Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 3/22 kur. 18-19
  • Kukabiliana na Maradhi ya Utumbo Mwembamba

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kukabiliana na Maradhi ya Utumbo Mwembamba
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Kinachoweza Kufanywa?
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Magonjwa Je! Kuna Siku Yatakapokwisha?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
  • Mambo Ambayo Watunzaji Waweza Kufanya
    Amkeni!—1998
  • Ulimwengu Bila Maradhi
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 3/22 kur. 18-19

Kukabiliana na Maradhi ya Utumbo Mwembamba

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA FINLAND

“Ulitumia unga gani kuoka keki hii?”

“Mbona, si nilitumia unga wa mahindi.”

“Na ulitia nini kwenye sufuria?”

“Nilitia makombo ya mkate.”

“Basi, nasikitika, siwezi kula keki hii.”

IKIWA unaugua maradhi ya utumbo mwembamba au celiac labda umekuwa na mazungumzo kama hayo yasiyostarehesha. Ugonjwa huu unaoathiri umeng’enyaji wa chakula husababishwa na hali ya mwili kutoweza kustahimili kitu fulani kipatikanacho katika vyakula vingi. Kitu hicho ni gliadin ambacho ni sehemu ya gluten, ambayo hupatikana katika ngano na aina mbalimbali za shayiri. Hiyo gluten haidhuru watu wengi, lakini kwa watu ambao wana maradhi ya utumbo mwembamba, yaweza kudhuru utando wa utumbo mwembamba, na kuufanya usiweze sana kuingiza lishe mwilini kutoka kwa chakula.

Dalili za maradhi ya utumbo mwembamba zaweza kutia ndani maumivu ya tumbo, kujaa kwa gesi tumboni, kuhara, na kupungua mwili. Bila shaka, magonjwa mengine vilevile yana dalili hizo na hiyo inafanya iwe vigumu kutambua maradhi ya utumbo mwembamba. “Kwa miaka mingi niliambiwa kwamba nina ‘ugonjwa wa kuhara,’” asema mwanamke mmoja mwenye kuugua aitwaye Judy.

Mara nyingi maradhi ya utumbo mwembamba hudhihirika utotoni, lakini watu wengine hawaonyeshi dalili hizo mpaka wanapofikia umri wa makamo. Lakini, madaktari wanasema kwamba katika angalau baadhi ya hali hizo, huenda watu hao walikuwa na ugonjwa huo ingawa haukuwa ukionekana. Lakini maradhi ya utumbo mwembamba yaweza kudhuru sana yasipotibiwa. Kwa kawaida, watoto wenye ugonjwa huo wana miili midogo na wamedhoofika, wana tumbo kubwa na misuli midogo. Kwa kuwa ugonjwa huu huzuia vitamini zisiingie mwilini, maradhi kadhaa yaweza kufuata, kutia ndani upungufu wa damu, matege, na kiseyeye. Ugonjwa huo ukizidi unaweza kusababisha kasoro za mifupa au mifupa dhaifu. Katika hali chache sana, maradhi ya utumbo mwembamba yaweza kusababisha kifo, hasa miongoni mwa watu wazima ambao wameugua sana ugonjwa huo na kwa muda mrefu. Lakini, watu wengi ambao wana maradhi ya utumbo mwembamba wakipata matibabu mazuri, wao wanaweza kukabiliana na maradhi hayo na hata kupata nafuu.

Ni Nini Kinachoweza Kufanywa?

Tiba bora kwa maradhi ya utumbo mwembamba ni vyakula visivyo na gluten—yaani, kuepuka vyakula vyote vyenye ngano na shayiri. Si rahisi kuepuka vyakula hivyo. Mtu mmoja anayeugua ugonjwa huo asema: “Mara ya kwanza niliposikia kwamba siruhusiwi tena kula ngano au shayiri, nilifikiria, ‘Hiyo si vigumu. Nitaepuka tu kula mkate na vitu vitamu vilivyotayarishwa kwa ngano.’ Lakini nilipotambua hatimaye kwamba kuna vyakula vingi vinavyotia ndani nafaka hizi—hasa ngano—nilishtuka sana!”

Ni lazima watu wenye maradhi ya utumbo mwembamba wasome kwa uangalifu vibandiko vya vyakula. Ingawa watu wenye maradhi ya utumbo mwembamba ni lazima waepuke kula ngano na shayiri, wao wanaweza kula buckwheat, Indian corn, mchele, maharagwe aina ya soya, mtama, na vyakula vyenye viazi. Vilevile kuna michanganyiko kadhaa inayokubalika ya unga ambao hauna gluten. Ni kweli kwamba mtu anaweza kuvunjika moyo sana kwa sababu mara nyingi sana maduka hujaa tu vyakula ‘asivyopaswa kula.’ Lakini usivunjike moyo. Badala yake, zingatia vyakula ambavyo unaweza kula badala ya kufikiria vyakula usivyoweza kula. Baada ya muda haitakuwa shida sana kununua vitu.

Huenda ikaonekana kwamba kula vyakula visivyo na gluten kwaweza kuvuruga maisha yako ya kijamii. Lakini usijitenge na wengine eti kwa sababu una maradhi ya utumbo mwembamba. Badala yake, uwaambie rafiki zako juu ya maradhi ya utumbo mwembamba na uwajulishe jinsi wanavyoweza kukusaidia kuepuka vyakula visivyo na gluten. Wengine wakijua mahitaji yako, yaelekea watafurahi kukusaidia. Wengine wakisema maneno bila kufikiri, usikasirike. Majibu yako ya kirafiki yatawafanya wawe wenye hisia-mwenzi zaidi.

Baada ya muda, wengine ambao hawana maradhi makali ya utumbo mwembamba wanaweza kuanza tena kula vyakula vyenye gluten. Iwe hivyo au isiwe hivyo kwako, wewe endelea kuwa na mtazamo mzuri. “Zingatia mambo mazuri yanayohusika,” apendekeza mwanamke mmoja anayeugua maradhi ya utumbo mwembamba. Mambo mazuri? Aendelea kusema: “Mtu hawezi kuambukizwa maradhi ya utumbo mwembamba, na tiba yake ni sahili na rahisi kueleweka—kuwa mwangalifu kwa vyakula unavyokula. Kadiri uendeleavyo kuifuata tiba hiyo, ndivyo utakavyoendelea kupata nafuu. Yaelekea kwamba utasikia vizuri japo unaugua maradhi ya utumbo mwembamba.”

[Sanduku katika ukurasa wa 19]

Kuandaa Utegemezo

Ikiwa mtu anaugua maradhi ya utumbo mwembamba, usifikiri kwamba yeye anasumbua tu kwa sababu anakataa kula aina fulani ya chakula. Na uepuke kusema maneno yaumizayo kama vile, “Mtu aonekanaye kuwa mwenye afya nzuri hivi awezaje kuwa mgonjwa?” Jambo kubwa zaidi, usijaribu kumshawishi mtu mwenye ugonjwa wa utumbo mwembamba ale chakula chenye gluten, labda ukisema: “Kidogo tu hakitakudhuru.” Hakika kinaweza kudhuru! Kumbuka kwamba utumbo mwembamba wa mtu anayeugua ugonjwa huo unauona gluten kuwa sumu, na kupatwa na madhara.

Si vigumu kufuata mahitaji ya vyakula vya mtu ambaye ana ugonjwa wa utumbo mwembamba. Ukifanya marekebisho machache tu ya vyakula unavyonunua dukani, utapata kwamba kuna vyakula vya kutosha ambavyo vinakubalika. Hata inawezekana kutayarisha vyakula vingi ambavyo havimdhuru mwenye ugonjwa wa utumbo mwembamba. Kwa kweli wageni wote wanaweza kufurahia kula vyakula ambavyo havina gluten. Labda hata hawataweza kutambua tofauti iliyoko. Kwa kuongezea, mtu mwenye ugonjwa wa utumbo mwembamba asiaibishwe—naye atafurahi!

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ni lazima watu wenye maradhi ya utumbo mwembamba waepuke ngano na aina mbalimbali za shayiri

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki