Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w84 3/1 kur. 4-7
  • Magonjwa Je! Kuna Siku Yatakapokwisha?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Magonjwa Je! Kuna Siku Yatakapokwisha?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msingi wa kuwa na Tumaini
  • Mwisho wa Magonjwa Ni Karibu!
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • Ulimwengu Usio na Magonjwa
    Amkeni!—2004
  • Kichocho—Je, Kitaondolewa Karibuni?
    Amkeni!—1997
  • Ulimwengu Bila Maradhi
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
w84 3/1 kur. 4-7

Magonjwa Je! Kuna Siku Yatakapokwisha?

Kama wewe ungalipatwa na kansa ya mifupa karibu miaka 10 iliyopita, mataraja yako ya wakati ujao yangekuwa ya kuhuzunisha sana. Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Kansa, miaka 10 iliyopita asilimia 80 ya watu wazima vijana waliokuwa na kansa ya mifupa walikufa katika muda wa miaka mitatu. Lakini, leo, kwa sababu ya maendeleo ya sayansi, inadaiwa kwamba asilimia 90 ya wagonjwa hao wanaondokwa na ugonjwa huo miaka mitatu baada ya ugonjwa huo kujulikana.

Maendeleo ya namna iyo hiyo yamefanywa katika kutibu magonjwa mengine. Kwa mfano, mwaka wa 1979 tume ya duniani pote iliyowekwa na Tengenezo la Afya Ulimwenguni ilitangaza kwamba ugonjwa wa ndui ulikuwa umeangamizwa kabisa ulimwenguni pote. Kwa habari ya ugonjwa wa kifua kikuu, ingawa watu wapatao milioni 3 bado wanauawa na ugonjwa huo kila mwaka, gazeti World Health linadai hivi: “Sisi tumekwisha kupata silaha zote zinazohitajiwa ili kufagilia mbali ugonjwa wa kifua kikuu. Vitu vya pekee tunavyohitaji ili kuushinda ugonjwa wenyewe, sasa na milele, ni pesa na nia ya watu wa siasa ya kutaka kuumaliza.

Haiwezi kukanwa kwamba sayansi imefanya jitihada kubwa katika kupambana na magonjwa. Hata hivyo uhakika huu ungali upo: Sayansi iko mbali sana na kushinda magonjwa na maradhi. Kwa mfano, ugonjwa wa moyo bado ndio kisababishi kikubwa zaidi cha vifo vya mapema mno katika nchi zenye maendeleo ya viwanda. Tena, tafadhali angalia lile sanduku lililo katika makala hii, linalouliza “Je! Sayansi Inamaliza Magonjwa?” Sehemu hiyo inaeleza magonjwa mengine yanayoendelea kutatiza sana sayansi ya tiba.

Jambo la kuvuruga akili ni kwamba hesabu ya magonjwa yenye kuua inaelekea kuongezeka. Magonjwa ya zamani yanashinda na magonjwa mapya yanazidi kutokea. Ni wazi kwamba, ingawa sayansi imefanya maendeleo makubwa na imetufanyia mengi tunayopaswa kutolea shukrani, kwa vyovyote haimalizi magonjwa na maradhi. Basi je! hakuna tumaini kwa wakati ujao?

Msingi wa kuwa na Tumaini

Kuna sababu kamili za kuwa na tazamio zuri la kweli kwamba magonjwa na maradhi yatafikia mwisho. Lakini hayatamalizwa na jitihada nzuri za wanasayansi, hapana. Yatamalizwa na chanzo cha juu zaidi.

Ili kushinda magonjwa daima, kuna mambo mawili ya maana sana yanayohitajiwa: (1) Uwezo wa kuyashinda na (2) nia ya kutaka kuyashinda. Moja la mambo hayo mawili haliwezi kufanikiwa bila ya lile jingine. Kumbuka kwamba gazeti World Health lilidai kwamba mwanadamu anaweza kufagilia mbali milele ugonjwa wa kifua kikuu, lakini amekosa “pesa na nia ya watu wa siasa ya kutaka kuumaliza.”

Kuna mtu mmoja tu katika ulimwengu nzima aliye na uwezo kamili kabisa na nia ya kutaka kufutilia mbali magonjwa yote milele, yaani, Mungu mwenyewe! Kwa kweli, Yesu Kristo, ambaye aliiga sifa za Baba yake kwa ukamilifu, alipokuwa duniani alionyesha kwa njia nzuri ajabu namna uwezo wenye kutolewa na Mungu unavyoweza kushinda magonjwa na hali za udhaifu wa mwili.​—Yohana 14:9.

Hakuna shaka kwamba kwa kutumia “uwezo wa Mungu,” Yesu Kristo aliweza kushinda magonjwa. (Luka 9:43, NW) Katika maana halisi kabisa Yesu aliwarudishia afya wagonjwa wengi, wenye udhaifu wa mwili na wenye kulemaa​—viwete, wasio na mikono au miguu na vipofu (Mathayo 15:30, 31), wenye kifafa, wenye miili iliyopooza (Mathayo 4:24), wenye ukoma (Luka 17:12-14), mwanamke mwenye kutokwa sana na damu (Marko 5:25-29), mtu mwenye mkono uliokauka (Marko 3:3-5), mwanamume mwenye ugonjwa wa safura (Luka 14:2-4) na watu wenye “maradhi mbali mbali.” (Luka 4:40) Hata kuna visa vitatu vilivyothibitishwa kuwa vya kweli kuonyesha Yesu alifufua wafu! (Luka 7:11-15; 8:49-56; Yohana 11:38-44) Katika visa vingi kati ya hivyo, maponyo yalitokea dakika iyo hiyo, bila ya wenye kuponywa kuhitaji kupewa kipindi cha kupata nafuu ya polepole au kurudia hali yao ya afya njema.

Bila shaka, ni wazi kwamba Yesu Kristo alikuwa na nia ya kutaka kushinda magonjwa. Jambo hilo linaonyeshwa na maponyo mengi aliyofanya. Lakini, Biblia inatumia njia yenye kugusa sana moyo kwa kufunua wazi tamaa ya moyoni ambayo Yesu alikuwa nayo ya kurudishia wengine afya nzuri.

Alipopata habari za kifo cha Yohana Mbatizaji, Yesu alisafiri kwa mashua akaenda mahali pa kuwa peke yake. Lakini inaonekana kuwa kundi la watu liliiona mashua ikiondoka nao wakagundua ilikokuwa ikielekea. Yesu alipofika alikuta wakiwa wanamngojea yeye. Yesu alitendaje? Je! aliona uchungu? Aliudhika? Yeye alikuwa na haki ya kupata pumziko na utulivu, sivyo? Ijapokuwa hivyo, yeye hakuwahesabu kuwa wasumbuaji, bali masimulizi yanaeleza hivi:

“Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.” (Mathayo 14:13, 14) Mwanachuo mmoja wa Biblia anasema hivi juu ya neno la Kigiriki lililotafsiriwa hapo kuwa “akawahurumia”: “[Hilo ndilo] neno lenye mkazo zaidi ya maneno yote ya kuonyesha huruma nyingi katika lugha ya Kigiriki. Limetokana na neno splagchna, maana yake matumbo, nalo linaeleza hali ya huruma inayomwingia mtu mpaka kwenye sehemu zilizo ndani zaidi za utu wake.” Ndiyo, Yesu hangeweza kukubali kuona taabu ya wengine akose kuwapunguzia maumivu yao.”​—Luka 5:12-14.

Hakuna shaka juu ya jambo hilo. Kwa kupewa uwezo na Mungu, Yesu Kristo aliweza kushinda magonjwa na pia alikuwa na nia ya kutaka kufanya hivyo. Na ndivyo alivyo hata sasa! (Waebrania 13:8) Maponyo aliyofanya alipokuwa angali duniani yalikuwa kivuli cha baraka za maponyo watakayofanyiwa wanadamu duniani pote chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu. ‘Lakini hayo yatafika wakati gani?’ huenda ukauliza.

Mwisho wa Magonjwa Ni Karibu!

Kama vile imeonyeshwa mara nyingi katika gazeti Mnara wa Mlinzi, “ishara” yenye matukio mengi, ambayo moja ni ‘magonjwa ya kipuku,’ au maradhi, imeonekana wazi-wazi kabisa tangu mwaka wa 1914. Ukiuchunguza ushuhuda wenyewe, utaona bila shaka kwamba maneno ya Yesu yametimia. Kwa hiyo, kiasi kikubwa cha magonjwa na maradhi tunayoona leo kinatimiza unabii wa Yesu kwenye Mathayo 24:3-7 na Luka 21:10,11. Maana yake ni kwamba sisi tunaishi kwenye “umalizio wa mfumo wa mambo”!

Karibuni Ufalme wa Mungu utauondoa mfumo mbovu huu kisha ulete mahali pa huo Taratibu Mpya yenye uadilifu. (2 Petro 3:13) Ndipo chini ya utawala ya Ufalme magonjwa ya kipuku, au maradhi, yataacha kutunyang’anya afya yetu na uhai wetu. Hakika tunaweza kushukuru sana kwa sababu Baba yetu wa kimbingu mwenye upendo ana uwezo na hata nia ya kufutilia mbali magonjwa na maradhi kabisa, hata milele!—Ufunuo 21:3, 4.

Je! wewe ungependa kupata habari zaidi juu ya baraka hizo zilizoahidiwa na Mungu kisha ujue mambo ambayo ni lazima ufanye ili ufaidike kutokana nazo? Mashahidi wa Yehova watafurahi kukusaidia. Unaombwa uwafikie wale wanaokaa katika mtaa wenu au uandikie watangazaji wa gazeti hili.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Je! Sayansi Inamaliza Magonjwa?

Kansa: Ilikadiriwa kwamba mwaka jana tu kungekuwa na visa vipya 835,000 vya kansa katika United States (Amerika). Wakati uo huo, watu kama 430,000 wangeuawa na ugonjwa huo. Nalo Tengenezo la Afya Ulimwenguni linadai kwamba kati ya vile visa vya kansa milioni 37 vilivyokadiriwa kuwa vingetokea ulimwenguni pote, nusu kati yavyo viko katika nchi za ulimwengu zinazoendelea.

Influenza: Bila shaka influenza (homa kuu) ya Kispania ndiyo iliyokuwa ugonjwa wa fluu wenye kupiga watu wengi sana kuliko ugonjwa mwingine wote. Uliua watu wanaokadiriwa kuwa milioni 20 mwaka wa 1918 na wa 1919. Ijapokuwa kuna dawa za kuchanja, viini vipya vyenye kuleta fluu hiyo vimekwisha kutokea tangu wakati huo. Viini vya fluu vina uwezo unaoshangaza sana wa kubadili mara nyingi umbo lavyo lililo dogo sana, na kwa njia hiyo vinaleta maambukizo mapya yenye kupata watu wengi. Hivyo, fluu ya Kiasia iliua watu wapatao 57,000 ulimwenguni pote mwaka wa 1957. Fluu ya Hong Kong iliua watu 33,000 mwaka wa 1968 na 1969. Muda wa miaka 20 iliyopita, Waamerika wapatao 500,000 wameuawa na fluu hiyo.

Upofu Unaotokana na Mto: Upofu unaotokana na mto ni ugonjwa unaoendelea daima ambao unaenezwa wakati mainzi weusi wanapouma watu. Ambukizo la ugonjwa huo likiingia ndani ya mwili wa kibinadamu kovu linatokea katika ngozi na ndani ya macho. Ingawa ugonjwa huo unaweza kupofusha mtu, kwa kawaida hauwi hatari sana. Kwa ujumla, watu wapatao milioni 40 katika Afrika, Meksiko, Guatemala, Venezuela, Kolombia na Brazili wana upofu uliotokana na mto. Wachunguzi wangali wanatafuta matibabu salama zaidi ya kuponya ugonjwa unaotokana na mto.

Lupasi: S.L.E. (systemic lupus erythematosus) au kwa ufupi lupus, nyakati nyingine unakuwa ugonjwa hatari wa mfumo wa chembe zinazozuia maambukizo mwilini, nao unapata Waamerika kuanzia 500,000 kufika milioni moja. Mtu anapokuwa na ugonjwa wa lupasi viungo vya mwili vyenye kushikamana, ambavyo vinaunganisha na kutegemeza chembe za mwili, vinashambuliwa na zile chembe zenyewe zinazopasa kukinga mwili na maambukizo. Uwezekano wa kuepuka kifo kwa wagonjwa walio wengi umeongezeka katika miaka ya majuzi, kukiwa na asilimia kati ya 80 na 95 ya wagonjwa wenye kuishi miaka isiyopungua 10 baada ya ugonjwa wenyewe kuonekana. Lakini, mpaka sasa hakuna maponyo yanayojulikana ya ugonjwa wa lupasi.

Homa Inayotokana na Konokono (au Kichocho): Homa inayotokana na konokono inaenea kwa kasi sana. Tayari imekwisha kupata watu wanaokadiriwa kuwa milioni 200 katika nchi 71. Wanadamu wanapata ambukizo kwa kuoga au kuogelea katika maji yaliyo na konokono wenye kijidudu kinachofyonza mtu cha ugonjwa huo. Kikiisha kuuingia mwili wa mwanadamu, mayai ya kijidudu hicho yanaweza kuharibu sana kibofu na ini, na mara nyingi matokeo yanakuwa ya hatari. Bado ni vigumu kuizuia homa inayotokana na konokono (hasa katika nchi zilizo maskini zaidi), kwa maana uzuiaji wenyewe unategemea kuweka takataka mahali panapofaa.

Maleria (Ugonjwa wa mbu): Maleria ni ugonjwa unaosababishwa kwa kuumwa na mbu wa kike wanaoitwa anofelesi, nao umekuwapo tangu zamani za kale. Baada ya kuondolewa katika nchi kama India na Sri Lanka, katika miaka ya majuzi ugonjwa wa maleria umerudi tena ukiwa na maangamizi makubwa! Kila mwaka, katika Afrika, unaua watoto milioni moja walio chini ya umri wa miaka mitano. Tena, sasa watu zaidi ya milioni 150 ulimwenguni pote wanataabishwa na hali za kuona baridi, kuwa na homa kuu na dalili nyingine zinazotokana na maleria. Wachunguzi wangali wanatafuta dawa ya kuchanja ili wapambane nao.

Magonjwa Yanayoletwa na Uasherati: Kupatikana kwa dawa ya penisilini kuliipa tumaini hakika jamii ya watu yenye wendekevu. Sasa kisonono cha namna isiyoweza kugandamizwa na dawa ya penisilini kimekuwa kikienea.

Kumetokea ugonjwa mpya wa viungo vya uzazi unaoitwa herpisi, ambao unasemwa kuwa unapata watu kama milioni 20 katika nchi ya United States (Amerika) peke yake. Ugonjwa huo unasababishwa na kiini fulani na kwa kawaida kinapitishwa ndani ya mtu mwingine kwa kufanya ngono. Vivyo hivyo, ule ugonjwa mpya wa AIDS unaenea kwa kasi sana kati ya wanaume wenye kulalana na wenzao na kati ya watu wengine. Wachunguzi stadi wa ugonjwa huo wanauhesabu kuwa mmoja wa magonjwa ya kipuku yanayoua watu wengi zaidi. Hakuna maponyo yanayojulikana ya ugonjwa wa viungo vya uzazi wa herpisi wala ya ugonjwa wa AIDS.

Moltipo Siklerosisi: Huu ni ugonjwa wa mfumo mkuu wa mishipa ya fahamu​—ubongo na uti wa mgongo. Ugonjwa huu unasumbua watu wapatao 500,000 katika nchi ya United States (Amerika) peke yake. Kwa kawaida unawapiga watu wanapokuwa na umri wa miaka 20 na kitu na miaka 30 na kitu. Kuna dalili nyingi sana za ugonjwa huo, na nyingine zinatia ndani kufa ganzi, kukosa usawaziko mzuri wa miendo ya mwili, kuona vitu kwa kiwi (kwa njia isiyo waziwazi), kukokoteza maneno wakati wa kusema na kushindwa kuzuia mkojo usitoke katika kibofu au kushindwa kuzuia kinyesi kisitoke matumboni. Ingawa uchunguzi mwingi unaendelea kufanywa, hakujapatikana maponyo yo yote.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Yesu alikuwa na uwezo hata nia ya kushinda magonjwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki