Anemia ya Sickle-Cell—Ujuzi Ndio Kinga Bora Zaidi
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA NIGERIA
KULIKUWA na watu 32 katika chumba cha mkutano, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Tope, mwenye umri wa miaka sita, akiwa dhaifu na kuvalia nguo ya rangi ya pinki aliketi kwa utulivu kando ya mama yake, katika kiti cha mbao. Alisikiliza muuguzi alipokuwa akiongea nao mambo wanayopaswa kufanya maumivu yajapo.
Tope aliyajua maumivu—maumivu ambayo huja kwa kutisha na kwa ghafula na kudumu kwa siku kadhaa kabla ya kupungua. Labda ni maumivu ambayo amekuwa akiyapata yaliyomfanya kuwa mwenye kuchukua mambo kwa uzito zaidi ya wengine wa umri wake.
“Yeye ni mtoto wangu wa kwanza,” mama yake akasema. “Tokea mwanzoni alikuwa mgonjwa siku-zote. Nilienda makanisa mengi, nao walimwombea. Lakini bado alikuwa mgonjwa. Hatimaye nilimpeleka hospitalini. Waliipima damu yake na kugundua kwamba alikuwa na anemia ya sickle-cell.
Hiyo Ni Nini?
Katika Kituo cha Sickle-Cell Anemia katika Benin City, Nigeria, mama ya Tope alijifunza kwamba anemia ya sickle-cell ni kasoro ya damu. Kinyume cha itikadi za ushirikina, haisababishwi na uchawi au roho za wafu. Watoto hurithi anemia ya sickle-cell kutoka kwa wazazi wote wawili. Si ugonjwa uambukizwao. Hamna uwezekano wa kuambukizwa kasoro hiyo na mtu mwingine. Ama unazaliwa nayo ama huzaliwi nayo. Mama ya Tope alijifunza pia kwamba ingawa hamna ponyo, dalili zaweza kutibiwa.a
Anemia ya sickle-cell mara nyingi hutokea miongoni mwa wale wenye asili ya Kiafrika. Dakt. I. U. Omoike, mkurugenzi wa Kituo cha Sickle-Cell Anemia, aliliambia Amkeni!: “Nigeria ina idadi kubwa zaidi ya Waafrika kuliko taifa jingine lolote na hivyo basi ina idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wenye anemia ya sickle-cell kuliko taifa jingine lolote. Hili hufanya nchi hii kuwa kitovu cha sickle-cell duniani.” Kulingana na Daily Times la Lagos, karibu Wanigeria milioni moja wana anemia ya sickle-cell, na 60,000 hufa kila mwaka kutokana nayo.
Tatizo Fulani Katika Damu
Kuelewa kasoro hiyo, tunapaswa kuelewa kile ambacho damu hufanya na jinsi inavyozunguka mwilini. Kielezi kimoja kitasaidia. Fikiria nchi ambayo hutegemea chakula kinachoingizwa kutoka nje ili kulisha watu wanaoishi vijiji vya mashambani. Malori huenda hadi jiji kuu, ambapo yanajazwa chakula. Malori hayo huondoka jiji kupitia barabara kuu, lakini yafikapo maeneo ya mashambani, barabara zinakuwa nyembamba.
Kila kitu kikienda sawa, malori hufika mwisho wa safari zayo, hushukisha chakula, kisha hurudi jijini kubeba chakula zaidi kwa ajili ya ugavi unaofuata. Hata hivyo, malori mengi yakiharibika, chakula huharibika na magari mengine huzuiwa yasipite. Kisha watu vijijini wanakosa chakula.
Katika njia iyo hiyo, chembe nyekundu zilizo katika damu husafiri kwenye mapafu ambako hizo huchukua ugavi wa oksijeni—chakula kwa mwili. Kisha hutoka kwenye mapafu na kusafiri haraka kupitia mishipa mikubwa ya damu hadi sehemu zote za mwili. Hatimaye, “barabara” huwa nyembamba sana hivi kwamba chembe nyekundu zaweza kusafiri katika safu moja tu kupitia mishipa midogo ya damu. Ni hapo katika mishipa midogo ya damu ambapo hizo huweka mzigo wao wa oksijeni, ambayo hulisha chembe za mwili.
Chembe nyekundu ya damu ya kawaida ni mviringo kama sarafu na husafiri kupitia mishipa midogo kabisa ya damu kwa urahisi sana. Lakini kwa watu wenye anemia ya sickle-cell, chembe za damu huvunjika. Hizo hupoteza umbo lazo la mviringo na kuchukua umbo la ndizi au mundu—zana ya mkulima. Chembe hizi nyekundu za damu zenye umbo la mundu hukwama katika mishipa midogo ya damu mwilini, kama lori linalokwama katika matope, zikizuia chembe nyingine nyekundu za damu kupita. Mtiririko wa damu kwenda sehemu fulani ya mwili unapopunguka, oksijeni inazuiwa na tokeo ni maumivu makali ya ghafula.
Tatizo la kawaida la sickle-cell hutokeza maumivu makali katika mifupa na vifundo. Maumivu hayatabiriki, yaweza kutokea mara chache au mara nyingi kama kila mwezi. Yatokeapo yanataabisha mtoto na mzazi. Ihunde ni muuguzi ambaye hufanya kazi katika hicho kituo cha sickle-cell. “Siyo rahisi kumtunza mtoto mwenye sickle-cell,” yeye asema. “Ninajua kwa sababu binti yangu ana kasoro hiyo. Maumivu huja ghafula. Yeye hupiga kelele na kulia, nami hulia. Maumivu hupungua baada ya siku mbili au tatu, au labda baada ya juma.”
Dalili
Kwa kawaida dalili huonekana mtoto afikapo umri wa miezi sita. Moja ya dalili za mwanzo ni uvimbe wenye maumivu mkononi au miguuni. Mtoto aweza kulia mara kwa mara na bila kula sana. Sehemu nyeupe ya macho yaweza kuonekana manjano. Ulimi, midomo, na viganja vyaweza kuwa na rangi hafifu kuliko kawaida. Watoto wanaoonyesha dalili hizo wapaswa wapelekwe hospitali, ambako kupimwa kwa damu kwaweza kuonyesha ikiwa tatizo ni anemia ya sickle-cell.
Wakati chembe zilizo kama mundu zinapoziba mishipa ya damu, kwa kawaida maumivu huathiri vifundo. Maumivu makali pia yaweza kuvuruga kazi ya ubongo, mapafu, moyo, figo na wengu—mara nyingine kukiwa na matokeo ya kufisha. Vidonda katika eneo la kifundo cha mguu vyaweza kudumu kwa miaka mingi. Watoto huwa katika hatari ya kupatwa na kifafa au maradhi ya ghafula. Wale wenye anemia ya sickle-cell wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na magonjwa ya kuambukizwa, kwani kasoro hiyo hudhoofisha uwezo wa asili wa kujikinga. Ambukizo la ugonjwa ni kisababishi cha kawaida cha kifo.
Bila shaka, si kila mtu mwenye anemia ya sickle-cell huwa na dalili zote hizo. Na wengine hawapatwi na matatizo mpaka wafikiapo miaka yao ya mwisho ya utineja.
Utibabu
Wazazi wengi wamepoteza wakati na fedha kutafuta matibabu ambayo yalionekana yangeponya watoto wao. Lakini kwa sasa hamna ponyo kwa anemia ya sickle-cell; hiyo ni kasoro ya kipindi chote cha maisha. Hata hivyo, yapo mambo rahisi ambayo yaweza kufanywa ili kupunguza ukawaida wa maumivu hayo, na zipo njia za kuyashughulikia yatokeapo.
Maumivu makali yatokeapo, wazazi wapaswa wawape watoto wao maji mengi ya kunywa. Pia waweza kuwapa dawa zisizo na nguvu sana za kupunguza maumivu. Maumivu makali yaweza kuhitaji madawa yenye nguvu ambayo yaweza kupatikana kwa daktari tu. Hata hivyo, kwa kusikitisha mara nyingine hata madawa yenye nguvu sana hayawezi kuleta nafuu sana. Hata hivyo, hamna haja ya kubabaika. Karibu katika visa vyote, baada ya muda wa saa chache, maumivu hupungua na mgonjwa hupata nafuu.
Wanasayansi wanatafuta madawa ya kusaidia kutibu kasoro hiyo. Kwa mfano, mapema katika 1995, Taasisi ya Kitaifa ya Moyo, Pafu, na Damu katika Marekani ilitangaza kwamba dawa iitwayo hydroxyurea ilipunguza kwa nusu ukawaida wa maumivu makali ya wagonjwa wa sickle-cell. Inafikiriwa hiyo hufanya hivyo kwa kuzuia chembe nyekundu za damu zisibadilishe umbo lao na kuziba mishipa ya damu.
Madawa hayo hayapatikani kwa urahisi kila mahali, na si yenye msaada katika kila hali. Na ingawa kuna hatari zenye kujulikana sana, madaktari katika Afrika na sehemu nyingine kwa kawaida hutia damu mishipani kutibu wagonjwa wa sickle-cell katika hali ya dharura.
Kuzuia Maumivu Makali
“Sisi huwaambia wagonjwa wanywe maji mengi kusaidia kuzuia maumivu makali,” asema Alumona, mshauri wa mambo ya jeni kwenye kituo cha sickle-cell. “Maji hufanya iwe rahisi kwa damu kusambaa katika mishipa ya mwili. Watu wazima wenye anemia ya sickle-cell wapaswa wanywe lita tatu hadi nne za maji kila siku. Bila shaka, watoto watakunywa kidogo kuliko hiyo. Sisi huwafundisha watoto wenye anemia ya sickle-cell kubeba chupa za maji waendapo shule. Walimu wapaswa kuelewa kwamba watoto hawa wanaweza kuomba ruhusa mara nyingi zaidi ili kwenda kujisaidia. Wazazi wapaswa kuelewa kwamba watoto hawa waweza kukojoa kitandani mara nyingi kuliko watoto ambao hawana kasoro hiyo.”
Kwa vile ugonjwa waweza kusababisha maumivu makali yenye hatari, wale wenye anemia ya sickle-cell wapaswa wajitahidi sana kudumisha afya nzuri. Waweza kufanya hivyo kwa kudumisha usafi wa kibinafsi, kwa kuepuka utendaji wa muda mrefu wa kutumia nguvu na kwa kula mlo uliosawazika wa chakula kizuri. Madaktari pia hushauri kwamba mlo unapaswa utiwe nguvu na vidonge vyenye mchanganyiko wa vitamini na asidi folike.
Katika maeneo ambako malaria ni kawaida, wale wenye anemia ya sickle-cell wanapaswa kuwa wenye busara kujilinda wenyewe, kwa kuepuka kuumwa na mbu na pia kwa kunywa dawa kujilinda dhidi ya ugonjwa huo. Kwa vile malaria huharibu chembe nyekundu za damu, inaweza kuwa hatari sana kwa mgonjwa wa anemia ya sickle-cell.
Wale wenye anemia ya sickle-cell pia wapaswa kuchunguzwa afya kwa kawaida. Maambukizo, magonjwa, au majeraha yoyote yapaswa yatibiwe haraka. Kwa kufuata kwa uangalifu miongozo kama hiyo, inawezekana kwa wengi wenye anemia ya sickle-cell kuishi maisha ya kawaida, yenye furaha.
Namna Inavyopitishwa kwa Watoto
Kuelewa namna maradhi haya yanavyopitishwa kutoka kwa wazazi hadi kwa watoto wao, tunapaswa kuelewa aina za damu. Aina ya damu ni tofauti na kundi la damu; aina ya damu inahusiana na jeni. Watu wengi wana aina ya damu iitwayo AA. Wale ambao hurithi jeni-A kutoka kwa mzazi mmoja na jeni-S kutoka kwa mzazi mwingine wana damu aina ya AS. Watu wenye damu-AS hawana anemia ya sickle-cell, lakini wanaweza kupitisha kasoro hiyo kwa watoto wao. Watu ambao hurithi jeni-S kutoka kwa mzazi mmoja na jeni-S nyingine kutoka kwa mzazi mwingine wana damu aina ya SS, aina ya damu ya anemia ya sickle-cell.
Hivyo, kwa mtoto kurithi damu aina ya SS, ni lazima awe amerithi jeni-S yenye kasoro kutoka kwa kila mzazi. Kama vile inahitaji watu wawili kuzaa mtoto, inahitaji watu wawili kupitisha anemia ya sickle-cell. Kwa kawaida, kasoro hiyo hupitishwa wakati wazazi wote wawili wana damu aina ya AS. Mtu mwenye damu aina ya AS afungapo ndoa na mtu mwingine mwenye damu aina ya AS, kuna uwezekano wa asilimia 25 kwamba mtoto yeyote watakayemzaa atakuwa na damu-SS.
Hii haina maana kwamba ikiwa wana watoto wanne, mmoja atakuwa na anemia ya sickle-cell na wale wengine watatu hawatakuwa nao. Ingawa yaweza kuwa kwamba mmoja kati ya wale wanne ni SS, ingeweza kutukia pia kwamba wawili, watatu, au hata wote wanne ni SS. Inaweza kutukia pia kwamba hamna mtoto yeyote mwenye SS.
Maamuzi Yenye Ujuzi Kabla ya Ndoa
Ni jambo lenye hekima kwa watu wenye asili ya Kiafrika kutafuta kujua aina ya damu yao muda mrefu kabla hawajafikiria ndoa. Hili laweza kufanywa kwa kupimwa damu. Watu wenye damu aina ya AA waweza kuwa na hakika kwamba hamna yeyote kati ya watoto wao atakayekuwa na anemia ya sickle-cell hata wafunge ndoa na nani. Wale wenye damu aina ya AS wapaswa kuelewa kwamba ikiwa wanafunga ndoa na mtu mwenye damu aina ya AS pia, wajihatarisha sana kuzaa mtoto ambaye atakuwa na anemia ya sickle-cell.
Ingawa madaktari wengi hawapendekezi kabisa mtu mwenye damu aina ya AS kufunga ndoa na mwingine mwenye AS, washauri katika kituo cha sickle-cell huwaruhusu watu kufanya uamuzi wao wenyewe. Dakt. Omoike asema: “Kazi yetu si kutisha watu au kuwaambia ni nani wanaopaswa au hawapaswi kufunga ndoa nao. Hakuna mtu awezaye kutabiri kwa uhakika kwamba mtoto azaliwaye kutokana na wenzi wenye damu ya AS atakuwa na damu SS, kwani hilo ni jambo la nasibu. Hata kama wana mtoto mwenye SS mtoto huyo aweza kuvumilia kasoro hiyo bila matatizo mengi. Lakini tunataka watu waelewe aina yao ya damu. Na sisi hujitahidi kusaidia watu kimbele wafahamu kile kiwezacho kutokea ili kwamba wakipata watoto wenye SS, hawatashtuka. Kwa njia hiyo wapo katika nafasi si ya kufanya uamuzi ukitegemea ujuzi wa mambo ya hakika tu lakini kujitayarisha wenyewe kiakili kukubali matokeo ya maamuzi hayo.”
[Maelezo ya Chini]
a Kasoro nyinginezo za sickle-cell ambazo huathiri uwezo wa damu kubeba oksijeni ni maradhi ya sickle-cell ya hemoglobini C na sickle beta thalassemia.
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Umuhimu wa Upendo
Joy, ambaye sasa yupo katika miaka ya mapema ya 20, augua anemia ya sickle-cell. Kwa vile yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, kamwe hajakubali kutiwa damu mishipani. Mama yake, Ola, asema: “Nyakati zote nimehakikisha kwamba Joy anakula chakula kizuri ili kujenga damu yake. Ninaamini kwamba uangalizi wa upendo wa mzazi ni muhimu. Maisha yake, kama ya watoto wangu wengine ni ya thamani kwangu. Bila shaka, watoto wote huhitaji upendo, lakini jinsi gani zaidi sana wale wanaong’ang’ana na ugonjwa!”
[Picha katika ukurasa wa 23]
Tope ana “sickle cells,” kama ionyeshwavyo na mishale
[Hisani]
Sickle cells: Picha #1164 imetoka kwa American Society of Hematology Slide Bank. Imetumiwa kwa idhini