Bado Wanalima Mashamba kwa Kutumia Farasi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
KATIKA enzi hii ya tekinolojia ya juu, baadhi ya watu waweza kuona vigumu kuamini kwamba kuna wakulima ambao bado wanalima mashamba yao kwa kutumia farasi. Bado zipo sehemu ambazo vikundi vya farasi wenye nguvu za kukokota mizigo wanatumiwa badala ya matrekta.
Kwa kweli, mashamba yalimwayo na farasi yamekuwa haba. Lakini bado kuna faida ya kutumia farasi.
Matumizi Katika Kilimo
Tokea nyakati za mapema farasi wamekuwa wakitumiwa wakiwa wanyama wa kufanya kazi ngumu. Wanatajwa katika historia za Wasumeria, Wahiti, Wamisri, na Wachina. Lakini kwa karne nyingi matumizi yao katika kilimo yalikuwa kidogo. Hii ni kwa sababu maksai walifikiriwa kuwa rahisi kutunzwa na wangeweza kutumika wakiwa chakula kwa familia washindwapo kufanya kazi. Lakini maksai wanafanya kazi polepole kuliko farasi.
Kufikia karne ya 19, farasi walichukua nafasi ya maksai katika ulimaji wa ardhi katika mabara mengi ya Magharibi. Kichapo kimoja kilieleza kwamba sababu moja ilikuwa “uvumbuzi wa mashine bora za mashamba [ambazo] zilitengenezwa zifae wepesi wa farasi kuliko maksai wenye kufanya kazi polepole.”
Baadaye aina za farasi kama vile Clydesdale katika Scotland, Suffolk Punch na Shire katika Uingereza, na Percheron zaidi sana katika Ufaransa walikuwa wakitumiwa katika kilimo. Farasi hawa wenye kufanya kazi polepole lakini wenye nguvu walizalishwa na wale wasio wazito sana ili kutokeza farasi wenye nguvu kiasi lakini wenye kufanya kazi haraka. Farasi hao waliozalishwa kipekee walikuja kuitwa farasi wa kukokota mizigo, ikielekeza kwenye uwezo wao wa kukokota mizigo mizito.
Farasi kwa Kulinganisha na Trekta
Bila shaka hamna aina ya farasi ambaye aweza kulinganishwa na uwezo wa kuvuta wa trekta la kisasa. Lakini waweza kushangazwa kujua kiasi cha nguvu walizo nazo farasi! Katika 1890, farasi wawili wa kukokota mizigo wa aina ya Clydesdale walivuta behewa lililojaa mizigo likiwa limeshika breki! Na katika 1924 jozi ya farasi wa Uingereza aina ya Shire pia walifanya jambo la kushangaza sana kama hilo, wakivuta uzito unaokadiriwa kuwa tani 50!
Farasi wa kukokota mizigo pia ni wenye akili na wenye kujichukulia hatua. Kwa kielelezo, kikundi cha farasi kilimacho shamba ni kama hakihitaji mwongozo kabisa ikiwa kuna farasi mzuri wa kufuata mtaro. Huyo farasi atakiongoza kikundi, akifuata mtaro siku nzima. Inafikiriwa kwamba vikundi vyaweza kulima kwa mistari iliyonyooka kabisa kwa sababu farasi huvaa vitu vinavyowazuia wasiweze kuona kando-kando na hawawezi kuangalia nyuma, jambo ambalo watu wanaolima kwa kutumia trekta huelekea kufanya.
Zaidi ya hayo, wakati wa mavuno farasi waweza kuwa wenye ubadilifu zaidi ya trekta. Uwezo wao wa kuzunguka digrii 90 barabara—na inapokuwa lazima, kuzunguka kwa digrii 180—huonyesha kwamba hawaachi kulima sehemu yoyote ya shamba wakati wa kulima.
Vikundi vya Farasi Vikiwa Kazini
Kikundi cha farasi kinachoitikia maagizo kutoka kwa mwelekezi hutazamisha sana. Kikundi kinazoezwa kuitikia maagizo maalum kwa kufanya mambo fulani maalum, ingawa lugha hasa na maneno yatumiwayo hubadilika kutegemea mwelekezi. Hawa farasi huzoea maneno na namna ya sauti ya kila mwelekezi. Mbinja maalum, pamoja na maneno ya kutia moyo kutoka kwa mwelekezi, yaweza kuwa ishara kwa farasi kuanza kwenda.
Katika Australia farasi aliye upande wa kulia wa kikundi (kutoka mahali alipo mwelekezi) hujulikana kuwa farasi wa kulia na farasi aliye kushoto, farasi wa karibu. Labda majina hayo yalitokana na namna ambayo wafanyakazi wa zamani waliendesha vikundi vyao, kwa kawaida wakitembea upande wa kushoto wa farasi zao.
Inasisimua kama nini kuangalia mstari wa farasi kumi waliofungwa pamoja wageukapo kwa digrii 90, wakiitikia miito ya mwelekezi! Kugeuka kushoto, farasi wa karibu apaswa kuchukua hatua fupi-fupi kurudi nyuma wakati kikundi kilichobaki kinapogeuka digrii 90 kumzunguka. Kisha, ikiwa wanapaswa kugeuka kulia, farasi wa kulia apaswa kuchukua hatua fupi-fupi kurudi nyuma. Katika nyakati kame inasisimua kama nini kuona kikundi kikipotea katika wingu la vumbi kisha kuonekana tena kwa kishindo baada ya kumaliza kuzunguka!
Kila farasi anaitwa kwa jina lake na huliitikia hilo kulingana na namna ya sauti itumiwayo na mwelekezi. Ikiwa farasi mmoja anakuwa mzembe, sauti kali yenye kukemea ikiita jina lake, kwa kawaida hutosha kumwamsha. Katika mafunzo ya mapema farasi kwa kawaida wapaswa kujifunza kwamba sauti kama hiyo hufuatana na kupigwa kidogo kwa fimbo au mjeledi. Somo hilo linapoeleweka, ni nadra sana nidhamu kali ihitajike.
Mfano wa Siku ya Kazi
Mkulima aweza kuamka saa kumi na moja asubuhi ili kulisha farasi na kupata kiamsha-kinywa chake mwenyewe farasi walapo. Farasi wajua ni lazima wanywe maji mapema kabla kazi ya siku haijaanza kwani hawatapata chochote cha kunywa kabla ya chakula cha mchana. Kila farasi hupigwa brashi kabla hajavishwa lijamu. Hili huzuia mwasho wa ngozi nayo hutokeza hisia nzuri. Kwa kawaida farasi humzunguka mkulima na kwa subira hungoja zamu zao. Kisha farasi huvishwa lijamu na kuwekwa nira pamoja. Yote haya yaweza kuchukua muda wa saa moja au zaidi, ikitegemea ukubwa wa kikundi. Pia mfuko wa puani hutayarishwa kwa ajili ya chakula cha mchana cha farasi. Hivyo basi, si mwelekezi peke yake astahiliye chakula cha mchana!
Bila kulalamika kikundi hufanya kazi ngumu kwa muda wa saa nane au kumi, na ikiwa ukanda wa shingoni na vifaa vyakaa sawasawa, farasi hao hawatamaliza kazi wakiwa na mabega yenye vidonda na yaliyochubuka. Jioni ianzapo, mtu na mnyama wanafuraha kuelekea nyumbani kufurahia chakula kwa amani, kinywaji cha kutosha na pumziko zuri.
Wale ambao bado hulima mashamba yao kwa kutumia farasi waweza kuwa wenye haraka kusema kwamba hii inafurahisha zaidi kuliko kusikia mngurumo wa mashine siku nzima. Utulivu humfanya mkulima ajisikie ni sehemu ya shamba. Aweza kuona kwa ukaribu zaidi uumbaji umzungukao—sauti za ndege wanaochakura-chakura, wakaguapo udongo uliotokea katika mitaro iliyolimwa, harufu ya majani yenye unyevu; kutatarika kwa ukungu plau ipasuapo udongo ulioganda katika baridi ya asubuhi—mambo madogo ambayo yaelekea kutochukuliwa kwa uzito mkulima apigwapo na kelele za trekta.
Kweli, trekta yaweza kufanya kazi kwa muda wa saa 24 kwa siku, kazi ambayo farasi hawawezi. Ni kweli pia kwamba matrekta yaweza kulima shamba kubwa na huhitaji ukarabati kidogo. Lakini hamna trekta iliyozaa trekta nyingine ndogo, na hili ni moja tu ya mambo mengi ambayo hufanya kufanya kazi na farasi kuwe jambo lisilo na kifani. Mwelekezi pia aweza kufurahia “mazungumzo” pamoja na farasi wake wafanyapo kazi. Na wao hujibu kwa utii wao, masikio yao yakielekezwa mbele kunasa kila neno lake.
Ukulima ni kazi ngumu na mara nyingine ni kazi yenye kuchosha. Lakini kwa wale ambao bado wanalima mashamba yao katika njia ya zamani, kwa farasi, kwaweza kuwa na shangwe tele kutokana na kufanya kwa ukaribu na wanyama hawa walio uumbaji wa Mungu ambao wana nguvu na bidii!
[Picha katika ukurasa wa 26]
Farasi waweza kuwa wenye ubadilifu zaidi ya trekta