Wanatafuna Kuelekea Taabu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
NYIMBO fupi zenye kunasa upendezi redioni huwatia moyo watu kuitumia. Wahusika wakuu wa sinema huchangia kuitangaza katika televisheni, magazeti na magazeti ya habari kuwa kitu ambacho kingeweza kuongoza kwenye njia ya maisha yenye kusisimua na ya sifa. Lakini maandishi ya herufi ndogo yanayopatikana chini ya matangazo ya tambuu huonya kwamba kuitumia bidhaa hiyo kwaweza kudhuru afya yako. Hiyo ni nini? Ni kitu chenye kuraibisha na chenye kudhuru kiitwacho tambuu.
Tambuu hutumiwa Asia—kwa kiasi kikubwa—katika India. Katika hali yayo ya asili, hiyo huwa na mchanganyiko uliopondwa wa popoo, tumbaku na vichanganyiko vinavyoongeza ladha. Tumbaku na popoo hufanya tambuu iraibishe. Hivi huwekwa juu ya jani la mpopoo ambalo limepakwa chokaa na catechu, kitokezwaji cha mmea chenye athari ya kukausha. Jani hilo hukunjwa ili kufungia vitu vilivyomo kisha kifurushi chote hutumbukizwa kinywani. Aina inayopendwa sana inaitwa pan masala, iliyo na vichanganyiko vivyo hivyo vilivyochanganywa vikiwa vikavu na kufungwa katika vifuko vidogo viwezavyo kubebeka kwa urahisi na kutumiwa wakati wowote.
Kutafuna huchukua wakati mwingi na hutokeza kiasi kikubwa cha mate, ambayo yapaswa yatemwe kwa vipindi tofauti. Nyumba nyingi ambapo tambuu hupendwa huwa na chombo cha kutemea mate, lakini nje ya nyumba kijia au ukuta huwa mahali pa kutemea mate. Hiyo ndiyo sababu ya madoa ya rangi ya kikahawia ambayo yanaweza kuonekana katika ngazi na kumbi za majengo mengi katika India.
Kulingana na uchunguzi wa Tata Institute of Fundamental Research, kila mwaka asilimia kumi ya visa vyote vipya vya kansa nchini India ni kansa ya kinywa—kiasi cha mara mbili ya wastani wa ulimwenguni. Dakt. R. Gunaseelan, daktari-mpasuaji wa kinywa, taya na uso, aungana na madaktari-wapasuaji wengine kote katika India kulaumu hasa utafunaji wa tambuu. Ataarifu hivi katika India Express: “Aina zote za tambuu ni zenye madhara kwa kinywa.” Alitaja kwamba tambuu “bila shaka yaweza kuongoza kwenye kansa ya kinywa” na kwamba “kuitafuna ni kama kualika uharibifu wa uso.” Hivyo kuitumia tambuu kungeweza kumaanisha mtu kutafuna kuelekea taabu.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Asilimia kumi ya visa vipya vya kansa katika India ni kansa ya kinywa
[Hisani]
Picha ya WHO ya Eric Schwab