu, ambayo itatawala juu ya sayari yote. Biblia hutabiri: “Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu nao utasimama milele na milele.”—Danieli 2:44.
Huenda unafahamu ile sala ya kiolezo ipatikanayo katika Biblia kwenye Mathayo 6:9-13. Sehemu ya sala hiyo husema: “Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni.” Kupatana na sala hiyo, Ufalme wa Mungu karibuni ‘utakuja’ na kutimiza kusudi la Mungu kwa dunia.
Chini ya utawala huo wenye upendo wa Ufalme wa Mungu, kutakuwako amani na usalama wa ulimwengu wote mzima. Hakutakuwa tena na chuki na mapigano kati ya vikundi vya watu na mataifa ya dunia. (Zaburi 46:9) Hakutakuwa kamwe na mamilioni ya wakimbizi wanaotoroka ili kuokoa uhai wao au wanaonyong’onyea katika kambi.
Neno la Mungu laahidi kwamba Mfalme wa Ufalme wa Mungu, Kristo Yesu, “atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, na damu yao ina thamani machoni pake.”—Zaburi 72:12-14.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Karibuni wote watatendeana kama ndugu na dada wa kweli