Soko Linalofanywa Oktoba “Soko la Farasi la Kimataifa la Kale Zaidi Katika Ulaya”
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA IRELAND
JUMA lililopita mji huu mdogo ulikuwa wenye amani na utulivu huku watu wakiendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu. Lakini juma hili hali ni ya kelele. Mji umesongamana kwa sababu ya wageni zaidi ya 50,000 waliokaribishwa na wakazi wapatao 6,000 wa mji huu. Ingawa hivyo, kwa kweli, kinachovutia uangalifu, si kusukumana kwa umati wa watu au vibanda vingi vilivyoko sokoni na wala si watumbuizaji wenye uchangamfu wa barabarani. Kinachovutia ni farasi! Wako kila mahali!
Tuko wapi? Katika mji mdogo wa Ballinasloe, ulioko kilometa zipatazo 140 upande wa magharibi wa Dublin, jiji kuu la Ireland. Mabadiliko haya makubwa katika hali ya kawaida ya utulivu ya mji huu yameletwa na nini? Ni kile kinachoelezwa na wapangaji kuwa “Soko la farasi la kimataifa la kale zaidi katika Ulaya,” Soko Linalofanywa Oktoba.
Kwa Nini Lifanywe Ballinasloe?
Ni nini kinachofanya Soko Linalofanywa Oktoba lipendwe na wengi? Gazeti Amkeni! lilimhoji George, aliye mkulima wa mahali hapa na ambaye ameuza farasi wengi katika soko hilo. “Katika Ballinasloe,” yeye asema, “mtu yeyote—awe tajiri au maskini—anaweza kuleta na kuuza farasi wa aina yoyote. Hiyo ndiyo sababu peke yake.” Lakini kwa nini hilo ni tofauti sana na mahali penginepo? “Katika sehemu nyinginezo, uuzaji wa farasi ni jambo linalowekewa mipaka na kudhibitiwa,” aeleza George. “Masoko mengine ya umma huuza farasi wa jamii moja pekee. Na mara nyingi uuzaji huhusisha kuwekwa kwa maandishi mengi sana. Ni katika masoko machache sana hapa ambapo mtu yeyote aweza kuleta farasi kwenye uwanja, halafu amuuze bila mambo mengi! Hapa katika Soko Linalofanywa Oktoba, biashara ya farasi hufanyika tu jinsi ilivyokuwa ikifanyika katika muda wa miaka mia mbili au mia tatu hivi iliyopita—biashara ya moja kwa moja bila kufuata utaratibu fulani rasmi, kwenye uwanja wa soko.”
‘Ballinasloe ulikujaje kuwa kituo cha utendaji wa aina hii wenye shamrashamra? Ni kwa nini wafanya-biashara walitoka mbali sana kama vile Urusi ili kuja kununua farasi hapa?’ tukastaajabu. Kuchunguza kidogo historia kunatoa jibu.
Baadhi ya wafalme wenye cheo cha juu katika Ireland walitawala wakiwa Tara, jiji lililo umbali wa kilometa 30 kaskazini-magharibi ya Dublin. Hiki kilikuwa kituo cha kidini, na baadaye cha kisiasa katika Ireland. Watu walienda Tara ili kulipa kodi na kupata habari juu ya sheria mpya zilizokuwa zimeanzishwa. Tara inahusianaje na Ballinasloe? Mji wa Ballinasloe ulisitawi kuzunguka kivuko cha mto kwenye moja ya njia za kawaida zinazotoka magharibi na kuelekea Tara. Wasafiri waliotoka na kwenda kwenye makao ya kifalme walikiona kivuko hiki cha mto kilichokuwa umbali wa safari ya siku nzima kwa farasi kutoka pwani ya magharibi, kuwa mahali panapofaa pa kubadilishana bidhaa na habari. Wapangaji wa Soko Linalofanywa Oktoba wanasema kwamba, ‘kuna ushuhuda wa kuwapo kwa biashara ya farasi katika eneo hili mapema katika karne ya tano W.K.’
Katika nyakati za karibuni zaidi, eneo linalofaa sana la Ballinasloe liliufanya uwe mahali bora kwa ajili ya Soko kubwa lililo rasmi, lililoanzishwa hapa mapema katika karne ya 18. Baadhi ya wakulima wangefunga safari yao mwezi mmoja hivi mapema kabla ya wakati ili wakauze mifugo yao kwenye soko hili, hata ingawa kwa wengine ilimaanisha kusafiri kilometa zipatazo 200. Baada ya muda, farasi wakawa kitu chenye kuvutia zaidi hapa.
Nchi ya Ballinasloe ina rutuba sana na inafaa kwa ufugaji wa mifugo. Inatokeza wanyama wenye nguvu, afya, na wanaozaa. Mwandikaji Mark Holdstock aeleza hivi, “Farasi wa Ireland, wanajulikana sana kwa sababu ya nguvu zao.” Aendelea kusema: “Farasi kama wale wa jamii ya Irish Draught wamestawi kwa mamia ya miaka kwenye nchi hii, huku wakizidi kuwa wenye nguvu karne baada ya nyingine.”
Uhitaji wa Farasi
Leo jambo kuu zaidi la mahali hapa ni biashara ya farasi! Ni nini kilichofanya farasi wawe wa maana sana? Katika karne ya 18 na 19, wakulima kotekote katika Ireland walitumia sana farasi katika ulimaji wa mashamba. Walihitaji farasi wenye nguvu, wenye kutegemeka katika kulima kwa plau kwenye mashamba ambayo mara nyingi yalikuwa yenye majimaji na matope. Lakini kulikuwa na sababu nyingine ya uhitaji mkubwa wa farasi. Majeshi yalihitaji farasi wenye nguvu ambao hawangeogopeshwa na kelele za pigano na ambao wangekuwa na nguvu na wasiochoka upesi ili kusafirisha vifaa vizito kupitia kwenye nchi yenye mabonde. Farasi wa jamii ya Irish Draught alikuwa na sifa hizi zote na kwa hivyo alitafutwa sana. Uzalishaji wa huyu farasi pamoja na yule wa Thoroughbred ulitokeza farasi aliyekuwa jasiri, na shupavu aliyefaa sana kutumiwa na askari-jeshi wa farasi.
Maelfu ya farasi na askari-jeshi waliuawa vitani. Ili kuchukua nafasi ya farasi waliouawa katika vita vingi vilivyopiganwa Ulaya, wawakilishi wa jeshi kutoka katika nchi nyingi za Ulaya, na hata kutoka nchi za mbali sana kama vile Urusi, walikuwa tayari kufunga safari kwenda Ballinasloe ili kununua farasi wengine, wa jamii ya Thoroughbred wenye kutegemeka. Kufikia katikati ya karne ya 19, Soko Linalofanywa Oktoba likawa “soko kubwa zaidi la farasi katika Ulaya.” Holdstock asema, “Uvumi ulienea kwamba, nusu ya farasi waliotumiwa katika lile Pigano la Waterloo walinunuliwa Ballinasloe.”a
Mbinu za Kufanya Biashara ya Farasi
Bila shaka, uhitaji huo wa pekee wa farasi ulipungua sana katika karne ya 20. Magari ya kivita yalichukua mahali pa askari-jeshi wa farasi, na trekta zikachukua mahali pa plau zinazovutwa na farasi. Kwa kweli, biashara ilikuwa karibu kukoma katika Ballinasloe. Hata hivyo, miaka 40 hivi iliyopita, soko hili lilifunguliwa tena.
George aliyetajwa pale mwanzoni, alifanyaje biashara ya farasi hapa? “Nilikwenda kwenye uwanja wa soko nikiwa na farasi niliotaka kuwauza, na baada ya muda usio mrefu mtu fulani angetokea na kuniuliza pesa nilizozitaka kwa ajili ya farasi hao,” yeye asema. Kisha George aeleza baadhi ya mbinu katika biashara ya farasi: “Kwa muda fulani tungebishania bei, na mara nyingi sana tungefanya hivyo kwa hima. Na ikiwa yule mnunuzi alitaka sana farasi wangu, angekuwa mwangalifu kwa kuepuka kuonyesha upendezi mwingi, akihofu kwamba huenda nikaongeza bei. Angeweza kwenda na kurudi baadaye, akitumaini kwamba kwa wakati huo hakuna mtu aliyetoa pesa zaidi ya zile alizozitoa yeye. Aweza hata akamtuma mwenziye aje abishane nami juu ya bei na hivyo akinifanya niwe mwenye shughuli, ili kuwazuia wengine wasije kumnunua yule farasi. Mwishowe tungepatana juu ya bei na tungethibitisha hilo kwa salamu. Kwa kawaida, angelipa pesa taslimu, na papo hapo farasi huyo angekuwa mali yake. Kwa kuwa hakukuwapo na shirika fulani lililosimamia shughuli hizi, mara baada ya muuzaji kupokea pesa, hakukuwa na dhamana!”
Huenda ikawa vigumu kwa mtu asiyehusika kujua farasi aliyekuwa akiuzwa na yule asiyeuzwa. “Ikiwa farasi yuko kiwanjani,” George asema, “basi anauzwa.” Kisha anataja baadhi ya desturi za mahali hapo: “Wakati wa zamani—na hata nyakati fulani leo—donge la udongo liliwekwa kwenye miguu ya nyuma ya farasi aliyeuzwa. Kama sivyo, farasi huyo angechukuliwa tu na mwenye kumnunua. Kwa kufuata desturi nyingine ya kale katika biashara ya farasi hapa Ireland, muuzaji alimrejeshea mnunuzi ‘pesa za bahati’ baada ya mnunuzi kulipa. Hiki kilikuwa kiasi kidogo cha pesa alichorudishiwa mnunuzi baada ya kumalizika kwa shughuli ya kibiashara. Pesa hizo zilipaswa zimletee farasi huyo pamoja na mmiliki wake ‘bahati njema.’
“Unahitaji kuwa na ujuzi mzuri sana juu ya farasi na thamani yao,” aonya George. “Watu wengi hutoka kwenye soko hilo wakiwa wameridhika, kwa sababu kwa kawaida unapata farasi kulingana na pesa unazolipa. Wafanya-biashara ya farasi wenye uzoefu wanahitaji pia kujihadhari. Namfahamu mwuza-farasi mmoja aliyeuza farasi kisha akaenda kunywa pombe kwenye baa kabla ya kwenda nyumbani. Wakati huohuo, yule aliyemnunua farasi alichana na kunyoa singa za yule farasi, akibadilisha sura ya farasi huyo kwa njia yenye kutazamisha. Huyu farasi ‘mpya’ aliletwa kwa yule mwuza-farasi, naye akidhania kwamba alikuwa farasi mwingine tofauti, alimnunua mara moja kwa bei ya juu zaidi!”
Kuna hatari nyinginezo mbali na kufanya ununuzi usio wa hekima. “Uwe mwangalifu mahali unaposimama!” ashauri George. “Usisahau kwamba kukiwa na farasi wengi wanaosimama karibu-karibu—labda hata kwa muda mrefu sana—na kukiwa na shughuli hizo zote, farasi wengi hupatwa na woga nao huelekea kupiga teke. Nimewaona farasi wengi waliokuwa na woga mwingi wakisimama kwa miguu yao ya nyuma, hata walipokuwa wakishughulikiwa na mpanda-farasi mwenye uzoefu.” Yeye aendelea kusema: “Na zaidi ya hayo! Vaa jozi inayofaa ya viatu vya mpira. Huenda kile unachokikanyaga kisiwe matope!”
[Maelezo ya Chini]
a Pigano la Waterloo lilipiganwa Ulaya katika mwaka wa 1815. Lilihusisha majeshi mbalimbali na jumla ya askari 185,000. Yaelekea kwamba huenda kulikuwa na maelfu ya farasi waliotumiwa na askari katika pigano na pia katika usafirishaji.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Farasi mfupi mnene mwenye rangi mbalimbali akisubiri kuuzwa
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Uwanja wa soko katika Ballinasloe kwenye siku ya kwanza
[Picha katika ukurasa wa 17]
Farasi wa jamii hii ni mchanganyiko wa Irish Draught na Thoroughbred