Redio—Uvumbuzi Uliobadili Ulimwengu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA
MLIO wa bunduki ulivunja ukimya wa sehemu za mashambani za Italia. Ishara hiyo ilimpa Guglielmo Marconi uhakikisho wa kwamba chombo alichokuwa akitumia, ambacho kilikuwa cha kwanza kutumika, kilikuwa kinafanya kazi. Mawimbi ya sumakuumeme yaliyofanyizwa na transmita na kurushwa angani yalinaswa na kipokezi umbali wa kilometa mbili na nusu. Ilikuwa mwaka wa 1895. Ingawa wakati huo hakuna mtu aliyefahamu yote yaliyohusika katika jaribio hilo, mlio huo wa bunduki uliokuwa ishara, ulifungua njia kwa tekinolojia ambayo tangu wakati huo imebadili ulimwengu wetu—mawasiliano ya redio.
Asili ya mawimbi ya sumakuumeme tayari ilikuwa imechunguzwa na wanasayansi kadhaa. Katika 1831, mwanafizikia Mwingereza Michael Faraday alionyesha kwamba mkondo wa umeme ungeweza kutokeza uga sumaku na kuvuta mkondo katika saketi ya pili iliyotenganishwa na saketi ya kwanza lakini ikawekwa karibu nayo. Katika 1864, mwanafizikia wa Scotland James Maxwell alitoa nadharia kwamba nishati inayofanyizwa na huo uga sumaku iliweza kutokea kwa njia ya mawimbi—kama viwimbi juu ya uso wa kidimbwi—lakini kwa mwendo wa nuru. Baadaye, mwanafizikia Mjerumani, Heinrich Hertz alithibitisha nadharia ya Maxwell, akitokeza mawimbi ya sumakuumeme na kuyaona kwa ukaribu, kama alivyofanya Ernest Rutherford (baadaye, Lord Rutherford) katika New Zealand, ambaye baadaye alitenganisha atomi. Lakini kwa kurekebisha na kuboresha vifaa vilivyokuwapo na kuongeza antena isiyo kamili aliyojitengenezea mwenyewe, Marconi alifanikiwa kupeleka taarifa kwa kutumia ishara za umeme katika umbali fulani. Telegrafu isiyotumia waya ilikuwa njiani!
Katika 1896, Marconi mwenye umri wa miaka 21 alihama Italia kwenda Uingereza, ambako alikabidhiwa kwa William Preece, mhandisi mkuu wa Ofisi Kuu ya Posta. Preece alitaka kutumia mfumo wa Marconi katika mawasiliano ya baharini kati ya sehemu mbili ambazo hazingeweza kuunganishwa kwa waya. Alimtolea Marconi msaada wa mafundisanifu na matumizi ya maabara kwa majaribio yake. Katika miezi michache, Marconi alifanikiwa katika kuongeza nguvu ya ishara zilizopelekwa kwa umbali wa kilometa kumi. Katika 1897, Marconi alianzisha kampuni iitwayo, Wireless Telegraph and Signal Company, Ltd., kwa kusudi la kubadili telegrafu isiyotumia waya kuwa mfumo wa kufaa kibiashara.
Katika 1900, kiunganishi cha kilometa 300 cha telegrafu ya redio kilifanywa kati ya Cornwall na Visiwa vya Wight katika Uingereza kusini, ikionyesha kile ambacho zamani kilifikiriwa kwamba hakiwezekani—kule kueneza dunia yote kwa mawimbi ya redio. Ilikuwa imefikiriwa kwamba ishara hizo zisingeweza kupokewa umbali unaozidi upeo wa macho, kwa kuwa mawimbi ya sumakuumeme husafiri yakiwa yamenyooka bila kupinda.a Kisha maombi muhimu ya kwanza ya redio yakaanza kuwasili. Maofisa wa jeshi la maji la Uingereza waliagiza ujenzi wa redio 26 kwenye meli, na pia ujenzi na udumishaji wa vituo sita vya barani. Mwaka uliofuata Marconi alifanikiwa kuvusha Atlantiki kwa ishara hafifu za nukta tatu ambayo ilionyesha S katika mfumo wa Morse. Kulikuwa na uhakika wa uvumbuzi huo.
Maendeleo ya Kitekinolojia
Mwanzoni, telegrafu isiyotumia waya haikuweza kupeleka maneno au muziki, bali mfumo wa Morse pekee. Hata hivyo, katika 1904 maendeleo makubwa yalifanywa kwa uvumbuzi wa diodi, neli-ombwe ya kwanza, ambayo ilifanya kupitisha na kupokea sauti kuwezekane. Hii ilibadili telegrafu isiyotumia waya kuwa redio kama tuijuavyo leo.
Katika 1906, katika Marekani, Reginald Fessenden alitangaza muziki ambao ulinaswa na meli zilizokuwa umbali wa kilometa 80. Katika 1910, Lee De Forest alitangaza moja kwa moja wonyesho uliofanywa na mwimbaji maarufu wa sauti nyembamba Mwitalia Enrico Caruso kwa manufaa ya wenye redio zisizo za makusudi ya biashara katika New York. Mwaka mmoja kabla ya wakati huo, kwa mara ya kwanza ishara za kurekebisha saa zilipitishwa kupitia Mnara wa Eiffel katika Paris, Ufaransa. Katika mwaka huohuo, 1909, uokoaji wa kwanza uliosaidiwa na redio ulitokea, ukiokoa watu kutoka meli Florida na Republic, ambazo zilikuwa zimegongana katika Atlantiki. Miaka mitatu baadaye, zaidi ya waokokaji 700 wa msiba wa Titanic waliokolewa pia, kwa sababu ya kupeleka maombi SOS kwa njia ya redio.
Mapema kufikia 1916, uwezekano wa kuwa na redio katika kila nyumba ulifikiriwa. Matumizi ya vali yalifanya iwezekane kutengeneza vipokezi vyenye gharama nafuu, yakifungua mlango ambao uliongoza kwenye maendeleo yenye kuenea ya redio ya biashara. Ongezeko la haraka lilikuja kwanza katika Marekani, ambako kulikuwa na vituo 8 vya redio kufikia mwisho wa 1921 na vituo vingine 564 vilikuwa vimepewa leseni na serikali ya Marekani kufikia Novemba 1, 1992! Katika nyumba nyingi, ukitoa mfumo wa umeme, redio ilikuwa chombo cha kwanza kuunganishwa kwa umeme.
Katika kipindi cha miaka miwili cha matangazo ya biashara, Wanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, walikuwa pia wanatumia redio kutangaza ujumbe wao. Katika 1922, J. F. Rutherford, aliyekuwa msimamizi wa Watch Tower Society wakati huo, alitoa hotuba yake ya kwanza katika redio, huko California. Miaka miwili baadaye, WBBR, kituo kilichojengwa na kumilikiwa na Watch Tower Society, kilianza kutangaza kutoka Kisiwa cha Staten Island, New York. Hatimaye, Sosaiti ilipanga mifumo ya ulimwenguni pote ya kutangaza programu za Biblia. Kufikia 1933 kilele cha vituo 408 vilikuwa vinatangaza ujumbe wa Ufalme wa Mungu.—Mathayo 24:14.
Hata hivyo, katika mataifa mengi, redio ikadhibitiwa na Serikali. Katika Italia, serikali ya Mussolini iliona redio kuwa chombo cha propaganda za kisiasa na ilikataza raia zayo kusikiliza matangazo ya kigeni. Uwezo mkubwa wa redio ulionekana wazi katika 1938. Katika matangazo ya Hadithi zenye kubuniwa za sayansi katika Marekani, Orson Welles alitokeza hofu miongoni mwa watu, ambao baadhi yao walifikiri kwamba watu kutoka sayari ya Mihiri walikuwa wametua katika New Jersey na walikuwa wakitumia “miale ya joto” mibaya sana kuua watu wote ambao waliwapinga!
Miaka Mia Moja ya Redio
Katika 1954 kipitisha-wakati kilichopendwa zaidi na Waitalia kilikuwa kusikiliza redio. Ingawa televisheni imefanikiwa, redio bado inapendwa sana. Katika nchi nyingi za Ulaya, redio inasikilizwa na asilimia 50 hadi 70 ya watu ili kupata habari au kwa ajili ya vitumbuizo. Inakadiriwa kwamba katika Marekani, kuna redio katika asilimia 95 ya magari, asilimia 80 ya vyumba vya kulala, na zaidi ya asilimia 50 ya majiko.
Moja ya sababu za kupendwa kwa redio hata katika kizazi cha televisheni ni ule uwezekano wayo wa kubebeka kwa urahisi. Na zaidi, kulingana na uchunguzi, redio ina “uwezo wa kukufanya uwe mwenye hisia-moyo na mwenye ubuni kupita televisheni.”
Wakati wa 1995, sherehe katika Italia za kukumbuka miaka mia moja ya jaribio la Marconi zilitoa nafasi za kuangalia maendeleo yaliyofanywa na redio. Wanasayansi wengi wamechangia kubadili chombo cha kwanza kisicho kamili hadi mifumo ya hali ya juu ya leo. Sasa, kwa sababu ya utangazaji wa kutumia tarakimu, ambao ni mfumo wa kufanya ishara kuwa wa tarakimu, kuna ubora kabisa wa sauti. Lakini, kwa kuongezea matumizi mengi sana ya redio kila siku, uvumbuzi huo ulikuwa mwanzo wa televisheni, rada, na tekinolojia nyinginezo nyingi.
Kwa kielelezo, astronomia ya redio inategemea mapokezi na uchanganuzi wa mawimbi ya redio yatolewayo na magimba ya anga. Bila redio, maendeleo ya tekinolojia ya anga za juu hayangewezekana. Matumizi yote ya satelaiti—televisheni, simu, ukusanyaji-habari—hutegemea matumizi ya mawimbi ya redio. Maendeleo ya kitekinolojia ya kufanya transista kuwa mikrochipu kwanza yalitokeza vikokotozi vya kuwekwa mfukoni na kompyuta na baadaye mfumo wa kimataifa wa habari.
Simu za kubebeka zenye uwezo wa kuunganisha sehemu zozote mbili katika uso wa dunia, tayari zimetokea. Matumaini yaliyopo ni kuja kwa vipokezi visivyo na waya vyenye ukubwa wa kiganja cha mkono—vikiwa na televisheni, simu, kompyuta, na faksi pamoja. Vipokezi hivi vitakuwa na uwezo wa kufikia programu nyingi za video, za sauti na za maandishi navyo vitaruhusu watumiaji kuwasiliana kupitia elektroni.
Huwezi kuwa na hakika juu ya wakati ujao wa redio. Lakini tekinolojia ya redio inazidi kufanya maendeleo, hivyo maendeleo mengine makubwa yaelekea kutokea.
[Maelezo ya Chini]
a Ajabu hiyo ilifafanuliwa katika 1902, wakati wanafizikia Arthur Kennelly na Oliver Heaviside walipotoa nadharia kuhusu kuwapo kwa tabaka ya angahewa ambayo iliakisi mawimbi ya sumakuumeme—ile angaioni.
[Blabu katika ukurasa wa 21]
Ingawa televisheni imefanikiwa, redio bado inapendwa sana
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]
Juu kushoto na kulia, chini kushoto: “MUSEO della RADIO e della TELEVISIONE” RAI--TORINO; chini kulia: Picha ya NASA